dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Tuesday, June 18, 2013

Upinzani watoa bajeti ya trilioni 20/-

NA SHARON SAUWA

18th June 2013

Spika wa Bunge,Anne Makinda
Kambi ya Upinzani Bungeni jana ilishindwa kuwasilisha bajeti mbadala bungeni kwa mwaka wa fedha 2013/2014 baada ya wabunge wake kutohudhuria kikao hicho.
Hata hivyo, kambi hiyo ilitoa hotuba yake kwa vyombo vya habari ikieleza kutumia Sh. trilioni 20 pamoja na kueleza mikakati mbalimbali ya kupungua matumizi ya serikali na kuokoa Sh. bilioni 741.
Wabunge hao wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) walifikia maamuzi hayo juzi ili kuwapa nafasi ya kuomboleza vifo vya watu waliouawa na mlipuko wa bomu na kujadiliana kuhusiana na tukio hilo lililotokea katika mkutano wa kufunga kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani uliopangwa kufanyika Jumapili iliyopita katika kata nne za jijini Arusha.
 
Spika wa Bunge, Anne Makinda, jana alisikika akisema kuwa hajapata taarifa kuhusiana na kutokuwapo kwa wabunge hao na hivyo kumpa nafasi Mbunge wa Bariadi Mashariki, John Cheyo (UDP) kuchangia bajeti ya serikali iliyosomwa bungeni Alhamisi iliyopita.Waziri Kivuli wa Fedha, Zitto Kabwe, alisema kambi rasmi imependekeza bajeti mbadala ya mwaka 2013/2014, kambi imepanga kutumia Sh. bilioni 20,710.537, kati yake makusanyo ya ndani ni  Sh. bilioni 15,698.937.
 
Kwa mujibu wa Zitto, watajikita katika kupanua wigo wa mapato ya ndani na kuachana na mikopo yenye masharti ya kibiashara ili kupunguza mzigo mkubwa ulioingizwa katika deni la taifa.
 
 “Asilimia 75.8 ya bajeti nzima ni mapato ya ndani ikijumuisha mapato ya halmashauri. Hivyo ni asilimia 24.2 tu ya bajeti ndiyo itatokana na misaada ya kibajeti na mikopo isiyo na riba za kibiashara,” alisema.
 
Alisema Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapendekeza kuondoa kabisa mikopo yenye masharti ya kibiashara na kupendekeza vyanzo mbadala vya mapato ili kuondokana na adha ya madeni na kukusanya mapato ya ndani kugharimia uendeshaji wa bajeti.
 
Alisema pia kupunguza matumizi yasio ya lazima na ili fedha hizo zielekezwe katika miradi ya maendeleo.

KUPUNGUZA MATUMIZI
 
Alisema kutokana na ongezeko kubwa la matumizi yasiyo ya lazima katika bajeti ya serikali, kambi rasmi ya upinzani imependekeza kupunguza asilimia 30 ya gharama za posho za vikao, semina, usafiri, viburudisho, mafuta na vilainishi.
 
Alisema mwaka 2012/2013 serikali inatumia Sh. billion 681 kwa matumizi yasiyo ya lazima na 2013/2014 imepanga kutumia Sh.
 
bilioni 714 (kwa mujibu wa taarifa ya Shirika la Sikika) sawa na ongezeko la asilimia tano kinyume cha kauli ya Waziri Mkuu ya kupunguza gharama za matumizi yasiyo ya lazima.
 
Kwa mujibu wa kambi hiyo, hatua hiyo itasaidia kuokoa Sh. bilioni 741.

VIPAUMBELE VYA BAJETI
 
 Kambi hiyo inapendekeza vipaumbele katika bajeti ya mwaka 2023/2014 kuwa ni kujenga mazingira ya ukuaji wa uchumi vijijini kwa kuboresha miundombinu ya umeme, barabara, maji na miundombinu ya umwagiliaji.
 
 “Tunapendekeza kutumia Shilingi bilioni 450 kila mwaka katika eneo hili. Fedha hizi zitasimamiwa na Mamlaka ya Maendeleo Vijijini itakayokuwa chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu,” alisema.
 
Vipaumbele vingine ni kukarabati Reli ya Kati na matawi yake ya Tanga-Arusha na Mpanda. 
 
“Tutatenga Shilingi bilioni 212.498 kwa RAHCO kwa ajili ya Reli. Fedha za ujenzi wa Reli zitakuwa ni fedha endelevu kutoka Railways Development Fund itakayotokana na tozo maalumu tunayopendekeza,” alisema.
 
Alivitaja vipaumbele vingine kuwa ni kuboresha elimu na afya hasa kwa shule, zahanati, vituo vya afya vya vijijini kwa kutoa motisha kwa wafanyakazi wa sekta hizi walio kwenye halmashauri za wilaya.
 
Zitto alisema wanapendekeza posho za mazingira ya vijiji sawa na mara moja na nusu ya mishahara yao.

KIMA CHA CHINI JUU
 
Kipaumbele kingine ni kuongeza kima cha chini cha mshahara kwa watumishi wa umma hadi Sh. 315,000 kwa mwezi.

PENSHENI YA UZEENI
Vipaumbele vingine ni kuuanzisha pensheni ya uzeeni kwa wazee wote nchini wenye umri wa zaidi ya miaka 60 na kupunguza mzigo wa matumizi ya magari ya serikali kwa kupiga mnada baadhi ya magari ya kifahari na kuweka mfumo wa kukopesha magari kwa watumishi wote wa umma wanaostahili magari.
 
Vingine ni kuanzisha Chuo Kikuu cha Mtwara (Mtwara University for Petroleum Studies) ili kuzalisha wataalamu wa kutosha wa sekta ya mafuta na gesi na kuliandaa taifa kuwa na wasomi mahiri wa maeneo hayo, hivyo kunufaika na utajiri wa mafuta na gesi uliopo nchini.
 
“Ni lazima kuongeza wigo wa kodi ili kuondokana na utamaduni wa kupandisha kodi zile zile kila mwaka na hivyo kuonekana kana kwamba hatuna ubunifu wowote,” alisema.

DENI LA TAIFA
Zitto alisema mfumo wa sasa wa kuweka pamoja malipo ya Deni la Taifa na malipo kutoka mfuko mkuu wa Hazina hauweki uwazi wa kutosha.
 
Pia alisema kwa taarifa ni kwamba baadhi ya vigezo vya kimataifa ambavyo serikali inasema Tanzania imekidhi na hivyo inaweza kukopesheka, vimeshapitiliza ukomo wake.
 
Alisema deni hilo lilofika Sh.  23,673,530,000,000 siyo ihimilivu tena.
 
“Kambi  Rasmi ya Upinzani Bungeni kwa muda mrefu imekuwa ikiitaka serikali ipunguze au iachane kabisa na mikopo yenye masharti ya kibiashara ambayo inazidi kuliongeza Deni la Taifa,” alisema na kuongeza:
 
“Kinyume cha nia hii njema ya Kambi ya Upinzani ya kujitegemea kibajeti, serikali hii ya CCM imeendelea kupuuza mawazo haya mazuri kwa kisingizio kwamba Deni la Taifa ni himilivu na kwamba nchi yetu inakidhi vigezo vya kimataifa vya kukopesheka.”
 
VYANZO VIPYA VYA MAPATO 
Kambi hiyo inavitaja vyanzo vya mapato kuwa ni pamoja na kongeza ufanisi wa bandari ya Dar es Salaam, kufanya marekebisho ya kodi za misitu, kupunguza misamaha ya kodi na kodi  katika mauzo na manunuzi ya nje kwa ajili ya kujenga reli.

 MFUMO WA FORODHA
Kambi hiyo ilisema inakusudia kupeleka hoja binafsi bungeni kutaka kuundwa kwa kamati teule kuchunguza mfumo wa forodha na ukwepaji kodi katika Idara ya Forodha ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa lengo la kuhakikisha ukwepaji kodi unadhibitiwa na wahujumu wote wanachukuliwa hatua stahili za kisheria.
 
“Suala la ukwepaji wa kodi linahusu pia wanasiasa wakiwamo wabunge. Ni dhahiri wabunge wana stahili za kisheria za kupata msamaha wanapoagiza magari yao na mambo mengine,” alisema.
 
Aliwashauri wabunge wote ambao ni wafanyabiashara waliosajili biashara zao katika Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na kupata vyeti vya misamaha ya kodi wawe wa kwanza kuhakikisha kuwa hawatumii misamaha hiyo vibaya.
 
“Natumaini baada ya CAG (Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali) kuanza kukagua misamaha ya kodi kama matumizi mengine ya serikali, tutashuhudia aibu kubwa tutakayopata kwa kutumia vibaya misamaha ya kodi,” alisema.
  
 
CHANZO: NIPASHE

No comments :

Post a Comment