NA RAHMA SULEIMAN
13th January 2014
Sherehe hizo, ambazo kilele chake kilihitimishwa katika Uwanja wa Aman, mjini Unguja, kwa kuhutubiwa na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) na Baraza la Mapinduzi la Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein, zilihudhuriwa marais wastaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa.
Viongozi wengine wakuu waliohudhuria ni Rais wa Uganda, Yoweri Museveni; Rais wa Comoro, Dk. Ikililou Dhoinine; Naibu Waziri wa Uchukuzi wa Kenya, Ali Hassan Joho; na Mjumbe aliyemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Watu wa China, Jiang Weixin.
Wengine ni Makamu wwa Rais; Dk. Mohamed Gharib Bilal; Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mizengo Pinda; Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Malim Seif Shariff Hamad; Mjane wa Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere, Mama Maria Nyerere, mawaziri, naibu mawaziri, majaji wakuu na spika, mabalozi, wawakilishi wa mashirika ya kimataifa, viongozi wa serikali na vyama vya siasa na kiraia.
Sherehe hizo zilianza muda mfupi baada ya Rais Shein kuwasili katika viwanja hivyo akiongozwa na msafara wa pikipiki.
Rais Shein alipokewa na wananchi kwa shangwe na nderemo akiwa katika gari la wazi kabla ya kupokea salamu za utii za rais na kukagua gwaride lililoandaliwa na vikosi vya ulinzi na usalama.
Baadaye, alipokea maandamano kutoka taasisi mbalimbali, zikiwamo za serikali na zisizo za kiserikali pamoja na mandamano ya wananchi kutoka mikoa mitano ya Unguja na Pemba.
Sherehe hizo zilipambwa na vijana wa halaiki 2,235 kutoka shule za msingi, ambao walionyesha matukio mbalimbali na vitu vinavyoonesha mambo yanayotokana na Mapinduzi.
Kabla ya hapo, sherehe hizo zilirindima mji mzima wa Unguja usiku wa kuamkia jana, huku kila kona ya mji ikiwa imepambwa kwa mabango yenye picha ya Rais wa kwanza wa SMZ, Abeid Amani Karume.
Akihutubia sherehe hizo, Shein aliwahakikishia wananchi kuwa SMZ itaendelea kuimarisha Muungano na kuiunga mkono Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Alisema kwa kuwa tume hiyo imeshatimiza wajibu wake, hatua zilizobaki zitakamilishwa kwa kuzingatia sheria ili kupata katiba mpya iliyo bora.
Alimpongeza Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Joseph Warioba na wajumbe wake kwa kazi kubwa waliyoifanya kukamilisha rasimu ya pili ya katiba mpya waliyoikabidhi kwa Rais Kikwete na kwake.
Alisema katika kipindi cha miaka 50 iliyopita Zanzibar imepita katika mifumo miwili ya kisiasa na kidemokrasia kwa mujibu wa katiba ya nchi na mara tu baada ya Mapinduzi ya mwaka 1964 ilikuwa na mfumo wa chama kimoja.
Shein alisema mfumo wa vyama vingi vya siasa umepanua demokrasia kwa kuwapa fursa wananchi kujiunga na chama chochote cha siasa.
Alisema katika kuimarisha umoja na mshikamano miongoni mwa wananchi, mwaka 2010 Zanzibar ilifanya mabadiliko ya 10 ya katiba yake ya mwaka 1984 iliyoiwezesha vyama vya siasa vyenye uwakilishi katika Baraza la Wawakilishi kushirikiana katika kuongoza nchi.
Alisema hatua hiyo iliiwezesha Zanzibar kuunda serikali ya umoja wa kitaifa, ambayo kwa kiasi kikubwa imesaidia kuimarisha umoja na mshikamano na kuchangia kuongeza kasi ya maendeleo.
Alisema katika kipindi cha miaka 50 Dk. Shein kabla ya mapinduzi Zanzibar elimu ilikuwa ikitolewa kwa ubaguzi na ilikuwa ya kulipia lakini baada ya mapinduzi elimu ilitangwazwa bure bila ya ubaguzi wowote.
“Watoto wa wananchi walio wengi ambao ni maskini hawakuwa na uwezo wa kupata elimu lakini baada ya mapinduzi watu wote wameweza kupata elimu,” alisema.
Aidha alisema wanyonge hawakuwa na uwezo wa kuishi kwenye nyumba bora lakini baada ya mapinduzi serikali iliamuwa kuwajengea wananchi makaazi bora ya kisasa bila ya ubaguzi wowote.
Alisema Zanzibar ina kila sababu ya kujivunia matunda ya mapinduzi kwani kila Nyanja huduma za kijamii zimeimarishwa na wananchi wanazitumia fursa hiyo katika kuendesha maisha yao ya kila siku.
Aliwahakikishia wananchi kwamba serikali ya SMZ itaendelea kutekeleza wajibu wake wa kikatiba na kisheria kwa kulinda amani,utulivu,mali na maisha ya watu.
Shein, alisema mafanikio makubwa ya kiuchumi, kijamii na kisiasa yamepatikana Zanzibar katika miaka 50 ya Mapinduzi visiwani humo.
UCHUMI
Alisema kabla ya Mapinduzi, enzi za wakoloni (Sultani) hali ya uchumi pamoja na bajeti ya serikali kwa jumla vilikuwa havijulikani kwa wananchi kutokana na utawala huo kuvifanya vitu hivyo kuwa kuwa ni siri yake tofauti na hivi sasa.
Dk. Shein alisema hadi utawala wa wakoloni unapinduliwa, hali ya uchumi wa visiwa hivyo ilikuwa ni duni ukilinganisha na sasa.
Alisema hivi sasa mapato ya serikali yameongezeka kufikia Sh. bilioni 56.2, huku uchumi ukikua kwa asilimia saba na kwamba, wanatarajia mwaka huu utaongezeka kufikia asilimia 7.5.
ELIMU
Pia alisema wakoloni walipoondoka, waliiacha Zanzibar ikiwa na shule za msingi 62, lakini sasa zimeongezeka kufikia 342 zikiwa na wanafunzi 247,000.
Alisema vilevile, waliviacha visiwa hivyo vikiwa na shule za sekondari nne tu, tofauti na sasa, ambazo zimeongezeka kufikia 18,496.
Rais Shein alisema mbaya zaidi walipoondoka waliiacha Zanzibar ikiwa haina hata chuo kimoja.
Lakini akasema kwa kipindi cha miaka 50, visiwa hivyo sasa vina vyuo vitatu, huku Chuo Kikuu cha Zanzibar kikiwa kimeanzisha elimu ya udaktari.
AFYA
Alisema katika sekta ya afya, Zanzibar imepiga hatua kubwa kutokana na Rais wake wa kwanza, marehemu Abeid Amani Karume, kuahidi kutoa huduma za afya bila malipo.
Rais Shein alisema wakoloni waliiacha Zanzibar ikiwa ina vituo 36 vya afya, lakini sasa vimeongezeka kufikia 134.
Alisema mafanikio hayo yamesaidia kwa kiasi kikubwa kuwafanya wananchi wasiende masafa ya kilomita tano kutafuta huduma za afya na kwamba, hivi sasa wanatarajia kiwango cha masafa kitapungua hadi kilomita tatu.
Pia alisema uwezo wa serikali wa kusambaza dawa umeongezeka kati ya mwaka 1990 na 2005 kufikia asilimia 12, huku kiwango cha ugonjwa wa malaria kikishuka kufikia asilimia 0.3
Alisema mbali na hayo, miongoni mwa kazi kubwa zilizofanywa na marehemu Karume enzi za uongozi wake visiwani humo, ni pamoja na kuwajengea Wazanzibari makazi mapya, huku akiwa ameacha jumla ya maghorofa 2,928 yamejengwa.
Rais Shein alisema hivi sasa Wazanzibari wana uwezo wa kujenga nyumba za kisasa tofauti na zile za udongo na makuti.
Alisema barabara zilizoachwa na wakoloni hazikuwa za viwangoi, lakini hivi sasa serikali imejenga wastani wa kilomita 680 zote zikiwa za lami.
Rais Shein alisema mafanikio mengine yaliyopatikana ni katiba ya Zanzibar kufanyiwa marekebisho na kuleta Serikali ya Umoja wa Kitaifa, ambayo imeanza vizuri.
LEO MAPUMZIKO
Dk. shein alitangaza kuwa leo ni siku ya mapunziko kwa taasisi zote za serikali za Zanzibar na Tanzania bara baada ya kufanya kazi kubwa ya kutimiza maadhimisho ya miaka 50 ya mapinduzi tangu sherehe hizo zilipozinduliwa agosti 15 mwaka jana.
Awali, akimkaribisha Rais Shein kuhutubia, Makamu wa Pili wa Rais wa SMZ, Balozi Seif Ali Iddi, alisema sherehe za Mapinduzi za mwaka huu zimenoga kutokana na kuhudhuriwa na viongozi wakuu wa nchi za nje.
KAULI YA MUSEVENI
Mapema Rais Museven akiwasilisha salamu za wananchi wa nchi yake, alisema uhusiano kati ya Zanzibar, Tanganyika, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) siyo wa leo wala jana, bali ni wa zamani.
“Sisi Uganda tulikuwa hatutengenezi nguo za pamba, zote zilikuwa zinatoka hapa (Zanzibar) hata zile za mkononi. Tulikuwa hatutengenezi shanga, zote zilikuwa zinatoka hapa,” alisema Rais Museven.
Aliishukuru Zanzibar kwa msaada ilioutoa kwa Uganda, ambao alisema ulichangia kujikomboa.
Alisema Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere na Karume wamewaachia urithi wa vitu kadhaa, ambavyo anavijua kwa sababu aliwahi kuishi nchini.
Alivitaja vitu hivyo kuwa ni umoja, kutokuwa na ukabila, umoja wa Afrika uliosababisha Zanzibar na Tanganyika kuungana, ukombozi wa bara la Afrika na elimu.
Aidha, alisema amefurahishwa na kwenda kwake Zanzibar na Tanzania kuwa nchi mojawapo barani Afrika, ambayo haina matukio ya umwagaji wa damu.
Aliwatakia kheri Wazanzibari na kuwaomba waendelee kudumisha urithi wa wazee.
Alisema nchini Uganda amekuwa akipambana na mawazo tofauti ya watu baada ya kuvumbuliwa mafuta na madini mengi.
Museven alisema kumekuwa na kawaida kwa baadhi ya watu kuanzisha matatizo pindi mafuta na madini yanapogunduliwa katika nchi kwa kujiona kuwa wao ni bora kuliko wengine na hivyo, kusababisha machafuko. Hata hivyo, alitoa angalizo akisema ingawa maliasili ni utajiri, lakini watu ni utajiri mkubwa zaidi kuliko maliasili.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment