A K Khiari
Hivi karibuni Scotland itapiga kura ya maoni (Referendum) kuamua kwamba inataka kubaki katika United Kingdom ama laa.
Kura hii ni muhimu sana kwa mustakabali wa nchi ya Scotland ambayo kwa miaka mingi imekuwa chini ya himaya ya Uingereza baada ya kujiunga pamoja na kuunda United Kingdom of Great Britain and Northern Ireland.
Umoja huu uliundwa mwaka 1801.
Kura ya maoni itafanyika tarehe 18 Septemba 2014 na kwenye karatasi ya kura kutakuwa na suala moja tu nalo ni : Je unataka Scotland iwe ni nchi huru? Na jibu liwe ima ni ‘Ndiyo’ au ‘Hapana’.
Scotland, kama Zanzibar, ilikuwa ni nchi huru ambayo kwa kuungana na Uingereza mwaka 1801 ikapoteza utaifa wake kama Zanzibar ilivyopoteza utaifa wake walipoungana na Tanganyika.
Scotland, kama Zanzibar, illiingia katika muungano huu kwa kupoteza utaifa wake na kubakia raia wake kuwa raia wa Uingereza kama walivyobaki raia wa Zanzibar kuwa ni raia wa Tanzania baada ya kuungana na Tanganyika.
Scotland, kama Zanzibar, ilipoteza sarafu yake na benki Kuu na hivi kuamuliwa chini ya UK wakitumia Pauni ya kiingereza kama ilivyo kwa Zanzibar kutumia sarafu ya Shilingi.
Scotland, kama Zanzibar, ilibakia na bunge lake dogo ambalo huchaguliwa na wapiga kura na kuwepo kwa miaka mine na Zanzibar tuna baraza la wawakilishi ambalo pia huchaguliwa kwa kura kwa muda wa miaka mitano.
Scotland, tofauti na Zanzibar, imeweza kupata uanachama wa FIFA na hivyo kuweza kushiriki katika michuano inayotambuliwa na FIFA kama ni nchi kamili licha ya kutokuwa na mamlaka (Sovereignty) wakati Zanzibar imekosa uwakilishi huu.
Scotland, tofauti na Zanzibar, imeweza kupata uanachama wa FIFA na hivyo kuweza kushiriki katika michuano inayotambuliwa na FIFA kama ni nchi kamili licha ya kutokuwa na mamlaka (Sovereignty) wakati Zanzibar imekosa uwakilishi huu.
Scotland, tofauti na Zanzibar, imeweza kuienzi na kuitunza historia yake na ya nchi yake wakati Zanzibar inaonesha mwelekeo wa kupoteza historia yake kwa kutoitunza kikamilifu.
Scotland, tofauti na Zanzibar, ilivienzi na kuviboresha vituo vyake vya elimu kama vyuo vikuu na kuwa kitovu cha elimu kwa vyuo vyake hasa vikuu wakati Zanzibar iliyokuwa kitovu cha elimu kabla ya Mapinduzi kupoteza umaarufu wake huo.
Moja katika hoja kuu ambazo Scortland imeamua kuzitumia katika kutafuta uhuru wao kupitia kura ya maoni ni kwamba Scotland iliyo huru itaweza kukuza uchumi kwa kasi kubwa na kuweza kufungua milango mingi ya ajira kwa vizazi vijavyo .
Waziri wa kwanza wa Scotland, bwana Alex Salmond, alitaja mambo makuu 6 ambayo kama yakiwa chini ya himaya ya Scotland iliyo huru na mamlaka kamili yana viashiria vizuri vya maendeleo
- Udhibiti wa moja kwa moja wa kodi ya Biashara
- Udhibiti wa mapato kwa ujumla
- Udhibiti wa kodi ya usafiri wa anga
- Udhibiti katika kuajiri
- Udhibiti katika sera za kibiashara
- Udhibiti katika uhamiaji
Mambo haya sita kwa mujibu wa Alex Salmond yakiwa chini ya Scotland iliyo huru yenye mamlaka kamili na inajitegemea , basi Scotland itakuwa ni nchi yenye kukua kwa kasi kiuchumi kwani itakuwa na uwezo kamili wa kutengeneza ajira zitakazowanufaisha waskotishi.
Mambo haya sita yanaweza kufanana kwa kiasi kikubwa na hoja za kimsingi ambazo Zanzibar, ndani ya kivuli cha muungano, imeona zinawakandamiza na kama tulivyosikia karibuni kuwepo mjadala wa kuvutana ilipokuwa ikijadiliwa sura ya 14 ya Katiba inayohusisha mapato na matumizi ndani ya muungano.
Wakati tukishuhudia na kuona kasi ya kimaendeleo upande wa pili wa muungano haiendani sambamba na kasi ya maendeleo upande wa Zanzibar ambayo haina vyanzo muhimu vya kiuchumi vya kujitegemea na kujikuta imebaki tegemezi wa muungano wakati, kama ni mshirika katika muungano,anatakiwa apate haki kwa kulingana na uhusiano wake.
Zanzibar pia inaweza kujifunza mengi kutoka Scotland hasa katika mfumo mzima na utaratibu wa kujenga hoja mpaka kufikia suala la kuamuliwa ifanyike kura ya maoni na waulizwe wananchi kama wanataka kubaki katika muungano na ama laa.
Moja katika fundisho la kuzingatia ni uwezo wa upande mmoja wa muungano kuweza kuleta hoja ya kura ya maoni ya kujiridhisha kama muungano uliopo uendelee au uvunjike. Upande mmoja wa muungano, kwa mfano Zanzibar, una uwezo kisheria na kikatiba kuileta hoja hii na kura ya maoni ikapigwa Zanzibar tu wakati Tanganyika hawatokuwa na haja ya kupiga kura hii.
Waziri Mkuu Mizengo Pinda aliwahi kunukuliwa kwamba kama wangelijua mapema hili jinamizi la muungano liko kubwa kiasi hiki wangekwenda kuwauliza wananchi kwanza ni muungano upi wanaoutaka kabla ya kufikiria masuala ya katiba mpya.
Serikali ya umoja wa kitaifa kama imeliona jambo hili kuwa ni muhimu kwao japo kwa kuweza kupata kujifunza tu vipi mfumo hii unatumika ingelifanya busara ya kuingia hasara ya leo kwa faida ya kesho kwa kutuma viongozi wake waandamizi hasa Tume ya uchaguzi, kwenda kuwa kama Watazamaji “observers” kwenye kura hii ya kihistoria ambayo kimazingira inawezekana kufanyika Zanzibar na kujifunza kivitendo vipi mfumo wa kura ya maoni unavyofanyika katika kutafuta mamlaka kamili.
Hapa wasisubiri mwaliko kutoka Scotland bali wafanye haraka kutafuta njia ya kuweza kuhudhuria kura hii hata kama ni kwa gharama ya walipa kodi kwani ninaamini kutakuwa na maslahi muhimu kwa taifa letu ambalo linapita katika kipindi kigumu katika kuwepo kwake.
Ni kweli tayari tumeweza kufanikisha kura ya maoni kwa mara ya kwanza Zanzibar iliyopelekea kuundwa Serikali ya umoja wa kitaifa, na kama tutaitumia fursa hii ya kushuhudia kura hii ya maoni itakayofanyika Scotland mwezi ujao, ninaamini tutapata mengi yenye faida kwa mustakbali wa nchi yetu bila ya kujali kitu gani waskotishi wataamua kama ni kubaki au kujitoa katika muungano wao na Uingereza.
Chanzo: ZanziNews
No comments :
Post a Comment