Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Monday, November 25, 2013

Zitto, Dk. Kitila waeleza siri zao

NA WAANDISHI WETU

25th November 2013


  Zitto Kabwe autaka uenyekiti
  Asema hataondoka Chadema
Zitto Kabwe (kulia) na mwenzake Dk. Kitila Mkumbo, ambao walivuliwa uongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wakizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani), jijini Dar es Salaam jana.
Aliyekuwa  Mjumbe wa Kamati Kuu (CC) ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Kitila Mkumbo, amekiri kushirikiana na aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba, kuandaa waraka uliokuwa na mkakati wa kupata Mwenyekiti wa taifa wanayemtaka.

Dk. Mkumbo alitoboa siri hiyo na kusema mtu ambaye kwenye waraka walimtambulisha kama MM kuwa ni Zitto Kabwe na ndiye waliyekuwa wanamuandaa kuwania nafasi ya Mwenyekiti wa taifa.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, akiwa ameambatana na aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu, Zitto Kabwe na mwanasheria wa chama hicho na diwani wa kata ya Mabogini, wilaya ya Moshi Vijijini,  Albert Msando, Dk. Mkumbo alisema M1 ni Mwigamba na M2 ni yeye na kwamba MM ambaye ni Zitto hakuwa amejulishwa.

Dk. Mkumbo alitetea waraka wao kuwa umefanya ‘sort analysis’ ambayo inataka kufanya uchambuzi wa nguvu kwa upande mgombea wanayemuandaa na udhaifu, uchambuzi wa nguvu na udhaifu wa upande wa pili (unayepambana naye) ili kujipanga.

“Kwenye waraka wetu ambao Zitto hakuufahamu, tumeeleza madhaifu saba ya tunayeona anafaa kuwa Mwenyekiti, mfano tumeeleza MM maneno yake mara nyingi hayazingatii anazungumza katika mazingira gani na hivyo kuwasha masikio ya wanataasisi na kumfanya asikubalike…huu ni udhaifu, tumeainisha udhaifu takribani saba ili kuyashughulikia ukishajua, unajua unatumia njia gani kufunika,” alibainisha.

Kauli ihiyo iliungwa mkono na Zitto kuwa hakuwahi kuona waraka wala kilichomo ndani zaidi ya kuusikia kwenye kikao cha CC na kwamba iwapo angeuona mapema angefanyia kazi madhaifu yote.

Dk. Mkumbo alisema kwenye suala la uchaguzi, ni kawaida kuwa na mikakati kwa makundi yanayoshindana na wao walifanya hivyo kuanisha mapungufu na nguvu zao na za wanayetarajia kushindana naye.

“Ni lazima ujue nguvu za mpinzani wako na zitapunguzwaje na udhaifu wake utatumiaje kama mbinu ya ushindi, bahati mbaya waraka umevuja ulikuwa wa siri sana… waliovujisha ni viongozi, wasome madhaifu wajitetee, vinginevyo tutayatumia kuwashinda uchaguzi mkuu ujao, hapo hakuna suala la kusababisha mkanganyiko wala mgogoro kwenye chama,” alisema.

Alisema ni jukumu la viongozi kurekebisha na kuyafanyia kazi yaliyoanishwa kwenye waraka huo kwani ni ngumu kwa kiongozi kama yeye (Mkumbo) kusema Mwenyekiti wake ni mbadhirifu na ndiyo maana kwenye kikao hicho aliomba msamaha baada ya waraka kuvujishwa na viongozi wenyewe pasipokujua wanajianika.

Alisema katika kudhihirisha kuwa kuna makundi ya uongozi kwenye chama hicho, kuna mkakati wa kundi linalowataka viongozi waliopo kuendelea na madaraka yao ambao wameandaa waraka wa siri wa kumchafua Zitto na wameusambaza kwenye mitandao ya kijamii ikiwa ni pamoja na kusema yeye (Dk. Mkumbo) amehongwa Sh. 200,000 na Zitto, jambo ambalo alilitafsiri kama ujinga.

Dk. Mkumbo aliongeza kuwa wakati wa kikao cha CC, aliomba kujiuzulu kwa sababu ya wajumbe wenzake kukosa imani naye na alimuomba msamaha Mwenyekiti juu ya lugha iliyotumika kwenye waraka ule ambao ulivujishwa na viongozi.

Alisema Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu, alishauri kamati kutokubali wajiuzulu badala yake wawafukuze ili waaibike na kwamba kwa hali iliyopo sasa, jamii na wana-Chadema wasome waraka neno kwa neno na kuona anayeadhirika ni yupi.

Aidha, Dk. Mkumbo alisema ushauri wa Lissu ni wa kijinga unakiweka chama katika mazingira magumu kwa kuweka hadharani waraka na kuwasimamisha pasipo kuwasikiliza.

ZITTO ATANGAZA MAPAMBANO
Katika mkutano huo, Zitto alitangaza mapambano na chama chake na kwamba hana mpango wa kukihama chama na atakuwa wa mwisho kufanya hivyo kwa hiari yake.

Alisema kinachoendelea ndani ya chama hicho ni mapambano ya kukuza demokrasia, mapambano baina ya wapenda demokrasia dhidi ya waafidhina, waumini wa uwajibikaji dhidi ya wabadhirifu na wapenda siasa safi dhidi ya watukuzao siasa majitaka.

AUTAKA UENYEKITI

Hata hivyo, Zitto hakutaka kuweka hadharani wazi msimamo wake kama atawania nafasi ya uenyekiti au la, bali alisema wakati ukifika na wanachama na viongozi wenzake wakaona anafaa, atafanya hivyo.

“Muda utakapofika taratibu za chama zikitangazwa na watu ambao wanaamini kama ninaweza kutoa mchango wangu kwenye chama, nitafanya hivyo…suala la uongozi si suala binafsi lazima wenzako waamini kama unaweza, siwezi kusema nitafanya hivi au la kwa sasa,” alisema Zitto.

Alisema atashauriana na wenzake na kuona kama inafaa, lakini lazima katiba, kanuni na taratibu za chama zizingatiwe, wakati ukifika atajua la kufanya.

Aidha, alisema ni vyema wana-Chadema wakaelewa kuwa kinachoendelea ndani ya chama hicho ni mpambano wa demokrasia na ni hatua ambayo lazima chama kupitia ili kukomaa na kuwa tayari kushika dola.

Alisema Chadema si cha kwanza kupita kwenye migogoro kwani vyama vyote vimepita kwenye migogoro na mgongano wa kimawazo ndani ya chama ni jambo la kawaida ni mchakato lazima watu wajifunze.

Zitto alisema wapo viongozi waliofukuzwa na kusimamishwa kwenye uongozi, lakini baadaye wakawa viongozi wakubwa wa nchi, na kwamba suala hilo ni changamoto ambazo lazima wazipitie katika kujenga demokrasia ya kweli.

Alisema aliamua kujitoa kuwa mtia sahihi kwenye akauti za Chadema kutokana na kutoshirikishwa kwenye masuala ya fedha na dhamira yake ilimsuta na kumkataza na kumtuma kuhakikisha kunakuwa na misingi ya uwajibikaji kwani ni vigumu sana Mawaziri wa CCM wanawajibishwa huku udhaifu ukiwa ndani ya chama chake.

Aidha, alisema kwa mara ya kwanza waraka huo aliusikia ndani ya kikao cha Kamati Kuu na kwamba alisikitika kutomfikia mapema ili aufanyie kazi  kabla kwani mara moja angeanza kutekeleza yaliyoshauriwa na kina Dk. Mkumbo wa ndani ya waraka

“Muono wangu ndiyo muono wa wajumbe wa kamati kuu?” Aliuliza na kuongeza: Katiba ya Chadema haionyeshi tafsiri ya neno uhaini nasi tumeitwa wahaini.”

Aidha, alisema siyo kweli kuwa waraka uliojulikana kama mkakati wa uchaguzi 2013 si sababu ya kuvuliwa nafasi za uongozi na badala yake ni tuhuma lukuki ambazo siyo mara ya kwanza kuzisikia zikijadiliwa ndani na nje ya vikao vya chama.

Alisema tuhuma hizo ni kuwa amekuwa akikisaliti chama kwa kutumika na CCM na Idara ya  Usalama wa Taifa.

 “Ninatambua kwamba chama changu kinapita katika wakati mgumu sana, nataka nitamke mapema kuwa sitakuwa chanzo cha Chadema kuvunjika, ndicho chama kilichonilea na kunifikisha nilipo, niliaza kuwa mwanachama nikiwa na umri wa miaka 16,” alibainisha Zitto.

Alisema zipo tuhuma nyingi ambazo zimekuwa zikirudiwarudiwa katika vikao vya chama na nje ya vikao na baadhi ya viongozi wenzake zenye lengo la kuonyesha kuwa ni mbinafsi na anapokea rushwa ili kukihujumu chama.

Alisema zipo tuhuma kuwa hakushiriki kumnadi mgombea urais mwaka 2010, jambo ambalo siyo kweli kwani alifanya kampeni za udiwani hadi urais katika majimbo 16 na kuzunguka na mgombea urais katika mkoa wa Kigoma, lakini alitupiwa lawama baada ya yeye pekee kushinda bila kujali yalikuwa maamuzi ya wana-Kigoma.

Tuhuma nyingine ni kuwashawishi wagombea wa Chadema katika baadhi ya majimbo kujitoa katika uchaguzi wa mwaka 2010 ili kuwapisha wagombea wa CCM wapite bila kupingwa kwa njia ya rushwa katika majimbo ya Sumbawanga, Musoma Vijijini na Singida Mjini na kwamba hadi sasa hakuna mahali tuhuma hizo zimetolewa ushahidi.

Tuhuma kuwa hashiriki kwenye operesheni mbalimbali za chama alisema siyo za kweli kwani amefanya hivyo mara nyingi na wakati mwingine kutumia gharama zake.

Tuhuma kuwa amekidhalilisha chama kwa tamko la Kamati ya kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kwamba hesabu za vyama hazijakaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na kwamba alipaswa kuwasiliana kwanza na uongozi wa chama ‘kuwatonya’ ili wajiandae.

Aidha, alisema walimtuhumu kuwa kutokuwatonya kumekidhalilisha chama na kukiweka kundi moja na CCM, hivyo anastahili kuadhibiwa vikali kwa kuwa katika taarifa yake alikuwa na nia mbaya na chama.

“Napenda kusisitiza kwamba hakuna chama ambacho kimewahi kukaguliwa na CAG, natambua kwamba mahesabu ya chama changu yamekaguliwa na wakaguzi wa nje kwa utaratibu tuliojiwekea, lakini matakwa ya kisheria ni kwamba mahesabu ya vyama vya siasa hayajakaguliwa na CAG, hili ni kosa la kisheria, bila kujali kosa limetendwa na nani,” alisema Zitto.

Tuhuma nyingine ni kuwa ni mnafiki kwa kukataa kuchukua posho za vikao tangu mwaka 2011 kama ishara ya kuonyesha msimamo wa chama wa kupinga posho za kukaa na matumizi mengine yasiyofaa katika fedha za umma kama ilivyoainishwa katika ilani ya chama hicho ya mwaka 2010-2015.

Alisema tuhuma za wazi za Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, kuwa anapokea rushwa kutoka kwenye mashirika ya umma siyo za kweli na hakuna posho yoyote anayopokea na kwamba suala hilo siyo la kati yake na Lema bali msingi kwenye chama.

Suala la usambazaji wa ripoti ya siri dhidi yake, uliojikita kuwa amehongwa fedha nyingi ili kukihujumu chama ukidaiwa kuchomolewa makao makuu ya chama, viongozi wa chama walikana kuwa haukuandaliwa wala kusambazwa na makao makuu.

Alisema katika kikao cha CC alilalamika kuwa baadhi ya viongozi waliokuwa wanasambaza waraka walikuwa ni viongozi wa chama na hakuna aliyechukuliwa hatua za kinidhamu.

Katika hatua nyingine, Zitto alisema hawataandika barua za kujieleza ndani ya siku 14 walizopewa hadi watakapopewa barua rasmi za kuvuliwa madaraka na kuwa hadi jana walikuwa hawajazipata.

NIPASHE iliwatafuta viongozi waandamizi wa Chadema ili kujibu baadhi ya tuhuma zilizoelekezwa kwao, lakini hawakupatikana.

Mwenyekiti, Freeman Mbowe, Katibu Mkuu, Dk. Willibrod Slaa na Mwansheria Mkuu  wa chama, Lissu, simu zao ziliita bila kupokelewa.

JIMBONI KWAKE WAMLILIA
Baadhi ya watu wanaodaiwa kuwa ni wafuasi wa Zitto katika Jimbo lake la Kigoma Kaskazini, wamechoma kadi, bendera na kuvunja vijiwe vya chama hicho, wakipinga hatua ya Kamati Kuu kumvua Zitto nyadhifa zote za uongozi.

Hali hiyo ilijitokeza katika kijiji cha Mwandiga baada ya wafuasi hao kukusanyika kwa lengo la kutoa tamko kuhusiana na maamuzi  hayo.

Watu hao walikuwa na mabango mbalimbali kumsifia Zitto, katika tamko lao, wameutaka uongozi kutafuta mwafaka juu ya mgogoro huo ili kukinusuru chama hicho, ambacho kinakua kwa kasi na kuanza kuaminiwa na Watanzania.

Akisoma tamko hilo, Ramadhani Bakari, alisema wanautaka uongozi wa chama hicho kutafakari upya hatua waliyoichukua na kama hawatafanya hivyo, wao watakuwa na maamuzi ya hatua za kuchukua baada ya kupata msimamo kutoka kwa mbunge wao.

“Tunasubiri Mheshimwa Zitto atuambie mwelekeo ukoje, hapo ndipo tutakapokuwa na maamuzi ya mwisho , ni kiongozi tunayempenda na kumwamini, hivyo tunasubiri atuambie,” alisema.

Kwa upande wake, Katibu wa Chadema Jimbo la Kigoma Kaskazini, Ramadhan Ruhaha, alisema tamko hilo siyo la chama bali ni la wapenzi na wanachama na kwamba chama kitakaa leo viongozi wote wa Chadema mkoa kujadili na kutoa mapendekezo yao juu ya hatua hiyo .

Mbeya: ALIKUWA MZIGO KWA CHAMA
Hata hivyo, wakati wafuasi wa Zitto wakimtetea, uongozi wa chama hicho Kanda ya Nyanda za Juu Kusini umeunga mkono uamuzi huo, huku wakiilaumu CC kwa kuchelewa kuchukua uamuzi huo.

Tamko la kuunga mkono uamuzi huo, lilitolewa jana jijini Mbeya kwa waandishi wa habari na Mwenyekiti wa Hamasa wa Chadema Kanda ya Nyanda za Juu Kusini ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Mbeya Mjini, David Mwangija, maarufu kama Mzee wa Upako.

“Vongozi wa Chadema Nyanda za Juu Kusini tumewasiliana na kwa kauli moja tunaunga mkono uamuzi wa Kamati Kuu ya chama chetu wa kumvua madaraka Zitto kwani tunaona hatua hiyo ilikuwa ni ya muhimu na pengine tunaweza kusema viongozi wetu walichelewa sana kuchukua hatua hiyo,” alisema Mwambigija.

Alisema Zitto licha ya kuwa na nyadhifa za juu ndani ya chama, amekuwa hashiriki kwenye shughuli nyingi za chama, jambo ambalo lilisababisha wamuone mzigo ndani ya chama.

Imeandikwa na Salome Kitomari Dar, Emmanuel Lengwa Mbeya na Deo Nsokolo, Kigoma.

CHANZO: NIPASHE

No comments :

Post a Comment