NA MWANDISHI WETU
25th April 2013
Aidha, wizara hiyo imewaomba wabunge na wananchi wengine kwa ujumla wanaoelewa umuhimu wa dhana ya kugawana rasilimali kushirikiana na serikali kueneza dhana hiyo kwa manufaa ya taifa kwa ujumla na hivyo kupunguza migogoro isiyo ya lazima.
Kauli hiyo ilitolewa jana bungeni na Naibu Waziri wa wizara hiyo, George Simbachawene, alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalum, Ritta Mlaki (CCM).
Mlaki alitaka kujua mpango wa serikali wa kuhakikisha gesi inayozalishwa nchini inahifadhiwa ili itosheleze badala ya kuuzwa nje ya nchi.
Akijibu swali hilo, Simbachawene alisema: “Ushauri wako Mheshimiwa mbunge ni mzuri sana kama tu hapa nchini tungekuwa tunazalisha gesi kidogo, lakini kiasi tulichonacho ni kingi na kinatosheleza kabisa katika matumizi ya ndani na pia kuuzwa nje.”
Alisema kampuni zilizoingia mkataba na serikali kwa ajili ya utafiti na uzalishaji wa gesi hiyo, zinatumia fedha nyingi kiasi kwamba serikali pekee haiwezi kuzilipa hivyo ni vyema gesi hiyo iuzwe kufidia malipo hayo.
Awali katika swali la msingi la Mbunge wa Viti Maalum, Ritta Kabati (CCM), alitaka kujua kiasi cha gesi kinachozalishwa.
Pia alitaka kufahamu kiasi cha gesi kinachofika kwenye mitambo ya Ubungo.
Akijibu maswali hayo, Simbachawene alisema jumla ya futi za ujazo milioni 105 za gesi zinazalishwa Mnazi Bay na Songo Songo kwa siku.
Alisema kwa wastani, kati ya futi za ujazo milioni 100 na milioni 103 za gesi hufika Ubungo kwenye kituo cha kupokelea gesi kila siku kwa ajili ya matumizi ya kuzalisha umeme, matumizi ya viwandani, hotelini, majumbani na magari.
Alisema kati ya kiasi hicho, futi za ujazo milioni 90 hutumika kuzalisha umeme katika mitambo ya kufua umeme ya Songas na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) iliyopo Tegeta.
Aliongeza kuwa kiasi cha futi za ujazo milioni 10 hadi 13 kilichobaki hutumika kwa matumizi mengine ya nyumbani, magari na viwandani.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment