Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Saturday, June 7, 2014

Uhaba wa fedha waathiri wagonjwa Zanzibar

  
Na Mwinyi Sadallah, Mwananchi

KWA UFUPI
Matatizo hayo yamefichuliwa na Mwakilishi wa Jimbo la Muyuni Jaku Hashim Ayoub, wakati akichangia makadirio ya matumizi ya Wizara ya Afya yaliyowasilishwa na Waziri wake Juma Duni Haji, kwenye Baraza la Wawakilishi.
Zanzibar. Wagonjwa wa akili katika Hospitali ya Kidongochekundu, wamekuwa wakipewa mlo mmoja kwa siku katika kipindi cha mwaka mmoja na wakati mwingine kulala giza kutokana na Wizara ya Afya Zanzibar kushindwa kutoa fedha za matumizi kwa muda mwafaka, imefahamika visiwani humu jana.
Matatizo hayo yamefichuliwa na Mwakilishi wa Jimbo la Muyuni Jaku Hashim Ayoub, wakati akichangia makadirio ya matumizi ya Wizara ya Afya yaliyowasilishwa na Waziri wake Juma Duni Haji, kwenye Baraza la Wawakilishi.
Alisema uongozi wa hospitali hiyo unakabiliwa na tatizo la ukosefu wa fedha na kulazimika kuwapa mlo mmoja wagonjwa na baadhi ya wakati wagonjwa kulala giza kutokana na kushindwa kumudu gharama za umeme.
Alisema kitendo hicho kinakwenda kinyume na misingi ya haki za binadamu kwa vile wagonjwa wa akili wana haki ya kutibiwa na kupewa huduma kama wanavyopata wagonjwa wengine.
“Mheshimiwa Spika hata vitanda wanavyotumia vinakabiliwa na uchakavu mkubwa nitakuwa mgumu kupitisha bajeti ya wizara hii,” alisema Jaku.
Hata hivyo, alisema kwamba matatizo mengi katika sekta ya afya Zanzibar yanachangiwa na Wizara ya Fedha kutoingiza fedha za matumizi ya Wizara ya Afya kama zinavyoidhinishwa na Baraza la Wawakilishi kila mwaka.
Hospitali hiyo hadi Machi mwaka huu ilipokea wagonjwa wa akili 995, wakiwemo wanawake 344 sawa na ongezeko la wagonjwa 479 wakiwemo vijana walioathirika na matumizi ya dawa za kulevya.
Alisema hospitali na vituo vya afya vya Serikali kumejitokeza uhaba wa dawa zikiwemo za kupunguza maumivu kwa wagonjwa, ukosefu wa vifaa na vitanda na kusababisha wagonjwa kulazwa kitanda kimoja watu watatu na wengine chini wakiwemo wagonjwa katika wodi ya wazazi ya Mnazimmoja.
Upande wake Mwakilishi wa Jimbo la Mji Mkongwe, Ismail Jussa Ladhu alisema SMZ haiwatendei haki wananchi wake kwa sababu imeshindwa kupanga vipaumbele katika matumizi ya fedha za umma na kusababisha wananchi wanyonge kukosa huduma bora za afya.
Alitoa mfano wa uhaba wa fedha kuwa Kitengo cha Tiba Unguja walikuwa watumie kiasi cha Sh670 milioni, lakini waliingiziwa Sh148 milioni sawa na asilimia 22.1 tu wakati kitengo cha tiba Pemba walikuwa watumie Sh310 milioni lakini walingiziwa asilimia 46.8 kati ya fedha zilizoidhinishwa na Baraza la Wawakilishi mwaka jana.
Jussa alisema kwamba wakati Hospitali ya Rufaa ya Mnazimmoja inakabiliwa na matatizo mengi na kulazimika kutoa huduma duni hadi Machi mwaka huu, imeingiziwa Sh 664.6 milioni kati ya Sh1.2 bilioni, sawa na asilimia 54 .5 ya fedha zilizoidhinishwa na Baraza hilo.


No comments :

Post a Comment