Na Mwinyi Sadallah, Mwananchi
Posted Jumapili,Juni29 2014
KWA UFUPI
Hali ya mahudhurio iliendelea kuwa mbaya zaidi baada ya wajumbe wengi wa CUF kuhudhuria Mkutano Mkuu wa chama chao uliokuwa ukifanyika jijini Dar es Salaam.
Zanzibar. Baraza la Wawakilishi Zanzibar (BLW) limekwama kukaa kama kamati ya matumizi na vikao kwa mara ya tano tangu kuanza kujadili bajeti za mwaka wa fedha 2014/15 Mei 14 mwaka huu kutokana na tatizo la wajumbe kuwa watoro wa kuhudhuria vikao.
Hali hiyo imekuwa ikimlazimu Spika wa Baraza la Wawakilishi, Pandu Ameir Kificho, Naibu Spika Ali Abdallah Ali na Mwenyekiti wa Baraza hilo Mgeni Hassan Juma kushindwa kuitisha Kamati ya Matumizi kutokana na kutotimia akidi ya asilimia 50 ya wajumbe 40 kati ya wajumbe 82.
Tukio la aina hiyo lililotokea mwishoni mwa wiki baada ya Naibu Spika Ali Abdallah Ali kujikuta akiahirisha Baraza hilo kutokana na uchache wa wajumbe wakati wakijadili bajeti ya Wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati iliyowasilishwa na Waziri Ramadhan Abdallah Shaaban.
Naibu Spika alisema pamoja na Waziri kukamilisha mjadala wa bajeti yake, Kamati ya Matumizi haitaweza kuendelea kukaa na kupitisha vifungu kutokana na akidi ya wajumbe kutofikia asilimia 50.
‘Kutokana na akidi ya wajumbe kutokamilika, Baraza halitaweza kukaa kama kamati na kupitisha vifungu, nalazimika kuahirisha kikao hiki,” alisema Naibu Spika.
Mwakilishi wa Jimbo la Rahaleo, Nassor Salim Ali alisimama na kutaka mwongozo akitaka kujua sababu ya wajumbe kutotimia ili wananchi waweze kufahamu mahali waliko wawakilishi wao hasa kwa kuzingatia kuwa tatizo hilo limekuwa likijitokeza kila mara.
Naibu Spika alisema tatizo hilo limekuwa likitokea kutokana na sababu mbalimbali na kuwataka wajumbe kuhakikisha wanahudhuria kwa wakati mwafaka ili kazi iliyokuwa imelala iweze kufanyika kwa wakati sahihi na mwafaka.
Mkasa huo ulitanguliwa na ule wa Baraza kushindwa kukaa kama kamati wakati ikijadiliwa Bajeti ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko kutokana na idadi ya wajumbe kuwa wachache ambapo kamati ya matumizi ilishindwa kukaa na kupitisha vifungu vya matumizi chini ya Mwenyekiti wa Baraza hilo Mgeni Hassan Juma mbali na matukio mawili yaliyotokea ya akidi kutotimia huku Spika wa Baraza hilo akikalia kiti.
Hali ya mahudhurio iliendelea kuwa mbaya zaidi baada ya wajumbe wengi wa CUF kuhudhuria Mkutano Mkuu wa chama chao uliokuwa ukifanyika jijini Dar es Salaam.
Wakati wajumbe wa CUF wakitingwa na vikao vya mkutano mkuu, wale wa CCM wamekuwa wakihudhuria vikao vya Bunge huko Dodoma kutokana na kuwa na kofia mbili kwa wakati mmoja kutokana na kuwa wawakilishi na wabunge wa kuteuliwa.
Aidha, Spika Pandu Ameir Kificho tayari amekwishakemea mara mbili tabia ya utoro na kuwataka wajumbe kutambua dhamana waliyonayo kwa taifa na umuhimu wao wa kuhudhuria vikao kama wawakilishi wa wananchi.
Wawakilishi hulipwa posho ya kikao kimoja kwa siku Sh150,000 mbali na mshahara wa Sh4.5 milioni kwa mwezi.
http://www.mwananchi.co.tz/habari/Kitaifa/Utoro-BLW-wakwamisha---bajeti-Z-bar/-/1597296/2365562/-/13tfll9z/-/index.html
No comments :
Post a Comment