Kwarara Msikitini

airbnb

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Sunday, February 22, 2015

CUF chazindua mkakati wa ushindi 2015

  Chakabidhi vifaa vya Sh. mil 515

Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad.
Chama cha Wananchi (CUF) kimezindua mkakati mzito wa ushindi utakaotekelezwa na kamati za uchaguzi, kuanzia ngazi ya tawi, hadi taifa.
 
Aidha wajumbe watakula kiapo hadharani kuhakikisha wagombea wa chama hicho wa nafasi za udiwani, ubunge, uwakikishi na urais, wanashinda katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu katika visiwa vya Unguja na Pemba.
 
Katika mkakati huo, chama hicho kimekabidhi vifaa vyenye thamani ya Sh. milioni 515 vya kufanikisha ushindi huo, yakiwamo magari aina ya Hilux, ambayo kila wilaya katika wilaya 10 zilizoko katika visiwa vya Unguja na Pemba imekabidhiwa gari moja.
 
Kila jimbo katika majimbo 50, limekabidhiwa pikipiki moja aina ya Vespa, huku kila zone zilizogawanywa mara nne kichama ikikabidhiwa lori moja na vifaa vya muziki kwa ajili ya kampeni.Vifaa hivyo vilikabidhiwa na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, katika mkutano wa hadhara ulioandaliwa kwa ajili ya uzinduzi wa kamati hizo, katika viwanja vya Mnazi Mmoja, mjini Unguja jana.
 
Wajumbe wa kamati hizo zitakazoongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar, walikula kiapo hicho mbele ya viongozi wakuu wa chama hicho kwa kuchukua dhima kwamba, watahakikisha ushindi huo unapatikana.
 
Walikula kiapo hicho mbele ya mkutano huo uliohudhuriwa na maelfu ya wafuasi wa CUF waliomiminika kutoka visiwa vya Unguja na Pemba wakiongozwa na Maalim Seif.
 
Akihutubia mkutano huo, Maalim Seif aliwaonya wajumbe wa kamati hizo kuwa atakayekwenda kinyume atachukuliwa hatua na chama na kwamba, kwa kuwa amechukua ahadi kwa kiapo, pia ataadhibiwa na Mwenyezi Mungu kwa kudanganya hadharani.
 
Alisema miaka yote ya uchaguzi mkuu wamekuwa wakijiandaa katika miezi ya Juni na Julai, lakini mwaka huu wameamua kufanya maandalizi ya aina yake mapema kwa kuwa wanaamini kuwa yanawapeleka kwenye ushindi.
 
Alisema ili kufanikisha ushindi huo, kuanzia sasa kazi za ofisini na za utawala wa chama hazina nafasi na kwamba, wajumbe wa kamati tendaji za chama wamebadilika na kuwa wajumbe wa kamati za kushughulikia uchaguzi.
 
Alisema wana matumaini makubwa kwamba, uchaguzi mkuu wa mwaka huu utakuwa ni wa mabadiliko ya kheri, kwani wanataka kuondoa utawala na kuweka uongozi visiwani utakaowaongoza Wazanzibari kwenye mamlaka kamili visiwani hapa na kwamba, safari ya kufikia lengo hilo imeanza.
 
Aliongeza: "Tunaelekea kuijenga Zanzibar mpya. Lengo la safari hii ni kuona CUF inakamata hatamu ya uongozi na kujenga Zanzibar mpya tunayoipenda itakayopoza kiu ya Wazanzibari ya kutaka mamlaka kamili ya Zanzibar."
 
Alisema pia wanataka kuondoa kasoro zote zilizopo, ikiwamo ubaguzi wa rangi, dini, nywele, pia ukandamizaji na unyanyasaji na kujenga umoja na mshikamano na wananchi, ambao watakuwa wa daraja moja.
 
Maalim Seif alisema wanataka kuhakikisha Wazanzibari hawaongozwi kutoka Dodoma wala Uarabuni, bali wanajiongoza wenyewe.
 
Alisema fomu za kuomba uteuzi wa kugombea udiwani, ubunge na uwakilishi katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, zitaanza kutolewa Machi mosi, mwaka huu.
 
Mshauri wa Katibu Mkuu wa CUF, Mansor Yussuf Himid, alisema chama kimeshaanza mikakati ya kina ya maandalizi ya kuelekea katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, ambapo maandalizi hayo ni ya aina yake yatakayopelekea ushindi mkubwa kwa chama katika uchaguzi huo.
 
Alisema serikali itakayoongozwa na Maalim Seif kila Mzanzibari atathaminiwa utu wake hivyo aliwasihi vijana kuwa na mshikamano na kuhakikisha wanaipigia kura CUF katika uchaguzi mkuu ujao. Alisema katiba iliyopendekezwa hawaitaki na hawatoshiriki katika kura ya maoni kutokana na kutojali maslahi ya Zanzibar.
 
Naibu katibu mkuu wa CUF Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui, alisema Wazanzibari wanataka misingi ya haki na usawa na hakuna chama kinachoweza kufanya hivyo ila ni CUF.
 
Akisoma risala ya wanachama katibu wa wilaya ya Wete wa chama hicho, Riziki Omar Juma, alisema mwaka huu ni kuona maamuzi ya serikali wanayoitaka ambayo itawapatia mamlaka kamili.
 
Alikipongeza chama hicho kwa kufanya maandalizi mapema ya uchaguzi tofauti na chaguzi zilizopita tokea mwaka 1995.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments :

Post a Comment