Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita), Philip Saliboko (pichani), amefuata nyayo za Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), Andrew Chenge, baada naye kukimbilia Mahakama Kuu na hivyo kukwamisha usikilizaji wa malalamiko yaliyowasilishwa katika Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma dhidi yake.
Saliboko analalamikiwa na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma katika baraza hilo kupokea mgawo wa zaidi ya Sh. milioni 40.4 kutoka kwa mmiliki wa kampuni ya VIP Engineering and Marketing Limited, James Rugemalira, kinyume cha sheria ya maadili ya viongozi wa umma.
Fedha hizo, ambazo Saliboko anatuhumiwa kupokea, zinadaiwa kuwa sehemu ya zaidi ya Sh. bilioni 200 zilizochotwa kifisadi katika akaunti ya Tegeta Escrow, iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).Hatua ya ‘kukimbilia’ Mahakama Kuu, ilichukuliwa baada ya Jaji Hamisi Msumi, kutupilia mbali pingamizi la awali la kuzuia malalamiko hayo kusikilizwa na baraza, yaliyowasilishwa na Saliboko kupitia Wakili wake, Jamhuri Johnson jana.
Jamhuri aliwasilisha pingamizi hilo baada ya Wakili wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Hassan Mayunga, kuwasilisha malalamiko hayo dhidi ya Saliboko katika baraza hilo na kuzua malumbano ya kisheria yaliyodumu takriban dakika 30 kati ya mawakili wa pande mbili hizo pamoja na Jaji Msumi.
Katika pingamizi hilo, Jamhuri alidai baraza halina uwezo wa kusikiliza malalamiko dhidi ya mteja wake kwa madai kwamba, kuna amri ya zuio la Mahakama Kuu kwa chombo chochote cha umma kushughulikia suala lolote linalohusu kampuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) pamoja linalohusu akaunti ya Tegeta Escrow.
Hata hivyo, Jaji Msumi katika uamuzi wake, alitupilia mbali pingamizi hilo kwa maelezo kwamba, baraza halimo miongoni mwa walengwa wa amri ya zuio hilo la Mahakama Kuu na kwa hiyo, haliwahusu.
Pia alisema pingamizi hilo linatupwa kwa sababu kitakachofanywa na baraza katika usikilizaji wa malalamiko dhidi ya Saliboko, hakitasababisha ripoti ya CAG ya ukaguzi wa muamala uliofanywa katika akaunti ya Tegeta Escrow usijadiliwe na Bunge.
“Bado tunasimamia hayo. Kwa hiyo, tunakataa (pingamizi la Saliboko),” alisema Jaji Msumi. Wakili Jamhuri hakukubaliana na uamuzi huo Jaji Msumi, hivyo akaomba mteja wake aruhusiwe na baraza kwenda Mahakama Kuu kuomba marejeo ili kupata tafsiri sahihi juu ya amri ya zuio hilo.
Jaji Msumi alikubaliana na ombi hilo la Wakili Jamhuri na hivyo, akaamua kusitisha usikilizaji wa malalamiko dhidi ya Saliboko hadi ombi la marejeo ya amri ya zuio hilo la mlalamikiwa litakapotolewa maamuzi na Mahakama Kuu.
Hatua hiyo ya Saliboko imechukuliwa wiki moja baada ya Chenge kuamua kutimkia Mahakama Kuu kukwepa malalamiko dhidi yake kusikilizwa na baraza hilo baada ya kuibua hoja ya amri ya zuio hilo mahakamani.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment