Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Sunday, June 15, 2014

Rasimu ya Katiba inavyowagawa viongozi SMZ

     



Na Na Mwinyi Sadallah, Mwananchi

   KWA UFUPI
Mawaziri watano CCM warushiana madongo na wenzao wa CUF
Tangu kutoka bungeni kwa Kundi la Wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananachi (Ukawa) kwenye Bunge la Katiba kwa madai ya kuchoshwa kwao na matusi, kejeli na ubaguzi, kumeibuka mijadala mikali, huku mawaziri na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wa chama tawala CCM, wakivunja ukimya na kuamua kupambana na umoja huo kwa hoja kwenye hadhara.
Ni wazi sasa hatua hii inaonyesha bado kuna mivutano kutokana na kila upande kubeba na kutetea hoja zake na kutupiana lawama za kuukwamisha Mchakato wa Katiba Mpya.
Wakati Ukawa wakidai wabunge wa CCM ndiyo chanzo cha kuvuruga na kukwamisha mchakato huo, CCM wanaubebesha msalaba wa lawama Ukawa na kusema ni wakimbizi wa hoja walioshindwa kujenga ushawishi na kuamua kuweka mpira kwapani baada ya hoja zao kukosa mashiko.
Madai ya Ukawa wanaeleza kuwa CCM imeacha kujadili Rasimu ya Jaji Joseph Warioba iliyowasilishwa bungeni na kuonekana wakiwa na rasimu yao kibindoni, wakitaka matakwa yao ya kisera na kiitikadi yapitishwe na Bunge la Katiba kinyume na taratibu.
Ukawa wanakazia msimamo wao na kusema kwamba Muundo wa Muungano wa serikali mbili si pendekezo la Tume ya Jaji Warioba iliyowasilishwa katika Bunge hilo maalumu la Katiba.
Hata hivyo, madai mengine ya CCM yanaeleza kuwa kundi la Ukawa halina nia njema, limeshindwa kujenga ushawishi na kuonyesha uhalisia wa faida za muundo wa serikali tatu ikiwa ni pamoja na rasimu ya Warioba takwimu zake kujikanganya na kukosa uchambuzi yakinifu.
Wadadisi wa masuala ya kisiasa visiwani hapa wanaeleza kuwa kukwama kwa Mchakato wa Katiba, kunaweza kuendelea kuiweka Zanzibar katika mzingira magumu ya kiuchumi na kujikuta madai au kilio chao cha muda mrefu kikakosa mnyamazishaji wa kuwafuta machozi.
Pia wako wanaosema kuwa ni lazima Zanzibar ipate hadhi yake kamili ili kuwa na polisi wake, uraia, uhamiaji, hati za kusafiria, elimu ya juu, sarafu na benki kuu yake ili kujitegemea na kujiendeleza yenyewe.
Hali hiyo pia inapingwa na baadhi ya watu wanaosema hakuna mahali popote duniani ambapo nchi mbili zimeungana zikaendelea kuwa na mamlaka kamili na kuyataja madai hayo yana dhamira ya kuvunja Muungano na kuusambaratisha.
Mifano yao katika kuungana na kubaki na mamlaka moja kamili wanayafananisha mataifa ya Uingereza, Marekani, Ujerumani na India.
Kundi la wabunge wa Ukawa tayari limefanya mikutano miwili mikubwa ya hadhara katika Kisiwa cha Unguja na Pemba huku CCM ikifanya mikutano mitatu katika visiwa hivyo kwa nyakati tofauti wakihimiza msimamo wao kuwa ni sahihi.
CCM imeamua kuwapandisha majukwani mawaziri watano ili kuwajibu Ukawa wakiongozwa na Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Idd, huku CUF kwa kutumia mwamvuli wa Ukawa, wamewapandisha viongozi wakuu wa vyama vya NCCR-Mageuzi, Chadema, CUF, NLD , DP na NRA ili kuweka msimamo wakiongozwa na Makamu wa Kwanza wa Zanzibar Rais Maalim Seif Sharif Hamad.
Mawaziri watano wa CCM waliopanda katika majukwa ya CCM ni Waziri wa Nchi Tawala za Mikoa na Vikosi Maalumu vya SMZ Haji Omar Kheir, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Ikulu na Utawala bora Dk Mwinyikaji Makame Mwadini, Waziri Kiongozi Mstaafu Shamsi Vuai Nahodha, Waziri asiye na Wizara Maalumu Machano Othman Said, Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar Balozi Seif Ali Idd na Naibu Waziri wa Miundombinu na Mwasiliano Issa Haji Gavu.
Wakati Ukawa wakiapa kutorejea bungeni na kushiriki mjadala wa uundwaji wa Katiba Mpya, kiongozi wa juu wa CUF na Msemaji wa chama hicho Salim Bimani, anasema ili Ukawa na CUF warejee bungeni wanawataka CCM waijadili Rasimu ya Warioba kama ilivyo bila ya kupunguzwa jambo, wabunge wa CCM waache matusi, kejeli na ubaguzi pia viongozi wa juu wa CCM wathibitishe hilo kwa maandishi.
Kauli hiyo imepingwa vikali mara baada ya Kikao cha Kamati Kuu ya CCM kilichokutana Dodoma ambapo Katibu wake wa Itikadi na Uenezi Nape Nnauye alisema CCM imeziagiza Serikali zake ziachane na mpango wa kuwabembeleza Ukawa kurejea bungeni.
Nape akasema kundi hilo halina nia njema kwa Taifa na kitendo chao cha kukimbia katika uwanja wa kikatiba na kisheria , kianaashiria kukosa hoja na kupungukiwa uzalendo kwa ajili ya kujenga mazingira bora ya utulivu, amani na mshikamano.
Wakati Balozi Seif akiwataka wabunge wa Ukawa kurejea bungeni kwa kutumia mlango ule ule waliotokea na kuacha kutoa masharti, Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad amesisitiza kuwa msimamo wake yeye ni ule wa Ukawa na hakuna haja ya kurejea katika Bunge litakaloanza Agosti mwaka huu.
Wakati Balozi Seif akiitupia lawama CUF kwa kukosa msimamo wa kisera tangu mwaka 1992 kuhusu mfumo wa Muungano kwa kutoa madai ya kutaka serikali tatu na baadaye Muungano wa mkataba kabla ya kubadilika na kutetea tena serikali tatu, anasema hilo ni jambo linalokiyumbisha chama hicho.
Katibu wa Bunge la Katiba, Yahya Khamis Hamad amesema Mwenyekiti wa Bunge la Katiba Samuel Sitta amechukua hatua kadhaa ya kujaribu kukutana na viongozi wa Ukawa ;lakini bado juhudi zake hazijazaa matunda hadi sasa ili kupata mwafaka.
Yahya amesema mahali lilipofikishwa Bunge la Katiba hakuna njia ya mkato zaidi ya kuwepo majadiliano na mapatano yatakayosaidia kulipatia nusura Bunge hilo na kupatikana Katiba Mpya.
Pia anaukosoa msimamo wa Ukawa wa kususia Bunge na kueleza kuwa kulikuwa na njia nyingi sahihi za kufikia maridhiano ikiwa ni pamoja na kuwasilisha malalamiko yao kwenye kamati ya uongozi na maridhiano ya Bunge la Katiba iwapo kulikuwa na kasoro zilizojitokeza na kuwakwaza.
Hayo yote yakiwa yamejitokeza bado wananchi walio wengi wanaona kuahirisha kupata katiba mpya si muafaka na kushauri ni vyema sasa pande mbili zikakutana na kushauriana.

Hatua hizo zote ikiwa zitakwama,ni dhahir shahir kuwa ile ndoto ya Tanzania kupata katiba mpya hapo mwakani itapotea hewani huku mamilioni ya fedha za umaa zikiwa zimepotea na kuwanufaisha watu wachache.

No comments :

Post a Comment