Wakiri alikuwa nguzo kampeni urais , JK kuongoza maelfu kuaga mwili leo
Makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanaotajwa katika harakati za kuwania nafasi ya urais kwenye uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba mwaka huu, wameelezea masikitiko yao juu ya kifo cha Mbunge wa Mbinga, John Komba na kueleza namna marehemu alivyokuwa amejiandaa kuwatungia nyimbo za kampeni.
Makada hao ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa na Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja.
Makada hao waliwasili nyumbani kwa marehemu Mbezi Beach, jijini Dar es Salaam jana kuanzia majira ya saa 4:00 asubuhi kwa nyakati tofauti na walipohojiwa na vyombo vya habari hawakusita kumwelezea Komba na maandalizi ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
MEMBE
Kwa upande wake, Membe ambaye pia ni Mbunge Mtama, alisema Komba, mauti yamemkuta kipindi ambacho chama na taifa linamuhitaji.Alisema chanzo kikubwa cha ushindi wa CCM katika chaguzi mbalimbali zilizowahi kufanyika nchini ni kutokana na utunzi mzuri na uimbaji wa Komba.
“Komba, chama kinamuhitaji sana wakati huu, tumepoteza kiongozi aliyekuwa akikiletea chama ushindi mkubwa kipindi chote cha chaguzi mbalimbali wakati wa kipindi chote cha uhai wake,” alisema Membe.
Aidha, alisema Komba alikuwa kiunganishi kikubwa katika mgogoro wa Ziwa Nyasa kati ya Tanzania na nchi ya Malawi.
“Komba alikuwa kiunganishi kwetu alishirikiana na watu wa Mbinga na wakazi wa maeneo ya kule kutuunganisha sisi ili kuondoa tofauti zetu dhidi ya jirani zetu Malawi,” alisema Membe.
MWIGULU
Naye, Nchemba ambaye pia ni Mbunge wa Singida Magharibi, alisema Komba alikuwa ni nembo ya CCM na ndiye aliyemwezesha kushinda katika uchaguzi uliopita wa mwaka 2010 kwenye jimbo lake kutokana na nyimbo zake.
“Komba ni nembo ya CCM, ukiacha nyundo na jembe, alikuwa balozi mzuri wa kutambulisha chama na hata kwenye kampeni za uchaguzi kwenye jimbo langu nilitumia nyimbo zake na hata hapa nilishamtania nikamwambia aniangalizie kama jina langu linaimbika, alifurahi akaniambia linaimbika na kashaanza kuliimba…(kicheko)” alisema Mwigulu.
Alisema, mara ya mwisho alizungumza naye Jumapili ya wiki iliyopita akimweleza masuala ya jimbo lake na kwamba, moja ya mambo anayomsifu ni ujasiri wake wa kusema ukweli na kutomuogopa yeyote.
LOWASSA
Kwa upande wake, Mbunge wa Monduli, ambaye aliwasili nyumbani hapo huku akiwa mwenye huzuni, alisema chama kinapita kwenye wakati mgumu wa kupoteza kiongozi shupavu.
“Taifa tuko kwenye wakati mgumu kumpoteza kiongozi na kada muhimu wa chama,” alisema Lowassa.
NGELEJA
Naye Ngeleja ambaye pia ni Mbunge wa Sengerema, alisema chama kimekosa fursa na uzalendo wa Komba.
Alisema alikuwa ni kiongozi mzalendo asiyekuwa na wasiwasi, mpenda nchi aliyejitoa wakati wa kipindi chote cha uhai wake kwa kutumikia chama.
“Komba aliishi kama mtumishi, alikuwa fundisho kwa chama, mwelimishaji asiyemuogopa yeyote na asiyevumilia maovu. Asilimia 75 ya Watanzania tunaishi tukiwa na vinyongo lakini Komba hakuwa anakaa na kitu moyoni,” alisema Ngeleja.
SPIKA ANENA
Mbali na makada hao, wengine waliomzungumzia marehemu Komba ni, Spika wa Bunge, Anne, Makinda, ambaye alisema kazi aliyoifanya mbunge huyo ni njema kwa taifa lake na kwamba Mungu ameamua kumchukua.
“Kama Bunge tumepoteza kiungo muhimu ni sawa na mwili wa binadamu ukate kidole kimoja, maumivu ni makali, hivyo kwetu sisi tumekutwa na maumivu hayo, lililoko mbele yetu ni kufanya kazi nzuri kwa kipindi hiki ili sasa na sisi tuvikwe taji kama Komba alivyo vikwa taji baada ya kufariki,” alisema Makinda.
DK. MIGIRO
Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Asha-Rose Migiro, alisema Komba alikuwa mtumishi bora wa taifa na kwamba ameweza kuwaunganisha Watanzania kwa matukio mawili makuu, likiwamo la kifo cha Mwalimu Nyerere na kifo chake (Komba).
“Komba kwa mara ya pili analiunganisha taifa pamoja baada ya kutuunganisha wakati wa msiba wa taifa wa Mwalimu Nyerere. Ni kweli katuachia pengo kubwa ila tunapaswa kumshukuru Mungu kwa kila jambo.”
Viongozi hao, walitoa masikitiko yao jana walipokuwa wakiwasili kutoa salamu za pole kwa familia ya marehemu Komba.
Miongoni mwa viongozi wengine wa serikali na makada wa CCM waliowasili msibani hapo ni, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mitaa (Tamisemi), Hawa Ghasia na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), Jenista Muhagama.
CCM YANENA
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, alisema chama kimeondokewa na mtu muhimu ambaye alishaanza kazi ya kurekodi nyimbo mbalimbali kwa ajili ya maandalizi ya uchaguzi.
“Kinachosikitisha zaidi jana (juzi) asubuhi niliongea na marehemu kuzungumza masuala ya chama na akaniamba Jumatatu tungeonana kwa ajili ya kuongea zaidi,” alisema Nape.
Alisema taarifa za kifo hicho zimewafikia wakati wako kwenye mchakato wa maandalizi ya kuanza kuboresha nyimbo yake ya mwisho aliyoiimba kwenye kilele za miaka 38 ya CCM mjini Songea mwezi uliopita ya ‘CCM mbele kwa mbele’.
Alisema kutokana na kifo chake, Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, ameahirisha ziara yake iliyokua ianze leo mkoani Dodoma, hivyo itaanza keshokutwa Jumatano.
JK KUONGOZA KUAGA MWILI LEO
Rais Jakaya Kikwete, anatarajiwa kuongoza viongozi wa serikali, makada wa CCM na wananchi kwa ujumla kuuaga mwili wa marehemu Komba.
Ratiba ya mazishi inaratibiwa na makundi manne, ambayo ni CCM, Jeshi la Wananchi Watanzania (JWTZ) ambako marehemu alifanyia kazi awali, familia na Bunge.
Kwa mujibu wa msemaji wa familia ambaye pia ni shemeji wa marehemu Komba, Dominick Mwakenja, alisema mwili wa marehemu ulilala nyumbani kwake kabla ya kuagwa leo kwenye viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam.
Alisema mwili wake utasafirishwa kwa ndege leo kuelekea mkoani Songea na majira ya sasa 9:00 alasiri utaagwa kwenye viwanja vya Majimaji mjini Songea, kabla ya kuelekea kijijini kwake Lituhi kwa maziko kesho.
Nyumbani kwa marehemu wageni mbalimbali waliwasili kuhani msiba huo, kwa kujiorodhesha kwenye kitabu cha rambirambi na kutoa salamu za pole kwa familia kabla ya kutoa heshima za mwisho kwa familia na mwili huo kulala nyumbani hapo.
APPT WAMLILIA
Chama cha APPT Maendeleo kimeeleza kupokea kwa maskitiko kifo cha Komba kikieleza kuwa CCM imepoteza mwanachama na mbunge muhimu.
Katibu Mwenezi wa chama hicho Taifa, Godfrey Davis, katika taarifa yake kwa vyombo vya habari alimwelezea Komba kama mbunge muhimu ambaye alikuwa kiunganishi kizuri kati ya wananchi na chama hicho.
Davis alisema marehemu Komba atakumbukwa daima kwa jinsi alivyokuwa mstari wa mbele katika kupigania maendeleo ya wananchi wa jimbo lake na kuwaunganisha Watanzania wakati wa kifo cha Hayati Mwalimu Julius Nyerere.
“CCM wamepoteza mtu muhimu sana, tunatuma salamu za rambirambi kwa Mwenyekiti wa CCM Taifa, Jakaya Kikwete, Spika wa Bunge, Anne Makinda, familia, ndugu na jamaa,” alisema.
Davis alisema APPT Maendeleo itaungana na Watanzania wote katika kipindi hiki cha majonzi.
SONGEA WAOMBOLEZA
Mamia ya wakazi wa Manispaa ya Songea, mkoani Ruvuma, wanatarajia kuupokea mwili wa marehemu Komba leo jioni.
Habari zilizopatikana mjini Songea ambazo zimezibitishwa na Katibu wa CCM Mkoa wa Ruvuma, Velena Shumbusho, zimesema kuwa mwili wa marehemu utawasili majira ya saa 10:00 joini kwenye uwanja wa ndege wa Songea Mjini, ambako wananchi wataupokea na baadaye utapelekwa uwanja wa Majimaji ambako wakazi wa Songea watauwaga.
Shumbusho alisema kifo cha mbunge huyo ni tukio la kushtua kwani alikuwa ni mtu mwenye uwezo mkubwa wa kufikisha ujumbe kwa wananchi kwa kupitia kipaji chake cha uimbaji kwenye kwaya yake ya TOT.
Alisema baada ya kuuaga mwili, marehemu atasafirishwa hadi kijijini kwake Lituhi, wilayani Nyasa ambako ndiko atazikwa.
Naye Katibu wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoani Ruvuma (RPC), Endru Chatwanga, alisema kuwa taarifa ya kifo cha Komba imewashtua waandishi kwa kuwa marehemu alikuwa ni mdau mkubwa wa wanahabari kwani kila alipokuwa anakwenda jimboni kwake alikuwa anaongozana na baadhi ya waandishi wa habari ambao walikuwa wakiripoti taarifa mbalimbali za maendeleo kwenye Jimbo la Mbinga Magharibi.
Mwenyekiti wa Ruvuma Ophans Association (Roa), Methew Ngalimanayo, alisema kuwa marehemu katika uhai wake alikuwa ni mtu wa watu na ndiyo maana wananchi wa Mbinga Magharibi walimchagua kuwa Mbunge wao na kazi kubwa ameifanya kama mwakilishi wao katika kuhakikisha kuwa huduma za jamii zinapatikana zikiwamo barabara, shule za msingi, sekondari, zahanati na vituo vya afya.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment