NA MWANDISHI WETU
4th September 2013
Alidai pia kama hitilafu inajitokeza kwenye gazeti, unatolewa wito wa simu ambao wakati mwingine ni barua kama angalizo, onyo au wito kutoka Idara ya Habari (Maelezo) jambo ambalo pia halijafanyika.
Kibanda ambaye kwa sasa ni Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya New Habari 2006 Limited, alidai bado anaamini kwa dhati kwamba makala hiyo haina matatizo yoyote, kwa sababu hakupata mrejesho wowote kutoka mahali popote kwa wasomaji wa gazeti lake ambao wana uelewa mkubwa wa kutoa malalamiko.
Alidai makala hiyo ilikuwa na lengo la kuelimisha na kuwapasha watu habari, na ilielekezwa kwa askari wote na kwa wananchi wote wanaoandamana wajue haki zao.
Kibanda alitoa madai hayo mahakamani hapo jana alipokuwa anatoa utetezi wake katika kesi ya uchochezi inayomkabili pamoja na mwandishi wa makala hiyo, Samson Mwigamba, mbele ya Hakimu Warialwande Lema.
Aliendelea kudai kuwa hajaona madhara yoyote yaliyotokana na makala hiyo wala hakuna askari ambao wameacha kutii amri za wakubwa wao.
Kibanda alidai kuwa wakati makala hiyo inachapishwa, yeye alikuwa amesafiri kikazi na makala hiyo ambayo ilikuwa kwa mfumo wa maoni ya mwandishi ilipokewa na Mhariri wa Tanzania Daima Jumatano.
Aliongeza kwamba hakuna askari aliyekwenda kulalamika ikiwa na maana kwamba hakuna aliyesoma gazeti hilo wala kulinunua zaidi ya shahidi aliyetoa ushahidi mahakamani, ambaye amewasilisha malalamiko kokote juu ya muktadha wa makala hiyo.
Aidha, Kibanda alisisitiza kuwa kama kuna hitilafu katika gazeti kwa kawaida siku moja au mbili viongozi wanaitwa Maelezo, ila hadi siku anaitwa Polisi ilikuwa zaidi ya wiki mbili na hakukuwa na dalili kwamba wangeitwa hadi shauri lilipofikishwa mahakamani.
Alidai badala ya Maelezo kulalamika, polisi ndiyo walipiga simu katika idara hiyo na kulalamikia makala kuwa ni ya uchochezi.
Naye Samson Mwigamba aliiomba Mahakama imuone hana hatia kwa sababu mashahidi upande wa Jamhuri wameshindwa kuonyesha mahali palipo na uchochezi katika makala hiyo.
Aliyejiita mlalamikaji ni Ofisa wa Polisi aliyekuwa amemuita na kumhoji naye pia alishindwa kuthibitisha mahakamani vielelezo vya mwenendo wa kikao alichodai alikifanya na askari wa chini yake.
Alidai katika makala yake hakuwataka askari washiriki maandamano, bali maandamano yanapotokea askari wanatakiwa wawapo kulinda amani na ndiyo maana kwenye makala yake ya ‘Waraka Maalum kwa Askari wote’ alitumia mfano wa Misri na Uingereza.
Aliendelea kudai kuwa lengo la makala lilikuwa kuwakumbusha askari kwa yale waliyofundishwa kwamba siyo kila amri ni ya kutii, nyingine zinakinzana hata na Biblia.
“Lengo la waraka huo lilikuwa kutoa maoni kwa askari wasivunje haki za katiba katika mambo mawili; haki za watu kukusanyika kwa maana ya maandamano na haki ya kuishi.
Shahidi huyo upande wa utetezi alidai kuna matukio mengi yaliyokuwa yamefanywa na askari likiwamo la Januari 2011, jijini Arusha baada ya viongozi na wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) walipokuwa wanaandamana kwa amani, lakini walivyofika eneo la Tengi la Maji Polisi wakawaua watu watatu.
Alidai baada Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kufanya uchunguzi walitoa ripoti iliyosema askari wamevunja katiba na sheria.
Mwigamba alidai kuwa makala yake hakuituma kwa Kibanda wala mshitakiwa mwingine Theophil Makunga, aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Mwananchi Communications LTD (MCL) bali aliituma kupitia internet.
Aidha, alidai upande wa mashtaka ulidai uliunda kikosi kufanya uchunguzi ila hakuna ripoti yoyote iliyotolewa.
Katika kesi hiyo, washtakiwa, Kibanda na Mwigamba wanadaiwa kutoa waraka wa uchochezi kinyume cha kifungu cha 32(1)(c) na 31(1) (a) cha Sheria ya Magazeti Sura ya 229 ya mwaka 2002.
Shtaka la pili, linamkabili Makunga la kuchapisha waraka wa uchochezi kinyume cha kifungu cha 32(1) ( c) na 31 (1)(a) vya Sheria ya Magazeti namba 229 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002 .
Ilidaiwa kuwa Novemba 30, mwaka 2011, MCL chini ya uongozi wa Makunga ilichapisha makala ya uchochezi iliyokuwa na kichwa cha habari kisemacho ‘ Waraka Maalum kwa askari wote’ ambayo iliandikwa na gazeti la Tanzania Daima Toleo Na. 2552 la Novemba 30, mwaka 2011.
Ilidaiwa kuwa washtakiwa hao kwa makusudi na kwa nia kuvunja sheria za mamlaka ya serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania walitenda kosa hilo la uchochezi kwa kuruhusu makala hiyo ichapishwe kwenye gazeti hilo Novemba 30, mwaka 2011 ambayo ilikuwa ikiwachochea askari wasitii mamlaka za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kesi hiyo iliahirishwa hadi Septemba 23, mwaka huu na Hakimu Lema aliagiza samansi itolewe kwa ajili ya shahidi mwingine.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment