Katie Gee (kushoto) na Kirstie Trup. Mabinti raia wa Uingereza waliopatwa na mkasa wa kumwagiwa tindikali eneo la Shangani, Zanzibar.
Na. Salim Said Salim
Hivi karibuni wasichana wawili wa Kiingereza,Kristie Trup na Katee Gee, walimwagiwa tindi kali wakati wa jioni na watu wawili katika eneo la Shangani, mjini Unguja.
Hivi karibuni wasichana wawili wa Kiingereza,Kristie Trup na Katee Gee, walimwagiwa tindi kali wakati wa jioni na watu wawili katika eneo la Shangani, mjini Unguja.
Mara tu baada ya kupatikana taarifa hizo zilizoushitua mji wa Zanzibar kwa vile kitendo hiki cha kinyama hakiwezi kukubalika na jamii inayojali utu zikasikika shutuma kali kwamba wahusika walikuwa wale wanaoitwa Waislamu wenye siasa kali.
Baadhi ya vyombo vya habari vya nchi za nje na hapa nchini vikapaza sauti za kuwalaumu Waislamu na vyengine, hasa vya nyumbani vikatoa tahariri zinazoeleza kuwa Zanzibar haikaliki na watalii wameanza kuwa na hofu ya kutembelea Zanzibar.
Sijui wataalamu hawa wa habari na baadhi ya maofisa wa Jeshi la Polisi walifanya uchunguzi wakati gani hata wakagundua waliofanya hivyo ni vijana wa Kiislamu wenye hiyo inayoitwa itikadi kali.
Bila ya kutafunia maneno hiki ni kielelezo chengine cha jinsi panapotafutwa sababu au kisingizio chochote kile, hata ikiwa hakiingii akilini kuwapaka matope Waislamu na dini yao.
Hii sio mara ya kwanza wala ya pili kutolewa kauli kama hizi zisio na mshiko ambazo unaweza kusema hazina lengo jengine isipokuwa kuonyesha Zanzibar wapo Waislamu wanaohusudu kufanya vitendo vya kijahili kama hivi.Jengine ni kutaka kuiharibu sifa ya Zanzibar kama nchi ya watu karimu na wanaopenda wageni ili kuichafua sekta ya utalii ambayo hivi sasa ni inategemewa sana kwa uchumi wa visiwa hivi vyenye mambo mengi yanayovutia watalii.
Kwanza tujiulize nini kilichopelekea kufikiriwa watu waliofanya unyama huo kuwa ni Waislamu au walikuwa na chapa inayoeleza “ Sisi ni Waislamu”? Vile vile nini kinachopelekea pasifikiriwe waliohusika ni watu wa dini nyengine au wasiokuwa na imani yoyote ya dini, bali ni majahali tu waliokuwa na lengo waliolijuwa wenyewe?
Katika nchi yenye utawala bora na vyombo vya habari vinaofuata maadili na kuwajibika ungelitarajia kufanya uchunguzi kwanza kabla ya kuwahusisha Waislamu au waumini wa dini yoyote ile, chama cha siasa au wenye utashi wa jambo fulani.
Kinachoshangaza ni kuona yapo magazeti ya nje ambayo yameibua mambo ambayo vyombo vingi vya habari na polisi hawajayaeleza, labda kwa makusudi au kwa vile undani wa suala hili haukutafutwa.
Kwa mfano, gazeti la The Telegraph la Uingereza la tarehe 12 Agosti kwamba mara mbili katika kipindi cha wiki moja kabla ya wasichana hawa kumwagiwa tindi kali walikuwa na mkwaruzano na watu katika maeneo ya Mji Mkongwe.
Gazeti hilo lilimnukuu rafiki wa wasichana hawa, Oil Cohen (21), ambaye alikuwa nao Zanzibar akisema katika tukio moja wakati wa mwezi wa mtukufu wa Ramadhani wasichana hawa walikuwa wanaimba hadharani na hilo liliudhi watu. Katika purukushani hii, kwa mujibu wa Cohen, dada mmoja alimchapa kibao cha usoni Kristie.
Rafki mwengine wa wasichana hawa, Oliva Moore, alikiambia kituo cha televisheni cha Channel 4 News cha Uingereza kuwa vijana wawili waliowamwagia wasichana hawa hilo tindi kali ambalo madaktari wa Uingereza walilieleza kama maji ya betri ya gari walipita katika kundi liliokuwa na wazungu wengi.
Vijana hao waliwaangalia vizuri hao wazungu na mmoja wao alionesha kidole na mwenzake alipoinua kichwa kuitikia “Ndio” ndipo walipomwagwa hilo tindi.
Jee matukio haya hayaonekani kama palikuwepo jambo hapa na kwamba kitendo hicho kiliwalenga wasichana hawa wawili tu kwa jambo ambalo lina taswira ya “kulipiza kisasi” au kutokana na tukio la hapo awali?
Hapa tujiulize kwa nini habari hii haitolewi maelezo na badala yake kukurupuka tu na kuwalaumu Waislamu na sio watu walioshukiwa kuwa na ajenda maaalum ya kuwasaka wasichana hawa?
Ukiangalia hizo tahariri zinazoeleza kuwa Zanzibar haikaliki hasa za kampuni moja ya gazeti binafsi utaona wazi hapana kigezo cha uhakika kilichotumika kufikia uamuzi huu.
Hapa tujiulize kama mtukio yamashambulizi ndio kipimo cha kuamua eneo fulani halikaliki ni wapi hapakaliki Bara au Visiwani?
Ukiangalia kwa undani utaona matukio ya mashambulizi ya Bara ukilinganisha na ya Zanzibar ni mengi na ya hatari zaidi.
Kwa mfano, tumeshuhudia Bara pakitokea mripuko kanisani (Arusha). Huu mripuko ulipotokea na baadhi ya watu kuuawa na wengi kujeruhiwa lawama wakatupiwa Waislamu wenye siasa kali.
Hapo tena wakaanza kusakwa Waislamu na miongoni mwao walikuwa raia wa nchi za Kiarabu waliokuwa nchini kama watalii. Hatimaye, wale Waarabu walionekana hawahusiki na hivi sasa ni vijana wa Kikristo ndio wanaokabiliwa na mashitaka ya kuhusika na mripuko huo.
Kwa nini hatuambiwi vijana hawa ni Wakristo wenye siasa kali kama inavyoelezwa kwa watu wanaotuhumiwa ambao huwa waumini wa dini ya kiislamu?
Kama ni matumizi ya tindi kali kutumika kushambulia watu basi Bara nako pia mwenendo huu nao umeshamiri.
Jee tunayaonaje mashambulizi ya risasi kupigwa katika mkutano wa Chadema yaliyofanyika Arusha mjini, upigwaji nondo wa imamu katika msikiti wa Mbeya, mauaji ya waandishi wa habari Iringa na Kigoma na mashambilizi mabaya ya mwandishi wa habari Dar es salaam.
Pamoja na haya ni hili tukio la kushambuliwa kwa Sheikh Issa Ponda Morogoro. Nalo hili ni tukio la kiusalama? Au ndio tuseme matukio yote haya sio makubwa na hayatishi kuliko ya Zanzibar?
Ukiitafakari hali ilivyo utaona kama ni eneo kutokalika kwa vile ni la hatari basi ni Bara na sio Zanzibar.
Hata hivyo, upo umuhimu wa kuachana na utamaduni huu mpya wa kuropokwa na taarifa zinazopalilia chuki dhidi ya watu wa dini moja, eneo au kabila. Hii ni hatari kubwa na inaweza kupeleka nchi hii katika hali mbaya zaidi kuliko inayoonekana sana.
Vyombo vya habari lazima vitambue kuwa vinao wajibu wa kuwaweka pamoja kwa maelewano wananchi na sio kupalilia chuki na mfarakano kwa misingi ya kidini au mengine yoyote ile. Kama vyombo hivi haviwezi kuwasaidia Watanzania kuwa wamoja basi visipalilie mfarakano.
Tanzania, Bara na Visiwani, hivi sasa inakabiliwa na mtihani mkubwa ulizusha vurugu, kutoelewana na kutoaminiana.
Mwenendo unaoonekana hivi sasa wa kuisakama Zanzibar kama eneo ambalo halikaliki na ni la hatari ni kutoitendea haki Zanzibar na watu wake. Miongoni mwa wanaoweza kuisaidia Zanzibar kuonekana kuwa ni nchi ya amani na sio hatari kwa watalii kutembelea ni vyombo vya habari, lakini kwa bahati mbaya baadhi yao ndio vinapaliliaa kuonekana Zanzibar sio salama na ni hatari kwa watalii kutembelea visiwa hivi.
Kwa kweli inasikitisha na ni matendo kama haya ndiyo yanayopelekea baadhi ya Wazanzibari kuona na kuamini kuwa hawatendewi haki na baadhi ya ndugu zao wa upande wa pili wa Muungano .
Ni hekima, busara na kutokurupuka na taarifa zisiokuwa na uchunguzi zinazoweza kuchochea balaa ndio zitazoweza kuinusuru nchi hii.
Chanzo: Fahamu
No comments :
Post a Comment