Walisema hayo walipozungumza na NIPASHE kwa nyakati tofauti jana.
Jumamosi kamati Kuu (CC) ya CCM ilikutana na kutoa taarifa kwa vyombo vya habari baada ya kikao hicho cha siku moja kwamba uchunguzi dhidi ya makada hao waliopewa adhabu hiyo kuanzia Februari, 2014 unaendelea kwa muda usiojulikana.
WASIRA
Mmoja wa makada hao, ambaye ni Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira, alisema anachojua yeye ni kuwa kamati hiyo bado haijamaliza muda wa kuwachunguza. Alisema ana imani kuwa ikishamaliza kazi hiyo itatoa taarifa kwa vikao husika kama wametekeleza adhabu dhidi yao au la. “CC haijaongeza muda. Kilichopo ni kwamba, kamati ndogo ya maadili bado haijamaliza kazi ya kutuchunguza,” alisema Wasira.
SUMAYE
Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, alisema anasubiri kitakachoamuliwa na vikao vya chama kuhusu suala hilo.
MEMBE
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, alisema anachokijua yeye ni kuwa hayumo katika makada wa CCM walioongezewa muda wa kuchunguzwa kama wametekeleza adhabu ya kifungo cha miezi 12 au la. Membe alisema hayo jana alipotakiwa na NIPASHE katika viwanja vya Karimjee, jijini Dar es Salaam jana, kutoa maoni yake kuhusu suala hilo.
“Nani kakwambia kama nimo katika watu walioongezewa huo muda? Someni mambo katika mstari,” alisema Membe bila kufafanua.
MAKAMBA
Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, alisema hana taarifa za muda wa uchunguzi dhidi yao kuongezwa. “Habari ya kuongezewa muda ndiyo naisikia kwako,” alisema Makamba kwa kifupi.
LOWASSA
Waziri Mkuu mstaafu, ambaye ni Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, hakupatikana jana kuzungumzia suala hilo kutokana na kubanwa na shughuli za msiba wa aliyekuwa Mbunge Mbinga Magharibi (CCM), marehemu John Komba.
NGELEJA
Pia Mbunge wa Sengerema (CCM), William Ngeleja, hakupatikana na hata muda wote alipopigiwa simu yake ya mkononi ilikuwa imezimwa.
Makada hao, ambao mwanzoni mwa mwaka jana, waliitwa na kamati hiyo na kuhojiwa kutokana na tuhuma za kuanza kabla ya wakati kampeni za uchaguzi mkuu wa urais wa mwaka huu.
Februari 18, mwaka jana, walitiwa hatiani na hivyo kufungiwa kugombea nafasi za uongozi ndani ya chama kwa miezi 12, pia wakiwa chini ya uangalizi.
Kitendo cha kuanza kampeni za uchaguzi mkuu kabla ya wakati, kilidaiwa na Kamati Kuu ya CCM kuwa ni kinyume cha taratibu za chama hicho, hivyo kutoa onyo kali dhidi ya makada hao. Adhabu ya onyo kali kwa mujibu wa taratibu za CCM ilimaanisha kuwaweka chini ya uangalizi kwa miezi 12 ili kuhakikisha hawajihusishi na vitendo vyovyote vinavyokwenda kinyume cha misingi ya chama hicho, vinginevyo hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.
Muda wa adhabu hiyo uliisha Februari 18, mwaka huu.
Uamuzi huo unawazuia makada hao kujitokeza rasmi kutangaza nia ya kuwania urais kwa tiketi ya chama hicho tawala.
Kutokana na hali hiyo, makada hao sasa watalazimika kusubiri hadi hapo kamati hiyo itakapomaliza uchunguzi wake, ikiwa imebaki miezi isiyopungua mitatu kabla ya wanachama kuanza harakati za kuwania nafasi mbalimbali.
Katibu wa Halmashauri Kuu (Nec), Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, alikaririwa akisema baada ya kumalizika kwa kikao cha CC kuwa kwa kuzingatia kanuni za maadili ya CCM, mwanachama aliyepewa onyo kali atakaa chini ya uangalizi kwa kipindi kisichopungua miezi 12.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment