NA MWANDISHI WETU
Wiki iliyopita, Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu, ilitoa taarifa iliyoeleza kuwa, Rais Kikwete atatoa maamuzi yake wiki hii kuhusiana na uchotwaji wa fedha za Escrow baada ya kupokea ripoti, nyaraka na ushauri wa Bunge kuhusu akaunti hiyo.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa, Rais Kikwete alipokea Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ripoti ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) na maazimio ya Bunge kuhusu akaunti hiyo.
Rais aliagiza vilevile kuwa ripoti hiyo itangazwe kwenye magazeti yanayosomwa na watu wengi nchini na mitandao ya kijamii ili isomwe na Watanzania wengi zaidi kujua kilichomo na kwamba atatolea maamuzi mambo yote yanayomhusu moja kwa moja na yale yanayohusu serikali atayatolea maagizo na maelekezo ya namna ya kuyashughulikia.
Kutokana na taarifa hiyo, kina Prof. Muhongo, Tibaijuka na viongozi wengine waliotajwa watakuwa njia panda kutaka kujua hatma yao katika maamuzi ya Rais.
Miongoni mwa maazimio ya Bunge yanayowaweka kwenye wakati mgumu viongozi hao ni yale yaliyopendekeza kuwa mamlaka ya uteuzi (Rais Kikwete) iwafute kazi wote wawili kutokana na namna walivyoguswa na kashfa hiyo. Wateule wengine wa Rais walio kwenye wakati mgumu kuanzia wiki hii ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema.
Awali, wakati wa mijadala ya Bunge kuhusiana na sakata hilo, wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na mawaziri kadhaa walijaribu kwa mbinu mbalimbali kuwakingia kifua waliotajwa ili kusitolewe azimio la kutaka mamlaka ya uteuzi iwaondoe viongozi waandamizi wa serikali waliohusika katika kashfa hiyo.
Hata hivyo, jaribio hilo lilikwama na mwishowe yakatolewa maazimio manane yakiwamo yanayopendekeza kuwa wote walioguswa wachukuliwe hatua.
Ni wazi kwamba Prof. Muhongo, Maswi, Prof. Tibaijuka na Werema wako katika kipindi kigumu, kwani uwezekano wa kubaki katika nafasi zao unaonekana kuwa mdogo; hasa kutokana na rai zinazotolewa kila uchao kutoka kwa makundi mbalimbali yanayopinga uchotwaji wa fedha hizo, zikiwamo nchi marafiki zinazofadhili miradi mbalimbali ya maendeleo kama Marekani na Ulaya.
Aidha, taarifa kwamba Marekani imesikitishwa na kashfa hiyo na kusitisha utekelezaji wa mkataba wa ufadhili wa miradi mbalimbali nchini kupitia shirika lake la changamoto za milenia (MCC) hadi hapo hatua zaidi zitakapochukuliwa kushughulikia, jambo hilo zimezidi kuongeza ugumu kwa viongozi waliopendekezwa kuenguliwa.
Tahadhari kuhusiana na hatari ya kutochukuliwa hatua zaidi kwa watu waliotajwa kuhusika na kashfa hiyo iliwahi pia kutolewa bungeni na Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila, ambaye alisema kuwa hadi sasa, nchi kadhaa marafiki zimesitisha kutoa fedha zilizoahidi kusaidia bajeti kutokana na kashfa ya Escrow.
Taarifa iliyotolewa na Ubalozi wa Marekani Alhamisi iliyopita, ilieleza kuwa wakurugenzi wa MCC waliokutana katika mkutano wao uliofanyika Desemba 10, mwaka huu wamesikitishwa na hali ya rushwa nchini Tanzania.
“Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Marekani la Changamoto za Milenia (MCC) ilikutana katika mkutano wa kila mwaka wa kuchagua nchi zitazopatiwa fedha na MCC, katika mkutano huo Bodi ilielezea hofu na masikitiko yake kuhusu hali ya rushwa nchini Tanzania, ikiwa ni pamoja na yale yaliyojitokeza hivi karibuni katika suala linalohusu kampuni ya kuzalisha umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL),” ilieleza taarifa hiyo.
“Tumetiwa moyo na tamko lililotolewa na Ikulu hapo tarehe 9, Desemba kwamba hivi karibuni itashughulikia maazimio ya bunge kuhusu IPTL. Tunatoa wito kwa serikali kuchukua hatua za haraka kuhusu suala hili hasa kutokana na uzito wake katika masuala muhimu kadhaa ya maendeleo.” ilieleza zaidi taarifa hiyo.
WABUNGE CCM
Sababu nyingine inayotajwa kuwaweka kina Muhongo katika wakati mgumu ni ukweli kuwa maamuzi ya Bunge yalitokana na taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) inayoundwa na wabunge wengi kutoka CCM (walishiriki 19 kati ya 24); na tena PAC ilitumia ripoti za vyombo vya umma kama CAG na Taasiasi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kabla ya kutoa mapendekezo yake.
Inaelezwa kuwa maamuzi ya haki ndiyo pekee yatakayoamua hatma ya watu waliotajwa kuhusika na kashfa hiyo kwani serikali haitapenda kujiingiza kwenye mgogoro wa moja kwa moja na Bunge linalotawaliwa kwa kiasi kikubwa na wabunge kutoka CCM.
MAAZIMIO YA BUNGE KUHUSU ESCROW
Baada ya mjadala mkali, Novemba 29, mwaka huu Bunge lilitoa maazimio manane, likiwamo la kutenguliwa kwa nyadhifa za Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Muhongo, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Prof. Tibaijuka na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Werema kwa kashfa ya uchotwaji wa zaidi ya Sh. bilioni 321 kutoka kwenye akaunti ya Tegeta Escrow, iliyokuwa BoT.
Wengine waliopendekezwa kuvuliwa nyadhifa zao ni wanakamati wa kamati za kudumu za bunge hilo, William Ngeleja (Sheria, Katiba na Utawala), Andrew Chenge (Bajeti) na Victor Mwambalaswa.
Pia wamo Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi na Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe, ndiye aliyesoma maazimio hayo baada ya kufikiwa kwa maridhiano baina ya kamati hiyo, kambi ya upinzani bungeni na Chama Cha Mapinduzi.
Zitto alitaja maazimio hayo kuwa ni pamoja na viongozi wa umma na maofisa wa ngazi za juu serikalini kutakiwa kuwajibika kwa sababu wamehusishwa na vitendo vya kijinai katika sakata hilo linalohusisha kampuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania (IPTL).
Bunge pia lilitaka Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru), Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya ulinzi na usalama, kufanya uchunguzi dhidi ya wote waliotajwa kuhusika na sakata hilo na wale watakaobainika kuhusika kwenye vitendo hivyo vya jinai.
Katika azimio jiongine, Bunge pia lilitaka Kamati za Kudumu za Bunge kuwavua nyadhifa wanakamati wake wakiwamo Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bajeti, Andrew Chenge, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Katiba, Sheria na Utawala, William Ngeleja na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Victor Mwambalaswa.
Kwa mujibu wa taarifa ya CAG, Chenge na Ngeleja wametajwa kunufaika na fedha za mwanahisa Rugemalira kwa Chenge kupewa Sh. bilioni 1.6 na Ngeleja Sh. milioni 40.2.
Maazimio mengine ni kumtaka Rais kuunda Tume ya Uchunguzi ya Kijaji kuchunguza tuhuma za utovu wa maadili dhidi ya majaji kuhusishwa kwenye kashfa hiyo. Majaji waliotakiwa na Bunge kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi ni pamoja na Jaji Aloysius Mujulizi na Jaji Prof. Eudes Ruhangisa wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
Bunge pia lilitaka mamlaka husika za kifedha na za kiuchunguzi kuitaja Stanbic Bank Tanzania Ltd na benki nyingine yoyote itakayogundulika baada ya uchunguzi wa mamlaka za kiuchunguzi kujihusisha na utakatishaji wa fedha zilizotolewa katika akaunti ya Escrow, kuwa ni taasisi zenye shaka ya utakatishaji wa fedha haramu.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment