NA MHARIRI
12th November 2013
Kwa ustadi wa hali ya juu, tena bila kujali tofauti zao za kiitikadi, wabunge wengi walikataa muswada wa marekebisho ya sheria hiyo, ambayo yalikuwa yakiongeza ukali wa adhabu ambazo hata sasa zinalalamikiwa kwa vile zinakwaza uhuru wa habari.
Kwa kauli moja, wabunge kutoka chama tawala (CCM) na wa kambi ya upinzani wakaitaka serikali iachane na marekebisho hayo ya baadhi ya vifungu vyenye kila dalili ya kupoka uhuru wa magazeti.
Badala yake, wabunge wakaikumbusha Serikali kuwa kinachotakiwa ni kukidhi matakwa ya muda mrefu ya wadau wa habari. Kwamba, iachane na marekebisho hayo machache yaliyoelezewa na wengi kuwa ni kandamizi na badala yake, ifikishe muswada mzima wa habari bungeni.
Hatimaye marekebisho hayo yakagonga mwamba. Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ambaye alitumia muda mwingi kuwashawishi wabunge kwa hoja mbalimbali ili wapitishe marekebisho hayo akakosa uungwaji mkono. Serikali ikashindwa vibaya. Sisi tunapongeza uamuzi wa Bunge letu.
Tunaamini kwamba kupitia uamuzi huu, walau Bunge limeonyesha kuwa linaweza kuendeleza wembe wake uleule wa kuisimamia Serikali katika kutekeleza mambo mbalimbali kwa maslahi ya umma na siyo kugeuzwa kuwa mahala pa kuhalalisha kila kinachopelekwa mbele yao na serikali.
Sababu ya kulipongeza Bunge letu kwa uamuzi wake huo iko wazi. Ni kwamba, limedhihirisha kuwa bado lina meno. Kwamba, licha ya changamoto zote zinazoripotiwa kuibuka bungeni katika siku za hivi karibuni kuhusiana na tofauti za vyama, bado wabunge wetu wanaweza kuamua mambo kwa tafakuri pana kama tunavyowatarajia siku zote. Zile fikra mbaya kuwa Bunge linazidiwa na nguvu ya hisia za itikadi ya vyama haikuonekana kuwa na nafasi.
Ni kweli kuwa, kama ilivyo ada, wapo wabunge walioendelea kutetea muswada huo. Kamati ya bunge inayoshughulikia masuala ya habari iliunga mkono marekebisho yaliyofikishwa kwao. Hilo halikuwa kosa. Wote walitekeleza wajibu wao katika kutoa mawazo wanayoona kuwa yanafaa kwa maslahi ya taifa.
Hata hivyo, mwisho wa siku sauti ya waliopinga marekebisho hayo ikawa kubwa zaidi. Kwa namna isiyotarajiwa, nguvu hii ikazidi kile ambacho sisi tunaona kuwa ni jitihada zisizofaa za kuviza uhuru wa habari.
Sisi tunaona kwamba huku ndiyo kuwajibika sahihi. Wawakilishi wetu wanaunga mkono mambo au kupinga kwa sababu ya hoja na siyo kutetea vyama vyao. Tunaamini huu ni mwendelezo wa ukomavu wa Bunge letu.
Wakati wote wa mjadala, wabunge wengi walidhihirisha kuwa bado wanaweza kuangalia maslahi ya umma kwa upana zaidi na siyo vyama vyao. Wengi walipinga marekebisho ya muswada huo.
Kimsingi, muswada huo, ambao ulirekebisha sheria 14 zilizopendekezwa na serikali bungeni, uliwastua wanahabari baada ya kuona kuwa Sheria ya Magazeti Namba Tatu ya Mwaka 1976 inaongezewa makali yanayoonekana kuwa ni kitanzi kibaya kwa magazeti.
Marekebisho hayao yalitaka vifungu kadhaa virekebishwe, vikiwamo vya 36 na 37 vinavyotoa adhabu ya faini ya Sh. 150,000 au kifungo cha miaka mitatu au vyote kwa pamoja kwa gazeti litakalofanya makosa ya kuchapisha habari ya uchochezi au inayoweza kusababisha uvunjifu wa amani kwa kuongeza faini yake hadi kufikia Sh. milioni tano.
Mbali na kuwapongeza wabunge wetu, NIPASHE tunaunga mkono kwa asilimia zote hoja ya kuitaka Serikali iwasilishe bungeni muswada mzima wa Sheria ya Habari, ambao ulishaandaliwa na kujadiliwa na wadau tangu mwaka 2006. Nchi hii ni ya kidemokrasia. Na sifa mojawapo ya nchi ya namna yetu ni kuzingatia uhuru wa habari.
Kinyume chake ni dalili kuwa nchi yetu sasa inaelekea kusiko. Na hili siyo jambo zuri hata kidogo. Kuminya uhuru wa habari ni sifa ya nchi zisizofuata demokrasia.
Hivyo, si sahihi hata kidogo kufanya marekebisho ya sheria ambayo ni mbovu na inayotakiwa kubadilishwa haraka.
Kwa kuzingatia ukweli huu, ndipo tunapooona kuwa sasa ni wakati mwafaka kwa serikali kufikisha bungeni muswada mzima wa habari na siyo kuhangaika na kazi ya kuziba 'viraka' vyenye kukandamiza waziwazi uhuru wa habari nchini.
Serikali iachane na sheria ya kibabe inayoipa nguvu za kulalamika, kukamata na kuhukumu yenyewe vyombo vya habari vinavyoripoti taarifa zinazoonekana kutowafurahisha baadhi ya viongozi wake. Iache pia sheria inayobana uhuru wa habari na kutaka kuwafunga watu au kutoza faini za mamilioni. Bali, ipeleke bungeni muswada mzima wa habari!
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment