Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akitoa hutuba yake kwa wananchi wa Kijiji cha Dongongwe Wilaya ya Kati Jimbo la Uzini Mkoa wa Kusini Unguja katika sherehe za Uzinduzi wa Umeme Kijijini hapo leo (kushoto) Waziri wa Ardhi,Makaazi,Maji na Nishati Ramadhan Abdalla Shaaban, Mbunge wa Jimbo la Uzini Mohamed Seif Khatib (wa kwanza kulia) akifuatiwa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kusini Unguja Ramadhan Abdalla Ali
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akitoa hutuba yake kwa wananchi wa Kijiji cha Dongongwe Wilaya ya Kati Jimbo la Uzini Mkoa wa Kusini Unguja katika sherehe za Uzinduzi wa Umeme Kijijini hapo leo.
Waziri wa Ardhi,Makaazi,Maji na Nishati Ramadhan Abdalla Shaaban alipkuwa akimkaribisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein kuzungumza na wananchi baada ya kuzindua rasmi nishati ya Umeme katika Kijiji cha Dongongwe Wilaya ya Kati Jimbo la Uzini Mkoa wa Kusini Unguja leo, [Picha na Ikulu.]
STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 18.12.2014
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amezindua umeme katika kijiji cha Dongongwe, Mkoa wa Kusini Unguja na kusema kuwa Serikali kuwapelekea huduma bora za kijamii, kiuchumi na maendeleo wananchi wake ni wajibu wake na kusisitiza kuwa hayo ndio malengo ya Mapinduzi ya Januari 12, 1964.
Dk. Shein aliyasema hayo leo katika hotuba yake aliyoitoa mara baada ya kuzindua umeme katika kijiji cha Dongoongwe, kiliopo wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja na kuhudhuriwa na viongozi wa vyama vya siasa na serikali pamoja na wananchi kutoka maeneo mbali mbali wa Jimbo la Uzini na vitongoji vyake.
Katika maelezo yake Dk. Shein alisema kuwa kufikish huduma za umeme ambazo amezizindua leo, huduma za maji ambazo tayari zimeshafika kijiji hapo pamoja na barabara ni wajibu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kama Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 ilivyoeleza.
Akinukuu Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 katika Ibara ya 10, Dk. Shein alisema kuwa Ibara hiyo imeeleza wazi kuwa “Kwa madumuni ya kuendeleza umoja na maendeleo ya watu na ustawi wa jamii katika nchi itakuwa ni wajibu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ...kutoa huduma za kutosha kwa ajili ya kuendeleza watu...”.
Aidha, Dk. Shein alisema kuwa maendeleo ni mchakato kwani ni jambo ambalo halikamiliki siku moja na badala yake huenda hatua kwa hatua hivyo Serikali itaendelea kuzipeleka huduma nyengine zilizobaki kijijini humo ikiwemo barabara na kuwaahidi wanakijiji hao kutengenezewa barabara yao hatua kwa hatua.
Dk. Shein alisema kuwa maendeleo hayachagui mtu wala eneo analotoka hivyo Serikali anayoiongoza itahakikisha inawapelekea maendeleo wananchi wote kwani hilo ndio jukumu la Serikali na pia ni malengo ya Mapinduzi ya Januari 12, 1964.
Alisema kuwa jitihada za kupeleka umeme vijijini ni kubwa sana kwa upande wa Unguja na Pemba na kusisitiza kuwa ingwa Zanzibar ni nchi ya mwanzo katika Afrika Mashariki kwua na umeme katika mwaka 1875 lakini sio watu wote waliobahatika kuupata.
Akitoa historia ya huduma hiyo hapa Zanzibar Dk. Shein alisema kuwa matumizi rasmi ya umeme kwa kisiwa cha Unguja yalianza mwaka 1908 na kwa kisiwa cha Pemba ni mwaka 1959 na kusema kuwa wananchi walio wengi walianza kupata huduma za umeme mara baada ya Mapinduzi matukufu ya mwaka 1964.
Dk. Shein alisema kuwa Mapinduzi ya Januari 12,1964 ndio yalioleta maendeleo ikiwemo kusambaza huduma za umeme kwa wananchi.
Aliongeza kuwa watawala wote walioitawala Zanzibar wakiwemo Wareno na Sultan kutoka Oman ambaye ametala zaidi ya miaka 100 hawakupeleka umeme katika kijiji hicho cha Dongoongwe lakini Serikali ya Mapinduzi Zanzibar chini ya Chama cha Mapinduzi kimepeleka huduma hiyo na nyenginezo.
Alisema kuwa hatua kubwa za maendeleo hapa Zanzibar zimefanywa kutokana na Sera za ASP na sasa ni CCM chama ambacho kimekuwa kikitekeleza Sera na Ilani yake. Aidha, Dk. Shein alitumia fursa hiyo kutoa pongezi na shukurani kwa shirika la umeme Zanzibar ZECO, Wizara husika pamoja na wananchi wa kijiji hicho na viongozi wao.
Katika sherehe hizo za uzinduzi Dk. Shein alitoa wito kwa wananchi wa Dongoongwe kuitumia huduma hiyo ya umeme kama inavyotakiwa kwa lengo la kuwapatia maendeleo pamoja na huduma zao nyenginezo za kijamii.
Dk. Shein katika Sherehe hizo za uzinduzi wa umeme kijijini hapo, alitoa vyeti maalum kwa viongozi wa Kamati za Umeme katika Jimbo hilo la Uzini huku sherehe hizo zikipambwa kwa tenzi na ngoma ya maubwa ambayo ilitoa burudani safi.
Nae Waziri wa Maji, Ujznei, Nishati na Ardhi Mhe. Ramadhan Abdalla Shaaban alisema kuwa hayo yote ni Matunda ya Mapinduzi kwani bado yanaendelea na kusisitiza kuwa umeme si anasa ni kitu muhimu hivyo ni lazima kitumike hasa katika dunia ya leo ya sayansi na teknolojia.
Mapema Mkurugenzi wa Shirika la umeme Zanzibar ZECO Bwana Hassan.. alisema kuwa Sera ya Serikali ya Mapindyuzi ya Zanzibar ni kuhakikisha kuwa inawasogezea huduma za kijamii wananchi wake popote walipo na kazi hiyo ni endelevu hadi Serikali ihakikishe wananchi wote wanafikiwa na huduma zote muhimu ikiwemo umeme.
Alisema kuwa gharama zilizotumika katika kupelekea umeme kijijini hapo ni shilingi milioni 100,480,500.00 ambapo kati ya fedha hizo Shirika limechangia jumla ya shilingi milioni 85,480,500.00 na Mbunge wa Jimbo hilo amechangia shuilingi milioni 15,000,000.00.
Alieleza kuwa kazi ziliyofanywa ni pamoja na ujenzi wa njia kubwa ya umeme ya mkondo wa kilovoti 33 yenye urefu wa kilomita 2.7, uwekani wa vitop viwili vya transfoma zenye uwezo wa 100KVA kwa Ghana na 50 KVA kwa Dongongwe, ujenzi wa njia ndogo zenye urefu wa kilomita 2.5 pamoja na malipo ya fidia ya vipato shilingi milioni 18,614,7000.00 huku akiwataka wananchi wa kijiji cha Mkuku kujiandaa kupata huduma hiyo hivi karibuni.
Katika risala yao wananchi wa Dongongwe walisema kuwa wanakamilisha safari ndefu ya kusaka umeme na wanakuwa kijiji cha mwisho katika jimbo la Uzini kupata umeme na kutoa shukurani kwa Serikali, Shirika la Umeme, pamoja na viongozi wao wa Jimbo akiwemo Mbunge wa Jimbo hilo Mhe. Mohamed Seif Khatib.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments :
Post a Comment