Written by Elbattawi // 14/12/2014 //
Na Rashid Seif – mzalendo.net
WAZANZIBARI WANAOISHI nchini Uingereza, jana walifanya maadhimisho ya miaka 51 ya Uhuru wa Zanzibar, ambao ulipatikana tarehe 10 Desemba 1963.
Uhuru wa Zanzibar, ambao ulipatikana mwezi mmoja kabla ya Mapinduzi ya Zanzibar ambayo huchukuliwa kuwa ya kishujaa na sehemu ya kujivunia katika historia ya kujitawala ya visiwa vya Unguja na Pemba.
Hata hivyo, baadhi ya wananchi wanaoishi ndani ya Zanzibar, hawajatafakari wala hawajawahi kudai kwenye taasisi za serikali ya mapinduzi kuadhimisha siku hiyo adhimu.
Pia, hata wawakilishi wao hawajawahi kufikiria kupeleka mswada kwenye Baraza la Wawakilishi, ili kufanya maadhimisho ya siku hiyo. Matukio yote makubwa yanahitaji kukumbukwa kwa muktada wa historia…hata kama yanachukiza.
Kuificha siku ya uhuru wa Zanzibar, ni kuipotosha historia ya kweli na kunatoa taswira ya woga. Pia, kunaleta athari ya kukosa ukweli wa historia ya nchi kwa vijana waliyozaliwa baada ya uhuru huo. Historia daima itabaki kuwa historia.
Kuificha siku ya uhuru wa Zanzibar, ni kuipotosha historia ya kweli na kunatoa taswira ya woga. Pia, kunaleta athari ya kukosa ukweli wa historia ya nchi kwa vijana waliyozaliwa baada ya uhuru huo. Historia daima itabaki kuwa historia.
Hapa ni sawa na mtu aliyesafiri kutoka Tabora hadi Marekani, kwenda kutembea lakini katika maisha yake yote hakuwahi kutoka nje ya mkoa wa Tabora, ni vichekesho.
Miaka 51 tangu kutolewa uhuru wa Zanzibar, ni umri unaoweza kumfanya mtu kuwa na wajukuu ambao wanahitaji kujua kabla ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari 12, 1964 hapo nyuma yake kulitokea nini?.
Wiki iliyopita tulisheherekea siku ya Uhuru wa Tanganyika, ama ‘Tanzania Bara’ kama wanavyotaka CCM, na siku hii huonwa kuwa ya kitaifa na hata maadhimisho yake ni ya kitaifa. Hapa nauliza:
Kama uhuru uliyotolewa na Muingereza kwa raia kuna haramu gani kufanyiwa kumbukumbu na maadhimisho na ni kwanini Tanganyika, wanafanya maadhimisho kila mwaka…tena kwa jina la Tanzania; Je, ni sahihi au ni upotoshaji?.
Katika nyaraka nyingi, za siku ya Uhuru wa Tanganyika zimepewa nembo tu, na hata wakati fulani katika skuli za Tanganyika, wanafundishwa kuwa Tanzania ilipata uhuru Desemba tisa. Wala si Tanganyika. Hii ni kwa sababu upande wa Zanzibar, wameiua siku ya uhuru wake.
Siku ya Uhuru wa Zanzibar imetekwa, ama imepotezwa na nafasi yake kuchukuliwa na siku ya uhuru wa Tanganyika wala siyo kweli kuwa nafasi yake imechukuliwa na Mapinduzi ya Januari 12.
Zaidi ya hayo, bado siku ya Mapinduzi huonekanwa kuwa siku ya Wazanzibari zaidi, na si ya kitaifa kama ilivyo siku ya Uhuru wa Tanganyika. Tanganyika kwa makusudi wanapotoshwa na Zanzibar, wanapotoshwa zaidi. Hatujui kuwa inafanyika hivyo kwa bahati mbaya kutokujua au kwa makusudi.
Kwanini siku hii ya Uhuru wa Zanzibar imepuuzwa, hata baadhi ya machapisho hayaitambui kama siku ya kukumbukwa na sijui kama hata kule Idara ya nyaraka za serikali (Zanzibar Archives) kama kuna nyaraka za asili za kukabidhia uhuru wa Zanzibar.
Waliyodai uhuru wa Zanzibar na waliyokabidhiwa uhuru huo picha zao zipo na wote ni wanzaniabri vindakindaki waliyokuwa na uchungu na nchi yao kuliko hali ilivyo sasa.
Siku moja mwanzoni mwa miaka 1980, nilimuuliza kiongozi mmoja wa ZPPP, Omar Hamad Mkamandume (marehmu) kutoka Ole, Pemba kuwa: “Bila ya uhuru wa Zanzibar wa Desemba 10, 1963 mapinduzi yengewezekana?.
Alinijibu kama kwa utani: “Said Washoto…Yussuf Himid…Kaujore na Said Bavuai…Bila ya kupata uhuru wetu ‘Kamati ya watu 14′ isingeweza hata kuchungulia Bomani…wacha kuingia na kupindua…chini ya himaya ya Muingereza”
Hata hivyo, hatua inayochukuliwa na wazanzibari wanaoishi nje waliyoko mataifa mbali mbali ya nchi za Ulaya, Marekani na Uarabuni inastahiki kupongezwa kwa sauti na ya wazi bila woga. Wanachokiadhimisha ni haki yao, ni kitu cha kweli ni historia inayojuilikana kote Duniani.
Jana Jumamosi, Desemba 13, kupitia Jumuiya za Wazanzibari zilizopo Uingereza, Wazanzibari kutoka kona zote za nchi hiyo walijumuika pamoja kuadhimisha miaka 51 ya uhuru wa Zanzibar, kwenye Mkahawa wa Global Buffet, Wilson Way, Ilford mji London.
Vijana wadogo wanaozaliwa kwenye mataifa hayo ambao wazee wao wanatoka Zanzibar, wana uelewa mkubwa wa historia sahihi ya Zanzibar, kabla ya uhuru, baada ya uhuru na Mapinduzi ya Januari 12, 1964. Na nifaraja kubwa kwao.
Serikali ya Zanzibar, kupitia wizara yake ya elimu inalazimika kuanza mchakato wa kufundisha somo sahihi la historia ya Zanzibar na kuachana na upotoshaji kwa sababu za woga na chuki zilizopitwa na wakati.
No comments :
Post a Comment