Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Wednesday, January 1, 2014

Wasomi wagawanyika kuhusu Serikali Tatu

Mhadhiri maarufu, Profesa Issa Shivji (kushoto) akizungumza jambo na mwanasiasa mkongwe, Sir George Kahama wakati wa hafla kukabidhi Rasimu ya Pili ya Katiba kwa Rais jijini Dar es Salaam juzi.Picha na Silvan Kiwale. 
Posted  Jumatano,Januari1  2014  saa 12:17 PM
KWA UFUPI
“Ingekuwa mimi ndiye mwenye maamuzi ya mwisho, ningependekeza muundo wa Serikali Moja tu kama tunataka kuufanya Muungano uwe wenye nguvu ya kiuchumi mbele ya mataifa mengine,” alisema Profesa Bee.
Dar na mikoani: Pendekezo la muundo wa Serikali Tatu lililomo katika Rasimu ya Pili ya Katiba, limewagawa wasomi na wanazuoni katika vyuo vikuu na taasisi mbalimbali za elimu ya juu nchini.
Baadhi ya wasomi waliohojiwa na waandishi wetu jana walisema pendekezo la Serikali Tatu litaimarisha Muungano kwani limezingatia matakwa ya wengi, huku baadhi wakitofautiana na wenzao kwa maelezo hatua hiyo ni kurudi nyuma na kuhatarisha kuvunjika kwa muungano.
Rasimu hiyo ambayo ilikabidhiwa juzi kwa Rais Jakaya Kikwete na Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba inapendekeza muundo wa Serikali Tatu, pendekezo ambalo linamaanisha kurejeshwa kwa Serikali ya Tanganyika.
Mwenyekiti wa Umoja wa Wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udomasa), Paul Loisulie alisema: “Vyote vilivyopo katika rasimu hiyo navikubali, lakini bado kuna majadiliano kuhusiana na uraia wa Zanzibar na Tanganyika.”
Alisema mjadala pia unahitajika juu ya gharama za kuendesha Serikali ya Muungano ambayo kwa mujibu wa rasimu ndiyo yenye dhamana ya kusimamia Idara ya Usalama wa Taifa na Polisi.
“Hapa sasa Serikali ya Tanganyika na ya Zanzibar zitabaki na nini kama Usalama na Polisi utakuwa chini ya Muungano?” alihoji.
Hata hivyo, alisema rasimu hiyo ya pili imekidhi kwa kiasi kikubwa mapendekezo ya wananchi... “Tume inahitaji pongezi, suala la Muungano linavuta hisia za watu wengi na litaendelea kuchukua sehemu kubwa ya mjadala, tunaomba Bunge la Katiba nalo lizingatie matakwa ya watu,” alisema Loisulile.
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (Sua), Dk Mikidadi Muhanga alisema licha ya pendekezo la Serikali Tatu kuwa la wananchi, muundo huo utazidisha gharama za uendeshaji wake.
“Kama nchi tulipaswa kuangalia uhalisia zaidi kuliko utashi wa wananchi. Kutakuwa na mahitaji makubwa ya fedha kwa ajili ya kuendesha Serikali Tatu tofauti na ilivyokuwa kwa Serikali Mbili,” alisema Dk Mikidadi.
Alisema kwa kuzingatia kuwa wananchi wengi wamependa muundo huo, basi wawe tayari kupokea changamoto zake na wasije lalama, wawe wavumilivu wakati watakapoanza kuonja uchungu wa gharama hizo.
Wapendekeza Serikali Moja
Mkuu wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Ushirika na Biashara Moshi (MUCCoBS), Profesa Faustine Bee alisema yangekuwa ni matakwa yake, angependekeza muundo wa Serikali Moja.
Hata hivyo, alisema kwa kuwa hisia za Watanzania wengi ni muundo wa Serikali Tatu na kama mapendekezo hayo yatapita, ni vyema Serikali ya Shirikisho iwe ndogo kukwepa mzigo wa gharama.
“Ingekuwa mimi ndiye mwenye maamuzi ya mwisho, ningependekeza muundo wa Serikali Moja tu kama tunataka kuufanya Muungano uwe wenye nguvu ya kiuchumi mbele ya mataifa mengine,” alisema Profesa Bee.
Kwa upande wake, Profesa Leo Donge wa chuo hicho alisema ikiwa mapendekezo ya Serikali Tatu yatapitishwa, Muungano ulioasisiwa kwa miaka mingi utakufa.
“Ule wasiwasi aliokuwa nao Nyerere (Julius), Baba yetu wa Taifa kuwa Serikali Tatu zitaua Muungano ndilo sasa linakuja… wasiwasi kuwa Muungano utakufa ni mkubwa zaidi kuliko kuimarika,” alisema.
Profesa Donge pia alionyesha wasiwasi kuwa kitendo cha Zanzibar kuachiwa kuwa nchi huru nje ya Muungano kunaweza kulifanya taifa hilo kuwa la Kiislamu jambo ambalo litaathiri Muungano.
Mhadhiri Mwandamizi katika Chuo Kikuu cha Nelson Mandela (Arusha), Dk Eliamani Laltaika alisema Serikali Tatu ni kinyume na mwelekeo wa dunia huku akitoa mifano ya mapendekezo ya kuimarishwa kwa umoja katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Ulaya (EU).
Badala yake, Dk Laltaika alisema Watanzania wanapaswa kufikiri kuwa na muundo wa Serikali Moja kama kweli wanahitaji muungano udumu.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Teofilo Kisanji, Mbeya, Stephen Chambanenge alisema kurejeshwa kwa Tanganyika ni kurudi nyuma katika Muungano.
Chambanenge alisema kilichotakiwa ni kuwa na nchi moja ya Tanzania pekee na siyo Serikali Tatu. “Ni afadhali mfumo wa Serikali Mbili uendelee kwani nchi nyingi zinazoungana kwa sasa zinakwenda kwenye Serikali Moja na siyo kuunda Serikali nyingi za umoja,’’ alisema.
Alisema Tanzania inapaswa kusonga mbele na siyo kurudi nyuma tena kuanza kuitafuta Tanganyika na kutahadharisha kwamba ipo siku yatakuja kutokea kama yale yaliyozikumba nchi za Ghana, Gambia na Guinea ambazo zilishindwa.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Saint Augustine (Saut), Mtwara, Charles Buteta alisema Serikali Tatu zitasababisha kuyumba kwa umoja, mshikamano na undugu baina ya wananchi wa Tanzania Bara na Zanzibar.
“Mwalimu (Nyerere) alikubali kuacha Tanganyika na Karume alikubali kuacha madaraka kwa sababu ya Muungano. Watanzania wanatakiwa wajiulize mwanzo tulijengaje muungano wetu, hapa utaona ni kwa namna gani tutajenga laana tusiporejea walipoanzia wazee wetu,” alisema Buteta na kuongeza:
“Tunapaswa kujiuliza kwamba itakuwaje kama kati ya marais watatu, tutawapata kutoka vyama tofauti, usimamizi wa Serikali hizo utakuwaje? Pia suala la idadi ya viongozi dhidi ya gharama za kuwatunza zitakuwaje?”
Waunga mkono Serikali Tatu
Profesa George Shumbusho wa Chuo Kikuu Mzumbe, alisema Tume ya Mabadiliko ya Katiba inastahili pongezi kwa kuzingatia maoni yaliyotolewa na wananchi na kutupilia mbali yale ya vyama vya siasa.
“Kitendo cha Tume ya Jaji Warioba kuyazingatia maoni ya wananchi na kuyaacha yale ya vyama vya siasa…. ni jambo la kujivunia,” alisema Profesa Shumbusho na kuongeza:
“Tume imekamilisha kazi ambayo wananchi walikuwa wakiisubiri hivyo ni wakati sasa kwa wajumbe watakaopata nafasi ya kuingia katika Bunge la Katiba kuhakikisha wanaweka mbele masilahi ya Taifa.”
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Profesa Tolly Mbwete alisema mapendekezo ya muundo wa Serikali Tatu hayana lengo la kuuvunja muungano, bali kuuboresha... “Yatasaidia kuuboresha… Bunge la Katiba linatakiwa kuweka mbele utaifa ili Katiba itakayopatikana iwe ya Watanzania wote.”
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Tumaini Makumira (Arusha), Dk Msafiri Mbilu alisema Serikali Tatu zitasaidia kuondoa kero za Muungano.
“Kuna wakati lazima kufanya uamuzi mgumu. Kung’ang’ania muundo wa Serikali Mbili ni kuhatarisha Muungano kwa sababu una kasoro zisizorekebishika ikiwamo Katiba ya Zanzibar inayoitambua kama nchi,” alisema Dk Mbilu.
Alisema tayari Zanzibar ina mamlaka ya mambo yasiyo ya Muungano huku ikiwa na katiba (inayoitambulisha kama nchi), bendera, wimbo wa Taifa na Bunge (Baraza la Wawakilishi), wakati Bara haina.
Alisema hoja ya gharama kubwa haina mashiko kwa sababu muundo unaopendekezwa utapunguza ukubwa wa Serikali kwa kuweka idadi maalumu ya wizara tofauti na sasa ambapo Rais ndiye anayeamua idadi ya wizara na mawaziri.
“Katiba siyo msahafu. Turuhusu Serikali Tatu na tukiona mfumo huo hautufai tutairekebisha kulingana na wakati na mahitaji,” alisema Dk Mbilu.
Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Raymond Mwaikasu alisema amefurahia kurejea kwa Tanganyika na kusema hilo lilikuwa miongoni mwa mapendekezo yake wakati wa kutoa maoni ya Katiba Mpya.
Jaji Mwaikasu alisema wabunge 75 wa Bunge la Jamhuri ya Muungano ni idadi inayotimilika hivyo Serikali ya shirikisho haitakuwa kubwa kwani mambo mengi yatafanywa na serikali washirika.
Mhadhiri wa SAUT, Stephen Dassu alisema lazima watu wakubali kubadili mtazamo kwani kama Serikali Mbili zilionekana zinafaa enzi hizo, mazingira ya sasa yamebadilika.
“Nyerere alifanya alichoona kinafaa kwa wakati ule kilikuwa sahihi, lakini kwa sasa hakifai tena, watu hao walioona kinafaa wametaka muundo mwingine. Hapa tunapaswa kukubaliana na mawazo yao kutokana na wakati kubadilika,” alisema Dasu.
 Imeandikwa na Ibrahim Yamola (Dar), Sharon Sauwa na Habel Chidawali (Dodoma), Frederick Katulanda (Mwanza), Daniel Mjema (Moshi), Peter Saramba (Arusha), Lauden Mwambona (Mbeya), Geofrey Nyang’oro (Iringa), Hamida Shariff (Morogoro) na Haika Kimaro (Mtwara).
 Chanzo: Mwananchi

3 comments :

  1. Profesa Donge hatujui mfahamike vipi? watu kama nyinyi ambao mnaokana ni wasomi kumbe hamna chochete kile! Kwanza iko wapi hiyo mamlaka kwa znz? Pili kivipi zanzibar itageuka kuwa nchi ya kiislamu itapokuru nje ya muungano? Basi Tanganyika vile2 itakuwa nchi ya kikiristo nje ya muungano! Mnajifanya wajuaji sana musitudanganye, kama znz ni mzigo hebu utuweni!

    ReplyDelete
  2. Hi issue ya Uislam kwa kweli ndio hasa kinachowaogopesha wengi hawa wanaojiita ETI WASOMI!!!???, Hawana lolote chuki zao kubwa ni waislam na uislam na waarabu. Ukitaka kuujua ubaya wa hawa watananyika (wadanganyika) lete issue ya waislam, wazanzibar au waarabu hapo utawaona nyoyo zao zilivyojaa chuki dhidi ya usilam.
    Kwanini huyu Donge asisime Tanganyika itakuwa nchi ya Kikristo?? Yeye kaona Zanzibar tuu, huko Tanganyika si mnasema kuna Makafiri kibao, sasa tena kwanini usiwe na wasiwasi wa kuna tanganyika litakuwa taifa la Kikiristo. Eti msomi, hata haielekei kuitwa msomi

    ReplyDelete
  3. Kwani kuna ubaya gani Zanzibar kuwa nchi ya kiislamu? Au tumuulize, Waislamu wa Tanganyika wana mnyima nini huyu Padre Donge Leo hivi sasa? Hebu atwambie kitu kwa mifano halisi.

    ReplyDelete