Abu Ammaar
‘Ibadah ya Hajj – nguzo ya tano katika nguzo za kiislam imekuwa adimu kutekelezwa na miongoni mwa jamii ya waislamu waswahili hasa waliopo katika nchi za kimagharibi.
Tumebahatika kuwaona ndugu zetu wakijibana na kujinyima kwenye matumizi ili wapate fedha za kwenda mapumziko “Holiday” pamoja na kuwazuru wazee, ndugu na jamaa. Baadhi ya ziara hizi hufanyika takriban kila mwaka .
Kwa siku za nyuma sababu nyingi zilikuwa zikitolewa kama kutopata makaratasi ya kuhalalisha ukaazi, uhalali wa aina za pesa zinazohitajika kuitekeleza nguzo hii kwani tunadai tunavuta kwa hivyo hatuna uhakika na “uhalali” wa pesa zetu. Pia ujana hutajwa kwani wengi tuliokuwa tulikuja tukiwa katika umri wa “kutanua” hivyo kwenda Hajj mapema huenda tukajizeesha na pia kutufunga katika mambo mengi ambapo labda kama tusingekuwa mahujaji tungelikuwa na uhuru wa kuyafanya kirahisi. Kutohamasishwa kikamilifu na wanaharakati wa kida’awah pia ni moja ya sababu zinazotajwa. Kauli ya wazee wetu pia kwamba “mpaka uitwe” ndio utaweza kuitekeleza nguzo hii nayo hugusiwa gusiwa .
Sababu ya kimsingi iliyotufanya tuje katika nchi hizi ni kutafuta hali bora za kimaisha na kuwa na uwezo wa kujikimu sisi wenyewe na familia zetu. Uwezo huu ndio ulioyafanya maisha yetu kuwa bora kwa kadri ya Allah Subhaanahu Wata’ala alivyotujaalia. Tumshukuru Allah Subhanahu Wata’ala kwa hili. Uwezo huu pia umetuwezesha kusaidia familia zetu huko walipo angalau kuwapunguzia makali ya maisha. Uwezo huu pia umetuwezesha kufanya mambo mengi muhimu katika maisha yetu kama kuwa na majengo, magari, mabiashara na mengineyo ambayo wengi tunaamini kama tungelikuwa nyumbani tusingekuwa kama hivi tulivyo.
Na kwa upande mwengine, ambao wengi tumeshindwa kutanabahi, uwezo huu huu umetufanya tayari tuwe na sifa ya kuitekeleza nguzo hii adhimu ambayo hutakiwa kila muislamu mwenye uwezo aitekeleze mara moja katika uhai wake.
Uwezo unaotakiwa kwa ajili ya kuitekeleza nguzo huu si lazima au shurti ya mtu awe na tajiri na mali nyingi sana. Kinachoangaliwa ni kuweza kupata pesa za nauli na matumizi ya safari nzima ya Hajj pamoja na kuiachia familia cha kuwatosheleza kwa muda wote wa safari. Kwa ufupi huu ndio uwezo unaotakiwa pamoja na uzima wa kiafya kuweza kuhimili mikiki ya safari. Kwa kuwa wengi tumeshawahi kusafiri hivyo tunajua jinsi na wapi pa kujibana mpaka tukamilishe kinachohitajika.
Kwa jinsi ya idadi ya waislamu waswahili waishio hapa Uingereza ilivyo na kwengineko katika nchi hizi za ulaya ulikuwa wakati huu tuwe tayari na “maqaafilah” - makundi – yetu ya mahujaji kila mwaka kama zilivyo jamii nyengine lakini bado ni wachache sana miongoni mwetu wanaoamua kuitekeleza nguzo hii. Nguzo ambayo ikitekelezwa ipasavyo humfutia muislamu madhambi yake yote yaliyopita.
Lakini hapo hapo tunasikia jinsi tunavyoshindana kimitindo kufanya safari za nyumbani na kwengineko wakati wa mapumziko kwa sababu mbali kama kubadilisha upepo, kupeleka watoto, kufuatilia miradi, kupumzika, kutembea na kadhalika. Haujafika wakati tukaanza kushindana kuwahi kuitekeleza Hajj na tayari uwezo wengi wetu tunao? Ni amali ya kheri, ni nguzo ya tano, hufuta madhambi na malipo yake ni pepo.
Moja katika malengo ya kuitekeleza nguzo hii ni ambayo ni wajibu kwa kila muislamu mwenye uwezo ni kufungua ukurasa mpya katika maisha yetu mafupi hapa duniani. Ni kama Allah Subhaanahu Wata’ala anatupa nafasi nyengine maishani mwetu kubadilika na kurudi kwake katika hali ya utiifu, uchamungu, kuwa na aqidah madhubuti sahihi kwani muda wote tunapokuwepo Makkah ni wageni rasmi wa Allah Subhaanahu Wata’aala. Ni yeye alietutaka waislamu wenye uwezo kwenda huko tukiwa katika hali moja kimavazi na kuzitekeleza ‘ibadah zote kwa pamoja hukusanyika katika Mlima Arafah sote siku moja wakati mmoja. Hakuna tofauti kati ya mwarabu na asiekuwa mwarabu, mzungu na mhindi, mchina na mswahili kama tunakumbushwa siku ya kiama. Tukirudi tuanze kama ni ‘jiyl’ – kizazi – kipya kwa jinsi ya faida, mafundisho na athari tukakazozipata.
Jamii ya waislamu waswahili haina utamaduni wa kuzitekeleza ibadah hizi mbili - Zakah na Hajj. Tulipotoka tulikuwa katika hali duni kimaisha(ingawa si wote) na hivyo kutokuwa na sifa za kuwajibika nazo. Kwa masikitiko na huzuni ninaweza kuungama kwamba bado utamaduni huu tunaendelea nao wakati tayari hali zetu zimeshabadilika. Na wakati sote tunafahamu wajibu wetu kuhusu nguzo hii adhimu na muhimu.
Ndugu yangu muislamu na katika imani, nnakuusia kama nnavyoiusia nafsi yangu, baada ya kuusoma waraka huu mfupi, tuazimie na kuanza kupanga mikakati ya kuitekeleza nguzo hii karibuni inshaallah kwani wengi wetu tumeshaqualify na hatujui lini Subhaana ataichukua amana yake na asije akatuuliza suala hili siku ya siku tukawa hatuna jibu la kumpa. Wakati umefika wa kubadilisha utamaduni huu na kujenga utamaduni wa kuzitekeleza nguzo hizi kikamilifu.
Pia kwa wale waliojaaliwa kuitekeleza wajibidiiishe katika kuwa katika msimamo thabiti katika dini na pia kuwahamasisha wengine kuitekeleza nguzo huu kama wao walivyofanikiwa kuitekeleza.
Chanzo: ZanziNews
No comments :
Post a Comment