Mwenyekiti wa Kamati ya Uandishi wa Bunge Maalu la Katiba, Mhe. Andrew Chenge akiwasilisha Rasimu iliyopendekezwa ndani ya bunge hilo leo 24 Septemba, 2014 mjini Dodoma. |
Jumla ya ibara 274 katika Rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zimependekezwa na Bunge Maalum la Katiba (BMK).
TAARIFA FUPI YA KAMATI YA UANDISHI YA BUNGE MAALUM KUHUSU IBARA ZA RASIMU YA KATIBA YA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA PAMOJA NA SURA MPYA
(Imeandaliwa kwa mujibu wa Kanuni ya 35(6), 35(6A), 35(7) na 35(9) ya Kanuni za Bunge Maalum za mwaka 2014)
______________________________
1.0 UTANGULIZI
(SHUKRANI)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kutumia fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyetuwezesha kujadili Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa na iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba na hatimaye kuandaa Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa ambayo leo inawasilishwa mbele ya Wajumbe wa Bunge Maalum.
Pia nichukue fursa hii kutoa shukrani kwa Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye alianzisha mchakato wa kuandika katiba mpya kwa ajili ya Watanzania wote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kuipongeza iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwa kazi kubwa waliyoifanya ya kukusanya maoni ya wananchi na kuandaa Rasimu ya Katiba ambayo ndio ulikuwa msingi mkuu wa majadiliano katika Kamati 12 za Bunge Maalum. Baada ya majadiliano, Kamati ziliandaa taarifa ambazo zimekuwa msingi wa kutayarisha Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa ninayowasilisha leo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile namshukuru Mwenyekiti wa Bunge Maalum, Mhe. Samuel John Sitta, kwa kuniteua kuwa Mjumbe wa Kamati ya Uandishi na hatimaye Wajumbe wa Kamati hiyo kunichagua kuwa Mwenyekiti. Kwa uteuzi huo umenifanya niwe sehemu ya historia ya nchi yetu katika kuandika katiba mpya. Aidha, nakupongeza wewe, Mhe. Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuliongoza Bunge Maalum kwa busara na weledi uliotuwezesha kufika katika hatua hii muhimu.
Pia, nawashukuru Wajumbe wote wa Kamati 12 za Bunge Maalum kwa kujadili na kutoa mapendekezo ambayo yameboresha Rasimu ya Katiba. Kamati zilitayarisha Taarifa na kuziwasilisha kwenye Bunge Maalum na Wajumbe walizijadili kwa pamoja na kutoa maoni yao. Matokeo ya Taarifa hizo na mijadala ndani ya Bunge Maalum ndivyo vilivyotoa mwongozo kwa Kamati ya Uandishi katika kuandaa Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kumshukuru Katibu wa Bunge Maalum, Ndugu Yahya Khamis Hamad, Naibu Katibu wa Bunge Maalum, Dkt. Thomas D. Kashilillah, na Sekretarieti ya Kamati ya Uandishi ikiongozwa na Mussa Kombo, Stephen Kagaigai, na Sarah Barahomoka, kwa umakini, weledi wa hali ya juu, na moyo wao wa kufanya kazi kwa kujituma bila kuchoka, usiku na mchana. Jitihada zao zimewezesha Kamati ya Uandishi kukamilisha kazi ya kuandaa Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa kwa wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, nawashukuru Wajumbe wa Kamati ya Uandishi kwa weledi na uzalendo waliouonesha kwa Taifa lao kwa kujitoa usiku na mchana, wakati mwingine hadi alfajiri bila kuchoka wala kulalamika ili kuhakikisha kazi inakamilika kwa wakati. Nawapongeza kwa kukamilisha kazi ya kuandaa Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa. Kazi waliyoifanya ni kubwa sana na haina kifani.
MAELEKEZO
Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe 15 Septemba 2014, kwa mujibu wa kanuni ya 35(6A) ya Kanuni za Bunge Maalum za Mwaka 2014, uliielekeza Kamati ya Uandishi kuzifanyia kazi Taarifa za Kamati pamoja na mapendekezo yaliyotolewa na Wajumbe wakati wa mjadala ndani ya Bunge Maalum.
MAJUKUMU YA KAMATI
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa kanuni ya 35(7) ya Kanuni za Bunge Maalum za Mwaka 2014, Kamati ya Uandishi ilipewa jukumu la kuandaa Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa. Katika kutekeleza jukumu hilo, Kamati ya Uandishi iliongozwa na mambo matatu ya msingi:
(a) Mapendekezo ya Wajumbe walio wengi katika Kamati 12 za Bunge Maalum kwa kila Ibara ya Rasimu ya Katiba na mjadala
katika Bunge Maalum. Wakati mwingine, kutegemeana na uzito wa hoja husika, mapendekezo ya Wajumbe walio wachache pia yalizingatiwa;
(b) Katiba za nchi nyingine; na
(c) Misingi ya uandishi wa Katiba.
Kwa kuzingatia misingi hii, Kamati ya Uandishi inawasilisha Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa yenye:
(a) Ibara zenye maudhui yanayozingatia uandishi wa Katiba;
(b) Ibara zenye mpangilio na mtiririko mzuri; na
(c) Kutumia lugha ya kisheria na Kiswahili fasaha.
2.0 RASIMU YA KATIBA INAYOPENDEKEZWA
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kupitia na kuchambua maoni na mapendekezo ya Taarifa za Kamati zote pamoja na maoni na
mapendekezo yaliyotolewa na Wajumbe wakati wa mjadala ndani ya Bunge Maalum, Kamati ya Uandishi ilibaini maeneo ambayo Wajumbe wengi waliyatolea mapendekezo wakati wa kuchangia kwenye Kamati za Bunge Maalum na ndani ya Bunge Maalum ambayo ni pamoja na yafuatayo:
(a) Muundo wa Muungano na Serikali;
(b) Tunu za Taifa;
(c) Usawa wa jinsia;
(d) Maadili na miiko ya uongozi wa umma;
(e) Uraia;
(f) Muundo na mamlaka ya Bunge;
(g) Uwiano wa asilimia 50 kwa 50 baina ya Wabunge wanawake na Wabunge wanaume katika Bunge la Jamhuri ya Muungano;
(h) Muundo wa Mahakama;
(i) Masuala ya uchaguzi kuhusu mgombea huru, Tume Huru ya Uchaguzi na kuhoji matokeo ya uchaguzi wa Rais mahakamani;
(j) Ardhi, maliasili na mazingira;
(k) Mahakama ya Kadhi;
(l) Mamlaka ya Rais wa Zanzibar;
(m) Mamlaka ya Zanzibar kukopa;
(n) Nafasi ya Rais wa Zanzibar katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano;
(o) Misingi ya matumizi ya fedha za umma;
(p) Tume ya Pamoja ya Fedha na Akaunti ya Fedha ya Pamoja;
(q) Serikali za Mitaa na Ugatuzi wa madaraka;
(r) Haki za vijana, haki za wanawake, haki za watu wenye ulemavu, haki za watoto, haki za wasanii, haki za wazee, haki za wakulima, wavuvi, wafugaji, na wachimbaji wadogo wa madini;
(s) Malengo muhimu ya kiuchumi;
(t) Ukomo wa ubunge na kumwajibisha Mbunge;
(u) Mawaziri kutokuwa Wabunge;
(v) Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa kuingiza katika Katiba;
(w) Baadhi ya viongozi wa kuteuliwa na Rais kuthibitishwa na Bunge; na
(x) Rais kuzingatia ushauri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati inapenda kusisitiza jambo moja la msingi nalo ni kwamba Katiba ya nchi yoyote ni sheria mama ya sheria zote. Hivyo basi, katika kuandaa Katiba mpya ya nchi yetu ni muhimu kuzingatia kwamba Katiba huandikwa kwa namna ambayo inaondoa ulazima wa kuifanyia mabadiliko ya mara kwa mara kama inavyofanyika kwa sheria za kawaida. Kwa kuzingatia msingi huo, Katiba ya nchi inapaswa iweke masharti magumu zaidi ya kuifanyia mabadiliko. Kwa mfano, ili kulinda kuwepo kwa Jamhuri ya Muungano, Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Mwaka 1977 inataka uamuzi juu ya suala hilo uungwe mkono na theluthi mbili ya kura za Wabunge wote kutoka Tanzania Bara na theluthi mbili ya kwa Wabunge kutoka Zanzibar. Kwa msingi huo, Rasimu ya Katiba, pamoja na mambo mengine, inapendekeza uamuzi wa kuwepo kwa Jamhuri ya Muungano uamuliwe na wananchi wenyewe kupitia kura ya maoni. Ni kwa mantiki hiyo, Kamati ya Uandishi imeandaa Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa, ikiwa na mambo machache ambayo ni ya msingi yanayohusu uongozi na utawala wa nchi na kuacha mambo mengine yote ya uendeshaji wa shughuli za Serikali yawekwe kwenye sheria za kawaida za nchi ili ziweze kubadilishwa kwa urahisi kulingana na mahitaji ya sekta husika yanavyobadilika, tofauti na mambo ya msingi ambayo kwa kawaida huwa hayabadiliki katika muda mfupi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba nieleze kwa kifupi kuhusu mapendekezo yaliyotolewa na Wajumbe wa Kamati za Bunge Maalum na namna ambavyo yamezingatiwa na Kamati ya Uandishi.
SURA YA KWANZA
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sura hii inahusu Jamhuri ya Muungano na imegawanyika katika sehemu kuu mbili. Sehemu ya kwanza inahusu Jina, Mipaka, Alama, Lugha na Tunu za Taifa na sehemu ya pili inahusu Mamlaka ya Wananchi, Utii na Hifadhi ya Katiba.
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA (IBARA YA 1)
Mheshimiwa Mwenyekiti, miongoni mwa mambo yaliyozua mjadala mkali katika Kamati za Bunge Maalum na ndani ya Bunge Maalum, ni mfumo na muundo wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Rasimu ya Katiba katika ibara ndogo ya (1) imependekeza Jamhuri ya Muungano iwe na muundo wa Shirikisho la Serikali tatu, yaani Serikali ya Tanganyika, Serikali ya Zanzibar na Serikali ya Shirikisho. Hata hivyo, licha ya kuwepo kwa Wajumbe wachache waliotaka Ibara hii ibaki kama ilivyo kwenye Rasimu, maoni na mapendekezo ya Wajumbe walio wengi kwenye Kamati zote 12 za Bunge Maalum pamoja na Wajumbe wengi waliochangia katika mjadala kuhusu Ibara hii, walipendekeza kufutwa kwa dhana ya Shirikisho kwa sababu zifuatazo:
(i) Hati ya Makubaliano ya Muungano ya tarehe 22 Aprili, 1964 iliyorejewa katika Ibara ya 1(1) ndio msingi mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hati hiyo ya Muungano haikuanzisha muundo wa Shirikisho lenye serikali tatu bali ilianzisha muundo wa Muungano wa serikali mbili, yaani Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Hivyo, kuleta dhana ya “Shirikisho” ni kukiuka Makubaliano yaliyopo katika Hati hiyo.
(iii) Mapendekezo ya kuanzisha muundo wa Shirikisho yanakinzana na masharti yaliyowekwa na kifungu cha 9(2) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83 kinachokazia kuwepo kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwa ni nchi moja na dola moja yenye muundo wa Muungano wa serikali mbili.
(iv) Muundo wa Shirikisho utasababisha mgawanyiko katika jamii ambayo kwa kipindi kirefu cha nusu karne imekuwa na utangamano uliojengeka kwa misingi ya udugu na mshikamano baina ya wananchi wa pande zote mbili za Muungano. Utengamano na mgawanyiko utasababishwa na wanashirikisho kuwa na hisia kubwa za utaifa wa nchi zao, na hivyo kuvunja Muungano.
(v) Utatuzi wa kero za Muungano hautegemei wingi au idadi ya serikali bali dhamira thabiti waliyonayo viongozi katika kukabiliana na changamoto hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wajumbe wa Kamati ya Uandishi baada ya kutafakari na kushauriana kwa kina kuhusu sababu zilizotolewa na Wajumbe walio wengi za kutaka kufuta dhana ya shirikisho, Kamati imerekebisha Ibara hiyo kama inavyosomeka katika Ibara ya 1 ya Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa.
ENEO LA JAMHURI YA MUUNGANO (IBARA YA 2)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mipaka ya Jamhuri ya Muungano lililobainishwa katika Ibara ya 2 ya Rasimu ya Katiba lilichangiwa na Wajumbe wengi ambao walipendekeza kuongeza baadhi ya maneno kama vile anga, mito, maziwa, milima, bahari kuu na kitanda cha bahari kwa lengo la kufafanua zaidi mipaka ya eneo la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Wajumbe wengine walipendekeza kurejesha mamlaka ya Rais wa Jamhuri ya Muungano kuigawa Jamhuri ya Muungano katika mikoa, wilaya na maeneo mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyapitia mapendekezo hayo na kwa kuzingatia masharti ya Sheria inayotawala masuala ya mipaka, Sura ya 238 (The Territorial Sea and Exclusive Economic Zone Act, Cap.238) ambayo imetamka wazi kwamba eneo la bahari linajumuisha eneo la anga juu ya eneo lake la bahari (air space), kitanda cha bahari (sea bed) na eneo la chini ya ardhi ya bahari (sub soil). Ibara kama ilivyo kwenye Rasimu ya Katiba inaainisha mipaka ya Kimataifa ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayotambulika na mikataba mbalimbali ya kimataifa na Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya Bahari wa Mwaka 1982. Hivyo basi, Kamati haikufanya marekebisho katika Rasimu ya Katiba kuhusu eneo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Hata hivyo, Kamati ya Uandishi imerekebisha Ibara hii kwa kuongeza ibara ndogo ya (2) na (3). Ibara ndogo ya (2) inaweka masharti kuhusu mamlaka ya Rais kuigawa Jamhuri ya Muungano katika mikoa, wilaya na maeneo mengine ya kiutawala. Aidha, ibara hii ndogo imempa uwezo Rais wa Jamhuri ya Muungano kukasimu kwa Rais wa Zanzibar mamlaka ya kugawa maeneo ya utawala kwa upande wa Zanzibar. Ibara ndogo ya (3) inaweka masharti kwa Bunge kutunga sheria itakayofafanua mipaka ya eneo la Jamhuri ya Muungano. Ibara hizo ndogo zimeandikwa kama zinavyosomeka katika Ibara 2 ya Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa.
TUNU ZA TAIFA (IBARA YA 5)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ibara ya 5 ya Rasimu ya Katiba ilipendekeza kuwe na Tunu 7 za Taifa ambazo ni: utu, uzalendo, uadilifu, umoja, uwazi, uwajibikaji na lugha ya Taifa. Aidha, Kamati zote 12 zilipendekeza kuongeza tunu za amani na utulivu, haki na usawa wa binadamu na usawa wa jinsia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, neno “tunu” linatafsiriwa na Kamusi ya Kiswahili Sanifu, Toleo la Pili (Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili, 2004) kuwa ni kitu anachopewa mtu na mwingine kuwa ni ishara ya mapenzi: hidaya, zawadi, addia, hiba, au azizi au kitu ambacho ni adimu kupatikana na chenye kutumika kwa nadra. Kwa mantiki hii, tunu ni kitu ambacho mtu au taifa linakiona kama tunu na ambacho inacho “mkononi” na si matarajio, matamanio au kitu ambacho mtu anapenda kuwa nacho. Vilevile, tunu ni kitu cha thamani ambacho taifa limetunukiwa, na si maadili ya kitaifa (tunu ni valuable, na siyo national values.)
Hivyo basi, Kamati ya Uandishi baada ya kuzingatia tafsiri ya neno tunu katika kamusi mbalimbali, na jukumu la Jamhuri ya Muungano “kuenzi na kuzingatia” tunu za Taifa, na mapitio ya katiba za nchi mbalimbali kama vile Kenya, Zimbabwe na Zambia, imeainisha tunu za taifa kwa kuzitenganisha na misingi ya utawala bora kama vile uzalendo, uadilifu, uwazi na uwajibikaji ambayo imewekewa ibara yake mahsusi. Kamati ya Uandishi imerekebisha Ibara hiyo kwa kubakiza tunu 4 za Taifa ambazo ni lugha ya Kiswahili, Muungano, utu na udugu, na amani na utulivu kama zinavyoonekana katika Ibara ya 5 ya Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa.
UTAWALA BORA (IBARA YA 6)
Mheshimiwa Mwenyekiti, misingi ya utawala bora ya uzalendo, uadilifu, uwazi na uwajibikaji iliyokuwa imependekezwa katika Rasimu ya Katiba kama tunu, imetengenezewa Ibara yake pamoja na misingi mingine ya utawala bora ambayo haikuzingatiwa. Ibara mpya iliyoongezwa inaweka masharti kuhusu misingi ya utawala bora ambayo ni uwazi, uwajibikaji, uadilifu, demokrasia, ushirikishwaji wa wananchi, utawala wa sheria, umoja wa kitaifa, uzalendo, haki za binadamu na usawa wa jinsia. Lengo la kuwa na Ibara hii mpya ni kustawisha utawala bora nchini kwa kuhimiza wananchi na Serikali kufuata misingi hiyo iliyotajwa katika kutekeleza shughuli na majukumu ya kila siku. Hivyo, Ibara hii isomeke kama inavyoonekana katika Ibara ya 6 ya Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa.
SURA YA PILI
MALENGO MUHIMU, MISINGI YA MWELEKEO WA
SHUGHULI ZA SERIKALI NA SERA ZA TAIFA
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sura ya Pili ya Rasimu ya Katiba inaweka masharti kuhusu malengo muhimu, misingi ya mwelekeo wa shughuli za Serikali na sera za Taifa. Maudhui makuu ya Sura hii ni kuainisha masharti kuhusu malengo muhimu ya nchi yetu na hivyo kutoa dira na mwelekeo kwa Serikali na taasisi zake. Malengo yaliyoelezwa katika Sura hii ni ya kisiasa, kiuchumi, kijamii na kiutamaduni. Aidha, Sura hii inaweka misingi kuhusu namna malengo na sera zitakavyotekelezwa kitaifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Rasimu ya Katiba ilikuwa ikiainisha malengo yote katika sehemu moja. Kamati ya Uandishi, kwa kuzingatia mapendekezo yaliyotokana na mjadala ndani ya Bunge Maalum, imeainisha malengo hayo kwa kuyapanga katika sehemu tano za Sura ya Pili. Sehemu ya Kwanza inahusu malengo makuu kwa ujumla; Sehemu ya Pili inahusu malengo ya kisiasa; Sehemu ya Tatu inahusu malengo ya kiuchumi, kijamii na kiutamaduni; na Sehemu ya Nne inahusu utafiti, dira ya maendeleo, mipango na utekelezaji wa malengo ya Taifa na Sehemu ya Tano inahusu Sera ya Mambo ya Nje. Ibara ndogo ya 10(3)(e) ya Rasimu ya Katiba imehamishiwa kwenye Sura mpya, Sura ya Tatu, inayohusu ardhi, maliasili na mazingira. Kamati ya Uandishi imefanya marekebisho machache ya kiufundi katika sehemu zote isipokuwa Sehemu ya Tatu ambayo imefanyiwa marekebisho ya kimaudhui.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu ya tatu inaainisha lengo la kujenga uchumi wa kisasa wa Taifa linalojitegemea kwa kuzingatia elimu ya sayansi na teknolojia katika nyanja zote za uzalishaji mali kwa kuhimiza mapinduzi ya kilimo, ufugaji, na uvuvi, mapinduzi ya viwanda na kujenga sekta muhimu ya nishati, mawasiliano na miundombinu. Vile vile, katika Sehemu ya Nne yamewekwa masharti yanayoitaka Serikali ya Jamhuri ya Muungano kuwasilisha taarifa ya hatua ilizozichukua katika utekelezaji wa malengo ya Taifa katika Bunge la Jamhuri ya Muungano mara moja kwa mwaka.
NB SOMA IBARA YA 13, 14, 16 ISIPOKUWA IBARA 20 NA 21.
SURA YA TATU
ARDHI, MALIASILI NA MAZINGIRA
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sura ya Tatu ya Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa ni kati ya Sura mpya zilizopendekezwa na Kamati mbalimbali za Bunge Maalum. Kamati Sita (6) kati ya Kamati Kumi na Mbili (12) zilipendekeza kuongezwa kwa Sura mpya inayohusu ardhi, maliasili na mazingira. Maeneo yaliyojadiliwa ni pamoja na umiliki na utatuzi wa migogoro ya ardhi, umiliki na usimamizi wa maliasili za taifa, na haki na wajibu kuhusu mazingira. Kamati ya Uandishi, kwa kuzingatia mapendekezo kuhusu Ibara za Sura mpya, na kwa kutambua kwamba ardhi, maliasili na mazingira siyo masuala yaliyopo katika orodha ya mambo ya Muungano, inapendekeza Sura mpya inayohusu Ardhi, Maliasili na Mazingira kama inavyosomeka katika Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa. NB SOMA IBARA ZA 22, 23, 24, 25 NA 26.
SURA YA NNE
MAADILI NA MIIKO YA UONGOZI NA UTUMISHI WA UMMA
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sura ya Nne ya Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa inahusu maadili na miiko ya uongozi na utumishi wa umma na imegawanyika katika sehemu mbili. Sehemu ya kwanza inaweka masharti yahusuyo maadili ya uongozi na utumishi wa umma na sehemu ya pili inahusu miiko ya uongozi wa umma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wajumbe wa Bunge Maalum walikuwa na maoni kuwa maadili na miiko ya uongozi na utumishi wa umma ni mambo muhimu katika kujenga uwajibikaji, uadilifu na uzalendo wa viongozi na watumishi wa umma kwa maendeleo ya wananchi. Aidha, Wajumbe wengine walieleza kuwa wako viongozi ambao hawawajibiki na siyo waadilifu kutokana na kukosekana kwa misingi mikuu ya maadili na miiko ya viongozi na utumishi wa umma katika Katiba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati ya Uandishi, kwa kuzingatia mapendekezo yaliyotolewa katika Kamati za Bunge Maalum na wakati wa mjadala ndani ya Bunge Maalum, na msingi kwamba Katiba inapaswa kubeba misingi mikuu tu na kuacha ufafanuzi wa misingi hiyo katika sheria za nchi, imefanya marekebisho ya kiuandishi katika Sura hii. Hivyo Ibara za Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa baada ya kufanyiwa marekebisho ni kama zinavyoonekana kwenye Ibara za 27, 28, 29 na 30 za Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa. NB SOMA IBARA YA 27, 28, 29 NA 30 ZA RASIMU YA KATIBA INAYOPENDEKEZWA
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusoma maudhui ya Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa kwenye eneo hili, ni dhahiri kwamba madai yanayotolewa kuwa mapendekezo makubwa yaliyowekwa katika Rasimu ya Katiba yamefutwa, si kweli.
HAKI ZA BINADAMU, WAJIBU WA RAIA, JAMII NA
MAMLAKA YA NCHI
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sura hii inahusu haki za binadamu, wajibu wa raia, jamii na mamlaka za nchi na imegawanyika katika Sehemu Kuu Mbili. Sehemu ya kwanza inahusu haki za binadamu na Sehemu ya Pili inahusu wajibu wa raia na mamlaka za nchi na mipaka ya haki za binadamu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Sura hii mjadala kwenye Kamati na ndani ya Bunge Maalum ulijikita katika maeneo yafutayo:
(i) Uhuru wa vyombo vya habari,
(ii) Uhuru wa imani ya dini;
(iii) Haki ya kumiliki mali;
(iv) Haki ya mtoto;
(v) Haki na wajibu wa vijana;
(vi) Haki za watu wenye ulemavu;
(vii) Haki za wanawake;
(viii) Haki za wazee; na
(ix) Haki za wasanii
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Ibara ya 32 ya Rasimu ya Katiba inayohusu uhuru wa imani ya dini, Kamati ya Uandishi, kwa kuzingatia hukumu ya Mahakama ya Rufani katika kesi ya Zakaria and 126 others vs the Minister of Education and Vocational Training and the Attorney General, Civil Appeal No. 3 of 2012 iliyoamua kuhusu uhuru wa dhamiri, imeongeza neno dhamiri katika ibara ndogo ya (1) ili kuondoa upungufu ulio katika Ibara hii kuhusu dhamiri ya mtu. Ibara hiyo inasomeka kama inavyoonekana katika Ibara ya 40 ya Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Rasimu ya Katiba, haki zote za msingi zilizingatiwa kwa ufasaha. Hata hivyo, Kamati 12 za Bunge Maalum zilipendekeza maboresho katika maeneo machache ikiwa ni pamoja na haki za watoto, wanawake, walemavu na wazee. Pia zilipendekeza kuongeza haki za wabunifu na wagunduzi. Ibara zilizoboreshwa zinasomeka kama zinavyoonekana katika Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu haki za vijana, wakati wa mjadala ndani ya Bunge Maalum Wajumbe wengi walipendekeza kuundwa chombo huru cha vijana kitakachosimamia masuala ya haki na wajibu kwa vijana. Kamati ya Uandishi kwa kuzingatia mapendekezo hayo, imeongeza ibara ndogo (2) inayotoa uhuru wa vijana kuanzisha Baraza la Vijana kwani vijana ndio nguvu kazi ya Taifa ambayo inakadiriwa kufikia asilimia zaidi ya sabini ya wananchi wa Tanzania. Ibara ndogo ya (2) inasomeka kama inavyoonekana kwenye Ibara ya 51 ya Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu haki za wasanii, Kamati mbalimbali za Bunge Maalum na Wajumbe walio wengi waliochangia mjadala ndani ya Bunge Maalum walipendekeza haki za wasanii ziingizwe kwenye Katiba ili kuainisha Haki za wasanii kwa lengo la kuwapatia haki na ulinzi wa kikatiba. Kamati ya Uandishi baada ya kutafakari mapendekezo haya imeongeza Ibara mpya ili kuweka masharti ya Katiba ambayo pamoja na mambo mengine, inaipa Serikali jukumu la kukuza na kuendeleza sanaa na kutambua haki miliki za wasanii. Ibara husika inasomeka kama inavyoonekana katika Ibara ya 56 ya Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa.
SURA YA SITA
URAIA KATIKA JAMHURI YA MUUNGANO
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sura hii inayohusu uraia katika Jamhuri ya Muungano inaainisha aina mbili za uraia kuwa ni uraia wa kuzaliwa na kuandikishwa. Kamati ya Uandishi, kwa kuzingatia taarifa za Kamati 12 za Bunge Maalum na mjadala ndani ya Bunge Maalum, imefanya maboresho ya Ibara za Sura hii ikiwa ni pamoja na kuainisha maeneo ambayo Bunge litatunga sheria ili kuwawezesha watu waliozaliwa Tanzania lakini waliopoteza uraia kurejeshewa uraia huo. Maboresho haya yako kama yanavyosomeka kwenye Ibara ya 67(6) ya Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ibara ya 69 ya Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa inahusu hadhi maalum ya watu wenye asili au nasaba ya Tanzania. Maudhui ya Ibara hii ni kuwatambua na kuwapa hadhi maalum watu wenye asili au nasaba ya Tanzania ambao wameacha kuwa raia wa Tanzania kwa kupata uraia wa nchi nyingine pindi wanaporudi Tanzania. Kamati nane zimependekeza Ibara hii ibaki kama ilivyo katika Rasimu ya Katiba. Kamati nne zimependekeza marekebisho yanayolenga kuboresha maudhui yaliyomo kwenye Ibara hii, kwa kupendekeza uraia wa nchi mbili (uraia pacha).
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati ya Uandishi baada ya kupokea mapendekezo ya Kamati pamoja na mapendekezo ya Wajumbe katika mijadala ya Bunge Maalum, ilifanya rejea katika Katiba za nchi nyingine kuhusu suala hili. Katika utafiti huo, Kamati ya Uandishi ilibaini kuwa Katiba za nchi mbali mbali ambazo haziruhusu uraia wa nchi mbili, zimewapa hadhi maalum watu hao. Moja ya nchi hizo ni India ambayo huwapa watu wenye nasaba ya nchi hiyo hadhi maalum inayoitwa "Persons of Indian Origin" ambayo huwezesha watu wenye nasaba ya India kupata haki mbali mbali ikiwa ni pamoja na; kutohitaji viza ya kuingia na kutoka, kuruhusiwa kukaa miezi sita bila kuhitaji kujiandikisha uhamiaji, kupata huduma za kiuchumi, kifedha na elimu kama ilivyo kwa raia wengine, kununua, kumiliki, kuhamisha na kuuza mali isiyohamishika isipokuwa mashamba makubwa ya kilimo, haki ya kupata makaazi n.k. Hata hivyo, watu hao hawaruhusiwi kupiga kura wala kugombea nafasi yoyote ya kisiasa wala kushika madaraka ya utawala.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati ya Uandishi baada ya uchambuzi huo, inaona hadhi maalum inayopendekezwa kutolewa kwa watu wenye nasaba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambao wameacha kuwa raia wa Jamhuri ya Muungano, inatosheleza mahitaji ya diaspora. Kwa mantiki hiyo, fursa mbali mbali zinazopendekezwa na Wajumbe wanaopendekeza dhana ya uraia wa nchi mbili, zinaweza kupatikana na kuwekwa vizuri kwa mujibu wa sheria baada ya msingi wake kuwekwa katika Katiba. Ibara hiyo inasomeka kama inavyoonekana Ibara ya 69 ya Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa.
SURA YA SABA
MUUNDO WA JAMHURI YA MUUNGANO
MUUNDO WA MUUNGANO (IBARA YA 70)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sura hii inahusu muundo wa Jamhuri ya Muungano, ambapo Rasimu ya Katiba imependekeza muundo wa Serikali tatu. Wajumbe walio wengi walipendekeza Ibara hii ifanyiwe marekebisho kwa kuondoa dhana ya Serikali tatu na badala yake kuweka dhana ya Serikali mbili kwani Hati ya Makubaliano ya Muungano ya Mwaka 1964 ndio msingi mkuu wa kuwa na muundo wa Serikali mbili ambapo Zanzibar ilikubali kuhamishia sehemu ya mamlaka yake hasa yanayohusu masuala ya Muungano kwenye Serikali ya Muungano na Tanganyika ilikubali kuhamishia mamlaka yake yote kwenye Serikali ya Jamhuri ya Muungano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati ya Uandishi, kwa kuzingatia maoni ya Wajumbe walio wengi na baada ya kutafakari kwa kina sababu za Wajumbe walio wengi za kutaka kufuta dhana ya muundo wa Serikali tatu na badala yake kuweka dhana ya muundo wa Serikali mbili, imerekebisha Ibara hiyo kama inavyosomeka katika Ibara ya 70 ya Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kufuatia maboresho ya Ibara ya 70, Kamati ya Uandishi imeongeza Ibara mpya ya 71 katika Rasimu ya Katiba Inayopendekeza ili kuweka masharti kuhusu utekelezaji wa shughuli za mamlaka ya nchi. Ibara hii iliyoandikwa upya inaainisha vyombo viwili vyenye mamlaka ya utendaji, vyombo viwili vyenye mamlaka ya utoaji haki na vyombo viwili vyenye mamlaka ya kutunga sheria na kusimamia utekelezaji wa shughuli za umma. Vile vile, Ibara hii inaweka bayana kuwa Mambo ya Muungano ni yale yaliyoorodheshwa kwenye Nyongeza ya Kwanza ya Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa ambayo ni:
1. Katiba na Mamlaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
2. Ulinzi na usalama wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
3. Usalama na Usafiri wa Anga.
4. Uraia na uhamiaji.
5. Jeshi la Polisi.
6. Sarafu na Benki Kuu.
7. Kodi ya Mapato inayolipwa na watu binafsi na Mashirika, ushuru wa forodha na ushuru wa bidhaa zinazotengenezwa nchini Tanzania na zinazosimamiwa na Idara ya Forodha.
8. Mambo ya nje.
9. Usajili wa vyama vya siasa.
10. Mahakama ya Juu na Mahakama ya Rufani.
11. Elimu ya Juu.
12. Baraza la Taifa la Mitihani na mambo yote yanayohusika na kazi za Baraza hilo.
13. Utabiri wa hali ya hewa.
14. Utumishi katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wajumbe walio wengi wa Kamati 12 za Bunge Maalum walipendekeza Ibara ya 62 ya Rasimu ya Katiba irekebishwe ili kuondoa dhana ya Serikali tatu na kuipa mamlaka Serikali ya Jamhuri ya Muungano kutekeleza mambo yasiyo ya muungano yanayohusu Tanzania bara. Baada ya marekebisho hayo, Ibara ya 72 ya Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa inahusu mamlaka ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano kwa mambo ya muungano na mambo yanayohusu Tanzania Bara.
MAMLAKA YA SERIKALI YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR KWA MAMBO YASIYO YA MUUNGANO (IBARA YA 73)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Taarifa za Kamati 12 za Bunge Maalum na mapendekezo wakati wa mjadala ndani ya Bunge Maalum kuhusu mamlaka ya Zanzibar juu ya mambo mbalimbali yahusuyo Zanzibar, Wajumbe walio wengi walipendekeza Katiba hii itoe mamlaka yafuatayo kwa Zanzibar:
(i) Mamlaka ya kuanzisha uhusiano au ushirikiano na jumuiya au taasisi yoyote ya kikanda au kimataifa;
(ii) Kuomba na kupata ushirikiano kutoka kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano endapo katika kufanikisha uhusiano au ushirikiano na jumuiya au taasisi za kikanda na kimataifa utahitaji dhamana au uthibitisho wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano; na
(iii) Mamlaka ya Zanzibar kukopa fedha kutoka katika taasisi za fedha za kikanda na kimataifa kwa ajili ya kufanikisha utekelezaji wa majukumu ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia mapendekezo ya Wajumbe walio wengi, Kamati ya Uandishi, baada ya kuzingatia mapendekezo ya Kamati zote na maoni ya Wajumbe waliochangia kuhusu mamlaka ya Zanzibar imerekebisha Ibara hii ili kuzingatia mambo yaliyotajwa hapo juu kama inavyosomeka katika Ibara ya 73 ya Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa.
MAHUSIANO KATI YA SERIKALI YA JAMHURI YA MUUNGANO NA SERIKALI YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR (IBARA YA 74)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ibara ya 74 inahusu mahusiano kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Kamati kwa kutambua umuhimu wa mahusiano kati ya Serikali hizi mbili zilipendekeza Ibara hii irekebishwe kwa kuondoa dhana ya Serikali tatu. Kamati ya Uandishi, baada ya kuzingatia mapendekezo hayo imeboresha Ibara hiyo kama inavyosomeka katika Ibara ya 74 ya Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa.
WAJIBU WA VIONGOZI WAKUU KULINDA MUUNGANO
(IBARA YA 75)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa za Kamati 12 za Bunge Maalum zilionesha kuwa suala la wajibu wa viongozi wakuu kulinda Muungano lilijadiliwa sana na Wajumbe kwenye Kamati na ndani ya Bunge Maalum. Mjadala ulijikita katika kubainisha ni viongozi gani wanaotakiwa kupewa wajibu wa kuulinda Muungano. Kamati, katika maoni ya Wajumbe walio wengi, zilipendekeza kufanya marekebisho madogo ya kuondoa maneno yenye dhana ya Serikali tatu kama vile kufuta maneno Rais wa Tanganyika. Aidha, Kamati zilipendekeza kuongeza viongozi wafuatao ili wawe miongoni mwa viongozi wakuu wenye wajibu wa kuulinda Muungano. Viongozi hao ni:
(i) Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano; na
(ii) Makamu wa Rais wa Zanzibar.
Mheshimiwa Mwenyekiti, viongozi hawa wanaongezwa kwa kuwa Rasimu ya Katiba ilikuwa na dhana ya nchi washirika kuwa na Katiba zao na hivyo kuwa na viongozi wao. Baada ya marekebisho hayo Kamati ya Uandishi imeiandika upya Ibara hiyo kama inavyosomeka katika Ibara ya 75 ya Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa.
SURA YA NANE
SERIKALI YA JAMHURI YA MUUNGANO
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sura ya saba ya Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa inahusu Serikali ya Jamhuri ya Muungano na imegawanyika katika Sehemu kuu mbili, Sehemu ya Kwanza inahusu Serikali, Rais na Makamu wa Rais na Sehemu ya Pili inahusu Baraza la Mawaziri la Serikali ya Jamhuri ya Muungano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sura hii imefanyiwa maboresho makubwa ya kimaudhui na kiuandishi katika Ibara zake mbalimbali pamoja na kuingizwa mambo mapya kwa kuzingatia muundo wa serikali mbili. Pamoja na mambo mengine, mambo hayo yaliyoingizwa ni kuhusu Makamu wa Rais, Rais wa Zanzibar kuwa Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Wakuu wa Mikoa, Naibu Mwanasheria Mkuu, Mkurugenzi wa Mashtaka na madaraka kwa umma.
NAFASI YA MAKAMU WA RAIS (IBARA ZA 96 – 104)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu nafasi ya Makamu wa Rais, Kamati 10 za Bunge Maalum, katika maoni ya Wajumbe walio wengi, zilipendekeza kuwepo kwa Makamu watatu wa Rais ambao ni Makamu wa Kwanza wa Rais, ambaye anachaguliwa pamoja na Rais katika Uchaguzi Mkuu; Rais wa Zanzibar ambaye anakuwa Makamu wa Pili wa Rais kutokana na nafasi yake ya kuwa Rais wa Zanzibar; na Waziri Mkuu ambaye anakuwa Makamu wa Tatu wa Rais kutokana na nafasi yake ya kuwa Waziri Mkuu. Ibara husika zinasomeka kama zinavyoonekana katika Ibara ya 96 hadi 104 za Rasimu ya Katika Inayopendekezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la Rais wa Zanzibar kuwa Makamu wa Rais ni la msingi kwani Rais wa Zanzibar ni kiungo muhimu kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano kwa kuzingatia kwamba alikuwa mmoja wa Makamu wa Rais tangu Muungano ulipoasisiwa Mwaka 1964 hadi hapo mfumo wa vyama vingi uliporejeshwa nchini Mwaka 1992. Hivyo basi, Rais wa Zanzibar anapokuwa Makamu wa Rais ni ishara ya kudumisha Muungano na kuimarisha muundo wa Serikali mbili. Kamati ya Uandishi imeiandika Ibara husika kwa kuainisha masharti yanayohusu nafasi ya Makamu wa Pili wa Rais kama inavyosomeka katika Ibara ya 103 ya Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa.
NAFASI YA WAZIRI MKUU (IBARA ZA 105 – 108)
Mhe. Mwenyekiti, Kamati 12 za Bunge Maalum, katika maoni ya Wajumbe walio wengi, kwa kuzingatia muundo wa Serikali mbili, walipendekeza nafasi ya Waziri Mkuu iingizwe kwenye Katiba kwani Waziri Mkuu ni Kiongozi muhimu anayeshika madaraka ya uratibu, usimamizi na utekelezaji wa shughuli za kila siku za Serikali ya Jamhuri ya Muungano. Marekebisho yaliyoingizwa katika Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa ni mahsusi kwa ajili ya kuweka masharti kuhusu nafasi ya Waziri Mkuu, kazi na mamlaka yake pamoja na masharti kuhusu kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu. Ibara husika zinasomeka kama zinavyoonekana katika Ibara ya 105 hadi 108 za Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa.
BARAZA LA MAWAZIRI (IBARA YA 109 – 112)
Mhe. Mwenyekiti, Wajumbe walio wengi katika Kamati 12 za Bunge Maalum walipendekeza marekebisho katika uteuzi wa Mawaziri na Naibu Mawaziri kwamba watokane na Wabunge na kwamba Mawaziri kwa idadi wasiozidi thelathini (30) wakati idadi ya Naibu Mawaziri itategemea mahitaji ya Serikali. Rasimu ya Katiba ilipendekeza Mawaziri na Naibu Mawaziri wasitokane na Wabunge na pia wasizidi 10 kutokana na kupungua kwa Mambo ya Muungano. Kamati zilipendekeza utaratibu uliozoeleka wa mfumo wa demokrasia, ambapo Serikali inawajibika Bungeni uendelee kwani unahakikisha uwajibikaji wa moja kwa moja kwa wananchi kupitia chombo chao cha uwakilishi. Kamati ya Uandishi imerekebisha Ibara husika kwa kuzingatia mapendekezo ya Wajumbe walio wengi wa Kamati za Bunge Maalum kuhusu suala hili. Ibara husika zinasomeka kama zinavyoonekana katika Ibara za 110 na 111 za Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa.
MADARAKA YA UMMA (IBARA YA 119 – 121)
Mhe. Mwenyekiti, kama ilivyo kwa Sura ya Tatu kuhusu ardhi, maliasili na mazingira, suala hili si la Muungano. Hata hivyo, kwa kuwa msingi wa mamlaka ya Serikali na vyombo vyake chimbuko lake ni wananchi, na kwa kutambua umuhimu wa ushiriki wa wananchi katika mambo yanayohusu maendeleo na ustawi wao, Kamati 12 za Bunge Maalum, katika maoni ya Wajumbe walio wengi, walipendekeza kuwepo Sura kuhusu madaraka ya umma. Sura hii inaanzisha Serikali za Mitaa ambazo ni vyombo muhimu vinavyoshughulikia madaraka ya Umma kwa kugatua madaraka kwa wananchi ili kuwapa haki na mamlaka ya kushiriki katika mipango na shughuli za utekelezaji wa maendeleo katika sehemu husika na nchini kote kwa ujumla. Aidha, Serikali za Mitaa ni kiunganishi kikubwa kati ya Serikali Kuu na wananchi. Kwa kuzingatia umuhimu huo, Kamati ya Uandishi imeandika Ibara zinazoweka masharti ya kikatiba yanayohusu uanzishwaji wa Serikali za Mitaa, mamlaka na uongozi wake. Hii itawezesha Bunge au Baraza la Wawakilishi, kwa kadri itakavyokuwa, kutunga sheria kuhusu serikali za mitaa. Ibara hizo zinasomeka kama zinavyoonekana kwenye Ibara ya 119-121 ya Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa.
SURA YA TISA
UHUSIANO NA URATIBU WA SERIKALI
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sura ya Tisa ya Rasimu ya Katiba inahusu uhusiano na uratibu wa Serikali. Pamoja na mambo mengine, Sura hii inaweka masharti kuhusu kuanzishwa kwa Tume ya Usimamizi na Uratibu wa Mambo ya Muungano, majukumu ya Tume hiyo na kuunda Sekretarieti ya Tume. Wajumbe walio wengi katika Kamati 12 za Bunge Maalum walipendekeza kuwepo kwa Tume hii kwani kuna umuhimu wa kuweka katika Katiba chombo kitakachosimamia na kuratibu utekelezaji wa Mambo ya Muungano na uhusiano kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ili kudumisha Muungano. Kamati ya Uandishi imeandika Ibara za Sura hii kulingana na mapendekezo ya Wajumbe walio wengi kama inavyoonesha katika Ibara za 122 na 123 za Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa.
SURA YA KUMI
BUNGE LA JAMHURI YA MUUNGANO
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sura hii inahusu Bunge la Jamhuri ya Muungano na imegawanywa katika sehemu sita. Sehemu ya Kwanza inahusu Bunge la Jamhuri ya Muungano; Sehemu ya Pili inahusu Uchaguzi wa Wabunge; Sehemu ya Tatu inahusu Uongozi wa Bunge; Sehemu ya Nne inahusu Uratibu wa Shughuli za Bunge; sehemu ya Tano inahusu Madaraka na Haki za Bunge; na Sehemu ya Sita inahusu Tume ya Utumishi wa Bunge na Mfuko wa Bunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo la muundo wa Bunge, Rasimu ya Katiba katika Ibara ya 113 ilipendekeza Wabunge wa aina mbili, yaani, wa kuchaguliwa kwenye majimbo ya uchaguzi na wa kuteuliwa na Rais kuwakilisha watu wenye ulemavu na kwamba kila jimbo la uchaguzi liwe na Wabunge wawili, mwanamke na mwanaume. Kamati 12 za Bunge Maalum, katika mapendekezo ya Wajumbe walio wengi, zilipendekeza muundo uliopo uendelee yaani, Bunge liendelee kuwa na sehemu mbili, Rais kwa upande mmoja na Wabunge kwa upande mwingine. Pia Kamati zilipendekeza aina zifuatazo za wajumbe wa Bunge yaani, Wabunge wa kuchaguliwa kutoka katika majimbo ya uchaguzi; Wabunge watano wenye ulemavu watakaoteuliwa na Rais; Wabunge kumi watakaoteuliwa na Rais; Mwanasheria Mkuu kutokana na wadhifa wake; na Spika kama hatokani Wabunge. Ibara ya 113 ya Rasimu ya Katiba kwa kuzingatia mapendekezo ya Kamati imeandika upya kama inavyoonesha katika Ibara ya 124(1-3) ya Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu uwakilishi wa Wabunge wanawake Bungeni Kamati ya Uandishi imerekebisha Ibara ya 113(3) ya Rasimu ya Katiba kwa kuzingatia mapendekezo ya Kamati ili kuweka msingi wa uwakilishi ulio sawa baina ya Wabunge wanawake na wanaume kama inavyoonesha katika Ibara ya 124(4) ya Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ukomo wa juu wa idadi ya wabunge, Rasimu ya Katiba, katika Ibara ya 113(2), kwa kuzingatia mapendekezo ya Serikali tatu na kwamba serikali ya Shirikisho ingekuwa na Bunge dogo, inapendekeza wabunge wasiozidi 75. Kamati ya Uandishi, kwa kuzingatia taarifa za baadhi ya Kamati za Bunge Maalum, muundo uliopo wa Serikali mbili, mahitaji ya kuwa na uwakilishi sawa kati ya wanawake na wanaume na ukomo wa juu wa ukumbi wa Bunge, imerekebisha Ibara ya 113(2) ya Rasimu ya Katiba na kuweka ukomo wa juu wa idadi ya Wabunge kuwa 360 kama inavyoonekana katika Ibara ya 124(5) Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ibara ya 114 ya Rasimu ya Katiba inahusu maisha ya Bunge ambayo ni muda wa miaka mitano unaoanzia tarehe ambapo Bunge Jipya litaitishwa ili kukutana kwa mara ya kwanza baada ya uchaguzi wa Wabunge na kuishia tarehe ya kuvunjwa kwa Bunge kwa ajili ya kuwezesha uchaguzi mwingine kufanyika. Kiuhalisia, Bunge huvunjwa takribani miezi miwili kabla ya siku ya uchaguzi na hivyo kipindi cha miaka mitano kinakuwa hakijakamilika. Baadhi ya Kamati ziliona kuwa katika kipindi hicho cha takribani miezi miwili baada ya Bunge kuvunjwa, kunakuwa na ombwe la mhimili wa Bunge na hivyo kwenda kinyume na Katiba inayotaka kuwepo kwa mihimili yote mitatu ya Serikali wakati wote. Kamati ya Uandishi imerekebisha Ibara hiyo ili maisha ya Bunge yatakuwa ni muda usiozidi miaka mitano, na pia kutoa tafsiri mpya ya maneno “maisha ya Bunge” kuwa ni muda wote unaoanzia tarehe ambapo Bunge jipya litaitishwa ili kukutana kwa mara ya kwanza mpaka tarehe ya uchaguzi mwingine wa Wabunge. Marekebisho hayo ni kama yanavyoonekana kwenye Ibara ya 125 ya Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu sifa za mtu kuchaguliwa kuwa Mbunge, taarifa za Kamati 12 za Bunge Maalum, katika mapendekezo ya Wajumbe walio wengi, zilipendekeza Ibara ya 125 ya Rasimu ya Katiba ifanyiwe marekebisho ili kuondoa sharti linalohitaji elimu ya kidato cha nne kama mojawapo ya sifa za kuwa Mbunge kwani elimu ya kidato cha nne sio kigezo muhimu cha kuwa na sifa ya kuwa kiongozi. Hoja hii ilijadiliwa na Wajumbe wengi ndani ya Bunge Maalum na kwamba sifa iwe ni kujua kusoma na kuandika Kiswahili au Kingereza.
Kamati ya Uandishi baada ya kupitia mapendekezo hayo, imerekebisha Ibara ya 125(1)(c) ya Rasimu ya Katiba na sasa inasomeka kama inavyoonekana katika Ibara ya 135(1)(b) ya Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Rasimu ya Katiba inapendekeza kuwepo kwa mgombea huru katika nafasi ya urais na ubunge katika Ibara za 79(1)(f) na 125(1)(c) mtawalia, kwa kuwa ni haki ya msingi kwa kila mwananchi kuchagua na kuchaguliwa. Hii inatoa fursa kwa mwananchi ambaye si mwanachama wa chama cha siasa kushiriki katika chaguzi mbalimbali. Hata hivyo, kwa kuwa chama kinachopendekeza mgombea ubunge kimewekewa makatazo na Katiba kama vile sera za mrengo wa kikanda, ukabila, udini na kutokuwa na sera za kuvunja Muungano, Kamati ya Uandishi iliangalia taratibu zinazotumika katika nchi nyingine zinazoruhusu mgombea huru ambazo zimeweka katazo katika Katiba zao kwa kuzuia Mbunge aliyegombea akiwa huru kujiunga na chama cha siasa baada ya kushinda uchaguzi na katika kipindi chote cha ubunge. Mfano ni Katiba za Kenya na Zambia. Hivyo basi, Kamati ya Uandishi imeongeza aya mpya ya (h) ya Ibara ya 138(1) ya Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa inayoweka masharti kuwa Mbunge aliyetokana na mgombea huru atapoteza ubunge wake iwapo atajiunga na chama chochote cha siasa wakati wote atakaokuwa madarakani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kujaza nafasi ya ubunge inapokuwa wazi kabla ya Bunge kumaliza muda wake, Rasimu ya Katiba katika Ibara ya 124(4) ilipendekeza kwamba uchaguzi usifanyike ila Tume Huru ya Uchaguzi, kwa kuzingatia orodha ya majina iliyowasilishwa na chama husika, yaani kile kilichopoteza Mbunge, ishauriane na chama hicho ili kujaza nafasi iliyoachwa wazi ili kupunguza gharama kwa Taifa. Taarifa za Kamati za Bunge Maalum zilionesha kuwa demokrasia ni gharama na kwamba demokrasia haiwezi kufifishwa kwa kigezo cha gharama. Ilijadiliwa pia kuwa wananchi ndio wanaoamua nani awe kiongozi wao kupitia uchaguzi na hivyo Katiba haiwezi kupokonya haki hiyo. Kamati ya Uandishi, kwa kuzingatia mapendekezo hayo, imerekebisha Ibara ya 124(4) ya Rasimu ya Katiba kama inavyosomeka katika Ibara ya 134(2) ya Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Rasimu ya Katiba, katika Ibara ya 125(2)(a) inapendekeza ukomo wa mtu kuwa Mbunge ili kuondoa dhana ya umiliki wa jimbo la uchaguzi. Vile vile, Ibara ya 129 inapendekeza haki ya wananchi kumwondoa Mbunge wao kabla ya kumaliza muda wake ili kuwapa fursa wananchi wengine wenye uwezo kugombea nafasi ya ubunge na kuongeza uwajibikaji wa Mbunge katika jimbo lake. Kamati Saba (7) kati ya Kamati Kumi na Mbili (12) za Bunge Maalum zimependekeza pasiwepo ukomo wa ubunge na pia pasiwepo na haki ya wananchi kumwondoa Mbunge madarakani kabla ya kipindi chake cha uongozi. Sababu za msingi zilizotolewa kwa ajili ya kufuta haki ya wananchi kumwajibisha Mbunge ni kuepusha kutumika vibaya kwa haki hii na kwamba mamlaka ya kumwajibisha Mbunge tayari yapo kwa kipindi cha ubunge kuwa miaka mitano na hivyo wananchi wanaweza kumwajibisha kwa kutomchagua tena. Kamati ya Uandishi baada ya kuzingatia mapendekezo hayo iliondoa ukomo wa ubunge na haki ya wananchi kumwajibisha Mbunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Spika na Naibu Spika, Rasimu ya Katiba ilipendekeza katika Ibara za 133(1)(a), 134(4) na 135(1)(d) na (2) kwamba viongozi hawa wasitokane na Wabunge au viongozi wa juu wa vyama vya siasa ili kuondoa uwezekano wa kuwepo upendeleo na kulinda maslahi ya chama au kundi katika uendeshaji wa shughuli za Bunge. Taarifa za Kamati 12 za Bunge Maalum na mjadala ndani ya Bunge Maalum ulionesha kuwa Spika anaweza kutokana na Wabunge au kutoka nje ya Bunge ilimradi ana sifa stahiki. Kwa upande wa Naibu Spika, mapendekezo yalikuwa lazima atokane na Wabunge. Kamati ya Uandishi, kwa kuzingatia mapendekezo hayo, imerekebisha Ibara husika ili kuweka masharti kuwa Spika wa Bunge atachaguliwa na Wabunge kutoka miongoni mwa watu ambao ni Wabunge au wenye sifa ya kuwa Wabunge. Msingi wa pendekezo hili ni kuwapa fursa watu wasio Wabunge nafasi ya kugombea na kuweza kuchaguliwa kuwa kiongozi wa mhimili wa Bunge. Vile vile, yamewekwa masharti kuwa kutakuwa na Naibu Spika ambaye atachaguliwa kutoka miongoni mwa Wabunge. Msingi wa pendekezo hili, ni kuondoa uwezekano wa idadi ya Wabunge kuongezeka endapo watakaochaguliwa watakuwa sio Wabunge. Marekebisho hayo yako kwenye Ibara ya 141(1) kwa upande wa Spika na Ibara ya 143(1) ya Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa kwa upande wa Naibu Spika.
SURA YA KUMI NA MOJA
SERIKALI YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR, BARAZA LA MAPINDUZI LA ZANZIBAR NA BARAZA LA
WAWAKILISHI LA ZANZIBAR
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati za Bunge Maalum zilipendekeza Sura Mpya yenye kuanzisha vyombo vyenye mamlaka ndani ya Zanzibar ambavyo ni Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ambayo itaongozwa na Rais wa Zanzibar; Baraza la Mapinduzi la Zanzibar ambalo litakuwa ndicho chombo kikuu cha kumshauri Rais wa Zanzibar katika masuala ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ; na Baraza la Wawakilishi la Zanzibar ambalo litakuwa na madaraka yote ya kutunga sheria katika Zanzibar juu ya mambo yote yaliyo chini ya mamlaka ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Kamati ya Uandishi, kwa kuzingatia mapendekezo hayo, imeandika Ibara za 158 hadi 161 kama zinavyoonekana katika Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa.
SURA YA KUMI NA MBILI
MAHAKAMA YA JAMHURI YA MUUNGANO
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sura ya Kumi imegawanyika katika sehemu kuu tatu. Sehemu ya Kwanza inahusu misingi ya utoaji haki na uhuru wa Mahakama; Sehemu ya Pili inahusu muundo wa Mahakama; na Sehemu ya Tatu inahusu Tume ya Utumishi wa Mahakama na Mfuko wa Mahakama. Maudhui makuu ya Sura hii ni kuanzishwa kwa Mahakama ya Jamhuri ya Muungano ambayo ndiyo chombo chenye mamlaka ya utoaji haki katika Jamhuri ya Muungano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Rasimu ya Katiba, katika Ibara ya 150 inaanzisha ngazi mpya ya Mahakama ya Juu katika mfumo wa Mahakama nchini. Mahakama hii pamoja na Mahakama ya Rufani ndiyo zitakuwa vyombo vya juu vya utoaji haki katika Jamhuri ya Muungano. Kamati za Bunge Maalum ziliafiki kuanzishwa kwa Mahakama ya Juu kwa kuona umuhimu wa kupanua wigo wa ngazi za Mahakama ambapo pamoja na mambo mengine, itaongeza ngazi za kukata rufaa. Vile vile, Mahakama ya Juu ndiyo itakuwa na mamlaka ya kusikiliza mashauri ya kupinga matokeo ya Urais, ili kwenda sambamba na muundo kama huo wa Mahakama unaotumika katika nchi nyingine za Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kamati ya Uandishi, kwa kuzingatia mapendekezo hayo imeandika Ibara za 87, 165(1)(a), 166 na 168(1)(a) kama zinavyoonekana katika Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati za Bunge Maalum zimependekeza marekebisho katika Ibara ya 150 ili kuanzisha Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Muungano kwa msingi kwamba Katiba hii ndio itakayotumika Tanzania Bara kwa mambo yasiyo ya Muungano. Kwa kuzingatia mapendekezo hayo, Kamati ya Uandishi imeongeza aya mpya ya (c) katika Ibara ya 165(1) na kuandika Ibara mpya ya 188(1). Kamati za Bunge Maalum pia zilipendekeza kuipa mamlaka Mahakama Kuu ya Zanzibar kwa kuongeza ibara ndogo ya (2) yenye masharti kuwa Mahakama Kuu ya Zanzibar itakuwa na mamlaka sawa na Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Muungano katika sheria zilizotungwa na Bunge zinazotumika katika pande mbili za Muungano. Kwa kuzingatia mapendekezo hayo, Kamati ya Uandishi imerekebisha Ibara ya 165 kwa kuongeza ibara ndogo ya (2) kama inavyoonekana katika Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati za Bunge Maalum pia zimependekeza kutambuliwa kikatiba kwa Mahakama Kuu ya Zanzibar. Kamati ya Uandishi, kwa kuzingatia mapendekezo hayo, imeandika Ibara mpya za 193 na 194 ili kuitambua Mahakama Kuu ya Zanzibar na mamlaka yake. Ibara hizo zinasomeka kama zinavyoonekana katika Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo hili la Mahakama, jambo la mahakama ya kadhi lilijitokeza katika baadhi ya Kamati za Bunge Maalum kwa upande wa maoni ya Wajumbe walio wachache. Wajumbe wengi walichangia hoja hii katika mjadala ndani ya Bunge Maalum. Hoja zilizojitokeza, pamoja na mambo mengine, zilihusu kuanzishwa kwa mahakama ya kadhi na kutambuliwa kwa maamuzi yanayohusu ndoa, talaka na mirathi yanayotolewa na vyombo vinavyotambuliwa na sheria za dini ya Kiislam.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati ya Uandishi, kwa kuzingatia mapendekezo ya Wajumbe wakati wa mjadala ndani ya Bunge Maalum, Taarifa za Kamati za Bunge Maalum, katiba za nchi mbalimbali kuhusu suala hili, na msingi kwamba Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa inaanzisha Mahakama za ngazi za juu katika Jamhuri ya Muungano, mahakama ya kadhi, kama ilivyo kwa mahakama nyingine za mahakimu, inaweza kuanzishwa kwa mujibu wa sheria inayohusu mahakama za mahakimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maboresho yaliyofanywa na Kamati ya Uandishi ili kukidhi maudhui na mtiririko wa kiuandishi, Sura ya Kumi na Mbili ni kama inavyoonekana katika Rasimu ya Katiba inayopendekezwa.
SURA YA KUMI NA TATU
UTUMISHI WA UMMA KATIKA JAMHURI YA MUUNGANO
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sura ya Kumi na Tatu ya Rasimu ya Katiba inahusu Utumishi wa Umma katika Jamhuri ya Muungano. Ibara hizo zinaainisha misingi mikuu katika utumishi wa Umma, ajira na uteuzi wa viongozi wa taasisi katika Serikali, Tume ya Utumishi wa Umma, Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma, mamlaka ya Tume ya Utumishi wa Umma na Tume ya Mishahara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati za Bunge Maalum zilipendekeza marekebisho katika Ibara ya 184 ya Rasimu ya Katiba na kuonesha kwamba Tume ya Utumishi katika Jamhuri ya Muungano itazingatia misingi mikuu iliyoainishwa katika Ibara hiyo na siyo misingi na kanuni kama ilivyopendekezwa kwenye Rasimu ya Katiba. Kutokana na mapendekezo hayo, misingi iliyobaki katika Ibara hii ni ile iliyokuwa katika aya ya (a), (d) na (f) ya ibara ndogo ya (1). Mambo mengine yanayopaswa kuzingatiwa na Tume hiyo ni utoaji wa huduma zake kwa wakati, usawa na bila upendeleo na kuzingatia usawa wa kijinsia na fursa kwa watu wenye ulemavu katika uteuzi na ajira. Kamati ya Uandishi imerekebisha Ibara hii kama inavyoonekana kwenye Ibara ya 203 ya Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati za Bunge Maalum katika Sura hii pia zilipendekeza marekebisho ili kuweka masharti kuwa ajira na uteuzi wa viongozi na watumishi katika taasisi na wizara za Muuungano utazingatia uwakilishi wa pande zote mbili za Muungano, jinsi na watu wenye ulemavu kama inavyoonekana kwenye Ibara ya 204 katika Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati za Bunge Maalum zilipendekeza marekebisho katika Ibara ya 188 inayohusu mamlaka na majukumu ya Tume ya Utumishi wa Umma ili kuleta maana iliyokusudiwa ikiwemo kuitaka Tume kupendekeza kwa Rais majina ya viongozi wanaoweza kuteuliwa na Rais na siyo kushauriana na Rais kuhusu uteuzi huo. Majukumu mengine yaliyopendekezwa na Kamati za Bunge Maalum ni kuhamasisha utekelezaji wa misingi ya Umma, kushughulikia rufani za migogoro ya watumishi ya Umma pamoja na nidhamu katika utumishi wa umma na kutekeleza majukumu mengine yatakayoainishwa na sheria. Aidha, Kamati za Bunge Maalum zimependekeza Ibara hii iweke masharti kuwa Bunge litatunga sheria kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu ya Tume ya Utumishi wa Umma. Kamati ya Uandishi, kwa kuzingatia mapendekezo hayo, imeandika Ibara ya 207 kama inavyosomeka kwenye Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa.
SURA YA KUMI NA NNE
UCHAGUZI KATIKA VYOMBO VYA UWAKILISHI
NA VYAMA VYA SIASA
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Sura hii, mapendekezo ya Tume kimsingi na kimaudhui yamebaki kama yalivyopendekezwa kwenye Rasimu ya Katiba isipokuwa masharti kuhusu mgombea huru.
Mhe. Mwenyekiti, mapema katika Taarifa hii suala la mgombea huru katika nafasi za uongozi kitaifa yaani urais na ubunge liligusiwa. Napenda kuhitimisha kwenye eneo hili kwa kusema kwamba Kamati 12 za Bunge Maalum zilitamka kwamba pamoja na suala hili kuwa ni haki ya msingi ya mwananchi, tahadhali lazima ichukuliwe ili mgombea huru kwa nafasi ya urais au ubunge asifanye vitendo ambavyo vinakatazwa kwa wagombea wanaopitia vyama vya siasa. Hivyo, Kamati ya Uandishi imetekeleza mapendekezo ya Kamati za Bunge Maalum kwa kuweka Ibara ya 210 ya Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa ambayo inatoa fursa kwa Bunge kutunga sheria itakayoweka masharti kwa mgombea huru kuhusu mambo yaliyoanishwa kwenye Ibara hiyo. SOMA IBARA YA 210(2)
SURA YA KUMI NA TANO
TAASISI ZA UWAJIBIKAJI
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sura hii inayohusu Taasisi za Uwajibikaji imegawanyika katika Sehemu tatu. Sehemu hizo zinaweka masharti kuhusu Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali. Taarifa za Kamati za Bunge Maalam pamoja na michango ya Wajumbe ndani ya Bunge Maalum inaainisha kuwa maudhui ya Ibara katika Sura hii kuwekwa katika Katiba kama yalivyopendekezwa katika Rasimu ya Katiba. Ibara husika, yaani, Ibara ya 222 hadi 242 ziko kama zinavyosomeka kwenye Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa.
SURA YA KUMI NA SITA
MASHARTI KUHUSU FEDHA ZA JAMHURI YA MUUNGANO
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sura ya Kumi na Sita inahusu masharti kuhusu fedha za Jamhuri ya Muungano na imegawanywa katika Sehemu Mbili. Sehemu hizo ni Mfuko Mkuu wa Hazina na Fedha za Jamhuri ya Muungano. Kamati za Bunge Maalum na katika mjadala Bungeni, Wajumbe walichangia kuhusu masharti ya sura hii na kutoa mapendekezo kwa lengo la kuhakikisha kuwa maudhui yake yanadumisha Muungano. Mjadala katika eneo hili ulijikita katika masuala yanayohusu misingi ya fedha za umma, Akaunti ya Pamoja, Tume ya Pamoja ya Fedha, pamoja na mamlaka ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kukopa. Aidha, michango mingi ya Kamati za Bunge Maalum na Wajumbe ndani ya Bunge Maalum ililenga kufanya marekebisho yafuatayo katika Sura hii:
(i) Kuweka Ibara mahsusi inayoweka masharti kuhusu misingi itakayoongoza matumizi ya fedha za umma katika Jamhuri ya Muungano ikiwemo uwazi, umakini na uwajibikaji; mfumo wa fedha kulenga maendeleo linganifu; na kuzingatia ustawi linganifu kwa faida ya kizazi cha sasa na vizazi vijavyo.
(ii) Kuweka masharti kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano itatunza fedha zake katika Akaunti ya Fedha ya Pamoja na
(iii) ambayo itakuwa ni Sehemu ya Mfuko Mkuu wa Hazina na Fedha za Jamhuri ya Muungano.
(iv) Kuweka masharti kuhusu Tume ya Pamoja ya Fedha. Bunge limepewa mamlaka ya kutunga sheria kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu ya Tume hii.
(v) Katika Ibara ya 223 ya Rasimu ya Katiba ambayo inaweka masharti kuhusu utaratibu wa kuidhinisha matumizi ya fedha zilizo katika Mfuko Mkuu wa Hazina, yameongezwa masharti mapya yatakayoitaka Serikali kuwasilisha makadirio ya mapato na matumizi kwanza kwenye Kamati husika ya Bunge kwa ajili ya tathmini na uchambuzi na kwamba Kamati hiyo itekeleze
(vi) jukumu hilo kwa kupokea maoni na ushauri wa wadau kama itakavyoonekana inafaa.
(vii) Ibara ya 226 ya Rasimu ya Katiba inayoweka masharti kuhusu mishahara ya baadhi ya watumishi kudhaminiwa na Mfuko Mkuu wa Hazina imefanyiwa marekebisho ili kuainisha watumishi ambao masharti hayo yatatumika kwao na kuwa sheria itatungwa na kuainisha mtumishi anayepaswa kuingizwa katika masharti haya.
(viii) Katika masharti kuhusu Mamlaka ya Serikali kukopa, Ibara ya 227 ya Rasimu ya Katiba imefanyiwa marekebisho ili kuwezesha Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kukopa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano yaweza kutoa dhamana kwa
(ix) mkopo unaoombwa baada ya kushauriana na kukubaliana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
(x) Katika Ibara ya 232 ya Rasimu ya Katiba inayoweka masharti kuhusu Ununuzi wa Umma, yameongezwa masharti kwamba Bunge litatunga sheria itakayoainisha mfumo wa manunuzi ya Serikali na taasisi pamoja na misingi itakayozingatiwa na Bunge wakati wa kutunga sheria hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati ya Uandishi, kwa kuzingatia mapendekezo yaliyoainishwa hapo juu kutoka katika taarifa za Kamati za Bunge na mjadala ndani ya Bunge, imeandika Ibara za Sura hii kama zinavyoonekana kwenye Ibara ya 243 hadi 257 za Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa.
SURA YA KUMI NA SABA
ULINZI NA USALAMA WA JAMHURI YA MUUNGANO
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sura ya Kumi na Saba inahusu ulinzi na usalama wa Jamhuri ya Muungano ambayo inabebwa na maudhui ya ulinzi na usalama wa Taifa. Sura hii pia inaanzisha vyombo vya ulinzi ambavyo ni Jeshi la Ulinzi la Wananchi, Jeshi la Polisi la Jamhuri ya Muungano na Idara ya Usalama wa Taifa ya Jamhuri ya Muungano. Katika Sura hii, sehemu kubwa ya mapendekezo ya Kamati za Bunge Maalum yalikuwa kuhusu marekebisho madogo ya kimaudhui na kiuandishi kwa ajili ya kuboresha Ibara mbalimbali za sura hii. Hata hivyo, baadhi ya Kamati za Bunge Maalum zilipendekeza uanzishwaji wa huduma nyingine za ulinzi na udhibiti wake kutokana na uhalisia kwamba vipo vyombo vingine vinavyojishughulisha na ulinzi wa raia na mali zao. Kamati ya Uandishi, kwa kuzingatia mapendekezo hayo, imefanya marekebisho ya kiuandishi na kuandika Ibara inayohusu uanzishwaji wa huduma nyingine za ulinzi kama inavyoonekana kwenye Ibara ya 267 ya Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa.
SURA YA KUMI NA NANE
MENGINEYO
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sura ya Kumi na Nane inahusu masharti mengineyo ikijumuisha utaratibu wa kujiuzulu katika utumishi wa umma; masharti kuhusu kukabidhi madaraka, ufafanuzi, Jina la Katiba na kuanza kutumika kwa Katiba na kufuta Katiba iliyopo. Kimaudhui, Sura hii imebaki kama ilivyopendekezwa katika Rasimu ya Katiba ukiacha mambo machache yaliyoboreshwa kama inavyoonekana katika Ibara ya 270 hadi 274 za Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa.
SURA YA KUMI NA TISA
MASHARTI YATOKANAYO NA MASHARTI YA MPITO
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati ya Uandishi imeyapitia masharti ya Ibara hizo na kuandaa Muswada wa Sheria ya Masharti ya Mpito na Masharti Yatokanayo. Muswada huu unajumuisha masharti kadhaa ya mpito na masharti yatokanayo na kutungwa kwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Mwaka 2014. Aidha, Kamati ya Uandishi haijajumuisha katika Muswada, masharti ya Ibara ya 129 (1)(a),(c),(d),(e),(f) na (i) kwa kuwa masharti hayo hayaendani na mfumo wa Serikali mbili unaopendekezwa.
Muswada huo umeandaliwa kwa lugha ya Kiswahili na Kiingereza kama ulivyoandaliwa na Kamati ya Uandishi ambao utawasilishwa kwenye
Bunge Maalum kwa ajili ya kupitishwa mara baada ya mchakato wa mabadaliko ya Katiba kukamilika.
_____________
NYONGEZA YA KWANZA
_____________
[Imetajwa katika Ibara ya 71(3)]
Mambo ya Muungano
Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu hii inahusu Nyongeza kuhusu Mambo ya Muungano. Kamati zote Kumi na Mbili zimetoa mapendekezo ya kuboresha Nyongeza kuhusu Mambo ya Muungano kwa kuongeza idadi kutoka mambo saba yaliyo kwenye Rasimu ya Katiba hadi mambo 14 kwa kutumia kigezo cha mambo makuu ya kidola ambayo yanapaswa kuendelea kubaki. Kamati ya Uandishi, kutokana na mapendekezo ya Kamati za Bunge na sababu hizi, Nyongeza ya Kwanza ya Rasimu ya Katiba imeandikwa upya na inasomeka kama inavyoonekana mwishoni mwa Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa.
_____________
NYONGEZA YA PILI
_____________
[Imetajwa katika Ibara ya 129(1)(b)]
(sheria ambazo mabadiliko yake yanahitaji kuungwa mkono na theluthi mbili ya Wabunge wote kutoka Tanzania Bara na theluthi mbili ya Wabunge wote kutoka Zanzibar)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati ya Uandishi imependekeza kuwepo kwa Nyongeza ya Pili inayohusu masharti ya kuungwa mkono kwa wingi wa theluthi mbili ya Wabunge kutoka kila upande wa Jamhuri ya Muungano katika Miswada ya Sheria inayohusu kubadili masharti ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano, yanayohusu Mambo ya Muungano na kuongeza au kupunguza jambo lolote la Muungano.
_____________
NYONGEZA YA TATU
_____________
[Imetajwa katika Ibara ya 129(1)(c))
(Mambo ambayo mabadiliko yake yanahitaji kuungwa mkono kwa idadi ya nusu ya kura halali zilizopigwa na wananchi wa Tanzania Bara na zaidi ya nusu ya kura zilizopigwa na wananchi wa Zanzibar katika kura ya maoni)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati ya Uandishi inapendekeza kuwepo kwa Nyongeza ya Tatu ya Katiba kwa ajili ya kuainisha Sheria ambazo mabadiliko yake ili yapate uhalali wa kisheria ni sharti kwanza yaungwe mkono na theluthi mbili ya Wabunge wote kisha yapelekwe kwa wananchi ili kupigiwa kura ya maoni.
1. Muundo wa Jamhuri ya Muungano.
2. Kuwepo kwa Jamhuri ya Muungano.
3. Kubadilisha masharti ya Ibara ya 129(1)(c).
Mheshimiwa Mwenyekiti, Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa ina jumla ya Ibara 274. Kati ya Ibara hizo, Ibara 233 zimetokana na Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa kwenye Bunge Maalum, 47 kati ya hizo hazikufanyiwa marekebisho yoyote wakati Ibara 186 zimefanyiwa marekebisho ya kiuandishi na kimaudhui. Ibara 28 tu za Rasimu ya Katiba zimefutwa na Ibara 41 ndio mpya. Ibara 14 za Sura ya Kumi na Tisa ni za Masharti ya Mpito.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo mapya katika Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa ni pamoja na:
SURA YA KWANZA
1. Misingi ya utawala bora – Ibara ya 6
SURA YA PILI
2. Utafiti na Maendeleo – Ibara ya 16
3. Dira ya Maendeleo – Ibara ya 17
4. Tume ya Mipango ya Jamhuri ya Muungano – Ibara ya 18
5. Matumizi ya masharti ya Sura ya Pili – Ibara ya 20
SURA YA TATU
6. Ardhi katika Jamhuri ya Muungano – Ibara ya 22
7. Matumizi bora ya ardhi - Ibara 23
8. Fidia – Ibara ya 24
9. Maliasili – Ibara ya 25
10. Mazingira – 26
SURA YA TANO
11. Uhuru wa taaluma, ubunifu na ugunduzi – Ibara ya 56
12. Sheria kuhusu haki, uhuru na wajibu
SURA YA NANE
13. Majukumu ya Makamu wa Kwanza wa Rais – Ibara ya 98
14. Makamu wa Pili wa Rais – Ibara ya 103
15. Makamu wa Tatu wa Rais – Ibara ya 104
16. Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano – Ibara ya 105
17. Kazi na Mamlaka ya Waziri Mkuu – Ibara ya 106
18. Uwajibikaji wa Serikali – Ibara ya 107
19. Kura ya Kutokuwa na Imani na Waziri Mkuu – Ibara ya 108
20. Naibu Mwanasheria Mkuu – Ibara ya 114
21. Mkurugenzi wa Mashtaka – Ibara ya 115
22. Wakuu wa Mikoa – Ibara ya 118
23. Serikali za Mitaa – Ibara ya 119
24. Mamlaka za Serikali za Mitaa – Ibara ya 120
25. Uongozi katika Serikali za Mitaa - Ibara ya 121
SURA YA KUMI NA MOJA
26. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar – Ibara ya 158
27. Rais wa Zanzibar na Mamlaka yake – Ibara ya 159
28. Baraza la Mapinduzi la Zanzibar - Ibara ya 160
29. Baraza la Wawakilishi Zanzibar – Ibara ya 161
SURA YA KUMI NA MBILI
30. Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Muungano – Ibara ya 188
31. Uteuzi wa Jaji wa Mahakama Kuu – Ibara ya 189
32. Muda wa Jaji wa Mahakama Kuu Kushika Madaraka – Ibara ya 190
33. Utaratibu wa kushughulikia nidhamu ya Jaji wa Mahakama Kuu Ibara ya 191
34. Kiapo cha Jaji wa Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Muungano – Ibaraya 192
35. Mahakama Kuu ya Zanzibar – Ibara 193
36. Mamlaka ya Mahakama Kuu ya Zanzibar – Ibara ya 194
SURA YA KUMI NA NNE
37. Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa – Ibara ya 220
SURA YA KUMI NA SITA
38. Misingi ya matumizi ya fedha za umma – Ibara ya 243
39. Akaunti ya Fedha ya Pamoja – Ibara ya 244
40. Tume ya Pamoja ya Fedha – Ibara ya 245
SURA YA KUMI NA SABA
41. Uanzishwaji wa huduma nyingine za ulinzi – Ibara ya 267
Mheshimiwa Mwenyekiti, huu ni muhtasari wa Ibara mpya zilizoingizwa na Kamati ya Uandishi kwa kuzingatia mapendekezo ya Kamati kumi na mbili za Bunge Maalum na yale yaliyojadiliwa ndani ya Bunge Maalum.
HITIMISHO:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Kamati ya Uandishi ya Bunge Maalum, kwa mara nyingine tena naomba nichukue fursa hii kukushukuru wewe binafsi pamoja na Makamu wako, Mhe. Samia Suluhu Hassan. Imani kubwa mliyoionesha kwetu ilitutia nguvu ya kutekeleza jukumu hili zito lakini muhimu la kupitia mapendekezo ya Kamati zote Kumi na mbili za Bunge Maalum, pamoja na mapendekezo yaliyotolewa nbe wa Bunge Maalum wajumewakati wa mjadala.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikiri kwamba Wajumbe wote wa Kamati ya Uandishi walifanya kazi hii kwa weledi, kwa uzalendo na kwa nia thabiti ya kulitumikia Taifa lao. Rasimu hii ninayoiwasilisha ni matokeo ya juhudi zetu za pamoja tukisaidiwa na timu ya wataalam ambao walifanya kazi usiku na mchana kuhakikisha kwamba Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa inakamilika kwa wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kwa namna pekee tunatoa shukrani zetu za dhati kwa Katibu wa Bunge Maalum, Ndg. Yahya Khamis Hamad na Naibu wake, Dkt. Thomas Didimu Kashilillah, kwa uratibu wao na huduma mbalimbali zilizoiwezesha Kamati ya Uandishi kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi. Aidha, napenda kuishukuru Sekretarieti ya Kamati ya Uandishi kwa kazi kubwa ya kuisaidia Kamati na kuiwezesha kukamilisha majukumu yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba sasa niwatambue Wajumbe wa Kamati ya Uandishi kwa majina kama ifuatavyo:
1. Mhe. Andrew John Chenge
2. Mhe. Mgeni Hassan Juma
3. Mhe. Dr. Natujwa Mvungi
4. Mhe. Ali Ahmed Uki
5. Mhe. Amina Mweta
6. Mhe. Almas Athuman Maige
7. Mhe. Magdalena Rwebangira
8. Mhe. Dr. Mahadhi Juma Maalim
9. Mhe. Jaji Frederick Mwita Werema
10. Mhe. Dr. Tulia Ackson
11. Mhe. Ummy Mwalimu Ally
12. Mhe. Dr. Harrison George Mwakyembe
13. Mhe. Valerie Ndeneingo-Sia Msoka
14. Mhe. Elizabeth Maro Minde
15. Mhe. Angellah Jasmine Kairuki
16. Mhe. Dkt. Pindi Chana
17. Mhe. Dkt. Asha-Rose M. Migiro
18. Mhe. Prof. Costa Ricky Mahalu
19. Mhe. Amon Anastaz Mpanju
20. Mhe. Evod Herman Mmanda
21. Mhe. Dkt. Mwinyi Talib Haji
22. Mhe. Khadija Nassor Abdi
Wajumbe wa sekretarieti:
1. Ndg. Mussa Kombo Bakari - Mkuu wa Idara ya
Uandishi wa Sheria
2. Ndg. Stephen Kagaigai - Naibu Mkuu wa Idara ya
Uandishi wa Sheria
3. Ndg. Sarah K. Barahomoka - Mwandishi Mkuu wa
Sheria
4. Ndg. Oscar Godfrey Mtenda - Mwandishi wa Sheria
5. Ndg. Optat J. Mrina - Mwandishi wa Sheria
6. Ndg. Juliana Munisi - Mwandishi wa Sheria
7. Ndg. Bavoo Junus - Mwandishi wa Sheria
8. Ndg. Shabani Kabunga - Mwandishi wa Sheria
9. Ndg. Jacob Sarungi - Mwandishi wa Sheria
10. Ndg. Victor Kahangwa - Mwandishi wa Sheria
11. Ndg. Mark Mulwambo - Mwandishi wa Sheria
12. Ndg. Sarah D. Mwaipopo - Mwandishi wa Sheria
13. Ndg. Ali Ali Hassan - Mwandishi wa Sheria
14. Ndg. Fatma Saleh Amour - Mwandishi wa Sheria
15. Ndg. Mtumwa Said Sandal - Mwandishi wa Sheria
16. Ndg. Thabit Mlangi - Mwandishi wa Sheria
17. Ndg. Agnes Ndumbati - Mwandishi wa Sheria
18. Ndg. Nicodemus Chuwa - Mwandishi wa Sheria
19. Ndg. Pius Mboya - Mwandishi wa Sheria
20. Ndg. Prudence Rweyongeza - Mwandishi wa Sheria
21. Ndg. Matamus Fungo - Mwandishi wa Sheria
22. Ndg. Nesta Kawamala - Mwandishi wa Sheria
23. Ndg. Richard Mbaruku - Mwandishi wa Sheria
24. Ndg. Fatma Mtumweni - Mwandishi wa Sheria
25. Ndg. Ephery Sedekia - Mwandishi wa Sheria
26. Ndg. Angaza Mwipopo - Mwandishi wa Sheria
27. Ndg. Alice Mtulo - Mwandishi wa Sheria
28. Ndg. Paul Thomas Kadushi - Mwandishi wa Sheria
29. Ndg. Nasra Awadh - Mwandishi wa Sheria
30. Ndg. Mossy V. Lukuvi - Mwandishi wa
Sheria/Katibu Kamati
31. Ndg. Evangelina Manyama - Katibu Muhtasi
32. Ndg. Josephine Chalamila - Katibu Muhtasi
33. Ndg. Maryam R. Moh’d - Katibu Muhtasi
34. Ndg. Beatrice Mphuru - Katibu Muhtasi
35. Ndg. Salama Mwinyi Khamis - Katibu Muhtasi
36. Ndg. Ramadhan S.Khatibu - Katibu Muhtasi
37. Ndg. Catherine Kitutu - Mhudumu
38. Ndg. Kelvin Chiwangu - Tehama
39. Ndg. Tumaini A. Fungo - Mwandishi Taarifa Rasmi
40. Silver S. Chindandi - Mwandishi Taarifa Rasmi
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba Bunge Maalum lipokee Taarifa ya Kamati ya Uandishi ya Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa ili ifanyiwe uamuzi kwa kupigiwa kura kwa mujibu wa kanuni ya 35(9) na 36 ya Kanuni za Bunge Maalum za mwaka 2014.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa hoja.
Andrew John Chenge, (MB)
Mwenyekiti,
Kamati ya Uandishi ya Bunge Maalum.
24 Septemba, 2014
No comments :
Post a Comment