zanglassworks

AirFreight

Kwarara Msikitini

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Sunday, November 10, 2013

Wabunge: Msimamo wa JK EAC ni sahihi

NA MUHIBU SAID

10th November 2013


  Lowassa alaumu utendaji wa baadhi ya mawaziri
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya masuala ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Edward Lowassa akitoa hoja ya Bunge kuunga mkono hotuba ya Rais Jakaya Kikwete aliyoitoa katika Bunge mjini Dodoma jana.
Bunge limeazimia kuunga mkono msimamo wa Rais Jakaya Kikwete kwamba Tanzania haitajitoa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Hata hivyo, wabunge wamewatupia lawama baadhi ya mawaziri, wabunge, pia kasi ndogo ya utendaji wa serikali na vyombo vya habari, kwa kuchangia Tanzania kutengwa na nchi wanachama wa jumuiya hiyo.
Azimio hilo, ambalo lilitolewa kwa lengo la kupongeza tamko la Rais Kikwete kuhusu msimamo wa Tanzania kwenye EAC, liliwasilishwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Edward Lowassa, Bungeni jana.
Liliungwa mkono na wabunge wote waliohudhuria kikao cha jana cha Mkutano wa 13 wa Bunge, ambao walipiga kura ya kupaza sauti ya ‘ndiyo’, baada ya kuhojiwa na Spika wa Bunge, Anne Makinda, kama wanaliafiki azimio hilo au la.
Azimio hilo liliwasilishwa bungeni siku mbili, baada ya Rais Kikwete kulihutubia Bunge Alhamisi wiki hii na kutangaza msimamo wa Tanzania katika EAC.
Awali, kabla ya wabunge kupitisha azimio hilo, Lowassa alisema Tanzania imekuwa mwanachama wa EAC tangu mwaka 2005, lakini nchi za Kenya, Uganda na Rwanda zimekuwa zikifanya vikao na majadiliano mbalimbali bila kuishirikisha.
“Tanzania haijawahi kufanya jambo lolote la kuashiria kutaka kujitoa wala kutamka kuwa inataka kujitoa kwenye EAC,” alisema Lowassa na kuongeza:
“Kwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika hotuba yake aliyoitoa tarehe 7 Novemba, 2013 kuwa Tanzania haina mpango wa kujitoa kwenye shirikisho la Afrika Mashariki, Bunge linaazimia kwamba, linamuunga mkono kuwa Tanzania isijitoe kwenye shirikisho hilo na kuwataka watu wa Afrika Mashariki kuilinda na kuitetea jumuiya hiyo.”
Hata hivyo, wakichangia mjadala wa azimio hilo, baadhi ya wabunge walisema kauli za baadhi ya mawaziri na wabunge, hasa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na vyombo vya habari vya hapa nchini, zilichangia kuchochea mvutano uliojitokeza uliosababisha Tanzania kutengwa. Sababu nyingine walisema ni kasi ndogo ya utendaji wa serikali katika mambo ya EAC.
Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ulinzi na Usalama, Anna Abdallah, alisema wakati Watanzania wanaona boriti katika macho ya marais; Paul Kagame (Rwanda), Yoweri Museveni (Uganda) na Uhuru Kenyatta (Kenya), nao pia watambue kuwa kwenye macho yao kuna vibanzi.
Alisema iwapo Watanzania hawataviondoa vibanzi hivyo kwenye macho yao, basi watakuwa wametoa mwanya kwa watu wasiowatakia mema kuendelea kuwaona kuwa wao ndiyo hawaitaki EAC.
Abdallah alisema pamoja na matatizo yanayoonekana kwa marais hao, Tanzania pia kuna mambo madogo madogo, ambayo kasi ya watendaji wa Serikali ya Tanzania katika utekelezaji wake imekuwa ndogo katika kufikia malengo ya EAC.
Hoja hiyo iliungwa mkono na Mbunge wa Kuteuliwa (NCCR-Mageuzi), James Mbatia, ambaye aliwashauri wanasiasa na viongozi kwamba, linapotokea jambo linalohusu Taifa, kutafakari yakinifu kabla ya kutoa kauli, ambazo zinaweza kuwaudhi wengine.
Pia aliishauri serikali kufanya kasi katika mambo inayoyazungumza kuhusiana na EAC ili Tanzania iendelee kuwa kiongozi hata kama ni masuala yanayolalamikiwa na nchi hizo, kama vile bandari na reli.
Pia alisema tatizo lingine ni wabunge wa Tanzania wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) kutopata maelekezo sahihi ya mambo wanayokwenda kujadili katika vikao vya Bunge hilo na hivyo, kushindwa kurudisha mrejesho sahihi. Alishauri kuwapo kitengo maalumu kitakachokuwa kikiratibu jambo hilo.
Mbunge wa Hai (Chadema), Freeman Mbowe, alisema matatizo hayo na mengine ndiyo ambayo nchi hizo zinaiona Tanzania haiko makini katika EAC.
Alisema pia kauli zisizokuwa za kidiplomasia dhidi ya marais hao na nchi zao, ambazo zimekuwa zikitolewa na baadhi ya mawaziri na wabunge wa CCM Bungeni, pia zimechangia mvutano huo.
“Tukubaliane katika dunia ya diplomasia, kauli ni jambo la msingi sana. Kauli wakitoa kina Mbowe mtasema kina Mbowe hawa ni wapinzani, lakini kauli zinapotoka kwa cabinet ministers (Baraza la Mawaziri), kauli zinapotoka kwa wabunge ndani ya Bunge ya wabunge ambao ni wa chama tawala kuashiria ubabe katika masuala ya kidiplomasia, hakuna ubabe hapa katika diplomasia,” alisema Mbowe.
Alisema amekuwa kama mgonjwa aliposikia kauli hizo za mawaziri na wabunge zilipotolewa.
Mbowe alisema katika mvutano huo, vyombo vya habari vilisimama upande wa serikali na kuripoti vibaya suala hilo kwa kuwaona majirani wa Tanzania ni wabaya, huku vikiacha kuripoti kasoro za Tanzania.
Badala yake, alisema vimekuwa na utaifa, ambazo unazidi kutafakari kwa kina na kusema hata mitandao ya kijamii pia imeendelea kukuza mvutano huo, ikiwa ni pamoja na kuzidharau nchi hizo.
Kutokana na hali hiyo, aliishauri serikali kuacha kulalamika kutengwa na nchi hizo, badala yake itafakari tatizo hilo.
“Tusilalamike, tutafakari. Kenya, Uganda watuache? Haiwezekani, tuna tatizo la ndani,” alisema Mbowe na kuishauri serikali kutengeneza timu ya diplomasia kushughulikia jambo hilo kujua sababu za nchi hizo kufanya vikao vya siri.
Aliitaka serikali kuwasaidia Watanzania kujua Tanzania inataka nini EAC. Alisema ugomvi wa Tanzania na nchi hizo haupo tu kwenye EAC, bali kuna ukweli kwamba, hata katika Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za Kusini mwa bara la Afrika (SADC) nako hakueleweki vizuri.
“Sasa tunalalamikiwa kwenye SADC, tunalalamikiwa kwenye EAC…Hebu tuchague tunataka patner (mshirika) gani? Tusiwe mke mmoja wa waume wengi,” alisema Mbowe.
Alisema ana uhakika kama nchi hizo zinajua mambo hayo, hawajaiambia. Mbowe alisema Tanzania imekuwa nyepesi sana kuwaona Wakenya na Waganda kuwa ni watu wabaya, lakini ikiwa tayari kuwakumbatia Wachina na Wahindi au mataifa mengine ya mbali na kuitaka serikali ijiangalie ilichozidiwa na watu hao (Wakenya na Waganda) na inachopasa kujifunza kwao.
Wengine waliochangia mjadala wa azimio hilo, ni Mbunge wa Mkanyageni (CUF), Mohammed Habib Mnyaa, na Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Amina Makilagi.
Wakati huo huo, akitoa maoni yake Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Benson Bana, alisema Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki Samwel Sitta alikuwa na jukumu la kufahamu tofauti zinazojitokeza katika jumuiya hiyo.
Alisema kama kuna matatizo alipaswa kuyatatua kutokana na uzoefu wa miaka mingi wa Muungano wa Tanzania na Zanzibar.
Alisema kuwa Sitta wakati akiwa Mbunge na Spika wa Bunge alionyesha umahiri wa kutatua mambo Bungeni.
"Iweje leo ashindwe hata kujua tatizo? ...Kama angetaka umoja huo uwapo angeweza kwa kutumia uzoefu wake," alisema na kupendekeza Rais Kikwete amuweke mtu atakayeweza kuiendesha wizara hiyo.
Aliongeza kuwa kauli aliyoitoa kuwa Tanzania itatoa talaka ni ishara kuwa hapendi jumuiya hiyo. Alisema umoja wa Afrika Mashariki ni wa wananchi, wanatakiwa watoe maoni yao kama wakati wa mchakato wa kupata katiba ya Tanzania.
Alisema hata wabunge wa Afrika Mashariki hawana udhoefu wa kutatua kero za kimuungano. "Walipaswa kujiuliza kwanini tutengwe kwenye vikao wakati shirikisho tumeanzisha pamoja?" alihoji.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments :

Post a Comment