TUNASUBIRI KUPEWA TALAKA MOJA!
Na Thobias Mwanakatwe
22nd October 2013
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard MembeWaziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, amesema nchi za Rwanda, Kenya, Burundi na Uganda hazina haja ya kuanzisha shirikisho lao la siri kwani Tanzania itakapofikia hatua ya kutaka kujiondoa katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), suala hilo litapelekwa Bungeni ili lijadiliwe na wabunge wataliridhia.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard MembeWaziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, amesema nchi za Rwanda, Kenya, Burundi na Uganda hazina haja ya kuanzisha shirikisho lao la siri kwani Tanzania itakapofikia hatua ya kutaka kujiondoa katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), suala hilo litapelekwa Bungeni ili lijadiliwe na wabunge wataliridhia.
Akihojiwa jana asubuhi na Cloud Radio, Membe alisema kuwa nchi hizo hazina sababu ya kufanya mambo kwa siri kwani kama wameshindwa na ni vema kuieleza Tanzania. “Kama ni talaka moja watupe tu. Sisi tunasubiri kupewa talaka.”
Afafanua msimamo wa Tanzania baada ya nchi hizo kuonekana zikifanya jitihada za kuanzisha shirikisho lao na kuitenga Tanzania, Membe alisema nchi hizo ziwe wazi na wakweli kama zinaona kuna jambo ambalo hazilidhiki nalo ambalo Tanzania inalifanya na busara itumike kulizungumza kwenye mikutano badala ya hivi sasa zinapoamua kuanzisha muungano wao wa siri.
Tutakapoamua ku-suspend relationship (kusimamisha uhusiano) na Afrika Mashariki, tutakapoamua kujiondoa kwenye utaratibu huu wa shirikisho la haraka haraka, tutapeleka suala hili bungeni. Bunge litajadili na nina uhakika wabunge wataangalia busara ya kutokuharakisha wala kudhulumiwa wala kuburuzwa, tutawaacha waendelee kwa raha mustarehe, ila sisi tunachoomba tu wawe wakweli, wawe wawazi si kutengeneza muungano wa siri siri,” alisema.
Alipoulizwa kama hali hii inachangiwa na nini hasa, kama ni kutokana na msuguano baina ya Rais Jakaya Kikwete na Rais wa Rwanda Paul Kageme, wa hivi karibuni au ni msukumu wa Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, kutaka kutimiza azma yake ya kuwa rais wa kwanza wa Shrikisho hilo, Membe alisema yanawezekana.
Hata hivyo, alifafanua kuwa kuna mambo kadhaa yanachangia, moja, ni msimamo wa Tanzania kukataa suala la ardhi kuingizwa katika mambo ya Jumuiya na kwamba ni jambo ambalo serikali haiwezi kukubali hasa ikizingatia kuwa ardhi ndiyo dhahabu ya nchi.
Alisema jambo la pili linalolalamikiwa na nchi hizo ni hatua ya Tanzania kuwa mwanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc) na Katibu Mkuu wa Sadc kuwa ni Mtanzania. “Hivyo wanaona Tanzania damu yao ipo Sadc, kitu ambacho ni kweli, lakini hata hivyo, nao wasilalamike kwa sababu wapo IGAD na Comesa.”
Aliongeza kuwa jambo jingine linalolalamikiwa ni hatua ya Tanzania kupeleka majeshi yake Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na kuwapa kipigo kizuri kikundi cha waasi cha M23 kati ya Agosti 26 na 28 mwaka huu hatua ambayo nchi hizo zinakiona ni kama kudhoofisha Muungano wa Afrika Mashariki.
Kuhusu jinsi gani kitendo cha kuwapiga M23 kinavyodhoofisha muungano alisema: “Kwa sababu wale M23 Tanzania inakwenda kwa principle (misingi) inayosema tunapoona nchi ya Afrika Mashariki au ya Sadc inakwenda kinyume cha matakwa ya wananchi au haifuati kanuni za uongozi bora, sisi huwa tunaingilia, siyo maana kwamba tunavunja Jumuiya Afrika Mashariki.”
Membe alisema nchi za Rwanda, Uganda, Kenya na Burundi baada ya kuona Tanzania haitaki suala la ardhi kuingiza EAC, na bado ni wanachama wa Sadc na kwamba haitaki kuanzisha Shirikisho la Afrika Mashariki haraka haraka na baadhi ya viongozi wa dunia kufanya ziara Tanzania, waliamua kuanzisha shirikisho lao la siri.
Viongozi wakuu duniani waliotembelea Tanzania mwaka huu pekee ni Rais wa China, Xi Jinping, na Rais wa Marekani Barack Obama..
Alisema nchi hizo zilipaswa kutumia utaratibu kama kuna mambo yanawakera ambayo Tanzania inayafanya ukiwamo.
Hatua hizo ni pamoja na kuiita Tanzania kuzungumza kwani msimamo wa serikali ni kwamba haiwezi kuburuzwa kuingia katika Shirikisho la Afrika Mashariki.
“Msimamo wetu hatuwezi kugawa ardhi yetu, hatuwezi kuwa waangaliaji, hivyo vingezo vyote wanataka tuvitake,’ alisema na kuongeza:
“Wala wasingepata shida yote hii, tungekutana kwenye kikao tukatoa kibali wakaendelea na utaratibu na sisi tukarudi tukaendelee na utaratibu wetu wa mwendo wa pole.”
Membe alisema katika kufikiwa kwa Shirikisho la Afrika Mashariki kuna hatua kadhaa za kufuata, moja ni soko la pamoja, ushuru wa forodha, sarafu moja na mwisho shirikisho la kisiasa.
“Hadi sasa bado tunahangaika na hatua hizi za awali, hatujaweza hata kufikia sarafu moja, sasa wenzetu wanataka shirikisho la kisiasa,” alisema Membe na kuongeza:“Mimi sioni hata hiyo monitory union (sarafu moja) ikifikiwa sasa hivi. Sisi bado tunaikataa.”
Alifafanua kuwa hata Waingereza wakati Umoja wa Ulaya wanakiunga kwenye sarafu ya Euro wao walibaki na sarafu yao, na mpaka sasa wanaendelea nayo. Hivi karibuni Tanzania imeonekana kuwekwa kando na nchi nyingine nne kati ya tano zinazounda EAC.
Tayari marais wa nchi hizo, Kagame, Museveni, Uhuru Kenyatta wa Kenya na Pierre Nkurunzinza wa Burundi wamekwisha kufikia makubaliano ya kuanzisha mchakato wa kuandikwa kwa Rasimu ya Katiba ya Shirikisho la Kisiasa la nchi wanachama wa EAC, bila kuishirikisha Tanzania.
Waziri wa Serikali za Mitaa wa Rwanda, James Musoni, amekaririwa na vyombo vya habari vya nchi hiyo akieleza kuwa makubaliano ya kuanzishwa kwa mchakato wa kuandikwa kwa Rasimu ya Katiba ya Shirikisho la Afrika Mashariki, yalifikiwa Septemba 12 mwaka huu, mjini Kampala na marais wa Rwanda, Kenya na Uganda na hivi karibuni Rais wa Burundi ambaye alialikwa katika mkutano huo na kushindwa kuhudhuria, naye sasa amethibitisha ushirika wake katika shirikisho hilo jipya.
Tayari nchi za Kenya, Uganda na Rwanda zimeshaanzisha mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Kenya hadi Rwanda.
Vile vile Bandari ya Mombasa nchini Kenya imeshafanyiwa upanuzi kuruhusu nchi za Uganda na Rwanda kupitisha mizigo yao.
Kufuatia hali hiyo ,Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, hivi karibuni alisema licha ya hatua zinazochukuliwa na nchi wanachama wa EAC za kuitenga Tanzania katika baadhi ya mambo, itabakia na msimamo wake na haitakubaliana kuingia kwenye Shirikisho la Kisiasa huku masuala ya ushuru wa forodha, soko la pamoja na sarafu moja, hayajatengamaa.
Waziri Sitta pia alieleza kuwa Tanzania imeiandikia barua sekretarieti ya baraza la mawaziri wa nchi wanachama wa EAC, ikilalamikia baadhi ya mambo yanayoendeshwa kwa usiri na baadhi ya nchi wanachama.
Kikao kingine cha viongozi wa nchi hizo kinatarajia kufanyika mwishoni mwa mwezi huu jijini Kigali, Rwanda bila kuishirikisha Tanzania.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment