Ahmed Rajab
Toleo la 322
23 Oct 2013
UPIGAJI ramli si moja kati ya ashki zangu. Na aghalabu ninapojaribu kubashiri kitu huambulia patupu. Sisemi kama nimepata ilhamu kutoka kwa Mwenyezi Mungu, lakini kila nikipiga bongo na kuiangalia Afrika na dunia, kwa jumla na jinsi itavyokuwa miaka 20 au 30 ijayo nahofia kwamba patazuka mchuano na mapambano makali.
Toleo la 322
23 Oct 2013
UPIGAJI ramli si moja kati ya ashki zangu. Na aghalabu ninapojaribu kubashiri kitu huambulia patupu. Sisemi kama nimepata ilhamu kutoka kwa Mwenyezi Mungu, lakini kila nikipiga bongo na kuiangalia Afrika na dunia, kwa jumla na jinsi itavyokuwa miaka 20 au 30 ijayo nahofia kwamba patazuka mchuano na mapambano makali.
Hayatokuwa ya kijeshi bali yatakuwa ya kifalsafa. Wakati Tanzania inapojiandaa kuwa na Katiba mpya itayoliongoza shirikisho jipya lijalo tunapaswa kuyapa kipaumbele pia hayo mapambano yajayo yatayojaribu kuamua ni itikadi ipi ya kisiasa iliyo bora kushinda nyingine.
Mapambano hayo yatasababishwa na mchuano wa falsafa za kisiasa, baina ya demokrasia kama tuijuavyo leo na mifumo mingine ya kisiasa. Kitachoichongea demokrasia ni udhaifu wake,
udhaifu ambao tayari tunauona katika jamii kama za kwetu ambako mfumo huo bado ni mchanga na hata katika jamii zenye mifumo ya kidemokrasia iliyokomaa ambako mifumo hiyo inahatarishwa na mifumo ya kiuchumi iliyo katika hatari ya kufilisika.
Nchi za Magharibi zinajivunia na demokrasia iliyotia mizizi nchini humo na wananchi wa nchi hizo wanaamini kwamba demokrasia ndio mfumo wa kisiasa ulio bora kushinda yote duniani.
Wanahoji kwamba mfumo huo unampa kila mwananchi fursa ya kuwa na usemi sawa juu ya namna nchi inavyoendeshwa. Chini ya mfumo huo wananchi wote wanakuwa sawa mbele ya sheria, wakiwa na haki sawa za kijamii, kisiasa na za kiuchumi.
Serikali huwa haiwabagui raia zake kwa sababu ni wa kabila fulani, dini fulani au jinsia fulani. Na wote wana haki sawa ya kuichagua serikali waitakayo.Hivyo ndivyo mfumo huo unavyotakiwa uwe, ingawa kwetu Zanzibar hivyo sivyo ilivyo.
Watetezi wa demokrasia wanahoji pia kwamba sifa kuu ya demokrasia ni kuwa mfumo huo unayalinda maslahi ya umma — yawe ya kisiasa, ya kiuchumi au ya kijamii.
Watetezi hao wanaongeza kuhoji kwamba mfumo huo pia unaweka utaratibu wa kuziondosha serikali kwa njia za amani au wa kuzichagua tena baada ya vipindi maalumu.
Hiyo, bila ya shaka, ni sura moja tu ya demokrasia. Mfumo huo una sura nyingine isiyopendeza, inayoufanya mfumo huo usawijike.
Sura ya demokrasia kwanza inafujwa na vyama vya siasa.Mfumo huo unategemea kuwako kwa vyama tafauti vya siasa. Kila chama cha siasa kina lengo moja, nalo ni kunyakua madaraka ya serikali. Jukumu la wanachama wake ni kuyalinda maslahi ya chama chao. Baadhi ya nyakati, wanayaweka mbele maslahi ya chama chao badala ya maslahi ya taifa.
Hayo tunayaona wazi siku hizi Bara na Zanzibar ambapo baadhi ya viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wamo mbioni kuukwamisha mchakato wa kulipatia taifa Katiba mpya ili kukinusuru chama chao badala ya kulinusuru taifa. Na Zanzibar tunaona jinsi wanachama hao wanavyofanya juu chini washinde katika kila uchaguzi kwa njia safi na chafu, za halali na za haramu.
Halafu tena kuna uzito wa mfumo wa kidemokrasia. Kwa kawaida, serikali za kidemokrasia zina urasimu uliomzito na kwa sababu ya uzito huo huwa hazina kasi; mwendo wao huwa wa kobe, wakati mwingine wa kusotasota hasa.
Badala ya kuwawezesha waamuzi wakate maamuzi yao kwa haraka huwa na tabia ya kuwazonga zonga na kuwazuia wasichukue hatua wanazotaka kuzichukuwa.
Akhasi zaidi ni kwamba mfumo huo unawawezesha wakereketwa na wafadhili wa chama kinachotawala wawe wanapendelewa kwa kupewa fursa za aina kwa aina toka za kazi serikalini hata fursa za kibiashara.
Zanzibar ambako mfumo huo hata haujashamiri na kutia mizizi sawasawa tunaona jinsi wale wanaoaminiwa na CCM kuwa ni ‘wenzetu’ wanavyopendelewa, ima wao au watoto wao, wakati wa kuwaajiri watu serikalini, wa kupandishwa vyeo au wa kupelekwa nje kwa masomo ya juu.
Kuna ushahidi, na ushahidi huu tumeushuhudia mara kwa mara wakati wa chaguzi nchini Tanzania, kwamba mfumo wa kidemokrasia husababisha kuporomoka kwa maadili miongoni mwa wanasiasa, hasa wale wanaopigania uchaguzi. Lengo pekee la wagombea uchaguzi ni kushinda uchaguzi. Ili kulitekeleza lengo hilo tumeshuhudia jinsi wagombea uchaguzi, toka ule wa bunge hadi wa urais, wanavyowapikia majungu washindani wao, wanavyowakashifu na walivyo tayari kutumia njia ovu na ushenzi ili wachaguliwe.
Lakini labda ila moja ya demokrasia ya kisasa yenye kutia sana wasiwasi ni ulazima wa kuwahonga wapigaji kura ili wampigie kura mtetezi mwenye kuwahonga. Huu ni mtindo mbaya. Ni mtindo unaowapa fursa wazembe, wajinga na mafisadi waweze kuchaguliwa na umma kwa sababu tu wana fedha za kuwanunua wapigaji kura.
Kwa hakika, katika demokrasia ya kisasa wenye kuchaguliwa aghalabu huwa ni wanaojiweza, matajiri wenye fedha zao. Hivyo, wanapochaguliwa na wakaunda serikali hizo serikali huwa ni serikali za matajiri zikijivyesha kanzu za kidemokrasia.
Serikali zenye kuundwa na watu aina hiyo huwa haziwajali walala hoi, wananchi wa kawaida. Huwa ni serikali za kidemokrasia kwa jina lakini uhalisi wao ni wa kitajiri, wa kibepari. Hayo pia tumeyashuhudia Tanzania na tumezishuhudia athari zake.
Wakati mwingine huwa ni chama chenye kuhonga na chama chenye kuhonga kinaposhinda uchaguzi na kuunda serikali hiyo, serikali baadaye hutumia fedha za umma kwa ubadhirifu ili iweze kutekeleza ahadi zote ilizozitoa wakati wa kampeni za uchaguzi.
Hali hiyo huisababisha serikali iingie katika madeni na isiaminike inapohitaji kukopa. Katika miaka ya hivi karibuni tumeyashuhudia hayo yakitokea katika nchi kadhaa za Ulaya, zikiwemo Jamhuri ya Ireland, Ugiriki na Uhispania.
Baadhi ya serikali za Ulaya sasa zinalazimika kulipa riba ya zaidi ya asilimia 10 ili ziweze kukopa; huo ni mzigo mkubwa wa kiuchumi. Baada ya hapo, nchi za Magharibi zitawajibika kukopa fedha ili kugharimia riba ya mikopo ya serikali.
Kila ukilitazama bara hilo la Ulaya, ulikozaliwa mfumo wa kidemokrasia, utaona kuwa hivi sasa bara hilo limo ukingoni na huenda likatumbukia katika shimo la waliofilisika.
Kodi za mapato zinazoongezeka kila uchao zinatishia chumi za hizo nchi za Ulaya zifuatazo mfumo wa kidemokrasia. Hatimaye chumi hizo zitashindwa kusimama imara kwa sababu kodi kubwa katika nchi hizo zitawakimbiza wawekezaji.
Ndio maana tukiuangalia mfumo wa demokrasia ya kimagharibi ulivyo hivi sasa tutauona kana kwamba mfumo huo umepangwa ujiangamize wenyewe. Unaweza ukanusurika. Lakini ukiporomoka je, nini utakuwa mustakbali wa nchi kama zetu?
Nina swali linaloweza kuwa nyeti lakini lazima tujiulize: mfumo huo wa kidemokrasia ukiporomoka tugeukie wapi? Tuugeukie udikteta au tuufuate utawala wa kirasimu kama wa China?
Kwa nchi za Magharibi China sio kitisho cha kijeshi wala cha kiuchumi tu. China ni kitisho cha misingi ya imani ya watawala wa madola ya Magharibi kwamba mfumo wa demokrasia ndio mfumo bora wa kisiasa duniani.
Lakini ni wazi kwamba lau China ingalikuwa inaufuata mfumo aina hiyo isingaliweza kupata mafanikio makubwa ya kiuchumi iliyoyapata katika kipindi cha miaka 30 iliyopita.
Changamoto kubwa zinazoukabili mfumo wa kidemokrasia hii leo ni madeni ya serikali, tabia nchi, ugaidi wa kimataifa na kunyanyuka kwa China. Na huko kunyanyuka kwa China ndiko kutakozusha mvutano wa kifalsafa wa itikadi gani ya kisiasa iliyo muwafaka kuifuata — hii ya mfumo wa kidemokrasia wa kisasa unaoonyesha kila dalili za kusambaratika au ule wa urasimu wa China ambao watabiri wanasema karibu utalifanya taifa hilo liipiku Marekani kiuchumi na kimaendeleo?
Chanzo: Raia Mwema
No comments :
Post a Comment