zanglassworks

AirFreight

Kwarara Msikitini

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Monday, September 2, 2013

Wangemfukuza tu, Mansour angebaki Mzanzibari imara

Mansoor Yussuf Himid ambaye amevuliwa uanachama wa  Chama Cha Mapinduzi (CCM) hivi karibuni.
Mansoor Yussuf Himid ambaye amevuliwa uanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) hivi karibuni.
DHAMIRA ya uongozi wa juu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) upande wa Zanzibar ya kufukuza wanachama wake muhimu, inashangaza sana. Si kwamba inashangaza kwa kuwa ni dhamira mbovu. Hapana.
Inashangaza kwa sababu inawaonesha hao viongozi wa juu kuwa wanamatatizo makubwa ya kutenda bila ya kwanza kutafakari. Wala si kwamba huwa hawatafakari kabisa, sivyo ilivyo. Huwa wanatafakari, isipokuwa, hawatafakari kwa kina.
Ingawa katika hali ya kawaida ya mitazamo ya mambo, nisingepaswa kujadili uendeshaji wa ovyo wa siasa CCM – maana ningewaacha tu wajifanyie watakavyo – nimeona vema wiki hii, niingie katika sakata la viongozi wa juu wa CCM Zanzibar kutengeneza mazingira ya kumfukuza chama kijana wao kinda kabisa, Mansour Yussuf Himid.
Naona kwa hatua yao hiyo, wamejithibitisha walivyo, kwa mengi.
Tangu pale Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (KM-NEC-CCM) ilipoamua kupokea kile walichokiita wenyewe, “mashtaka ya utovu wa nidhamu” dhidi ya Mansour, na kuruhusu mashitaka hayo yajadiliwe na hatimaye kutolewa pendekezo la kwenda Kamati Kuu Dodoma, niliwachukulia viongozi hawa kama watu waliochoka kifikra hivyo kutojali tena misingi ya uongozi katika zama za kisasa.
Awali ya yote nasema hapa, haikuwa jambo la busara kwa namna yoyote ile, wao kumjadili Mansour kama ni kweli kulitokana na msimamo wake wa kutaka mabadiliko ya mfumo wa Muungano. Mansour amekuwa akitaka mfumo wa Muungano wa Mkataba ambao unairudishia Zanzibar, kama dola huru, mamlaka yake kamili ya kuendesha mambo yake.
Sasa kama kweli walimtazama Mansour kwa msimamo wake huu, na wakaona haufai, bali wakajiaminisha kuwa ni muhimu wamchukulie hatua ambazo wenyewe wanaziita ni “za kinidhamu,” ndipo hapo ninapoona hawakuona mbali. Hawaendi na wakati wa sasa. Hawafikiri sawasawa, angalau kwa masuala haya ya uongozi na siasa za kileo.
Wakati ndivyo nilivyoamini tangu niliposikia wamemjadili Mansour na kufikia hatua ya kupendekeza kumtimua uanachama na pendekezo hilo kutaka na kufanikisha liwasilishwe mbele ya Kamati Kuu ya NEC, ile ya Makao Makuu ya Chama Dodoma, hawaoni leo walivyosutwa na viongozi wenzao Dodoma?
Ni nini kama siyo kusutwa watu wazima? Leo tunapata taarifa kwamba Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Jakaya Kikwete, pamoja na Katibu Mkuu wa Chama, Abdulrahman Kinana, wana mawazo tofauti na wenzao hao wa Zanzibar.
Kwa mujibu wa taarifa za ndani ya kikao cha Kamati Kuu kilichoketi Ijumaa hadi usiku wa manane kuamkia Jumamosi, na kuendelea Jumamosi, Mwenyekiti Rais Kikwete alitangaza mapema kabisa kikaoni, kwamba viongozi na wanachama wa CCM ni muhimu “wakawavumilia” wenzao watakaokuwa na mawazo tofauti kuhusu Rasimu ya Awali ya Katiba ya Tanzania. Kwamba wale wenye mawazo tofauti na msimamo wa Chama kuhusu mfumo wa serikali itakapokuja Katiba mpya, wavumiliwe, ndivyo anavyosema.
Kwa hivyo, kiongozi mkuu wa Chama, na mkuu wa Serikali iliyopo madarakani, Dk. Kikwete, yeye anaona kwamba “si tatizo sana” kwa chama kusikia baadhi ya wanachama wake wanawaza vinginevyo, tofauti na msimamo wake, au vile kinavyowaza chama chenyewe.
Kwa kweli sijuwi sababu za Mwenyekiti Dk. Kikwete kuamini hivyo. Sijuwi. Nafikiria hivi kwa sababu si kwa kuwa na msimamo huo anaonekana kupingana na viongozi wenzake wa ngazi ya juu vilevile walioko Zanzibar? Ndio, anatofautiana nao.
Anatofautiana nao kifikra ndio maana wao waliona Mansour alikosea, na kwa hakika waliona ana makosa mazito hata sasa, ndipo wakamuandalia ajenda maalum katika Kamati Maalum ya NEC, na kuiwasilisha, wakuruhusu ijadiliwe, na hatimaye wakaamua ipelekwe Kamati Kuu ile ya Makao Makuu, Dodoma kama “pendekezo mahsusi.” Ilipelekwa na imejadiliwa tayari.
Lakini, nataka kuamini kuwa Mwenyekiti Dk. Kikwete ameangalia mazingira halisi ya mambo yalivyo. Na kabla sijaendelea mbele zaidi, nipachike kabisa hapa kwamba hata Katibu Mkuu Kinana naye ameona vinginevyo. Naye amemkalia kooni msaidizi wake mkuu kwa Zanzibar, Naibu Katibu Mkuu Vuai Ali Vuai, ambaye anatajwa kuchangia sana kufanikisha “mpango mchafu” kwa Mansour.
Taarifa za ndani ya kikao cha Kamati Kuu Dodoma, zinasema Kinana alisema wazi hawafiki kufukuzwa Mansour katika hali iliyotengenezwa Kisiwandui. Hakubaliani nao viongozi wa Zanzibar. Kwake, hakuna kosa analoliona kutendwa na Mansour. Swadakta.
Hawa wao wanaona mbali. Je, tuseme wao miwani yao ya kuona ni tofauti na ile wanayotumia wenzao wa Kisiwandui? Inawezekana ni tofauti maana siku hizi si ipo miwani inatoka Uchina; miwani ya Kichina? Jibu la uhakika watalitoa wao.
Hapa ndipo unapoiona tofauti ya watu katika kufikiri. Wengine wanafikiri kwa sehemu tu ya ubongo wao, si ubongo kamili; wakati wengine wanafikiri kwa kuutuma ubongo kamili. Katika makundi haya ya watu wanavyofikiri, lazma utapata maamuzi tofauti.
Wengine watakuja na maamuzi ya ovyo. Mengine hayatekelezeki. Mengine yanatekelezeka ila kwa kuchelewa. Maamuzi mengine, hasa yaliyotolewa na watu waliofikiri kwa utulivu, yanakuwa yanayotekelezeka kwa wepesi.
Maamuzi ya kina Dk. Ali Mohamed Shein akisaidiwa na kina Vuai, yamepingwa kwa kuonekana hayatekelezeki hata yakipewa miaka. Ni maamuzi ya ovyo, yasiyokipa heshima chama. Yasiyokijenga wala kukiimarisha. Ni maamuzi yanayojenga taswira chafu; kwamba chama hiki kina watu, na hususan viongozi wake waandamizi, dhaifu wanaohitaji kuchangiwa mawazo, vinginevyo kwa kuachiwa watende na kuamua peke yao tu, kuna hatari ya kukisambaratisha chama mchana kweupe.
Basi Mwenyekiti Dk. Kikwete anasema “wavumiliwe” wanachama wenye mawazo tofauti na yale yaliyoamuliwa na chama. Na kwa hakika inajulikana si ndivyo Halmashauri Kuu ilivyotaka? Wanachama waichukuwe rasimu na kuichambua, na kutoa maoni yao, pamoja na kutambua kwamba chama kimetoa msimamo wake?
Tatizo liko wapi sasa hata viongozi wengine, hawa wa Zanzibar, wao waone ni dhambi kubwa mwanachama wa nje ya wale wa NEC, au hata wao, wakiwa nje ya kikao kile kilichoamua msimamo wa chama, kuamua na kuthutubutu kutoa maoni au msimamo tofauti na wa chama?
Viongozi wa juu wa Zanzibar wanafikiri leo kama walivyokuwa wakifikiri juzi. Wanafikiri sasa lakini huku wakikumbuka na kuamini zaidi misimamo ya zama zile. Huku ndio kufikiri kwa njia nyingine. Unafikiri kwa kutumia nywele. Sasa asiye nazo je? Yeye atafikiri kwa vipi?
Kwa kuujua ubaya wa watu kufikiri kwa njia isiyokuwa ile ya kuutuma ubongo kwa utulivu na kwa wakati muafaka, ndio maana kada mmoja wa CCM alipokuwa akikwaruzana na wabunge wa CCM watokao Mkoa wa Dar es Salaam, alipata ujasiri wa kuitaja njia ile nyingine ya kufikiri. Walikuwa wakifikiri kwa maslahi yao tu siyo ya chama. Haramu.
Hivi kumfukuza Mansour kipindi hiki kungeifundisha nini jamii ya Wazanzibari ambao wanafikiri kwelikweli kuhusu namna gani nchi yao, iliyokuwa na mamlaka kamili mpaka baada ya mapinduzi, na ikajipangia mipango yake yenyewe ya kuiendeleza kiuchumi na kiutamaduni, itarudisha hadhi ile.
Wazanzibari wanajiuliza katika hali ambayo CCM inatumia nguvu nyingi, bila ya shaka na raslimali nyingi za watu na fedha, kutaka kupeleka ajenda yake iaminike kwa Watanzania wengi zaidi, ni kwa vipi Watanzania hao watapata fursa ya kuitizama hali ya Zanzibar ili pia na kuifikiria itakavyokuwa katika huo mfumo inaokusudia CCM ukubalike?
Mawazo ya Wazanzibari yanalenga hapo. Kwamba je, ikiwa rasimu itakayoletwa mbele yao, baada ya zile hatua nyingine muhimu kukamilika, na ikiwa imekuja katika mtizamo wa ki CCM zaidi kuliko ule unaozingatia maslahi ya kweli ya Zanzibar kama nchi huru, na inayopaswa kujitegemea kwa kila kitu, Wazanzibari watatosha kuikwamisha?
Mansour aliamua kutoka nje ya duara la uovu. Aliamua kuutambua ukweli wa mambo. Aliamua kuwa muwazi mapema. Hakutaka kuwa mnafiki. Hakutaka kujiweka kwenye kona kwani alijua, na anaamini, ukishajiweka kona, inakuwa vigumu sana kumkabili mpinzani. Huyu mpinzani akikufuata pale kwenye kona huku akikupa majebu mazito, unatokaje pale ili nawe urushe mbili tatu za kumvunja nguvu wakati unajihami?
Mansour alifikiri kwa kutumia ubongo kamili. Alifikiri kwa ajili ya maslahi ya nchi yake, kwa ajili ya watu wake. Alifikiri kwa ajili ya mustakbali wa nchi yake na watu wake. Hakufikiri kwa ajili ya maslahi yake peke yake na familia yake. Hapana.
Kijana huyu ametoa mfano mzuri kwa wanasiasa wakongwe. Amewafunda wanasiasa chungunzima waliopo kabla yake. Hata wakisema alijiunga na CCM akiwa waziri, tatizo liko wapi? Kwani hao waliopo CCM tangu kilipozaliwa, wana mchango mkubwa kiasi gani wa kufaa kukumbukwa ni mchango muhimu? Kweli hawajatulia, kwani kukaa siku nyingi kwenye jumuiya ndiyo uadilifu? Ndi mchango unavyopimwa?
Wanasiasa hao wapo. Wapo tangu hapo nyuma. Wapo tangu CCM inazaliwa Februari 5, mwaka 1977, miaka 36 iliyopita. Sawa. Lakini mbona chama chao kinazidi kukimbiwa na watu? Ni nini maana yake una wanasiasa wanaojaa mv Mapinduzi mia lakini wameshindwa kukiimarisha chama na kinadhoofika siku hadi siku?
Masikini roho zao, hawajuwi kwa ujasiri wake Mansour amekijenga chama kwa upande huo? Amekijenga maana wapo wengi wanaompigia kampeni jimboni kwamba anaonewa. Wapo na wanasubiri tu afukuzwe waende nae.
Haya ni tofauti na asemavyo Dogo, eti chama ndicho kilimpa umaarufu na hadhi Mansour. Kwamba Dogo anaamini na anataka wana-CCM waamini, Mansour akifukuzwa hata sasa, chama hakitaterereka Kiembesamaki. Ndo kufikiri kwa nyewe huku.
Mimi si CCM lakini najua Kiembesamaki inamtegemea sana Mansour kuiokoa. Hili ni jimbo lenye watu wasomi sana. Watu wenye nguvu ya fedha. Watu wenye ushawishi mkubwa wakitaka jambo lao. Jimbo la Kiembesamaki wangependa wawe wanang’ara. Wangependa wawe na vitu vya kwao wenyewe.
Kwani wanajua Mansour alishatengenezewa zengwe muda mrefu huko nyuma. Ila wanajiuliza kwani amekosa nini kuwa na mawazo tofauti na chama chao? Chama ambacho kilitoa fursa kwa wanachama wake kuipata rasimu, kuichambua na kuitolea maoni. Hayo aliyoyatoa si ni maoni yake binafsi?
Hajakisemea chama kwa sababu anajijua yeye si msemaji wa chama na hajashawishi CCM wakubali mawazo yake.
Mansour ni mtu huru. Alivuliwa nafasi zake za uongozi ndani ya Chama. Ametulia. Anafanya shughuli zake. Anatumikia wapiga kura wake Kiembesamaki. Lakini hajazuiwa kufikiri kwa namna anavyotaka kufikiri. Tena, si sahihi na wala si halali chama kubana watu wake wasifikiri nje ya wigo wa fikra zake.
Na hali hii ndiyo waliyoiona Mwenyekiti Dk. Kikwete na Katibu Mkuu Kinana. Walijua kwa kuamua wanachama waichambue rasimu, watatokea tu wenye akili timamu wataona mambo kwa sura nyingineyo. Wala haikuelezwa kuwa ni lazima kila mwana-CCM afikiri kwa sura moja tu ya maslahi ya CCM. Hapana.
Nilikuwa nasubiri hatima ya mijadala katik vikao vya juu vya CCM nijuwe Mansour aliposimama. Sasa inawezekana sana asifukuzwe. Duu, angefukuzwa ningefurahi. Ningekuwa na furaha kwa sababu moja kubwa: Wenyewe CCM wanakikongozoa chama chao. Shauri yao. Mansour si chama. Angebaki Mzanzibari imara.

Chanzo: Fahamu

No comments :

Post a Comment