Kwa ufupi
- Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad ambaye pia ni Katibu Mkuu wa CUF, alitamka waziwazi kwamba anapendekeza muundo wa muungano wa mkataba lakini kama ikishindikana, walau wa Serikali Tatu.
Anazungumzia Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na Serikali ya Umoja wa Kitaifa, akisisitiza umuhimu wa kuendelea kuwa wamoja.
Zanzibar. Wakati wa kutoa maoni ya Katiba Mpya, baadhi ya Wazanzibari wakiwamo viongozi waandamizi wa Serikali ya Mapinduzi (SMZ), walitoa kauli zinazokinzana kiasi cha kuibua maswali juu ya mustakabali wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (Suk).
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad ambaye pia ni Katibu Mkuu wa CUF, alitamka waziwazi kwamba anapendekeza muundo wa muungano wa mkataba lakini kama ikishindikana, walau wa Serikali Tatu.
Msimamo huo unapingana na ule wa chama tawala CCM, ambacho Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein ni Makamu Mwenyekiti wake wa kutaka Serikali mbili kama ilivyo sasa.
Rasimu ya kwanza ya Katiba iliyotolewa na Tume ya Marekebisho ya Katiba imependekeza kuwapo kwa Serikali Tatu – Muungano, Tanganyika na Zanzibar.
Rasimu ya kwanza ya Katiba iliyotolewa na Tume ya Marekebisho ya Katiba imependekeza kuwapo kwa Serikali Tatu – Muungano, Tanganyika na Zanzibar.
Jumanne iliyopita, Dk Shein aliitisha mkutano wa waandishi wa habari kuzungumzia mafanikio ya Serikali yake katika kipindi cha miaka mitatu ambapo pamoja na kubainisha mafanikio na changamoto mbalimbali, alizungumzia utata na kupishana kauli kwa viongozi wa juu wa visiwa hivyo juu ya suala hilo na msimamo wa Zanzibar kuhusu Muungano.
“Serikali yangu haina msimamo wa jambo hilo. Kila mwananchi ana uhuru wa kutoa maoni yake, ninaweza kutoa msimamo kutokana uamuzi uliofikiwa na chama changu na kila mtu anaweza kufanya hivyo, na si kuisemea Zanzibar na wananchi wake,” anasema.
Anasema kauli na msimamo wa Makamu wake wa Kwanza wa Rais ni wake binafsi au chama chake, na kwamba mwenye mamlaka ya kuisemea Zanzibar katika masuala hayo ni Rais pekee.
Hata hivyo, Dk Shein anasema Serikali ya Umoja wa Kitaifa, ambayo imetimiza miaka mitatu, imepata mafanikio makubwa kutokana na kuvumiliana na kufanya kazi kwa pamoja bila ya kutanguliza itikadi za kisiasa.
“Nchi nyingi zimejaribu hili zimeshindwa lakini sisi tumefanikiwa kwa sababu tunavumiliana. Hili linahitaji stahamala kubwa vinginevyo tutagawana mbao na sitaki hili litokee kwenye uongozi wangu.”
Anasisitiza umuhimu wa kuendelea kushikamana na kupendana... “Tushindane kwenye mfumo wa vyama vingi vya siasa bila ya kugombana, kukashifiana, kulaumiana, kutukanana wala kudharauliana.
“Zanzibar haitajengwa kwa mambo hayo yasiyokuwa na tija wala faida. Huu ni wakati wa kuongeza kasi na kuijenga nchi yetu, ili tusije tukaachwa nyuma.”
Anasema kauli za baadhi ya wananchi wanaosema kwamba Serikali hiyo haijafanya jambo lolote hazina mashiko ingawa anaeleza kutoshangazwa kwake na kauli kama hizo, hasa kwa kurejea matokeo ya kura ya maoni kuhusu kuundwa kwa SUK ambapo asilimia 34 walipinga.
“Hao waliopinga si bado wapo? Hao ndiyo wanaosema. Sasa sisi hatuwezi kuwazuia kusema alimradi hawavuki mipaka na kuvunja sheria za nchi.”
Muungano
Licha ya kuwapo kwa sauti kutoka kwa baadhi ya wananchi wa Zanzibar kupinga Muungano, Rais Shein anaweka wazi msimamo wa Serikali yake katika hilo: “Napenda niwahakikishie wananchi wote kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuendeleza Muungano wetu, kuimarisha na kuwatumikia wananchi.
“Katika kuuimarisha Muungano wetu, sote tumetimiza wajibu kwa kutoa maoni yetu kwa ajili ya kuandaliwa Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” anasema na kuongeza: “Hatua zilizobakia nazo zitakamilishwa kwa kuzingatia sheria iliyopo ili hatimaye tupate Katiba Mpya itakayoliongoza Taifa letu na kuimarisha Muungano wetu.”
Rais Shein anampongeza Rais Jakaya Kikwete kwa kusimama imara kuutetea na kuuendeleza Muungano hasa utayari wake wa kuzizungumzia changamoto zinazoukabili na kutafuta njia za kuzipatia ufumbuzi kila zinapotokea.
Kiongozi huyo anaweka bayana umuhimu wa kudumisha na kuimarisha Muungano... “Ni lazima tuyaenzi na tuyadumishe Mapinduzi yetu na tuudumishe na tuuendeleze Muungano wetu kwani ndiyo nguzo yetu kubwa ya maendeleo na vilivyotufikisha hapa tulipofika hivi sasa, na tunakokusudia kufika katika miaka mingi ijayo,” anasema.
Changamoto
Anafafanua kuwa Muungano umeendelea kuwa imara zaidi tangu ulipoanzishwa na kuipa Tanzania heshima kubwa katika jumuiya ya kimataifa.
“Tumepata mafanikio makubwa ya kisiasa, kiuchumi na ustawi wa jamii, ingawa zimekuwepo baadhi ya changamoto lakini zitaendelea kushughulikiwa hatua kwa hatua.”
Moja ya changamoto hizo ni malalamiko kwamba mgawo wa mapato ya Muungano umekuwa mdogo kwa Zanzibar ambayo inapata asilimia 4.5 tu.
Kuhusu hilo, Dk Shein anasema: “Jeshi la Wananchi na JKT (Jeshi la Kujenga Taifa) wanatumia mabilioni mangapi, Mambo ya Nje, Mambo ya Ndani, Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia... Sisi (Zanzibar) tunatoa ngapi kakati hizo?”
No comments :
Post a Comment