Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Saturday, December 21, 2013

Operesheni Tokomeza: Bunge latikisika

NA JOHN NGUNGE

21st December 2013


  Unyama, mateso, ukabakaji, mauaji vyatawala
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira kuhusu tathmini ya matatizo yaliyotokana na Operesheni Tokomeza, James Lembeli, akipongezwa na wenzake Dodoma jana.
Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira kuhusu tathmini ya matatizo yaliyotokana na Operesheni Tokomeza, imefichua unyama, mateso, mauaji ya binadamu na mifugo na imesema viongozi wa kisiasa na serikali waliingilia utekelezaji wake.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, James Lembeli, alilieleza bunge kuwa agizo la kuwataka wahusika wa operesheni hiyo kutowagusa viongozi wa kisiasa wa ngazi zote.

“Kauli hiyo ilitafsiriwa kuathiri utekelezaji wake kwa kubagua Watanzania katika makundi ya viongozi na wananchi wa kawaida…hivyo basi, Bunge linaazimia kwamba Serikali ihakikishe kuna uwajibikaji wa pamoja pale inapoamua kutekeleza jambo la kitaifa kama Operesheni Tokomeza,” alisema.

Alisema ingawa lengo la operesheni lilikuwa ni kupambana na vitendo vya ujangili dhidi ya raslimali za taifa, utekelezaji wake ulikumbwa na mateso dhidi ya watuhumiwa yaliyosababisha maumivu, kupata ulemavu wa kudumu na hata wengine kupoteza maisha yao.

Ripoti hiyo imewataja waliokumbwa na dhahama hiyo hadi kufa ni Emiliana Gasper Maro wa Gallapo – Babati na mzee mmoja wa umri wa miaka 70 aliyeuawa kwa kupigwa risasi tatu.

Alisema katika operesheni hiyo nyumba za wananchi zilichomwa moto, mifugo kuuawa kikatili kwa kuchomwa moto na kupigwa risasi kama vile, ng’ombe 60 kuuawa kwa kupigwa risasi. Alisema askari waliotuhumiwa kukiuka taratibu walikataa kutoa ushirikiano wa kutosha pale walipohitajika na Kamati ya Bunge kufanya hivyo.

Kuhusu hujuma dhidi ya operesheni hiyo, alisema kulikuwepo na mamluki miongoni kwa washiriki kama vile kukamatwa kwa askari polisi na askari wanyamapori wakisindikiza gari lenye meno ya tembo na gari la Serikali kutumika kusafirisha meno ya tembo.

Alisema vyombo vya habari vilitumika kuvuruga operesheni kwa kueneza propaganda zilizolenga kushawishi wananchi kupinga operesheni hiyo na baadhi ya wamiliki wa silaha kutuhumiwa kutoa silaha zao ili zitumike kwa ajili ya vitendo vya ujangili.

WALIOTESWA WANENA KWA KAMATI
Katika mahojiano ya kamati na waathirika wa operesheni hiyo, ilibaini watuhumiwa walipekuliwa, kudhalilishwa na baadhi kutojulikana walipo.
Alisema baadhi ya wananchi wakiwamo viongozi, madiwani na wenyeviti wa vijiji na vitongoji na watumishi wa serikali walikamatwa na kudhalilishwa mbele ya wananchi wanaowaongoza.

“Baadhi ya watuhumiwa waliokamatwa walikuwa hawajulikani walipo hadi kamati ilipozuru maeneo hayo.

“Waliokamatwa walidai kudhalilishwa mbele ya wanafamilia kwa kupewa adhabu wakiwa uchi na wanawake kushikwa sehemu za siri bila ridhaa yao,” alisema na kutoa mfano wa Ali Nyenge (38) wa Kata ya Iputi, wilayani Ulanga alidai kuvuliwa nguo, kumwagiwa maji yaliyochanganywa na chumvi na kuchapwa viboko huku mwanae wa kiume (11) akishuhudia.

Pia alisema alilazimishwa kuchora picha ya chatu kwa kutumia wembe kwenye paja lake.

“Vile vile, Neema Moses wa Babati alidai kuvuliwa nguo na kulazimishwa afanye mapenzi na wakwe zake na pia kuingizwa chupa sehemu zake za siri,” alisema. Aidha alisema, baadhi ya akina mama walidai kubakwa na kulawitiwa kama vile katika Kata ya Iputi, wilayani Ulanga, mwanamke mmoja alidai kubakwa na askari wawili wa operesheni hiyo muda wa usiku.

Pia alisema mama mmoja mkazi wa Kata ya Matongo wilayani Bariadi, alibakwa na askari watatu wa operesheni hiyo huku akiwa ameshikiwa mtutu wa bunduki. Alisema watuhumiwa waliokamatwa walifanyiwa upekuzi bila kuhusisha viongozi wa serikali za maeneo husika na kutokuwepo kwa mashahidi na hati za upekuzi. Aliwataja watu hao kuwa ni Abdallah Pata, Flora Mwarabu wa Kata ya Iputi wilayani Ulanga na Elias Cosmas Kibuga wa Gallapo Babati walipekuliwa bila kufuata utaratibu.

Lembeli alitaja pia ukatili na udhalilishaji katika kambi za mahojiano ambapo Diwani wa Kata ya Sakasaka wilayani Meatu, Peter Samwel, alidai kuadhibiwa akiwa mtupu kwa kupewa adhabu za kijeshi kama kuning’inizwa kichwa chini miguu juu, kupigwa kwa vyuma na kulazimishwa kufanya mapenzi na mti.

Alisema kutokana na ukatili uliopitiliza, baadhi ya kambi za mahojiano zilipewa majina kama vile Guantanamo (Ruaha), Goligota (Ngorongoro), Duma na Andajega (Serengeti). Kuhusu upotevu wa mali za watuhumiwa na faini zisizoeleweka, alisema baadhi ya watuhumiwa walipoteza mifugo, mali na fedha zao.

Alisema kwa mfano, katika Wilaya ya Ulanga, Kata ya Iputi mwananchi mmoja alidai kuporwa sanduku la VICOBA lenye Shilingi laki 750,000 pamoja na simu ya mkononi.
Alimtaja pia Musa Masanja wa Sakasaka wilayani Meatu, alidai kuporwa Shilingi 300,000 pamoja na simu mbili za mkononi na askari hao.

WATUHUMIWA KUTESWA NA KUUMIZWA
Alisema baadhi ya watuhumiwa walidai kupigwa na kuumizwa na askari wa operesheni hiyo na wengine kupata ulemavu wa kudumu ambapo alitoa mfano katika Wilaya ya Itilima, kijiji cha Mbogo ambapo Sita Rumala alidai kupigwa na kuvunjwa mkono ambao aliwaonyesha mkono uliokuwa umefungwa bandeji ngumu.

Wengine aliwataja kuwa ni Diwani Peter Samwel Ndekija wa Kata ya Sakasaka, wilayani Meatu, aliyedai kupigwa na kuumizwa vibaya mgongoni na alionesha kwa wajumbe wa kamati makovu aliyopata.

Vile vile alisema Munanka Machumbe (24) ambaye ni bubu alipigwa risasi tatu zilizomjeruhi mapajani na kuharibu sehemu za siri wakati akijaribu kuwahoji askari wa operesheni kwa ishara sababu ya kumtesa baba yake. Aidha alisema katika tukio lingine Sheikh Mkuu wa Wilaya ya Ulanga, Ali Mohammed (70) aishiye kijiji cha Iputi alidai kurushwa kichura na kutandikwa bakora na askari hao.

Mwingine ni Nyasongo Magoro Serengeti wa Kata ya Majimoto Wilaya ya Mulele, alidhalilishwa mbele ya wananchi wake.
CHANZO: NIPASHE

No comments :

Post a Comment