dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Wednesday, December 25, 2013

Pinda ang`ang`aniwa

NA MUHIBU SAID

25th December 2013


  CUF: Ni chanzo mateso Tokomeza Ujangili
  Ni kwa kutoa ruksa polisi kupiga raia
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda
Shinikizo dhidi ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, limezidi kupamba moto, baada ya Chama cha Wananchi (CUF) kuungana na wabunge kumtaka ajiuzulu au Rais Jakaya Kikwete amfukuze kazi kufuatia udhalilishaji na mauaji ya wananchi yaliyofanywa na vyombo vya dola wakati wa Operesheni Tokomeza Ujangili.
 
Tamko hilo, ambalo ni azimio la nne kati ya 20 yaliyopitishwa na Baraza Kuu la Uongozi wa CUF Taifa, lilisomwa na Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba, alipozungumza na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam jana.Alisema Baraza Kuu limefikia azimio hilo kwa madai kwamba Pinda ndiye chanzo kikuu cha udhalilishaji na mauaji hayo.
 
“Kauli yake ya ‘piga tu, tumechoka’ aliyoitoa ndani ya Bunge imehamasisha unyanyasaji wa wananchi unaofanywa na vyombo vya dola. Kwa hivyo, Waziri Mkuu anapaswa kujiuzulu kwa matukio haya. La sivyo, Rais amfukuze kazi,” alisema Profesa Lipumba.
 
 Alisema Baraza Kuu linapongeza Bunge kwa kukubaliana na mapendekezo yaliyotolewa na kamati ndogo ya Bunge iliyoongozwa na Mbunge wa Kahama (CCM), James Lembeli na kusababisha mawaziri watatu kuvuliwa nyadhifa zao na mmoja kujiuzulu mwenyewe.
 
 Hao ni Dk. Emmanuel Nchimbi (Mambo ya Ndani ya Nchi), Dk. David Mathayo (Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi), Shamsi Vuai Nahodha (Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa-JKT) na Balozi Khamis Kagasheki (Maliasili na Utalii).
 
“Kamati hii imetoa mapendekezo mazuri juu ya uhalifu na unyanyasaji waliofanyiwa wananchi,” alisema Profesa Lipumba.
 
WAHUSIKA WAFIKISHWE MAHAKAMANI
Alisema Baraza Kuu linaitaka pia serikali kuwachukuliwa hatua za kisheria, ikiwa ni pamoja na kuwafikisha mahakamani wale wote waliohusika na uvunjwaji wa haki za binadamu na unyanyasaji wa wananchi wakati wa operesheni hiyo.
 
WAATHIRIKA WALIPWE FIDIA
Alisema pia linaitaka serikali kutazama utaratibu wa kuwalipa fidia wananchi wote walioathirika na vitendo hivyo.
 
DK. SHEIN AMUIGE JK
Pia linamtaka Rais wa Zanzibar, Dk. Shein kuiga mfano wa Rais Kikwete katika kushughulikia kero zinazoibuliwa na vikao vya Baraza la Wawakilishi kwa kuwawajibisha mawaziri wanaohusika.
 
Alisema hiyo ni kama ambavyo Rais Kikwete amekuwa akifanya katika kuunga mkono hoja zinazoibuliwa na bungeni. 
 
SERIKALI ISITUMIE JWTZ
Alisema Baraza Kuu pia linaitaka serikali kutolitumia Jeshi la Ulinzi wa Wananchi wa Tanzania (JWTZ) katika kushughulikia masuala ya uvunjifu wa sheria katika maeneo mbalimbali ya nchi, badala yake kazi hiyo ifanywe na Jeshi la Polisi kwa mujibu wa taratibu za kisheria.
 
Alisema Jeshi la Polisi linapaswa kuongezewa uwezo wa kutimiza majukumu yake huku likiheshimu haki za kisheria za watuhumiwa.
 
“Jeshi la Wananchi liachiwe majukumu yake ya kulinda mipaka ya nchi yetu. CUF inaona kwamba si vyema kulitumia Jeshi letu la kulinda mipaka ya nchi katika operesheni zinazohusu uvunjaji wa sheria unaofanywa na wananchi,” alisema Profesa Lipumba.
 
Aliongeza: “Askari wa JWTZ hawana mafunzo ya kukamata mwananchi mwenye tuhuma za uhalifu bila kuvunja haki zake za kisheria.” 
 
MUUNDO WA MUUNGANO, MCHAKATO WA KATIBA
Alisema Baraza Kuu linaitaka serikali kusimamia kikamilifu mchakato wa katiba mpya ili ipatikane kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, kwani wananchi hawatakubali kuingia kwenye uchaguzi huo kwa kutumia katiba ya sasa, ambayo imekataliwa na Watanzania wengi waliotoa maoni kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
 
SERIKALI YA UMOJA WA KITAIFA
Profesa Lipumba alisema Baraza Kuu linamshauri Rais Kikwete kuunda serikali ya umoja wa kitaifa ili kusaidia kupatikana kwa katiba mpya katika kipindi hiki cha mpito.
 
Alisema uwapo wa serikali hiyo utarahisisha mjadala wa Bunge Maalumu la Katiba na kulifanya kuchukua sura ya kitaifa zaidi na hivyo kurahisisha upatikanaji wa katiba taifa kwa misingi ya utashi wa wananchi.
 
Profesa Lipumba alisema serikali ya umoja wa kitaifa itampa fursa rais kuteua Baraza la Mawaziri lililo imara na kuondokana na mawaziri wanaoonekana ni mizigo ili ashughulikie matatizo mazito yanayolikabili taifa, ikiwamo ongezeko la gharama za maisha, ukosefu wa ajira, kuporomoka kwa elimu, huduma hafifu za afya na maji safi na salama na ukosefu wa umeme wa uhakika. 
 
DAFTARI LA WAPIGAKURA
Alisema Baraza Kuu limesikitishwa na Daftari la Kudumu la Wapigakura kutoboreshwa tangu kumalizika uchaguzi wa 2010. 
 
DAFTARI LA ZANZIBAR
Alisema pia kuwa Baraza Kuu linaitaka serikali ya Zanzibar kutoa vitambulisho vya Mzanzibari mkaazi (Zan ID) na kuandikisha wananchi waliofikisha umri wa miaka 18 katika daftari la wapigakura.
Pia alivitaka vyama vyenye wabunge kuacha kupigania maslahi ya vyama vyao wakati wa mjadala wa Bunge Maalumu la Katiba. 
CHANZO: NIPASHE

No comments :

Post a Comment