Zanzibar. Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Said Hassan Said amesema atahakikisha anatekeleza majukumu yake bila ya woga wala upendeleo, ikiwamo kazi ya kumshauri Rais wa Zanzibar na Serikali yake.
Msimamo huo aliutoa jana katika Kikao cha Baraza la Wawakilishi Zanzibar (BLW), alipokuwa akichangia Muswada wa Sheria ya Wauguzi na Wakunga na kuanzishwa kwa Baraza la Usajili la Waunguzi na Wakunga visiwani humo.
“Mheshimiwa Spika, nitafanya kazi kwa kuzingatia umakini, hekima na uadilifu wakati wote wa utekelezaji wa majukumu yangu,” alisema Said ikiwa ni mara yake ya kwanza kuzungumza katika chombo hicho toka alipoteuliwa Oktoba 7, mwaka huu.
Akizungumzia muswada wa sheria ya wakunga na wauguzi, alisema iwapo utapitishwa ili iwe sheria kamili itasaidia kulinda maadili ya watumishi hao ambao watasaidiwa na baraza Maalumu litakalofanya kazi ya kuwasajili na kusimamia maadili.
Wakati huohuo; Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Pandu Ameir Kificho aliwaonya wawakilishi kuacha tabia ya kubeza hoja zinazotolewa na badala yake waheshimu mawazo ya kila mmoja wao.
“Utaratibu wa kuingilia mazungumzo haupo katika baraza hili, tusifanye mambo kama yale ya lililokuwa Bunge Maalumu la Katiba. Spika nitakapokuwa nazungumza sitaki mtu mwingine azungumze, tunapaswa kuzingatia utaratibu na kanuni za baraza,” alisema Kificho.
Alitoa msimamo huo baada ya baadhi ya wawakilishi kuingilia mazungumzo ya Mwakilishi wa Jimbo la Kiwani, Hija Hassan Hija alipokuwa akitoa hoja ya kuomba baraza liahirishwe hadi Oktoba 27, mwaka huu ili kutoa nafasi kwa wawakilishi kusoma marekebisho yaliyofanyika katika muswada wa sheria wa kuanzisha Shirika la Nyumba la Zanzibar.
Chanzo: Mzalendo
No comments :
Post a Comment