Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad ameunga mkono uamuzi wa Walimu Wakuu wa Skuli za Sekondari Zanzibar wa kufanya tathmini ya kina ya hali ya elimu Zanzibar, ili baadae kutolewe mapendekezo yatakayo leta ufanisi katika sekta hiyo.
Maalim Seif ameeleza hatua hiyo leo, wakati alipokuwa na mazungumzo na viongozi wa Jumuiya ya Walimu Wakuu wa Sekondari Zanzibar, ambao walifika ofisini kwake Migombani mjini Zanzibar kwa ajili ya kujitambulisha na kumueleza dhamira yao hiyo.
Makamu wa Kwanza wa Rais amesema ukweli ni kwamba pamoja na mafanikio makubwa yaliyokwisha patikana, ikiwemo katika utekelezaji wa malengo ya Milenia, hadi sasa zipo changamoto nyingi zinazopaswa kupatiwa ufumbuzi.
Amesema Serikali pamoja na wananchi walio wengi bado hawaridhishwi na hali ya kushuka kwa matokeo ya mitihani ya Taifa kama inavyo jitokeza mwaka hadi mwaka, na hatua ya kufanya tathmini kuweza kujua sababu zake ni muhimu katika wakati huu.
“Jambo muhimu mkutano wenu uwe wa uwazi, muweze kuchambua kwa kina ubora wa elimu Zanzibar, mujiulize je sera ya elimu ya 2006 haihitaji kufanyiwa marekebisho? Je, mitaala yetu inakidhi haja na hali halisi iliyopo? Hapo mtaweza kujua changamoto ziko wapi”, alishauri Maalim Seif.
Katibu wa Jumuiya hiyo, Fadhil Hamad Mshamba amesema walimu wakuu wa Skuli za Sekondari hawaridhishwi na hali ya kushuka kiwango cha elimu na ufaulu wa wanafunzi Zanzibar, hivyo wameamua kufanya tathmini hiyo kwa lengo la kuainisha kasoro na kutafutiwa ufumbuzi.
Amesema miongoni mwa mambo yatakayo zingatiwa ni juu ya ufundishaji, utawala na utendaji wa walimu wakuu wa skuli za sekondari, Sera ya Elimu, pamoja na kuchambua kwa kina mwelekeo wa elimu Zanzibar, ikilinganishwa na nchi nyengine, ikiwemo za Afrika Mshariki.
Ameeleza kuwa wanaamini hatua hiyo ya walimu wakuu itaweza kuibua mambo mengi muhimu ambayo yataisaidia Serikali na jamii nzima kujua hatua za kuweza kuchukuliwa katika kukabilina na changamoto za kielimu.
Chanzo: ZanziNews
No comments :
Post a Comment