NA CYNTHIA MWILOLEZI
21st December 2013
Ndege aina ya Boeing 767 ya Shirika la Ndege la Ethiopia, hatimaye jana imefanikiwa kuruka salama kwenye uwanja wa ndege wa Arusha na kushangiliwa na mamia ya wakazi wa Jiji hilo waliofika kushuhudia.
Ndege hiyo yenye uwezo wa kubeba abiria 300, ambayo ilitua kwa dharura uwanja mdogo wa Arusha Desemba 18, ilianza kupasha moto saa 11:40 na ilipofika saa 11:47 asubuhi iliruka kuelekea uwanja wa KIA.
Kitendo hicho cha kuruka salama, kilishangiliwa na wananchi waliofurika uwanjani hapo kwa kupaza sauti kwa shangwe, huku baadhi ya wafanyakazi wa uwanjani hapo na wakaguzi waliofika kuikwamua ndege hiyo, wakionekana kukumbatiana kwa furaha.Ndege hiyo yenye uwezo wa kubeba abiria 300, ambayo ilitua kwa dharura uwanja mdogo wa Arusha Desemba 18, ilianza kupasha moto saa 11:40 na ilipofika saa 11:47 asubuhi iliruka kuelekea uwanja wa KIA.
Kilichoshangaza watu ni jinsi uwanja huo ulivyo mdogo, lakini rubani wa ndege hiyo ambaye hajafahamika mara moja jina lake, aliweza kuruka juu kabla ya kumaliza robo ya uwanja.
Baadhi ya mashuhuda waliofurika pembeni mwa uwanja huo kushudia ndege hiyo ni pamoja na raia wa kigeni, aliyejitambulisha kwa jina la Peter Swan, ambaye alisema ameacha kazi zote ili aone bahati nasibu ya ndege hiyo kuruka.
"Kweli kama rubani atafanikiwa kuruka anastahili zawadi na natamani sana nimwone rubani huyu na atapata umaarufu mkubwa," alisema Peter.
Naye Mkurugenzi wa viwanja vya ndege vidogo Tanzania, Thomas Haule, alisema anamshukuru Mungu ndege hiyo kuruka salama na saa 6:05 mchana ilikuwa imetua Uwanja wa KIA.
Alisema kuwa tukio la ndege kubwa kutua uwanjani hapo ni la kwanza na la kipekee, hivyo liliwapa wasiwasi mkubwa kama itafanikiwa kuruka.
"Kwa ushirikiano wa serikali ya mkoa, watu wa shirika la ndege toka Ethiopia na wadau wote wa ndege nchini, tumeshukuru kuwezesha ndege hii kuruka salama,"alisema Haule kwa furaha.
Alisema mbinu kubwa iliyotumika kurusha hapo ni ya kisayansi zaidi.
Aidha alisema pamoja ndege hiyo kuwa na uzito wa tani 300, lakini uwanja huo umeweza kumudu uzito huo, hivyo inaonyesha miundo mbinu ya uwanja huo ni mizuri.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment