NA MWANDISHI WETU
4th January 2014
Hafla hiyo ilikwenda sambamba na ufunguzi wa maonyesho ya Miaka 50 ya Mapinduzi na kushuhudiwa na Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad na Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi ambao pia walikabidhiwa sarafu hiyo.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa Sarafu hiyo na Naibu Gavana wa Benki Kuu, Juma Reli, Dk. Shein aliupongeza uamuzi wa benki hiyo wa kutoa sarafu hiyo maalum yenye thamani ya Sh. 50,000 katika maadhimisho hayo.Alisema uamuzi huo ni wa kimaendeleo na kubainisha kuwa yeye na viongozi wenzake wanathamini sana sarafu hiyo hivyo hawatakuwa tayari kuiuza hata kama thamani yake itapanda ili iendelee kuwa kumbukumbu sahihi ya maadhimisho hayo.
Akizungumza katika hafla hiyo Naibu Gavana, alisema kukabidhiwa kwa sarafu hiyo kunaashiria uzinduzi rasmi wa uuzaji wa sarafu hiyo katika matawi yote ya Benki Kuu nchini.
Alisema sarafu hiyo maalum ni kwa ajili ya kumbukumbu tu ya miaka 50 ya Mapinduzi na imefanya hivyo kama ilivyokuwa kwa miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara.
Alisema sarafu hiyo iliyotengenezwa kwa madini ya fedha haitatumia katika matumizi ya kawaida ya fedha lakini thamani yake baada ya muda inaweza kupanda na anayeimiliki anaweza kuiuza na kuhamasisha wananchi kuzichangamkia kwani ziko 3,000 tu.
Sarafu hiyo kwa mujibu wa Naibu Gavana upande wake mmoja una picha ya Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Mzee Abeid Amani Karume na upande wa pili kuna nembo ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Maelezo ya Miaka 50 na Mapinduzi ya Zanzibar.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment