Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Saturday, December 28, 2013

TANZANIA inatarajia kupata mgawo wa takribani shilingi bilioni 400 kutokana na kuza hisa za vitalu,no 1,3 na 4

TANZANIA inatarajia kupata mgawo wa takribani shilingi bilioni 400 kutokana na mauzo ya hisa yaliyofanywa na kampuni ya Ophir kwa kampuni ya Pavillion katika vitalu vya gesi vilivyopo nchini, Raia Mwema limeambiwa.
Kampuni ya Ophir inamiliki asilimia 40 ya hisa katika vitalu namba 1, 3 na 4 huku asilimia nyingine 60 ikimilikiwa na kampuni ya BG, lakini Ophir wameamua kuuza hisa zao 20, mwaka huu.
Mauzo ya hisa hizo yanatarajiwa kuiingizia Ophir kiasi cha dola bilioni 1.3 (shilingi trilioni mbili) na kutokana na mauzo hayo, Tanzania itapata kiasi cha dola milioni 260 (shilingi bilioni 400) kama kodi.
Hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa Tanzania kufaidika na mauzo ya hisa za rasilimali zake kupitia Kodi ya Ongezeko la Mtaji (Capital Gain Tax) ambayo ilipitishwa na Bunge mwaka jana.
Kodi hiyo ilipitishwa na Sheria ya Fedha (Finance Act) ya mwaka 2012 baada ya kuwasilishwa kama mapendekezo binafsi na Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CHADEMA), Zitto Kabwe na kisha Bunge kuridhia.
Katika miaka ya nyuma, Tanzania haikuwa ikifaidika na mauzo yoyote ya hisa kwa makampuni yanayouziana rasilimali zake kwa sababu Kodi hiyo ya Ongezeko la Mtaji haikuwepo.
Kwa sababu mauzo hayo ya hisa yana thamani ya dola hizo bilioni 1.3, serikali ya Tanzania inatakiwa kupata asilimia 20 ya kiasi hicho ambayo ni dola milioni 260.
Akizungumza na Raia Mwema wiki hii, Naibu Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene, alisema wanatarajia kupata fedha hizo wakati wowote mauzo hayo yatakapopitishwa.
“Inategemea na namna hao wanaouziana hisa watakavyokubaliana lakini sisi tunafahamu tu kwamba wakimalizana, yetu itakuwa asilimia 20. Kwa vyovyote vile, inaonekana mauzo yanaweza kufanyika kwenye robo ya kwanza ya mwaka ujao wa 2014,” alisema Simbachawene.
Ophir ina makao yake makuu katika miji ya London, Uingereza na Perth nchini Australia na kwa mujibu wa tovuti yake, ilianzishwa mwaka 2004. Kampuni ya Pavillion Energy inamilikiwa na serikali ya Singapore.
Vitalu ambayo vimeuzwa katika uuzianaji huo vinaelezwa kuwa na ujazo wa mita za ujazo trilioni 15 na mauzo hayo pia yameenda sambamba na uuzaji wa hisa nyingine 17.6 katika makampuni yatakayokuwa yakifanya biashara za gesi hiyo hapa nchini.
Kwa mujibu wa Simbachawene, makampuni hayo matatu ni Ruvuma Pipeline Company Limited, Mzalendo Gas Processing Company Limited na Fahari Marketing Limited.
Simbachawene alisema nia ya serikali kwa sasa ni kutaka kutumia fedha hizo kwa ajili ya kulipa madeni na kuliboresha Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), ingawa alisema itategemea pia na mahitaji mengine yatakayokuwepo wakati fedha hizo zitakapopatikana.
“Hizi ni fedha za Watanzania wote na si za wizara yetu pekee. Tunataka kuliwezesha shirika letu la umeme ili lifanye kazi vizuri na kuboresha upatikanaji wa nishati ya umeme kwa watu wengi zaidi.
“Hata hivyo, sisemi kwamba ni hela zote zitatumika kwa kazi hiyo au la lakini kuna mawazo hayo. Mambo mengine serikali itaamua kutokana na wakati fedha hizo zitakapopatikana. Huwezi kujua kutakuwa na nini wakati huo,” alisema Naibu Waziri huyo.
Alisema kwa miaka ya nyuma, Tanzania isingepata kitu kutokana na sheria zilizokuwepo na akasema serikali itajitahidi kuboresha sheria zake ili kuhakikisha inafaidika na utajiri uliokuwepo.
Mmoja wa wachambuzi wa masuala ya gesi aliyehojiwa na mtandao wa Bloomberg kuhusiana na uuzaji huu wa hisa, Tony Regan wa kampuni ya Tri Zen Inc alisema uamuzi wa kununua hisa hizo ni wa “roho ngumu” kwa sababu Tanzania ni eneo bichi kwenye sekta ya gesi.
“Mpaka sasa hakuna sheria rasmi iliyopitishwa kuhusiana na masuala ya gesi na hivyo Singapore inaingia katika eneo bichi kabisa katika sekta hii. Kumbuka pia kwamba gesi ya kwanza itaanza kuvunwa mwaka 2020 kutoka kwenye vitalu hivyo na utaona kwamba huu ni uamuzi mzito,” alisema.
Chanzo: RaiaMwema

No comments :

Post a Comment