zanglassworks

AirFreight

Kwarara Msikitini

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Monday, November 11, 2013

Kenya yaiunga mkono Tanzania

NA RAPHAEL KIBIRITI

11th November 2013


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, akiongozana na mgeni wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Amina Mohamed Jibril, wakati wakiwasili kuzungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana. Rais Kenyatta amemtuma waziri huyo ili kutuliza hali ya mambo kufuatia hotuba ya Rais Jakaya Kikwete, juu ya kutengwa kwa Tanzania na baadhi ya wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Kenya, Uganda na Rwanda.
Kenya imejitenga na maswaiba wake wa hivi karibuni katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, Uganda na Rwanda kwa kuunga mkono msimamo uliotolewa wiki iliyopita na Rais Jakaya Kikwete juu ya uvunjaji wa mkataba wa jumuiya hiyo.

Jana, Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Amina Mohamed, aliwasili nchini na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Tanzania, Bernard Membe, na kuelezea msimamo wa Serikali ya Kenya wa kuunga mkono kauli ya Rais Kikwete.

Akihutubia Taifa wiki iliyopita kupitia Bunge, Rais Kikwete alielezea kushangazwa na hatua za mataifa hayo matatu kuvunja makubaliano ya mkataba wa Afrika Mashariki na kuzitenga Tanzania na Burundi.

Katika hotuba hiyo, Rais Kikwete alitaja maeneo manane ambayo mataifa hayo yameanza ushirikiano wa walio tayari (Coalition of the willing) na kusisitiza miongoni mwao manne yanavunja moja kwa moja makubaliano ya jumuiya hiyo.

Mambo hayo ni, moja ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Mombasa-Kigali-Bujumbura-Sudan Kusini; mbili ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Kenya-Uganda-Sudan Kusini; tatu ujenzi wa kiwanda cha kusafisha mafuta; nne ushuru wa forodha wa pamoja; tano kuharakisha shirikisho la kisiasa la Afrika Mashariki; sita viza ya pamoja ya utalii ya Afrika Mashariki; saba kutumia vitambulisho vya taifa kama hati ya kusafiria; nane uzalishaji na usambazaji wa umeme wa pamoja.

Katika hayo, Rais Kikwete alitaja manne ambayo hayagusi makubaliano ya pamoja ya jumuiya kuwa ni bomba la mafuta, kiwanda cha kusafisha mafuta, umeme na reli ya kisasa. Hata hivyo, Tanzania ina maslahi ya moja kwa moja katika miradi hiyo, lakini haijui kwa nini haikushirikishwa.

Hata hivyo, Rais Kikwete alisema Tanzania haitajitoa EAC na itaendelea kuwa mwanachama wake mwaminifu kwa kuwa imetumia muda wake mrefu na rasilimali kwani inachangia Dola za Marekani milioni 12,000 kila mwaka.

Mara baada ya waziri huyo kukutana na Membe, jijini Dar es salaam jana, katika mkutano wa pamoja na waandishi wa habari, alisema ziara yake rasmi ya siku moja nchini, ilikuwa na lengo la kuonyesha namna Kenya ilivyoguswa na kuridhishwa na kauli ya Rais Kikwete kuhusiana na suala la EAC.

“Tumeipitia kwa tahadhari kubwa kauli ya Rais Kikwete kuhusiana na suala la shirikisho na tunakubaliana na hoja zake. Kama wanachama wa jumuiya, tunaiunga mkono Tanzania kuhusiana na jumuiya na tusingependa kwenda njia tofauti na Tanzania,” alisema.

Mohamed aliihakikishia Serikali ya Tanzania na watu wake kuwa nchi wanachama wa EAC hazitaitenga katika Jumuiya hiyo.

Alisema Tanzania ni moja ya zana muhimu ambazo nchi nyingine ndani ya Jumuiya zinaitegemea kwa ajili ya ustawi na maendeleo yao.

Mohamed alisema nchi nyingine ndani ya shirikisho ikiwamo Tanzania, zimetoka mbali na bado zina mengi ya kufikia ndani ya Jumuiya.

Alisema nchi wanachama zipo kwa ajili ya maendeleo yao pamoja na ya wananchi wake.

Mjumbe huyo kutoka Kenya alisema kwamba hakuna sababu ya Tanzania na watu wake kuwa na wasiwasi juu ya EAC kwa sababu bado wako pamoja na Jumuiya itaimarika.

Kwa upande wake, Membe aliwaambia waandishi wa habari katika mkutano huo kuwa Kenya ilikuwa imetambua kwamba ilikuwa imedanganywa kwa kufanya mikutano iliyojadili baadhi ya masuala ya Jumuiya bila ya kuikaribisha Tanzania. Kenya ilikujatambua kuwa ilikuwa ‘imeingizwa mjini’ na ndiyo sababu imetuma mjumbe wake nchini. Hili amelisema wazi waziri mwenzangu kwenye mkutano wetu,” alisema.

Membe alisema kuwa kabla ya kauli ya Rais aliyoitoa wiki iliyopita juu ya kadhia hiyo, Kenya haikujua kama mikutano waliyoifanya pamoja na Uganda na Rwanda, ilikuwa kinyume na Itifaki ya Shirikisho la Afrika Mashariki.

Katika hotuba yake, Rais Kikwete alisema huenda masuala ya uhamiaji, ardhi na ajira na kuharakisha shirikisho la kisiasa ambayo Tanzania imekataa kuwa sehemu ya Jumuiya, ndiyo yaliyozifanya nchi hizo kuitenga kwenye ‘ushirikiano wa walio tayari’.

Kwa upande mwingine, Mohamed alisema serikali yake inaishukuru Tanzania kwa kuwa mstari wa mbele kuiunga mkono Kenya katika kesi inayomkabili Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake William Rutto, inayoendelea huko The Hague nchini Uholanzi.

Rais Kenyatta na Rutto wanakabiliwa na tuhuma za kutenda uhalifu dhidi ya ubinadamu katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC).

Wanadaiwa kuhusika kupanga ghasia zilizosababisha vifo vya takribani watu 1,500 na wengine takribani 500,000 kubaki bila makazi.

Ghasia hizo zilitokea baada ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi wa urais wa mwaka 2007.
“Tunaitegemea Tanzania iendelee kutuunga mkono katika kesi hizi,” alisema Mohamed.
CHANZO: NIPASHE

No comments :

Post a Comment