zanglassworks

AirFreight

Kwarara Msikitini

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Wednesday, November 13, 2013

Majonzi:Dk.Mvungi afariki dunia Afrika Kusini

NA WAANDISHI WETU

13th November 2013


Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Dk. Sengondo Mvungi, ambaye alivamiwa na kujeruhiwa na majambazi nyumbani kwake, Mbezi Msakuzi jijini Dar es Salaam, wiki iliyopita amefariki dunia.
Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Dk. Sengondo Mvungi, ambaye alivamiwa na kujeruhiwa na majambazi nyumbani kwake, Mbezi Msakuzi jijini Dar es Salaam, wiki iliyopita amefariki dunia.

Vyanzo mbalimbali vya habari ikiwamo mitandao ya kijamii na baadhi ya wanasiasa, jana vilithibitisha kifo hicho ambacho kilitokea akiwa hospitalini Milpark Johannesbarg, iliyopo Afrika Kusini, alikokuwa akitibiwa.

Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia, alipopigiwa simu jana alisema kwa kifupi na sauti yenye majonzi: “Najua unataka kufahamu kuhusu kifo cha Dk. Mvungi, ni kweli amefariki lakini tutatoa taarifa baadaye.” 

Hata hivyo, baadaye alithibitisha kwamba Dk. Mvungi alifariki dunia jana saa 9 alasiri.

Taarifa ya Tume iliyotolewa na Katibu wake, Assaa A. Rashid, jana jioni ilisema Dk. Mvungi alifariki jana mchana.

“Kwa masikitiko makubwa, Tume ya Mabadiliko ya Katiba inawafahamisha wananchi kuwa Mjumbe wake Dk. Sengondo Mvungi aliyekuwa akipata matibabu katika Hospital ya Milpark iliyopo jijini Johannesburg nchini Afrika Kusini amefariki dunia leo (Jumanne, Novemba 12, 2013) saa 8:30 mchana kwa saa za Afrika ya Kusini,” ilieleza.

Rashid alisema taratibu za kuusafirisha mwili wa marehemu kutoka nchini Afrika Kusini kuja nchini kwa mazishi zinaendelea na taarifa zaidi zitatolewa.

Dk. Mvungi alisafirishwa siku ya Alhamisi, Novemba 7, 2013 kwenda nchini Afrika Kusini kwa uchunguzi na matibabu zaidi akitokea MoI aliokuwa amelazwa baada ya kuvamiwa nyumbani kwake.

Katika taarifa yake, Tume inawaomba Watanzania kuungana na familia, ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu Dk. Mvungi katika kuomboleza msiba huo.

Dk. Mvungi ambaye pia alikuwa Mkurugenzi wa Katiba, Sheria na Haki za Binadamu wa NCCR-Mageuzi, alipelekwa Afrika Kusini kwa matibabu zaidi baada ya hali yake kuwa mbaya katika Taasisi ya Mifupa (MoI), alikokuwa amelazwa tangu ajeruhiwe usiku wa Jumapili ya Novemba 03, mwaka huu na watu wasiojulikana. Polisi hadi sasa imekwisha kukamata watu tisa wanaotuhumiwa kuhusika na tukio la kumjeruhi.

Katika uvamizi huo, majambazi hao baada ya kumjeruhi walipora fedha, simu, bastola na kompyuta mpakato (laptop), vitu ambavyo havijapatikana isipokuwa simu moja aina ya Nokia waliokutwanayo watuhumiwa wanaoshikiliwa na Polisi.

CHADEMA WAMZUNGUMZIA

Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, amesema Dk. Mvungi alikuwa ni mtu mwenye malengo makubwa katika siasa za nchi.

Alisema katika enzi za uhai wake, alikuwa ni mtu anayepigania kupatikana kwa Katiba mpya ya nchi siku zote hadi mchakato huo ulipoanza.

Aliongeza kuwa kifo cha Dk. Mvungi siyo pigo kwa familia yake tu bali kwa wananchi wote wanaoitakia nchi mema.

“Sisi kama Chadema tunapeleka salamu za pole kwa familia na Watanzania wote walioguswa na msiba huu, nasi tunajiunga katika majonzi haya,” alisema Mbowe.

RAMBIRAMBI ZA CCM

Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alisema Dk. Mvungi alikuwa ni mmoja wa wanasheria aliyeliletea sifa taifa.

Alisema tangu ya uhai wake rekodi yake ilikuwa safi na kueleza kuwa alitumia elimu yake vizuri.

“Wapo wanasheria wengi ambao ni matunda ya Dk. Mvungi, wapo wanasheria ambao nimewahi kukutana nao wakasema sababu iliyowapelea kuingia katika masuala ya sheria ni Dk. Mvungi, hivyo alikuwa ni mwalimu wa watu,” alisema Nape.

Nape alisema Dk. Mvungi alishiriki katika demokrasia ya nchi hususani katika upatikanaji wa Katiba mpya na kuongeza kuwa ataendelea kuishi kwa mema aliyoyafanya nchini.

WASIFU WA DK. MVUNGI
Alizaliwa mwaka 1952, alisoma katika shule ya sekondari kidato cha Tano na Sita ya Mzumbe.

Mwishoni mwa miaka ya 70 aliajiriwa katika magazeti ya Chama Cha Mapinduzi, Uhuru na Mzalendo kama mwandishi wa habari.

Alifanyakazi kwa takribani miaka miwili na kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), kusomea sheria.

Alipohitimu alikuwa miongoni mwa vijana wa Kitanzania waliobaki kufundisha chuoni hapo, kisha akaenda Ujerumani kwa masomo ya Shahada ya Uzamivu.

Alirejea UDSM kufundisha na kupanda ngazi hadi Julai 1998 alipochaguliwa kuwa Mkuu wa Kitivo cha Sheria chuoni hapo hadi Julai, 2003.

Kazi nyingine alizofanya Dk. Mvungi alishirikiana na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kuanzisha Chuo Kikuu cha Bagamoyo ambacho alichaguliwa kuwa Makamu Mkuu wa Chuo hicho.

SIASA

Alikuwa miongoni mwa wanataaluma waliokuwa msitari wa mbele katika kupigania kuanzishwa kwa vyama vingi nchini, akitajwa kama mmoja wa waasisi wa chama cha NCCR-Mageuzi ambacho kilikuwa kimesheheni wanasheria mahiri nchini.

Aligombea urais mwaka 2005 akiungwa mkono na vyama vinne vya upinzani.

Katika uchaguzi huo, Dk. Mvungi alishika nafasi ya tano kati ya wagombea wa nafasi hiyo baada ya kupata kura 55,819 sawa na asilimia 0.43.

ALIKOTOKA
Dk. Mvungi alikulia katika maisha ya kawaida, katikati ya jamii ya wakulima, huko Kisangara Juu, Wilaya ya Mwanga, mkoani Kilimanjaro.

Ni mtoto wa pili kutoka kitindamimba katika familia ya watoto saba ya baba yao aliyekuwa mkulima wa kahawa, mahindi, ndizi, mihogo na maharage na pia mzee huyo alikuwa mfugaji wa ng’ombe wa maziwa.

Katika moja ya mahojiano ya Dk. Mvungi na gazeti moja la kila wiki nchini, alielezea maisha yake ya utotoni akisema: "Kwa hakika tulikuwa pia na mbuzi na jukumu langu mojawapo katika utoto wangu lilikuwa ni kuchunga hawa mbuzi na ng’ombe waliokuwapo. Baba yangu alinifundisha jinsi ya kulima, namna ya kulitumia jembe, panga na shoka."

Baba yake pia alimfundisha jinsi utamaduni wa jamii yao ulivyo.

Alimfundisha pia maadili mazuri, heshima kwa wakubwa na wengine. Imeandikwa na Gwamaka Alipipi, Muhibu Said na Thobias Mwanakatwe.
CHANZO: NIPASHE

No comments :

Post a Comment