Wakati dunia inaadhimisha siku ya haki za binaadamu duniani kote watuhumiwa wa ugaidi kutoka zanzibar wamefikishwa leo kwenye mahakama ya rufaa ilifanyika Vuga mjini Zanzibar katika kesi inayowakabili yakuhatarisha usalama wa taifa.
Mashitaka hayo ya kuhatarisha usalama wa taifa pamoja na maandamano bila ya kibali na kuharibu mali ya serikali, yalifunguliwa dhidhi ya washitakiwa hao 10 kutoka jumuiya ya uamsho na mihadhara ya kiislamu zanzibar tokea mwaka 2012. ambapo walikaa jela zaidi ya mwaka mmoja.
Waliofikishwa mahakamani leo ni Sheikh Farid Hadi Ahmed, Msellem Ali Msellem, Abdallah Said Madawa na Hassan Bakari ambao mwaka huu walikamatwa tena na kufunguliwa mashitaka ya ugaidi na kufadhili vijana kutoka nje ya nchi kuja kufanya ugaidi nchini.
Katika kesi ya leo ambayo ni rufaa ya kupinga uamuzi wa mahakama kuu ya Zanzibar kuwapa dhamana haikusikilizwa na imeakhirishwa kutokana na kutokuwepo kwa watuhumiwa wawili ambao ni Sheikh Azzan Khalid Hamdan ambaye ni mgonjwa na Mussa Juma ambaye taarifa zake hazijulikani.
Katika maelezo ya mahakama ya rufaa Upande wa mashtaka ukiongozwa na Raya Mselem kutoka ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar, ulikiri kwamba bila ya kuwepo hao wawili itakuwa vigumu kuendelea na rufaa hiyo, jambo ambalo halikupingwa upande wa utetezi. Lakini pia upande wa mashtaka ulitaka zitolewe taarifa kupitia vyombo vya habari ili watuhumiwa hao waweze kufika mahakamani tarehe itakayopangwa rufaa hiyo.
Baada ya kushindikana kusikilizwa kwa kesi hiyo mawakili wa upande wa utetezi wanaoongozwa na Salim Tawfik, Abdallah Juma na Rashid Abdallah walisema wanasubiri uamuzi utakaotolewa na mahakama ya rufaa ambao kwa mujibu wa ratiba mahakama hiyo hufanya vikao mara moja kwa mwaka.
Mahakama kuamua pingamizi la Uamsho
Mahakama kuamua pingamizi la Uamsho
Wakati huo huo; Hatima ya usikilizwaji wa maombi ya marejeo ya viongozi wa Jumuiya za Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (Jumiki), inatarajiwa kujulikana leo, wakati Mahakama Kuu Dar es Salaam itakapotoa uamuzi wa pingamizi la awali la Jamhuri dhidi ya maombi hayo.
Washtakiwa hao walifungua maombi hayo Mahakama Kuu, Dar es Salaam Oktoba 13, 2014, kupitia kwa jopo la mawakili wanaowatetea, pamoja na mambo mengine wakiomba mahakama hiyo iwafutie mashtaka ya ugaidi yanayowakabili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Hata hivyo, mjibu maombi (Jamhuri) iliweka pingamizi la awali dhidi ya maombi hayo, ikiomba maombi hiyo kuyatupilia mbali kwa madai kuwa hati ya kiapo inayounga mkono maombi hayo ina dosari za kisheria na kwamba mahakama hiyo haina mamlaka kisheria kusikiliza maombi hayo.
Jaji Dk Fauz Twaib alipanga kutoa uamuzi wa pingamizi hilo leo, baada ya kusikiliza hoja za pande zote juma lililopita, yaani hoja za pingamizi kutoka kwa Jamhuri na majibu ya hoja hizo za pingamizi kutoka kwa watoa maombi.
Ikiwa Jaji Twaib atakubaliana na hoja za pingamizi hilo la Serikali, basi maombi hayo yatatupiliwa mbali na hivyo washtakiwa hao kuendelea na mashtaka hayo, au watalazimika kuchukua hatua nyingine kadri Mahakama itakavyoelekeza katika uamuzi wake.
Pia, kama Mahakama itatupilia mbali hoja za Serikali za pingamizi lake basi itaendelea na usikilizwaji wa maombi ya msingi na hatimaye kutoa uamuzi wa kuyakubali au kuyakataa.
Washtakiwa katika kesi hiyo ni pamoja na Sheikh Farid Hadi Ahmed (43), Jamal Noorid Swalehe, Nassoro Hamad Abdallah, Hassan Bakari Suleiman, Anthari Humoud Ahmed, Mohamed Isihaka Yussuph na Abdallah Hassan Hassan.
Wengine ni Hussein Mohamed Ally, Juma Sadala Juma, Said Kassim Ally, Hamis Amour Salum, Abubakar Abdallah Mngodo, Salum Ali Salum, Salum Amour Salum, Alawi Othuman Amir, Rashid Ally Nyange, Amir Hamis Juma, Kassim Salum Nassoro, Said Shehe Sharif na Mselem Ali Mselem.
Katika maombi yao, pamoja na mambo mengine wanaiomba mahakama hiyo itupilie mbali hati ya mashtaka waliyofunguliwa, wakidai kuwa imefunguliwa bila ya ridhaa ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) na kwamba hati hiyo haielezi makosa ya ugaidi wanayotuhumiwa.
Chanzo: Gazeti la Mwananchi
No comments :
Post a Comment