Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Monday, June 23, 2014

Hazina ya maarifa na fedha iliyo ughaibuni

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akiwa pamoja na baadhi ya wanachama na viongozi wa Jumuiya ya Wazanzibari waishio ughaibuni. Picha: Ihsani ya Zanzibar Diaspora

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akiwa pamoja na baadhi ya wanachama na viongozi wa Jumuiya ya Wazanzibari waishio ughaibuni.
Picha: Ihsani ya Zanzibar Diaspora
Ahmed Rajab Toleo la 358 18 Juni 2014
HAKUNA ajuaye ni Wazanzibari wangapi wanaoishi nje ya mipaka ya Tanzania. Nimeandika “Wazanzibari” lakini nimewajumlisha katika kaumu hiyo wote wale wenye kujinasibisha na Unguja na Pemba ima kwa kuzaliwa au kwa damu.
Miongoni mwao mna wenye uraia wa kigeni, uraia walioupata ama kwa kukata tajinisi au kwa kuzaliwa ugenini. Miongoni mwa walioupata uraia huo kwa tajinisi kuna walioupata kwa njia za halali na kuna walioupata kwa njia za magendo.
Kuna waliokwenda ng’ambo kwa masomo au kwa kujitafutia riziki na halafu wakaamua kuselelea ughaibuni.
Wengine walilazimika kuvihajiri visiwa vya Zanzibar kwa sababu vilikuwa vi moto baada ya Mapinduzi ya Januari 12, 1964. Ndio maana miongoni mwa waliokuwa wakimbizi wa mwanzo baada ya Mapinduzi mna vijana walio na umri wa chini ya miaka 50 waliokuwa wadogo walipoondoka Zanzibar.
Tunakumbuka jinsi wasichana walivyokuwa wakihatarisha maisha yao walipokuwa wakivushwa kwa ngarawa kwenda Bara. Wakikimbizwa ili Serikali ya Mapinduzi isiwaozeshe kwa nguvu, na kinyume na Shari’a ya Kiislamu, waume wasiowataka.
Ngarawa hizo zikiitwa kwa utani “VC10” aina ya ndege za Shirika la zamani la Ndege la Uingereza (BOAC) zilizoingia mjini miaka hiyo.
Wengi wa Wazanzibari walio ughaibuni ni tofauti na wengi wa Waafrika wenye ujuzi waliozikimbia nchi zao. Ni tofauti, kwa mfano, na madaktari au wauguzi kutoka Ghana waliokimbilia Uingereza, Marekani, Canada na kwingineko wakivutiwa na mishahara minono na hali bora za kufanyia kazi na za maisha.
Mkondo kama huo umekuwa na athari mbaya juu ya sekta ya afya nchini Ghana.
Na kuna wanafunzi ambao baada ya kuhitimu tu masomo ya juu yaliyogharimiwa na serikali zao waliamua kufeleti wasirudi kwao.
Katika miaka ya 1970 na 1980 na hata katika miaka ya 1990 watu kama hao wakionekana kuwa ni wachoyo wenye ubinafsi wa kuyazingatia maslahi yao tu bila ya kuyazingatia maslahi ya mataifa yao.
Siku hizi mambo yamebadilika. Baadhi ya serikali za Kiafrika na hata taasisi za kimataifa zinawaona Waafrika walio ughaibuni kuwa ni wenye baraka kwa nchi zao. Serikali na taasisi hizo zinatambua kwamba Waafrika hao wana mengi ya kuchangia katika maendeleo ya nchi zao.
Utafiti umeonyesha kwamba misaada ya fedha wanazowapelekea jamaa zao na hata rasilimali zao wanazowekeza nchini mwao zimesaidia maendeleo ya nchi.
Nijuavyo ni Wazanzibari wachache walio ughaibuni wasiotaka kunasibishwa na Zanzibar au wanaoikanya nchi yao ya asili. Wengi wao, wa jinsia zote, wazee kwa vijana, wana raghba kubwa na nchi yao.
Hawa Wazanzibari wa ughaibuni — kama walivyo Waafrika wengine walio ughaibuni — si kwamba waliivuka tu mipaka ya taifa lao lakini wameivuka pia mipaka ya fikra za kikwao. Wanaishi katika mazingira yaliyoendelea yakilinganishwa na ya kwao ingawa mazingira yao ya sasa ni mageni.
Ugeni huo unaongeza thamani ya ubinadamu wao. Ikiwa wanastahiki wathaminiwe zaidi kwao sababu ni kwamba aghalabu huwa wamepitia mengi na wameona mengi yaliyotanua fikra zao na kuyafanya macho yao yafumbuke. Wamepata uwezo mpya wa kuuona ulimwengu vingine tofauti na vile ambavyo wangeliuona lau wangeselelea makwao.
Nikisema hivi sikusudii kuwadharau au kuwatoa maanani waliobaki nyumbani. La hasha.
Bila ya shaka mtu kwao na lau nchi yao isingekumbwa na masaibu yaliyoikumba tangu 1964 na ingelikuwa imeendelea basi Wazanzibari hao wasingeihama kwa mkururo na waliokuwako nje wasingelikataa kurudi kwao.
Ndugu zao wa Tanganyika hawakukimbia kwao kama walivyokimbia wao. Na hata hizo siku walizokuwa wakiihama nchi hawakuwa wengi hivyo na walikuwa sana wakielekea Afrika ya Kusini kutafuta kazi katika migodi ya dhahabu au Zanzibar kuchuma karafuu.
Hii leo kwa sababu ya kuanguka kwa uchumi wa Zanzibar aila nyingi za huko zinategemea kufadhiliwa na jamaa au marafiki zao walio nje ya Tanzania, hususan walio Arabuni, nchi za Ulaya na Marekani.
Hivi mwezi Mtukufu wa mfungo wa Ramadhani ukikaribia tayari fedha pamoja na mabunda ya nguo na vyakula yako njiani kuelekea Zanzibar kutoka nchi mbali mbali.
Pamoja na kuwasaidia jamaa zao kuna Wazanzibari kutoka nje wanaonunua viwanja na kujenga nyumba ili wawe wanarudi mara kwa mara kwa mapumziko. Wengine wanajiandaa na mapema ili watapostaafu warudi nyumbani. Na wapo waliowekeza katika miradi kadha wa kadha ikiwa pamoja na ya mahoteli, hospitali na ya skuli.
Hizo ni kati ya jitihada zinazofanywa na watu binafsi ama mmoja mmoja au kwa kushirikiana na wenzao. Zaidi ya hayo Wazanzibari walio nje wameasisi jumuiya za kuwafanya wawe pamoja kuisaidia nchi yao.
Jumuiya aina hizo ziko katika nchi kadhaa zikiwa pamoja na Canada, Denmark, Marekani na Uingereza. Zinajihusisha na miradi ya elimu, ya huduma za afya na ya biashara ndogo ndogo za kuwasaidia watu wa sehemu za mashambani.
Kinachozidi kuwatia hima waendelee na jitihada zao ni imani yao kwamba Zanzibar haitosalia vivi hivi ilivyo lakini itabadilika.
Kwa kweli, Wazanzibari walio nje na waliojitolea kuisaidia nchi yao wanastahiki wapongezwe. Serikali ya Zanzibar nayo inapaswa iwe ya mwanzokuwaunga mkono nakushirikiana naozaidi ya ifanyavyo sasa. Lengo liwe ni kuwashirikisha kikamilifu katika juhudi za kujenga nchi na kuleta maendeleo.
Serikali ya Zanzibar nayo inapaswa ipongezwe kwa kufungua idara maalum katika Ofisi ya Rais yenye kuwashughulikia Wazanzibari wa ughaibuni. Idara hiyo inajitahidi lakini ina mengi bado ya kutekeleza.
Kwanza serikali inahitaji ijiekeekipaumbele kipyacha kulishughulikia ipasavyo suala hili la Wazanzibari walio ughaibuni. Inafaa iiangalie Kenya yenye uchumi madhubuti na sarafu imara kulinganishwa na jirani zake katika kanda ya Afrika ya Mashariki.
Kenya ina sera na mkakati mahsusi wa kuwavutia Wakenya waishio nje ya nchi yao. Serikali ya huko inakisia kwamba Wakenya hao wanafika milioni tatu, kama asilimia 8 ya Wakenya wote kwa jumla.
Wakati maduhuli ya serikali kutoka mauzo ya bidhaa kama chai na kahawa yamekuwa yakipungua sana fedha zinazoingizwa nchini na Wakenya walio nga’mbo zimekuwa zikiongezeka kwa kima kikubwa sana cha kupindukia dola za Marekani bilioni tatu katika kipindi cha miaka mitano kufikia Desemba 2011.
Wengi wa Wakenya hao wana kazi nzuri huko waliko na wanajimudu kupeleka cho chote kwao. Hii ndiyo sababu iliyoifanya Serikali ya Kenya iwatie shime Wakenya wa ughaibuni washiriki katika maendeleo ya taifa lao.
Mwaka 2011, Benki Kuu ya Dunia iliipa Kenya dola za Marekani 500,000 kuisaidia katika jitihada zake za kuwashirikisha Wakenya wa ughaibuni katika shughuli za maendeleo ndani ya Kenya.
Nini cha ziada kinachoweza kufanywa Zanzibar kuhusika na suala hili?
Jibu ni kutunga sera zitazowavutia Wazanzibari walio nje wazidi kupeleka rasilmali zao Zanzibar na kuwakeza huko ili wachangie katika maendeleo ya nchi. Yote hayo yanawezekana endapo pana uongozi madhubuti wenye nia ya kuzifanikisha sera hizo.
Taasisi kama ya Zanzibar Institute for Research and Public Policy(ZIRPP), ambayo kama jina lake linavyoainisha inahusika na utafiti na sera ya umma, inaweza kuchangia mengi katika kutoa mwongozo wa jinsi ya kuliendeleza suala hili baada ya kufanya utafiti wa kina.
Zanzibar iko nyuma katika mambo ya elimu na teknolojia ilhali miongoni mwa Wazanzibari walio nje mna magwiji wa taaluma hizo. Tuna wahandisi wa mambo ya nyuklia, mafundi wa kompyuta walio Silicon Valley, Marekani, maprofesa chungu nzima wa nyanja mbalimbali za sayansi, maprofesa wa utibabu na wa magonjwa ya aina kwa aina.
Kwa hivyo, ni muhimu Wazanzibari walio ughaibuni wapewa vivutio vitavyozidi kuwavutia wende kuvisaidia visiwa vyao viwe vya kisasa.
Kivutio kikubwa kitachowatia moyo bila ya shaka ni kutungwa sheria itayowapa haki ya kuwa na uraia pacha.Wanaopinga uraia pacha wanahoji kwamba suala hilo linabidi liangaliwe kwa darubini ya usalama wa taifa. Hiyo ni hoja dhaifu.
Serikali ya Zanzibar ina wajibu wa kuandaa sera maalum juu ya suala hili muhimu kwa sababu hatimaye ni taifa litalonufaika.
Serikali ya Zanzibar ina fursa ya kipekee ya kuwavutia Wazanzibari wa nje wenye maarifa na ujuzi, wazidi kujihusisha na maendeleo ya nchi yao. Wazanzibari hao ni hazina kuu na ni rasilmali ambayo serikali lazima isiipuuze inapokuwa inatayarisha mipango yake kuhusu mustakbali wa Zanzibar tuitakayo — Zanzibar yenye amani, usawa, haki, ufanisi na maendeleo.
Chanzo: Raia Mwema

No comments :

Post a Comment