WANANCHI BARA WANASIKITIKA KWA UNYONGE KABISA KWA MAISHA YA RUSHWA NA WIZI YANAYOENDELEA NCHINI. SIKILIZA AUDIO YA HAPA JUU ILI UJUE TUTAELEKEA WAPI KAMA TAIFA LITAKUWA BILA YA ADHABU KALI YA KIFO KWA RUSHWA NA WIZI MKUBWA KAMA HUU WA ESCROW!
Baadhi ya Wazanzibari wanataka kuwashinikiza wajumbe wao wa Baraza La Wawakilishi mapema baada ya sherehe za mwaka mpya kumalizika kuandaa mswada ambao utatoa adhabu ya kifo kwa wizi mkubwa kama huu uliotokea kwenye Akaunti ya Escrow ya Tegeta huko Bara.
Hayo yanazungumzwa na baadhi ya Wazanzibari ambao wamechukia sana juu ya rushwa na wizi unaotokea nchini mara kwa mara na kuwanyima wananchi uwezo wa kujiendeleza kimaisha au kukwamisha miradi ya maendeleo nchini.
Mswada huu unaopendekezwa na wananchi unakuja baada ya wizi mkubwa kufanyika huko Tanzania Bara, na kama utakubalika kuwa sharia, itakuwa imepatikana njia madhubuti ya kuzuwia rushwa na wizi nchini.
Haijulikani ni wananchi gani hao wenye fikra na nia ya kuwaeleza wajumbe wao wa Baraza La Wawakilishi kuchukuwa hatua hio ya kutengeneza mswada kama huo, japokuwa inajulikana wazi kuwa wanachama wa vyama vyote vya Visiwani wamechoshwa na wizi kama huu unaotokea nchini.
Hii hatua ya wananchi inakuja baada ya kuonekana kuwa Rais Kikwete analegalega na kupatwa kigugumizi juu ya hatua madhubuti za kuchukuwa ili kukata kwa mara moja maini ya wezi na wala rushwa nchini.
Wengi wanaona kuwa wezi na wala rushwa nchini wanapewa nguvu na kuwa Jumaatatu (Dec 22, 2014) wataendelea kulindwa, vyenginevyo Prof Tibaijuka asingelikuwa na jeuri ya kusema hadharani kuwa hatojiuzulu kama angejua wembe mkali upo njiani unakuja - wakati yeye amekamatwa red-handed na bilioni 1.6 za wanyonge na maskini wa nchi hii. Kwa vyovyote vile, Prof Tibaijuka atalindwa na kuachwa huru na labda kubadilishwa wizara au kupumzishwa kwa muda, kabla hajapewa cheo chengine ili aje kutuibia tena zaidi ya bilioni 1.6 za hivi sasa chini ya pazia lile lile jekundu la 'donation'.
Mswada huu wa adhabu ya kifo kama ukipita kwenye Baraza La Wawakilishi na kuwa sharia, basi Zanzibar itakuwa sawasawa na China ambako walarushwa hukumbana na adhabu ya kifo au kifungo cha maisha. Kwa njia hii Wachina wameweza kuidhibiti rushwa na wizi nchini mwao, japokuwa kero hizi bado zipo nchini China lakini kwa kiwango kidogo sana.
Jitihada ziligonga ukuta za kumtafuta Speaker wa Baraza La Wawakilishi ili kumuuliza kama ukipelekwa mswada wa aina hio kwenye Baraza La Wawakilishi kama itawezekana Baraza kuushughulikia.
Zanzibar Ni Kwetu inawaunga mkono wananchi hao wenye nia hio na ipo pamoja nao bega kwa bega kwa njia yoyote ile, ili Taifa letu liweze kuiangamiza rushwa na wizi nchini kwetu.
No comments :
Post a Comment