Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Wednesday, June 11, 2014

BAJETI: Sh11 bilioni za safari za Rais Kikwete zafyekwa

         

        

“Katika bajeti ya 2013/14 safari za Rais zilitengewa Sh15 bilioni lakini inaonekana fedha zilizotumika ni nyingi zaidi maana ndani ya miezi miwili tu zote zilikuwa zimemalizika,”.PICHA|MAKTABA 
Kwa ufupi
“Kama wananchi wanakula mlo mmoja kwa siku, waliopo wizarani hawawezi kufa kwa kukosa chai asubuhi. Tutafanya hivyo ili fedha hizo zipelekwe katika shughuli za maendeleo.

Dodoma. Bajeti ya Sh50 bilioni zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya safari za Rais Jakaya Kikwete katika mwaka ujao wa fedha ni miongoni mwa mafungu ya fedha ‘yaliyopigwa panga’ ili kuwezesha kupatikana kwa fedha za kugharimia miradi ya maendeleo.
Habari kutoka ndani ya kikao cha majadiliano baina ya Serikali na Kamati ya Bunge ya Bajeti zinasema, Sh11 bilioni zimepunguzwa katika fungu hilo na kubakiza Sh39 bilioni.
Hata hivyo, kiasi kilichobakishwa ni ongezeko la asilimia 260 la Sh15 bilioni zilizopitishwa na Bunge mwaka jana kwa ajili ya safari za Rais katika mwaka wa fedha unaomalizika Juni 30 mwaka huu.
“Katika bajeti ya 2013/14 safari za Rais zilitengewa Sh15 bilioni lakini inaonekana fedha zilizotumika ni nyingi zaidi maana ndani ya
miezi miwili tu zote zilikuwa zimemalizika,” kilisema chanzo chetu na kuongeza:
“Kwa hiyo kwa mwaka 2014/15 Serikali ilimtengea Rais Sh50 bilioni za safari, ila tumekata Sh11bilioni ili kupelekwa katika shughuli nyingine za maendeleo. Kwa hiyo kwa mwaka ujao wa fedha, safari za Rais zitatengewa Sh39 bilioni”.
Awali, ilielezwa kuwapo kwa mvutano mkali baina ya Serikali na Kamati ya Bunge ya Bajeti, lakini jana mchana pande hizo zilikubaliana kukata asilimia 7.5 ya fedha katika baadhi ya mafungu ya matumizi mengineyo (OC) kutoka katika wizara zote ili kuwezesha kupatikana kwa Sh230 bilioni ambazo zinahitajika kwa ajili ya maendeleo hasa katika sekta tatu; afya, miundombinu na kilimo.
“Bado kikao kinaendelea na tangu asubuhi tumekata fedha katika fungu la matumizi mengineyo, mfano chai katika ofisi za wizara pamoja na ununuzi wa magazeti, ununuzi wa magari ya kifahari, mafuta, viburudisho, semina na makongamano pamoja na safari za ndani,” kilieleza chanzo chetu.
Chanzo kingine kutoka Serikalini kilisema: “Katika siku ambazo tumevutana kwenye kikao cha kamati ni leo (jana), lakini mwishoni tulifikia mwafaka wa kukata kati ya asilimia saba na nane ya fedha za matumizi mengineyo katika wizara zote, ili kupata fedha za maendeleo.”
Juzi, Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba alisema wizara yake inakusudia kupitia bajeti za wizara zote ili kuhamisha fedha kutoka katika matumizi yasiyo ya lazima ili zielekezwe katika mahitaji muhimu.
“Kama wananchi wanakula mlo mmoja kwa siku, waliopo wizarani hawawezi kufa kwa kukosa chai asubuhi. Tutafanya hivyo ili fedha hizo zipelekwe katika shughuli za maendeleo.
Kesho (jana) katika kikao cha mashauriano tutakwenda kuweka msimamo wa pamoja katika jambo hilo. Wizara zisielekeze macho Wizara ya Fedha pekee, nazo zinatakiwa kuwa na mikakati ya kubana matumizi yake.”
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti, Andrew Chenge alipoulizwa kuhusu hatua iliyofikiwa katika majadiliano alisema: “Subirini itakaposomwa bajeti mtajua kilichoamuliwa.”
Vyanzo vya mapato
Licha ya kuwapo kwa makubaliano kuhusu suala la matumizi, vyanzo vya mapato vimeendelea kuwa siri hata kwa wajumbe wa Kamati ya Bajeti.
Usiri wa vyanzo hivyo ni moja ya mambo ambayo yalizua mvutano kutokana na wabunge kutaka kufahamu ni kwa vipi Serikali itamudu kupata kiasi cha Sh19 trilioni kugharimia Bajeti ya 2014/15, wakati imeshindwa kutimiza malengo ya kukusanya Sh18.2 trilioni kwa mwaka huu wa fedha.
Mmoja wa wajumbe wa Kamati ya bajeti, Hamad Rashid Mohamed alisema Serikali imekuwa ikishindwa kukusanya mapato ya kutosha kutokana na kung’ang’ania kutekeleza miradi ambayo ingeweza kufanywa na sekta binafsi.
Mbunge huyo wa Wawi (CUF), alitoa mfano wa miradi mikubwa ya kujenga reli, bandari na barabara kwamba inaweza kutekelezwa na sekta binafsi kwa ubia na Serikali.
Alisema kutokana na mahitaji makubwa ya kifedha, Serikali imekuwa ikikisia makusanyo makubwa ambayo haiwezi kufikia malengo yake, hivyo kuathiri miradi mingi ya maendeleo.
“Sisi tumekuwa tukiwaambia kama fedha za ziada zinapatikana, Bunge lipo walete supplementy budget (Bajeti ya nyongeza) kuliko huu utaratibu wa sasa wa kupitisha bajeti ya mapesa mengi ambayo hatuna uwezo wa kuyapata,” alisema.
Alisema tatizo lingine ni kukosekana kwa nidhamu ya ukusanyaji na matumizi ya fedha... “Kuna miradi hewa na mingine fedha zinaonekana kwenda lakini haijatekelezwa, haya ni mambo ambayo yanaifanya bajeti yetu kutotekelezeka.”
Jana, Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum alisema Serikali itatangaza vyanzo vyake vipya wakati wa kusoma bajeti yake bungeni... “Huo ndiyo utaratibu wa kawaida kabisa miaka yote.”
Akizungumzia suala hilo, Nchemba alisema: “Hatuwezi kuweka wazi vyanzo vya mapato hivi sasa, kwa sababu tulichonacho ni mapendekezo tu.”
Alisema mapendekezo hayo yatapelekwa Baraza la Mawaziri ambalo litaongozwa na Rais Jakaya Kikwete ambaye anatarajiwa kuwasili Dodoma leo.

No comments :

Post a Comment