Kwarara Msikitini

airbnb

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Monday, December 22, 2014

DUBAI: Deira, Eneo, maarufu, Dubai, biashara, bei,uchumi

Deira: Eneo maarufu Dubai kwa biashara za bei ya chee 
Na Ibrahim Bakari, Mwananchi

KWA UFUPI
Kwa Tanzania, eneo hili linaweza kufananishwa na Kariakoo kwa kuwa na mvuto kibiashara
Ukiwa Tanzania, maeneo ya Kariakoo hasa Mtaa wa Kongo hukosi vurugu za wafanyabiashara na wanunuzi. Ni eneo lenye mkusanyiko mkubwa wa watu kutoka ndani na nje ya nchi.
Ukiwa Dubai kuna eneo linaitwa Deira. Eneo hili liko katikati ya mji wa kibiashara wa Dubai. Ni kati ya maeneo yenye wafanyabiashara wengi na hata watu wa mataifa mbalimbali hufika kwa ajili ya kufanya ununuzi kwa kuwa vitu vingi huuzwa kwa bei chee.
Wengi wanaofanya biashara ni kutoka India na Pakistani ambao ndiyo waliojaa hapa.
“Sehemu kubwa ya wenyeji hawafanyi biashara… wao wana majengo na wametupangisha wafanyabiashara na wao wanachukua kodi,” anasema Mohamed Mohsin raia wa Pakistan anayeuza mabegi na masanduku ya safari.
Deira ni kama eneo lililojitenga hivi na lango la bahari iliyotengenezwa. Eneo hili liko katikati ya mji lakini kufika kwake ni mpaka uvuke bahari kwa kutokea upande wa Kusini Mashariki.
Ili uvuke bahari kwenda Deira, hulazimiki kutumia mtumbwi, ngarawa au boti, bali kuna korido imejengwa chini ya bahari ya umbali wa mita 400. Huo ni umbali tu wa mtu kutembea kwa mguu na kisha kwa raha zako unajikuta umetokea eneo la Deira. Kwa hakika inapendeza!
Katika njia hiyo yenye viyoyozi na taa saa 24, hairuhusiwi mtu kuendesha baiskeli wala pikipiki.
Kila mmoja ni mstaarabu, kwani hakuna askari lakini mwenye baiskeli huteremka na kuikokota kupitia eneo hilo.
Utapata kila kitu
Hakuna kinachokosekana Deira, kuanzia mikufu ya dhahabu, fedha na almasi. Hata hivyo, Vito bei yake iko juu kiasi ikilinganisha na bidhaa nyingine.
Vitu ambavyo unaweza kupata ni nguo za kike na kiume, watoto, viatu, vifaa vya nyumbani, redio, televisheni za kila aina, kompyuta, kamera, simu za kisasa na zamani na bidhaa nyingine nyingi.
Fedha ya Dubai inaitwa Dirham na zikiwa 3.66 ni sawa na na Sh 1,730.
Nikiwa kwenye duka moja linalouza nguo za watoto, nilikutana na dada mmoja raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) aliyejitambulisha kwa jina la Nteza. Anasema amekuja Dubai kwa mapumziko na kufanya ununuzi.
Anasema DRC hakuna bidhaa nzuri ikilinganishwa na hizo alizozikuta Dubai.
Nikiendelea kuzunguka madukani, nilikutana na kundi la kina mama wakiwa katika duka moja linalouza viatu, walikuwa wamekusanya jozi zaidi ya 20.
Nilisilikiliza mazungumzo yao na kubaini kuwa wana lafudhi ya Afrika Magharibi hasa mataifa ya Nigeria au Ghana.
Niliwauliza sababu ya kununua jozi nyingi za viatu, mmoja alinieleza kuwa wao ni wafanyabiashara wa Nigeria na kwamba bidhaa wanazochukua kutoka Dubai, zinapendwa kwa kuwa nyingi zina ubora.
Bidhaa nyingi zinazouzwa hapa Dubai ni kutoka India, Malaysia, China, Hong Kong, Korea, Uingereza, Marekani na Taiwan zikiwa na ubora tofauti na zile zinazoingizwa Tanzania na maeneo mengine ya Afrika Mashariki na Kati kutoka China.
Wengine wanaofanya ununuzi ni Watanzania, Wakenya, Uganda na Sudan kwa kutaja kwa uchache.
Ukiacha wafanyabiashara hawa, kuna wengine wanatembea kama wenza wakifanya matembezi kuangalia mitaa na hata kufanya ununuzi. Kila mmoja hapa anashughulishwa na kilichomleta.
Mfumo wa uuzaji
Kwa wafanyabiasha wa Deira, hakuna wanaouza au kupanga bidhaa barabarani, kila mmoja ana eneo lake ndani ya fremu au nyumba. Kuna ustaarabu wa biashara ikilinganishwa na hali ilivyo nchini.
Wauzaji wenyewe ndiyo wanaosimama nje ya maduka yao kuita wanunuzi na kuwashawishi kuingia ndani. Pia baadhi ya maduka hutumia watu kushawishi wateja kununua na kisha kuwapa kamisheni.
Wakati mwingine, wafanyabiashara hutumia mbinu mbalimbali kuvutia wateja. Ikiwa mteja anauliza bei na kuonyesha nia ya kununua, hupatiwa juisi au kahawa ili waendelee kuzungumza biashara.
Maduka mengi katika soko la Deira hufanya zaidi biashara kuanzia saa 12 jioni hadi usiku wa manane.
Uzuri wake, hakuna uporaji. Unaweza hata kutoa burungutu la fedha, ukahesabu hadharani na hakuna anayeshtuka wala kukuangalia. Sasa jaribu kufanya hivyo katika mitaa ya Kariakoo yetu!
Maduka ya kuuza vito vya thamani, yamejaa dhahabu na ni ya vioo tupu, hakuna hata mlinzi wala wateja kusubiriana kuingia, ni mwendo wa fedha.
Dereva teksi mmoja raia wa India, anasema wakati wanapoingia wanapewa maelekezo na ustaarabu wa jinsi ya kuishi na kile wanachotaka wenyeji.
Mbali na maduka hayo, kuna migahawa mbalimbali ambayo wengine hutumia kupata mlo wa usiku na kabla au baada ya kununua mahitaji yao.
Usafiri wa kuingia na kutoka Deira wa ni wa mabasi na teksi kwa upande mwingine, ukiacha njia ile niliyotaja mwanzo ya kupita chini ya bahari.

Kwa hakika eneo la Deira linaichangamsha vilivyo Dubai, jiji lililosheheni majengo marefu. Kwa taarifa yako hapa ndipo penye ule mnara mrefu kuliko yote duniani. Mnara huu unaitwa Burj Khalifa. Mhh raha, raha sana kuwa Dubai!

No comments :

Post a Comment