Skuli ya Sekondari ya Lumumba, hapo zamani za kale ikijulikana kama 'Lumumba College' iko hatarini kunyofoka vipande vipande kutokana na uchimbaji mchanga uliokithiri kama unavyoonekana kwenye picha.
Uchimbaji huu sio wa leo, yaonekana umeendelea kwa kipindi kirefu kiasi ambacho hivi sasa unahatarisha jengo zima la skuli.
Jambo la kusikitisha inaonekana hakuna mwenye kujali. Jambo la kusikitisha yaonekana hakuna mwenye ubunifu.
Chimba chimba mchanga nayo inaendelea, pengine hadi jengo la skuli lianguke au lianze kuota nyufa ndipo wahusika washtuke!
Kama Lumumba ingekuwa na uongozi wenye kujali pamoja na ubunifu dawa ya uharibifu huu kwangu mimi ni ndogo tu. Zinunuliwe gari za mawe ambayo hayahitaji fedha za kigeni, halafu yatandikwe kwenye eneo lililochimbwa mchanga. Juu ya mawe hayo uwekwe udongo mwekundu kutoka Makunduchi au popote pale.
Hatua ya mwisho yapandwe majani 'pemba grass'. Maji ya kila mara yamwagiwe sehemu hii na hapo tatizo limekwisha. Hili linashinda jamani?
Basi kama skuli imeshindwa kwa nini uongozi usizialike jumuiya za mazingira hapa Zanzibar na kuzipa changamoto kushughulikia eneo hili? Wakati wa kukumbatia matatizo umekwisha.
Uongozi wa kileo unataka ushirikishaji wa jamii pale matatizo yanapotokea. Hebu tokeni humo ofisini mwende kwa wanajumuiya za mazingira na matunda yake mtayaona.
Aidha Skuli ya Lumumba mbona ina maswali mengi kuliko majibu? Mara baada ya Dkt Shein kuingia madarakani nakumbuka ilifanywa harambe kabambe yenye nia kuifanya Skuli hii kuwa 'center of excellence'.
Nakumbuka ilikubaliwa mazingira ya Skuli yaimarishwe kwa kuzungurusha ukuta skuli yote ili kuzuia eneo na mali za skuli kuwa salama. Mapesa yaliyokusanywa yamepelekwa wapi?
Zile juhudi za kuifanya Skuli hii kuwa 'center of excellence' zimeishia wapi? Au ndio povu la mkojo? Masikini Lumumba, kweli ndio unakufa?
Chanzo: ZanziNews
No comments :
Post a Comment