Na Mhariri
Maoni ya Katuni
Wakati serikali na wadau hususani mashirika ya wanaharakati wakielekeza
jitihada kati kupambana na vitndo vya ukatili mbalimbali wa kijinsia, bado
matukio hayo yanaendelea kufanywa na watu ambao ni wakatili.
Kuna matukio mengi ya ukatili wa kijinsia ambayo yamekuwa yakipingwa na
kupigwa vita na makundi hayo. Hata hivyo, matukio ya ukeketaji yanaonekana
kuendelea kushamiri kwa kasi kubwa na ya kutisha.
Takwimu zilizotolewa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto
zinaonyesha kuwa matukio ya ukeketeji wanawake na watoto yako juu kwa mfano,
mkoa wa Manyara bado unaongoza kwa ukeketaji kwa asilimia 71 huku mkoa wa Tanga
ambao una unafuu ni kwa asilimia 20. Mikoa mingine ni Dodoma asilimia 64,
Arusha 59, Singida 51, Mara 40 na Morogoro 21.
Kwa mujibu wa takwimu hizo, wanawake wenye umri wa miaka 15 hadi 49 kwa
asilimia 44 wamefanyiwa ukatili na wenzi au waume zao huku asilimia 15 ya umri
huo wanakeketwa.
Kinachodhihirisha kwamba matukio ya ukeketaji wa wasichana na watoto wa
kike bado katika kiwango cha juu, ni taarifa katika vyombo vya habari wiki
iliyopita kwamba wanawake zaidi ya 20 walikamatwa mkoani Kilimanjaro kwa
kujihusisha na kufanya tohara ya wasichana na watoto wa kike.
Wanawake hao maarufu kama ngariba, walitarajiwa kufikishwa mahakamani wiki
hii kwa ajili ya kusomewa mashitaka kuhusu kufanya tohara hiyo ambayo ni kinyume
cha sheria na ukiukaji wa haki za binadamu.
Hatutaki kulizungumzia suala hili kwa kuwa limeshaingia katika hatua za
vyombo vya dola, lakini hiyo ni ishara kwamba matukio ya ukeketaji ambayo
yanashika kasi na jitihada za dhati zinapashwa kuchukuliwa kwa lengo la
kuyapunguza kama siyo kuyamaliza kabisa.
Ziko hatua mbalimbali zinazoweza kuchukuliwa na kusaidia kupambana na
vitendo hivyo. Moja ya hatua hizo ni kutoa elimu kwa jamii ili ielewe athari
zitokanazo na ukeketaji, hivyo wazazi hawatakubali watoto wao wakeketwe.
Kadhalika, elimu inahitajika kutolewa kwa ngariba ili waache kukeketa
watoto. Elimu hiyo inaweza kuifikia jamii kubwa na kwa haraka ikiwa viongozi wa
dini watatumika kwa kuwa wako karibu na jamii na wana ushawishi mkubwa kwa
waumini wao.
Mbali na elimu, hatua za kisheria zinapaswa kuchukuliwa kwa maana ya
kuwasaka na kuwafikisha vyombo vya sheria wale wote ambao watabainika
kujihusisha na ukeketaji ili liwe fundisho kwa wengine.
Wakati hatua hizo zikichukuliwa, makundi ya kijamii hayana budi kushinikiza
kurekebishwa kwa baadhi ya sheria kutungwa mpya ambazo zitasaidia kudhibiti
vitendo hivyo.
Kwa bahati nzuri, serikali imeonyesha nia kwamba iko tayari kuzifanyia
marekebisho baadhi ya sheria ili kukabiliana na kasi kubwa ya vitendo vya
ukatili wa kijinsia.
Hivi karibuni Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto ilisema
inaendelea na jitihada mbalimbali ikiwamo kufanyia marekebisho sheria na kuweka
sera, kuandaa mpango ili kusaidia kupunguza ukatili na kuunda kamati ya kitaifa
ya kupinga ukatili wa aina zote.
Kwa kufanya hivyo, ni matarajio yetu kuwa zikitungwa sheria nzuri na
zinazokwenda na wakati, vitendo viovu vinavyofanywa na baadhi ya watu dhidi ya
ukatili wa kijinsia na haki za binadamu kwa ujumla vitakoma kwa kuwa wahusika
wataogopa mkono wa sheria.
Tunaamini kwamba ahadi hiyo pamoja na nyingine ambazo serikali imekuwa
inazitoa kupitia Wizara ya Katiba na Sheria zitatekelezwa na kuinusuru jamii
yetu kuondokana na mila potofu ukiwamo ukeketaji.
Kwa upande wake, mashirika ya wanaharakati nayo hayana budi kubuni na
kutekeleza miradi ya kudhibiti ukeketaji. Hata hivyo, baadhi ya mashirika hayo
kama Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa) kupitia mradi wa
GEWE ll kimehamasisha vita dhidi ya ukatili wa kijinsia ukiwamo ukeketaji.
Ushirikiano baina ya serikali, asasi za kiraia na jamii kwa ujumla
utasaidia kupunguza matukio ya ukeketaji na mengine ya ukatili wa kijinsia
ambayo kwa kiasi kikubwa yanawanyima wanawake na watoto wa kike haki zao kama
binadamu.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment