NA WAANDISHI WETU
26th October 2013
Amemuagiza Makamu Mwenyekiti wa CCM, Philipo Mangula, kuwashughulikia viongozi wote wala rushwa ndani ya chama hicho.
Onyo hilo alilitoa juzi mjini hapa alipokuwa akifunga mafunzo maalum ya siku nne kwa makatibu na wenyeviti wa wilaya pamoja na makatibu wa mikoa.
Alisema tabia ya viongozi wa chama hicho kujihusisha na rushwa ndiyo itakayochangia kwa kiasi kikubwa kuitoa serikali ya CCM madarakani.
“Kama hatutabadilika katika suala la rushwa mwaka 2015 tutakuwa na wakati mgumu sana na kama mwaka huo tutafanikiwa kuishika serikali basi mwaka 2020 hatutarudi tena madarakani,” alisema Dk. Kikwete.
Aliongeza kuwa tatizo la rushwa kwa viongozi wa chama hicho linazidi kuwa kubwa kila siku hali ambayo inawapotezea imani wananchi ambao ndiyo wapiga kura wao.
“Viongozi wa chama ndiyo mmekuwa mawakala wa kusambaza rushwa bila hata aibu nawaombeni tubadilike kama tutaendelea hivi hali yetu itakuwa ngumu sana katika chaguzi mbalimbali nawaambieni... siku hizi watu wana mbadala wa vyama vingine siyo CCM pekee yetu,” alisema.
Alitaka viongozi wanaojihusisha na vitendo vya rushwa waondolewe mara moja na nafasi zao wapewe watu wengine ambao watakisaidia chama katika kupata mafanikio.
“Tuna vijana wengi kutoka katika vyuo mbalimbali ambao wanaweza kufanya kazi kwa uadilifu wa hali ya juu hivyo hatuna budi kuachana na hawa wala rushwa ambao watatupotezea sifa yetu kwa wananchi...na tukipoteza urais ndiyo tumekwisha na chama kinaweza kufa,” alisema.
Aliwaonya viongozi wanaojihusisha na uuzaji wa mali za chama kama vile viwanja na baadhi yao kuingia mikataba yenye utata.
“Kuna watu wanapoingia mikataba sijui wanakuwa wamelewa...kwanza unashindwa hata kuelewa...kwa mfano utakuta mtu alipangishwa jengo la CCM kwa miaka 264 sasa unawaza huu mkataba wa aina gani kwa sisi tuliopo hapa miaka 50 ijayo hakuna atakae kuwepo duniani sasa mmiliki wa lile jengo atakuwa nani?” alihoji.
Hata hivyo, aliwataka makatibu hao na wenyeviti wa wilaya na mikoa kuhakikisha wanawatembelea wanachama wao na kutafuta wanachama wapya kwa ajili ya kujiimarisha kwa chaguzi mbalimbali zijazo.
“Viongozi wengi hatuna tabia ya kuwatembelea wanachama wetu na kuwatatulia kero zao hali ambayo inatugharimu wakati wa uchaguzi kupata kura kidogo tofauti na idadi ya wanachama tulionao,” alisema.
Pia, aliwataka viongozi hao kutambua majukumu yao na kukiweka chama katika mfumo mpya ili kuhakikisha kinashinda na kuendelea kuongoza dola.
Alisema safari ya kuelekea 2014/15 watoke na kauli moja ya ushindi wa hakika mwaka 2014 na 2015 kwani lengo kuu la CCM ni kushika dola.
"Unaweza ukaunda chama kwa ajili ya mpira lakini kama una lengo la kushika dola ni lazima uunde chama cha siasa hivi ndio ilivyo kwa CCM ni kushinda katika uchaguzi mkuu na serikali za mitaa," alisema.
Alisema chama lazima kiwe na nguvu ya kuongoza na kushinda uchaguzi na kutofanya mambo ambayo yatafanya wagombea wa CCM kushindwa.
"Kila mmoja ajiulize hilo analofanya linasaidia CCM kushinda...Inatupasa kuhakikisha chama kinashiriki katika uchaguzi wa serikali za mitaa," alisema Dk. Kikwete.
Alisema kuwa iwapo hawatafanya kazi vizuri chama hakitaweza kufanikiwa hivyo mafunzo na maarifa waliyoyapata wayatumie ipasavyo kuhakikisha chama kinakuwa imara na chenye uwezo wa kuongoza.
"Nendeni mkakipe chama mfumo mpya na uhai kwa kuongeza wanachama wapya na waliopo pia mhakikishe wanakuwa imara na wenye furaha ili wakaribishe wenzao.
"Lazima waendelee kuongeza wanachama sio kupanda majukwaani na kuimba...iyena iyena...Kinachotakiwa ni utendaji mpya wa kuongoza wanachama na kuwatambua na kuwapa majukumu," alisema.
Alisema kama wanataka ushindi lazima wahakikishe watu wao waliojiandikisha kupiga kura wanajitokeza kupiga na pia wajipange kuwatambua na kuwahamasisha kujitokeza.
"Kama ni udhaifu katika chama chetu ni huu kwani tuna wanachama lakini wakati wa kwenda kupiga kura hatuwafuatilii ni vyema suala hili nyie viongozi muanze nalo sasa.
Taarifa hii imeandaliwa na Paul Mabeja, Jacqueline Massano na Augusta Njoji
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment