Na Waandishi wetu
Nzigilwa:Watanzania ombeeni
rasimu ya pili
Wa Anglikana: Ondoeni hofu ya mchakato
Askofu Mkude apinga kupanda bei ya umeme
Wa Anglikana: Ondoeni hofu ya mchakato
Askofu Mkude apinga kupanda bei ya umeme
Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Geita, Mwashamu Damian
Dallu, akiongoza misa ya Krismas Kitaifa iliyofanyika Kanisa la Bikira Maria
Malkia na Amani mjini Geita jana. Picha: Daniel Limbe.
Katika mahubiri yake kwenye Kanisa la Mtakatifu Joseph jijini Dar es
Salaam, Askofu Msaidizi wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Eusebius
Nzigilwa, aliwataka Watanzania kuiombea rasimu ya pili ya Katiba Mpya ili
ipatikane katiba inayokidhi mahitaji ya watanzania kwa maslahi ya nchi na
ustawi wa jamii.
Aidha, alisema viongozi wanapopewa madaraka wametakiwa kuacha kujineemesha na kujilimbikizia mali na kushindwa kuwasaidia wale ambao wanatakiwa kuwahudumia na kuwaacha katika hali duni.
Aidha, alisema viongozi wanapopewa madaraka wametakiwa kuacha kujineemesha na kujilimbikizia mali na kushindwa kuwasaidia wale ambao wanatakiwa kuwahudumia na kuwaacha katika hali duni.
Alisema kipindi hiki cha maandalizi ya kupata katiba mpya wananchi
wanapaswa kuiombea nchi ibaki katika umoja, mshikamano na amani kwa kuwa mwaka
2013 amani ya nchi ilitikisika katika mambo mbalimbali.
Askofu Nzigilwa alisema ikipatikana katiba inayokidhi mahitaji ya
watanzania italeta ustawi wa nchi na jamii kwa ujumla na nchi itabakia kuwa
amani na utulivu.
Kuhusiana na viongozi wanapopata madaraka, alisema utakuta mtu akiwa duni
kabisa, lakini anapopewa nafasi anajineemesha kwa kununua magari, kujenga
majumba bila kuwasaidia watu wanaowatumikia.
Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Anglikan la Mtakatifu Alban, jijini Dar es
Salaam, Aidano Mbulinyingi, aliwataka Watanzania kuondoa woga juu ya mchakato
unaoendelea wa kupata katiba mpya, ambayo alisema imebeba mawazo
mbalimbali,yakiwamo potofu.
Mchakato huo wa katiba utafanikiwa kwa kuwa Kristo aliyezaliwa miaka 2,000
iliyopita aliwaasa Wakiristo kuwa wasiogope kwa jambo lolote litakalotokea mbele
ya jamii.
Alisema baadhi ya Watanzania wamekuwa na woga kuhusu mchakato wa katiba
huku wengine wakitafuta mbinu mbalimbali ili zoezi hilo la kuandika katiba
lishindikane.
“Tusiwe waoga kiasi hicho, bali tumtegemee Mungu na neno, usiogope katika
Biblia limeandikwa mara 360, hii nikionyesha yote yaliyopo sasa tayari Mungu
anayajua na kutuasa,” alisema.
Mchungaji Mbulinyingi alisema ni ajabu kuona wengine wakihofia uchaguzi
mkuu wa mwaka 2015 na kuanza kujitangaza kwa wananchi, na kusema kuwa hali hiyo
inapaswa kuombewa ili iwatoke wenye roho hizo na kuwa raia wema.
MAPIGANO YA ARDHI
Selyvester Thadey wa kanisa la International Evangilism Sinai Ipagala
mkoani Dodoma, alisema hivi sasa Watanzania wamechoshwa kusikia vurugu za
mapigano zinazotokea za wakulima na wafugaji, hivyo kuwataka viongozi wa
serikali waliokabidhiwa dhamana ya kiutendaji wanakomesha hali hiyo.
“Sisi kama kanisa tuna mashaka miongoni mwa viongozi wa serikali wananufaa
pindi inapotokea vurugu kati ya wakulima na wafungaji kuwa, wanapata maslahi kwa
ajili yao binafsi,” alisema.
ASKOFU PHAM APONGEZA MAWAZIRI KUJIUZULU
Askofu wa Kanisa la PHAM Kanda ya Kati Dodoma Julius Bundala, aliwapongeza
mawaziri ambao wizara zao zimeshutumiwa kuhusika katika unyanyasaji wakati wa
Operesheni ya Tokomeza Ujangili kwa kukubali kuachia madaraka yao.
Bundala akizungumza mara baada ya ibada iliyofanyika ya Krismas Kanisa la
Makole mjini Dodoma.
Alisema hatua walizochukua mawaziri hao kujiuzulu ni ukomavu.
Hata hivyo, alisema watendaji wengine wanapaswa kufahamu kuwa hakuna
kificho kutokana na mawaziri hao kuwekwa wazi na Kamati ya Ardhi, Maliasili,
Ardhi na Mazingira kwenye kikao kilichomalizika hivi karibuni mjini
Dodoma.
Hata hivyo Askofu huyo amemtaka Rais Kikwete kutoishia kwa Mawaziri hao
bali anatakiwa kuchunguza baraza lake hilo ili kuwabaini ambao wanaotumia
madaraka yao kinyume na sheria na utaratibu zilizopo ndani ya katiba ya Jamhuri
ya Muungano.
TAG yalaani TOKOMEZA UJANGILI
Mchungaji wa Kanisa la TAG Mlima wa Moto lililopo soko la Sabasaba mjini
Dodoma, Silivanus Komba, alisema njia iliyowezesha kuweka wazi unyama
waliofanyiwa wananchi na mawaziri ambao walioondolewa kwenye nyadhifa zao ni
baada ya kufanyika kwa mahojiano mbalimbali na kamati.
Alisema hali hiyo inatokana na vilio vingi vya wananchi ambao
walionyanyaswa wasiokuwa na hatia na kunyanganywa na mali na fedha zao kwa
watendaji wasiokuwa na huruma.
Hata hivyo, alisema kuwa ni matumaini yake na kanisa kuwa serikali pia
inasafisha safu yake kwa wale ambao bado wanaonyoshewa vidole kutokana na
utendaji wao mbovu.
ASKOFU MKUDE APINGA UMEME KUPANDA
Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Morogoro, Telesphory Mkude, alieleza
kushangazwa na serikali kwa kuruhusu bei ya umeme kupanda kwa asilimia 50 na
kueleza kuwa hali hiyo itazidi kuongezea mwananchi mzigo na kuendelea na hali ya
umasikini kwa kuwa watashindwa kumudu gharama hizo.
Badala yake Askofu Mkude alitaka serikali kutoruhusu kupanda kwa bei ya
umeme kwani wananchi watashindwa kutumia huduma hiyo na kubaki kwa watu wachache
ambao watakuwa na uwezo.
Katika mahubiri yake katika Kanisa la Mtakatifu Patrice, alisema
inasikitisha kuona bei ya umeme inapandishwa kwa kiwango kikubwa na kuendelea
kumuumiza mwananchi wa nchini ambaye kipato chake ni duni na kueleza hali hiyo
itasababisha watanzania waendelee kudidimia na hali ya umaskini.
Alisema cha kusikitisha ni kwamba Tanzania ndiyo nchi inayotoza gharama
kubwa za umeme ikilinganishwa na nchi nyingine duniani.
“Watanzania wanakipato duni sana, leo hii wanapandishiwa bei ya umeme, mimi
nadhani sasa watashindwa kuitumia huduma hiyo na kurudi katika matumizi ya
vibatari ,” alisema na kuongeza:
“Katika hili serikali inapaswa kulitafakari kwa kina suala hili la
kupandisha bei ya umeme.”
Alisema anadhani kwa nchi kama ya Tanzania ambayo inanza kupiga hatua ya
kutafuta maendeleo kwa kasi, huduma hiyo ilipaswa kutolewa kwa gharama nafuu ili
kila mtu amudu, lakini hali imekuwa tofauti kutokana na kupandishwa mara kwa
mara huku umeme ukiendelea kuwa tatizo.
ASKOFU MALASUSA
Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Alex
Malasusa, amesema viongozi na wanasiasa waliopo madarakari kwa njia zisizo za
halali wamekuwa wakihangaika kufanya jambo lolote liwezekanalo ili kuzilinda
nafasi zao, pindi unapotokea mtetereko katika nafasi walizopo jambo alilosema
linasababisha uvunjifu wa amani.
Aidha aliwafananisha viongozi hao na Mfalme Herode ambaye alikuwa mfalme
wa Wayahudi na baada ya kusikia kuwa Yesu Kristo amezaliwa ambaye atakuwa mfalme
wao, alitetereka na kuanza kutafuta mbinu za kumuangamiza.
Akihubiri katika Kanisa hilo Kuu la Azania Front, jijini Dar es Salaam,
Dk. Malasusa, alisema ni vema jamii ikasherehekea Krismasi kwa kuyafanya yale
mema ambayoYesu aliyatenda ili kudumisha amani na ushirikiano duniani
kote.
Aliwataka watanzania na dunia nzima kusherehekea sikukuu hiyo kwa kuishi
maisha ya amani ambayo yataendelea kutuunganisha dunia nzima ili kuepukana na
vitendo vya uvunjifu wa amani vinavyotokea duniani.
“Rasilimali nyingi duniani hutumika kutengeneza na kutafuta amani kwa
mambo ambayo hayampendezi Mungu badala ya kuelimisha watu ili kuzilinda imani
zao, mfano mzuri ni kwa watu ambao wamekuwa wakirekebisha maovu ya watu au
viongozi, huonekana hawafai kwa kupigwa vita badala ya kuungwa mkono,” alisema
Dk. Malasusa.
ASKOFU AICT: VIONGOZI NI WABINAFSI
Askofu wa Africa Inland Church (AICT) Jimbo la Geita, Mussa Magwesela,
alisema amani barani Afrika haitapatikana iwapo viongozi waliopewa dhamana ya
kuwaongoza wananchi hawataacha ubinafsi wa kung’ang’ania madaraka,
kujilimbikizia mali, rushwa na matumizi mabaya ya raslimali za umma
vinavyosababisha mataifa mengi duniani kumwaga damu.
Akizungumza katika Ibada ya mkesha wa Krismasi iliyofanyika kitaifa katika
kanisa hilo Kalangalala mjini Geita, alisema hali hiyo inatokana na viongozi
kukosa hofu ya Mungu na kutaka kujinufaisha kwa maslahi binafsi.
Askofu Mwagwesa, alisema viongozi hao wameshindwa kufuata misingi
iliyoachwa na watangulizi wao (waasisi wa mataifa hayo) Kwame Nkuruma, Mwalimu
Julius Nyerere, Jomo Kenyatta na Nelson Mandela ambao walikuwa wanyenyekevu
mfano wa Yesu Kristo alipojitoa na kukubali kufa msalabani ili kuwakomboa watu
na dhambi za ulimwengu.
“Viongozi hawa waliimarisha misingi ya Utawala bora, lakini suala la
uongozi katika Taifa letu na bara la Afrika kwa miaka 50 hadi 60 iliyopita
tumejionea matukio mengi ya umwagaji wa damu kwa sababu ya baadhi yao
kung’ang’ania madaraka,” alisema Askofu Magwesela.
Kadhalika, alisema sekta ya ardhi imekuwa kinara wa rushwa, hali ambayo
imekuwa ikisababisha uvunjwaji wa sheria na hatimaye mauaji baada ya viongozi
hao kutumia madaraka yao vibaya kama ilivyojitokeza kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa
Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mwanza, Clement Mabina.
Alisema kugoma kwa madakatari na walimu nchini kwa kisingizio cha ukosefu
wa vitendea kazi sehemu za kazi na mishahara midogo inatokana na kukosa wito wa
kazi zao licha ya kuwa elimu hiyo wameipata kutokana na kodi za wananchi.
“Serikali iboreshe miundombinu ya maji,barabara na hospitali badala ya
kuendelea kuwahadaa wananchi.
ASKOFU DALLU: RASILIMALI ZISITUGOMBANISHE
Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Geita, Damian Dallu, aliwataka
Watanzania kuepuka mafarakano na uvunjifu wa amani kunakosababishwa na
rasilimimali za nchi.
Aidha, aliwata kushirikiana katika kuondokana na mambo yanoyoleta uadui
kati ya wenye madaraka, vyeo na waliyonacho na wasiyo chacho kwani vinaweza
kuligawa taifa katika matabaka.
Rai hiyo aliitoa jana mjini Geita katika ibada ya Krismasi iliyoadhimishwa
kitaifa katika Parokia ya Bikira Maria Malkia wa Amani mkoani Geita.
Alisema ni vyema Watanzania kusherehekea Krisimas kwa amani na upendo wa
kweli kwa kusaidiana bila kujali tofauti zetu katika njia halali ya kujikomboa
na umasikini na kujenga mshikamano.
“Ni vema mambo yanayoonekana kuwa chanzo cha uvunjifu wa amani vikaepukwa
mapema kwa kushirikiana kwamba aliye nacho aumie kwa ajili ya yule asiye nacho
ili kuishi kwa amani na furaha, kiongozi bora ni yule anayeumia kwa ajili ya
watu wake na huo ndiyo upendo unaoleta amani,” alisema Askofu Dallu.
Alisema, ni vema Watanzania wakatafuta amani na furaha ya kweli kwa kuomba,
kusameheana yale yote yaliyopita pamoja na kushiriki sala, kuinua elimu na
kufanya kazi kwa bidii.
Pia aliwataka wakazi wa mkoa mpya wa Geita kuhakikisha wanauendeleza mkoa
huo kwa kusoma na kufanya kazi kwa bidii ili kujiinua kiuchumi hasa katika sekta
ya elimu na afya ambazo bado ziko chini.
ASKOKU MKUU ANGLIKANA
Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Jacob Chimeledya, ameitaka
serikali kuwa na mipango madhubuti ya kuwahudumia watu badala ya kupata dhiki
katika nchi yao yenye utajiri mwingi.
Akitoa salamu zake za Krismasi katika Kanisa la Dayosisi ya Mpwapwa mkoani
Dodoma, alisema ni lazima Watanzania wote wapate elimu.
”Kwa mfano ukizungumzia habari ya elimu mtanzania anahitaji kupata elimu
ambayo itakuwa mkombozi katika maisha yake na serikali iwe na kipaumbele chetu
kwa mfano kwenye elimu ya msingi na sekondari kuliko kwenye elimu ya chekechea,”
alisema Askofu Chimeledya.
Alibainisha kuwa Watanzania wanahitaji kupata elimu ambayo itakuwa mkombozi
katika maisha yao na kusema kuwa matarajio yake ni mtoto aingie elimu ya msingi
anajua kusoma na kuandika hivyo aandaliwe chekechea akiwa na miaka mitatu hadi
mitano.
“Pia Watanzania watapata matumaini kama serikali itashuka chini na kwenda
kushughulikia watendaji mmoja mmoja na waziri anawajibika kama mimi
ninavyowajibika kwa kanisa langu au dayosisi yangu kama kweli chini kuna watu
wanafanya vibaya kwa hiyo kuwajibika kwangu hakutaleta faraja kama bado
watendaji hao wapo,” alieleza.
Alisema kuwa inatia moyo mawaziri wanne wamewajibika kwa kujiuzulu na
anawapongeza sana, lakini serikali irudi kufuatilia watendaji wote katika ngazi
mbalimbali kamwe kuna mtu hataweza kutowatendea haki wananchi.
Askofu Shao: Tuwaombee Sudan Kusini
Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya
Kaskazini Dk. Martin Shao, amesema ingawa Tanzania inatajwa kukomaa kisiasa
katika ukanda wa Afrika, lakini iko haja kama taifa kuandaa funga maalumu kwa
ajili ya kumwomba mwenyenzi Mungu aingilie kati na kukomesha mapigano
yanayoendelea Sudan ya Kusini kati ya wanajeshi watiifu kwa Rais Salva Kiir na
wanaomuunga mkono hasimu wake, Riek Machar.
Alisema machafuko ya kisiasa yanayoendelea kuangamiza wanadamu katika
mataifa yenye utajiri mkubwa wa mafuta ikiwemo Sudan ya Kusini, Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Misri ni mwangwi ambao Tanzania haipaswi kukaa
kimya kama kinara wa ukombozi katika nchi za Afrika.
Dk. Shao alikuwa akihubiri katika ibada iliyofanyika katika Usharika wa
Moshi mjini.
“Asilimia 73 ya Wakristo duniani kote leo jana) wanaadhimisha kumbukumbu
ya kuzaliwa Yesu Kristo, lakini wakati tunashangilia na kufurahi kwa kula na
kunywa, kila kona ya nchi,wenzetu wanaendelea kufa huko Sudan ya Kusini,Kongo na
Misri kutokana na machafuko ya kisiasa na ulafi wa madaraka ambao tuna kila
sababu ya kuomba yasiendelee kuua maelfu ya wanadamu wenzetu,” alisema Dk.
Shao.
Kuhusu hatua ambazo zinapaswa kuchukuliwa na mataifa kwa ajili ya kuepusha
dhahama hiyo, askofu huyo alisema bila ya kujali ni dhehebu gani mtu anakoabudu,
watanzania kwa ujumla wake wanapaswa kuweka pembeni itikadi zao na kuomba
waafrika wenzetu waondoke katika mahangaiko na mateso yanayotokana na siasa hasi
za kung’ang’ania madaraka.
Paroko Msaidizi wa Parokia ya Kanisa Katoliki Sombetini, jijini Arusha,
Padre Peter Shibale, alisema kuwa inasikitisha kuona baadhi ya viongozi wa
Kikiristo wanaacha kufuata nyayo za Kristo na wanaanza kurubuniwa na baadhi ya
wahubiri wanaotoa mahubiri yanayokwenda kinyume na ya Yesu Kristo.
Akihubiri kwenye Kigango cha Utatu Mtakatifu Kwamurombo, alisema wahubiri
wanaopotosha wanadai wanatoa wokovu.
“Wokovu mwenye kuutoa ni bwana Yesu Kristo pekee na siyo mwingine, hivyo
tusiyumbe na tusimame imara katika makanisa yetu,” alisema Padre Shibale.
Padri Leonard Mariva wa Kanisa Katoliki la Bikira Maria Consolata Parokia
ya Mshindo mjini Iringa, aliwataka waumini kuendelea kuiombea dunia ili
yasitokee machafuko ya vita, matetemeko,utoaji wa mimba ovyo na mauji ya
kupigania mali.
Alisema siku hizi machafuko kama hayo yametokea na watu wengi kupoteza
maisha yao, hivyo tuna kila sababu za kumuomba machafuko kama haya yasitokee
tena.
Imeandikwa na Jimmy Mfuru, Leonce Zimbandu, Mary Geofrey, Dar;
Augusta Njoji na Peter Mkwavila, Dodoma; Ashton Balaigwa, Morogoro; Godgrey
Mushi, Moshi; Cynthia Mwilolezi, Arusha; George Tarimo Iringa na Daniel Limbe,
Geita.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment