Kwarara Msikitini

airbnb

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Monday, October 20, 2014

Siku Nyerere alipotishia kunichapa

JKN

Ahmed Rajab               Toleo la 375               15 Oct 2014
KIZA kilikuwa kimekwishaanza kutanda nilipoikaribia hoteli ya St. Ermins jijini London. Hoteli hiyo ni ya nyota 4 lakini ina haiba ya aina yake na ipo mahala ndipo — karibu na Kasri ya Buckingham ya Malkia wa Uingereza, Kasri ya Westminster mulimo Bunge la Uingereza na ile saa yenye kengele maarufu iitwayo kwa utani Big Ben na karibu sana na kanisa la Westminster Cathedral.
Majira ya kiangazi yalikuwa yamekwishaingia kwa hivyo hali ya hewa ilikuwa ya huruma siku hiyo ya mwanzoni mwa Juni 1997.  Hakukuwa na baridi, hakukuwa na mvua.
Nilikuwa nimekazana nikikimbilia hoteli ya St.Ermins ambako Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alikuwa mgeni wa heshima wa jumuiya moja iliyokuwa ikijishughulisha na mahusiano kati ya Muungano wa Ulaya na Bara la Afrika.
Dakika kama mbili kabla ya kufika hotelini simu yangu ya mkononi ililia. Aliyenipigia alikuwa mwandani wangu Chama Omari Matata, mtangazaji maarufu wa zamani wa Radio Tanzania, Dar es Salaam, ambaye baadaye akinguruma katika Idhaa ya Kiswahili ya BBC, London.
Chama alinipasha habari za msiba wa kifo cha Oscar Kambona.
Niliingiwa na huzuni kwa sababu nikimjuwa Kambona.
Nilikutana naye mara ya kwanza mwishoni mwa 1967 alipokimbia Tanzania lakini kwa muda mrefu nilijiepusha naye. Nikimuona kuwa ni kibaraka wa Wareno na mabeberu waliokuwa wakiupinga ukombozi wa Afrika.  Hata hivyo, katika miaka ya 1980 na ya 1990 Kambona alikuwa hatoki ofisini mwangu kwenye jarida la Africa Analysis. Siku hizo alikuwa akionyesha amechoka, uzito ulimzidi, akihema,na mara nyingi akija akiwa amebeba mkoba wa karatasi.
Ingawa alikuwa akija kupiga soga sikujali kwa sababu masoga yake yalikuwa ya kisiasa na yalinifunza mengi.
Nilipenda kumsikiliza alivyokuwa akimchambua Mwalimu na vijimambo vyake visivyojulikana na wengi. Sikuweza kuyathibitisha yote aliyonambia Kambona na kuna ambayo sikuyaamini hata chembe. Moja kati ya hayo ni dai kwamba Mwalimu alikuwa na akaunti ya benki nje ya Tanzania.
Mawazo mengi kumhusu Kambona na Nyerere yalinipitikia nilipokuwa naikaribia hoteli ya St. Ermins siku hiyo ya Juni, 1997. Nilikuwa na hamu ya kujuwa Nyerere atakuwaje akisikia kuhusu kifo cha rafiki yake wa zamani na hasimu yake wa miaka mingi.
Lakini Nyerere alinishangaza. Nilipokuwa ninamuarifu kuhusu msiba huo nilimuangalia kwa makini usoni mwake. Hakuonyesha hisia zozote za huzuni wala za kusisimkwa.
“Alaa, amekufa? Lini?” Nikamjibu kuwa muda mfupi uliopita. Ilikuwa kama tukimzungumza mtu asiyekuwa na maana yo yote kwake. Hakutaka kujuwa zaidi. Hakuuliza la kheri wala la shari.
Kambona alikuwa ni mtu aliyetoka naye mbali lakini Nyerere hakuonyesha huruma wala hakuonyesha kwamba alimsamehe huyo rafiki yake wa kale aliyefariki Juni 1997.
Ingawa mitandao mingi, pamoja na ule wa Wikipedia, imeandika kwamba Kambona alifariki Julai, 1997 kwa kweli alifariki Juni ya mwaka huo.
Hiyo ilikuwa mara yangu ya pili kukutana na Mwalimu katika hoteli ya St. Ermins. Mara ya kwanza ilikuwa miaka michache kabla wakati wa miaka ya mwanzo ya urais wa Ali Hassan Mwinyi.
Siku hiyo nilipoutia mguu hotelini nilikutana uso kwa uso na Nyerere. Aliponiona tu alinyanyua kifimbo chake akitishia kunipigana mimi nikimkwepa.
“We, we Rajab muongo we kwa nini ukaandika yale?” Alinifokea. Halafu akawageukia walinzi wake na kuwaambia: “Huyu hapa Rajab kazi kuandika uongo tu.
Kwa nini usiniulize? Ungenipigia simu ningekueleza yote.”
Alijifanya yu moto. Waliokuwa naye wakanicheka. Mara akapoa. Tukazungumza kama kawaida na tukapiga picha.
Niliyoyaandika yalimhusu yeye na Mwinyi. Kwa ufupi, nilisikia kwamba Nyerere alikuwa amevunjika moyo na  Mwinyi na namna alivyokuwa akiendesha nchi.
Miaka kadhaa baadaye nilikutana naye katika hoteli ya Intercontinental, Nairobi, Kenya na sikuweza kujizuia.  Nilimkumbusha siku aliyotaka kunipiga kifimbo na aliponiita muongo ilhali yeye mwenyewe baadaye aliandika kitabu Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania ambamo aliyaeleza kwa urefu niliyoyaeleza kwenye makala. Nilimwambia kwamba alinionea aliponiita muongo.
“Ulikuwa muongo tu,” alijibu, “kwa sababu nilikuwa sikuyasema bado.”
Nami nikamwambia kwamba basi angalau angenipongeza kwa kuweza kuyatabiri aliyoyaandika miaka michache baadaye. Alinyamaza kimya.
Tulipokutana safari hiyo Nairobi niliziona hulka zake nyingine. Tulikuwa tumealikwa kwenye mkutano kuujadili mustakbali wa Afrika katika karne ya 21. Yeye ndiye aliyekuwa mwenyekiti wa mkutano. Katika hotuba yake ya ufunguzi Mwalimu aliishambulia vikali Marekani na mfumo wake wa kibepari pamoja na utandawazi.
Baada ya hotuba yake alisimama Mzambia mmoja aliyewahi kuwa msaidizi wa Rais Kenneth Kaunda. Alimwambia hivi Mwalimu: “Unasema kuwa chumi za Afrika zinaumwa; mimi nasema kuwa kwa hakika ni mahtuti. Na kwa nini ikawa hivi?”
Akalijibu mwenyewe swali lake na bila ya kumtaja Mwalimu kwa jina alizitaja sera zake Mwalimu kuwa ndio sababu.
Nakumbuka Jenerali Mirisho Sarakikya, aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Kenya, na niliyekuwa nimekaa naye alininong’oneza: “Du huyu anampiga (Mwalimu) below the belt.”
Kilipomalizika kikao cha ufunguzi nilikwenda kumsalimia Mwalimu na mbele yangu alikuwa Aurelia Brazeal. Nilimsikia mama huyo aliyechanganya damu akijijulisha kwa Mwalimu kuwa yeye ni Balozi wa Marekani, Kenya.
Nilistaajabu kumsikia Mwalimu akimtaka radhi akimwambia kwamba aliyoyasema dhidi ya Marekani hajamkusudia yeye binafsi. Mwalimu hakuwa na haja ya kumtaka radhi. Nilijifanya kama sikumsikia nikajipurukusha kwenda chumba kulikokuwako vinywaji.
Alipoingia Mwalimu nilimwendea naye alikuwa akinijia mimi. Nikitaka kumuuliza iwapo akitaka kahawa au chai. Kabla sijafungua mdomo alinambia: “Mi-mi si-pe-ndi wa-tu wa-ji-nga ka-ma yu-le M-zam-bia.” Hivyo ndivyo alivyoitamka sentensi hiyo.
Nilipomuuliza nimhudumie nini alinambia: “Niachie mwenyewe; katika nyakati kama hizi ndo hujihisi binadamu wa kawaida.”
Niliporudi kwenye ukumbi wa mkutano nilimkuta Mwalimu tayari amekaa akilisoma jarida la Africa Analysis. Akanifanyia ishara ya kuniita. Nilipomwendea akaniuliza mambo mawili matatu kuhusu yaliyoandikwa kwenye toleo lile. Kulikuwa na habari kumhusu John Malecela. Akaniuliza: “Kweli haya?” Nikamjibu kuwa ndivyo tulivyosikia. Ilikuwa wazi kwamba wakati huo Malecela hakuwa shetani wake.
Nilichukua fursa hiyo kumuomba nikazungumze naye baada ya mkutano. Bila ya kusita alinijibu: “Sitaki.” Nilimbembeleza na kumtafadhalisha. Jibu lake lilikuwa lile lile: “Sitaki, utakwenda kuandika.” Tena akisema kwa sauti nzito.
Nilipomuahidi kwamba sitoandika alikubali.
“Njoo chumbani kwangu saa kumi na moja,” alinambia. Saa kumi na moja juu ya alama walinzi wake waliokuwa nje waliniingiza chumbani. Nilimkuta ameketi anakunywa bia na akitafuna njugu.
Siku hizo siasa zilikuwa zi moto Tanzania kwani kila mtu akitaka kujuwa nani atakuwa mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi wa 1995. Aliniuliza watu wanasemaje.
Nikamjibu: “Wanasema una mtu wako.”
“Nani?”
“Salim (Salim Ahmed Salim)”
“Kwa nini?”
“Kwa sababu mtoto wako.”
Kumwambia hivyo aliruka na akanambia kwa mkazo: “Lakini wote watoto wangu. Kwani hata Seif (Seif Sharif Hamad) nani unadhani kamjenga?”
Nilijuwa alitaka nimwambie yeye kwa hivyo nikamjibu: “Wewe.”
“Tena!”  Alisema kwa hamasa na kana kwamba akijipongeza akiwa anapiga soga barazani na vijana wa mjini.
Siku hiyo nilimfaidi Mwalimu.Kwa muda uliokaribia saa mbili tulihadithi mengi. Aliwachambua viongozi kadha wa kadha wa CCM, alizizungumza siasa za Zanzibar na ukabila wa viongozi wa CCM/Zanzibar. Na aliyajibu maswali yangu bila ya kubania. Ingawa alikuwa karimu kwa maelezo alikuwa mchoyo wa njugu; alizila asinigaie hata moja.
Kuiheshimu ahadi niliyompa sitoyaandika yaliyo nyeti ambayo hakutaka niyaandike. Lakini kuna mkasa mmoja ambao naweza kuuandika.
Safari moja akiwa London alialikwa na jumuiya ya Royal African Society. Nilikuwa na rafiki yangu Yusuf Hassan, ambaye siku hizi ni mbunge Kenya.
Tulizungumza na Mwalimu kwa muda Yusuf akimueleza alivyokulia Tanzania. Halafu tukapiga naye picha.
Tulipomuacha alinijia rafiki yangu mwingine wa muda mrefu Ronnie Mutebi, Kabaka wa sasa wa Buganda. Siku hizo alikuwa bado hajaupata ufalme.  Ronnie alinijia kwa shauku: “Ahmed nitambulishe kwa Mwalimu”.
Nikamshika mkono nikenda naye alipokuwako Nyerere.
“Mwalimu, huyu ni Ronnie Mutebi”. Nyerere alitabasamu akaanza kunyosha mkono lakini mimi nikafanya kosa. Nilimwambia: “Ni mtoto wa Kabaka Mutesa”. Nyerere akaurudisha mkono wake, akamtumbulia macho Ronnie,akageuza uso akenda zake.
Ronnie alighadhibika. “Umeona Ahmed alivyonifanyia? Umeona?”
Hadi leo Ronnie hakuisahau kadhia hiyo. Kuna wengi wasioweza kuyasahau yaliyowafika kwa Nyerere. Kuna Mtanzania mmoja (jina ninalihifadhi) ambaye siku hizi ni profesa Marekani. Kuna siku huyu bwana akiwa likizoni Tanzania alialikwa chakula cha mchana na Nyerere. Walikula, wakanywa na kuzungumza. Baadaye alikwenda kwenye steshini ya treni kupanda gari la moshi kwenda kwao sehemu za Mara.
Alipofika steshini alikamatwa na kuwekwa kizuizini.  Kumbe wakati wote ule alipokuwa anakula na Nyerere, tayari Nyerere alikuwa ameshatia saini hati ya kuamrisha awekwe kizuizini. Huko kizuizini alifanyiwa mambo asiyostahiki mwanamume kufanyiwa. Usuhuba wake na Kambona ndio uliomponza.
Nyerere amezitia saini hati nyingi za kuamrisha watu wawekwe kizuizini. Niliwahi kumuona akitia saini lakini kwenye kitabu. Ilikuwa katika hafla aliyoandaliwa katika School of Oriental and African Studies (SOAS), sehemu ya Chuo Kikuu cha London.
Tulikuwa tumesimama mimi, yeye na sahibu yangu Chama Matata. Akaja msichana mmoja wa Kihindi na kitabu alichokitunga Nyerere. Akamuomba Nyerere atie saini yake. Nyerere akaniomba nimshikie glasi yake ya mvinyo. Tukawa tunamuangalia alivyokuwa akiandika. Alianza kwa kuandika herufi ya J halafu K na alipoanza kuandika herufi ya N nilisema kama nalalamika: “Aaah…”
Mwalimu akaniuliza: “Nini?”
“Nilidhani utaandika J Kaisari,” nilimwambia. Akanambia: “Huwachi we mizaha yako…” Alijua nikimpiga kijembe na walinzi wake hawakupenda. Chama Matata hadi leo akiukumbuka mkasa huo hunieleza jinsi walinzi hao walivyokuwa wamevimbisha mashavu na kunikazia macho.
Ukweli ni kwamba wengi wetu Wazanzibari tunamuona Julius Nyerere kuwa kama Juliasi Kaisari (Julius Caesar) aliyezidhibiti siasa za Urumi ya kale kwa miaka na miaka. Julius huyu wetu ametuweza kwelikweli.
Chanzo: Raia Mwema

No comments :

Post a Comment