Na Khatib Suleiman
WAZIRI wa Biashara wa Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui amesema kazi ya uchumaji wa zao la karafuu, inaendelea vizuri Kisiwani Pemba, na tayari tani 1,500 za zao hilo zimenunuliwa kutoka kwa wananchi.
Amesema lengo la ZSTC ni kununua karafuu zaidi ya tani 4,500 kutoka kwa wananchi katika msimu huu, kutokana na kazi ya uchumaji wa zao hilo inavyoendelea, inatarajiwa kuvuuka lengo.
Mazrui amesema serikali imejipanga kuhakikisha kwamba inanunua karafuu zote kutoka kwa wananchi kwa malipo taslimu bila kuwasumbua, bila kuwakopa:
“Serikali imejizatiti kununua karafuu zote za wananchi kwa malipo taslimu wala haina nia ya kuwasumbua wala kuwakopa,” alisema Mazrui.
Alifafanua kuwa serikali imeimarisha vituo vyake vya kuuzia karafuu, na kwa upande wa Pemba, vituo vinne vipya vimejengwa, vikiwa na vifaa vyote muhimu kwa kazi hiyo.
Alitaka wananchi kuhakikisha wanauza karafuu zao kwa ZSTC na kuachana na tamaa ya kuuza karafuu kwa magendo ambayo huathiri uchumi wa Zanzibar.
Waziri huyo alisema wananchi hawaruhusiwi kuweka karafuu ndani ya nyumba zao. Na kwa mujibu wa sheria endepo mwananchi hajawa tayari kuuza karafuu zake, analazimika kuzipeleka ZSTC kwa kuhifadhi kwa njia ya usalama:
“Mwananchi haruhusiwi kuhifadhi karafuu ndani ya nyumba yake ‘sheria ya karafuu na uhifadhi wake ipo wazi’ kama hayuko tayari kuuza karafuu zake kwa wakati huu anatakiwa kuzipeleka ZSTC kuhifadhiwa hadi atakapoamua kuuza,” alisema Mazrui.
Kwa mujibu wa sheria hiyo mwananchi kama hajaamua kuuza karafuu zake, anatakiwa kuzipeleka kwenye maghala ya ZSTC, kuhifadhiwa kama utaratibu wa kuzuia kusafirishwa kwa magendo.
Biashara ya usafirishaji karafuu nje (maarufu magendo ya karafuu) ilishamiri sana kwenye miaka 1990/2000 hali hiyo imepungua, hasa tangu serikali kupandish maradufu bei ya karafuu.
Shirika la Biashara la Zanzibar (ZSTC) kwa msimu huu wa 2013/2014 linatarajia kutumia kiasi cha Sh79 bilioni kwa kununua zao hilo kutoka kwa wananchi, Unguja na Pemba..
Chanzo: HabariLeo
No comments :
Post a Comment