Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Tuesday, November 19, 2013

CCM:Mawaziri hawa ni mzigo

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye
Wapelekwa Kamati Kuu watoswe
Ikishindikana wabunge kuwang’oa
 
Na Waandishi wetu
 
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesema Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa; Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chiza na Naibu wake, Adam Malima, wameshindwa kazi na kupendekeza wang’olewe.

Kauli hiyo ilitolewa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, mbele ya Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdulrahman Kinana, akisema kuwa mawaziri hao wameshindwa kutimiza wajibu wao wa kuwatumikia Watanzania.

Alisema anasikitishwa na kitendo cha mawaziri hao waliopewa dhamana kushindwa kutambua wajibu wao na kwamba umefika wakati wa kuhojiwa na Kamati Kuu (CC) ya CCM ili wachukuliwe hatua kwani bila kufanya hivyo aibu itarudi kwa chama chake.
Nape alitoa kauli hiyo jana katika Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma wakati akielezea changamoto zinazowakabili wakulima ambao ni asilimia 80 ya Watanzania, huku mawaziri husika wakikaa kimya.

Alisema kuwa Waziri Chiza na Malima wamebaki wakifunga tai na kuvaa suti mjini wakati wakulima wa Ruvuma na mikoa mingine ya Tanzania wakiteseka.

Nape alisema Waziri Kawambwa naye anatakiwa kuchukuliwa hatua kwa kuingia mkataba na kampuni ya ujenzi ya Progressive iliyopewa zabuni ya kutengeza barabara ya Natumbo hadi Tunduru wakati mkandarasi huyo hana uwezo wa kuijenga na matokeo yake amefukuzwa kazi.

Dk. Kawambwa ametupiwa lawama hizo kutokana na kuipa kazi kampuni hiyo wakati akiwa Waziri wa Miundombinu pamoja na kushindwa kusimamia elimu.

Akiwazungumzia Chiza na Malima, Nape alisema inasikitisha kuona wakulima wakiteseka, lakini waliopewa dhamana ya kuwasaidia wakishindwa kuwasikiliza na kutafuta ufumbuzi wa matatizo yao.

“Nitahakikisha mawaziri hao wanachukuliwa hatua ikiwa pamoja na kuwajibishwa na chama na ikishindikana tutatumia wabunge wetu kufanya kazi hiyo,” alisema Nape ambaye anaongozana na, Kinana, katika ziara ya kichama kwenye mikoa ya Kusini na Nyanda za Juu Kusini.

Nape alisema akiwa katika mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma kila eneo wananchi wanawalalamikia Chiza na Malima kwa mambo mbalimbali hivyo suala hilo linapaswa kufikia mwisho wake maana chama hakiwezi kuwavumilia.

“Katibu Mkuu (Kinana), nilimuuliza Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Chiza na Malima wamefika lini kusikiliza matatizo ya wakulima wa tumbaku, korosho na mahindi, alinijibu hakumbuki kama wamefika mkoani hapa. Nikafuatilia na kubaini si yeye tu hata Waziri aliyetangulia Profesa Jumanne Maghembe naye hakuwahi kufika. Najiuliza sababu nini, hakuna majibu,” alisema Nape.

Nape alisisitiza kuwa yuko tayari kupoteza nafasi aliyonayo kuliko kuacha Watanzania wakiendelea kuteseka kwa ajili ya mawaziri wachache waliopewa dhamana na Serikali ambayo ni ya CCM, lakini hawatimizi wajibu wao.

“Kwa hili hata chama changu na Katibu Mkuu mkiamua kunifukuza nipo tayari, ni bora nikawe mkulima, lakini kwa kuwa nafanya kazi ya kuwatetea wananchi watanilinda tu,” alisisitiza Nape.

Alitumia nafasi hiyo kumuomba Kinana apeleke ripoti ya mawaziri hao kwa CC wachukuliwe hatua na ikiwezekana waitwe wahojiwe.

Nape aliongeza: “Wananchi naomba mnilinde, lakini niseme ukweli. Mawaziri ambao tumewapeleka jikoni wameshindwa kupika chakula, tunasubiri sebuleni, lakini chakula hakiji. Wanatukwamisha, ni bora wakaondoka kama wameshindwa kazi.”

“Mimi ni kijana, sipo tayari kuona CCM inakuwa chama cha upinzani bungeni kwa sababu tu ya hawa wenzetu wachache ambao wanafanya makusudi na uzembe katika kutekeleza wajibu wao.

Kuhusu barabara ya kutoka Songea hadi Namtumbo, alisema anamshukuru Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, kwa kumfukuza mkandarasi huyo, lakini

hiyo pekee haitoshi wale wote waliohusika kumpa mkataba wanapaswa kuchukuliwa hatua kwa kuwa Serikali imepata hasara.

“Dk. Kawambwa amekuwa akitukwamisha CCM katika kutimiza wajibu wake. Hii barabara ya Namtumbo hadi Tunduru kushindwa kukamilika imeleta aibu kubwa na kututia fedheha. Hivyo lazima waliotoa mkataba wawajibishwe,” alisema Nape.

Kwa mujibu wa Nape, Dk. Kawambwa pia ameshindwa kushughulikia matatizo ya walimu nchini na kumkumbusha kuwa alipewa muda wa miezi sita na CCM na inakaribia kumalizika. Hata hivyo, hakufafanua miezi sita aliyopewa Waziri Kawambwa inahusu nini.

“Muda ukimalizika tutataka kufahamu yale ambayo tumeyaagiza kama yamefanikiwa na iwapo atakuwa ameshindwa ajue hatutakaa kimya,” alisema
Nape.

Alifafanua kuwa yeye (Nape) kama msemaji wa CCM kamwe hatakaa kimmya wakati chama kikipata aibu kwa kutotekelezwa miradi mbalimbali iliyoahidiwa katika Ilani ya uchaguzi ya mwaka 2010.

Naye Katibu Mkuu Kinana alisema katika kikao cha CC kitakachofanyika mwezi ujao, kitamuandikia barua Rais Jakaya Kikwete ili mawaziri wake waende mbele ya kikao na kueleza kwa nini wasifukuzwe kwa kushindwa kazi.

Alisema kuwa haiwekani kuwa na Serikali ya walalamikaji kwa mfano mkuu wilaya analalamika, mbunge analalamika na kuweka wazi kuwa ni lazima yafanyika maamuzi magumu.

“Kama hali ndiyo iko hivi je, mwananchi wa kawaida atakwenda wapi. Hili sasa limefika mwisho, ni lazima wenzetu waliopewa dhamana wawajibike,” alisema Kinana.
Hii ni mara ya kwanza kwa viongozi wa CCM kuwataja kwa majina mawaziri hadharani kueleza wazi kuwa wamshindwa kutimiza wajibu wao na kuwataka wang’oke madarakani.

Kadhalika, ni mara ya kwanza kwa Katibu Mkuu wa chama tawala kuinga mkono kutajwa kwa majina ya mawaziri hadharani na kueleza wazi kuwa watawashitaki kwenye chama na kuwataka wajieleze mbele ya Kamati Kuu ya chama hicho.



CHANZO: NIPASHE

No comments :

Post a Comment