WAZIRI wa zamani na Mkuu
wa Usalama wa Taifa mstaafu, Dk. Hassy Kitine, amewataka Watanzania kutoacha
kupokea fedha wanazohongwa na baadhi ya watu wanaosaka urais, kwa sababu
zimeibwa kutoka kwao.
Katika mahojiano maalumu
aliyoyafanya na Raia Mwema jijini Dar es Salaam wiki hii, Kitine alisema
wananchi wanatakiwa kuzichukua fedha hizo lakini wachague viongozi wanaojua
watawafaa pasipo kujali walichukua fedha za mafisadi.
“Kuna wagombea watawapa
pesa. Kuleni hizo pesa. Msikatae. Pesa ni pesa. Aliyekuwa anazikataa labda Baba
wa Taifa tu (Mwalimu Julius Nyerere).
“Kuleni, lakini kura yako
ya kumchagua kiongozi wa kukuongoza haina thamani sawa na hizo pesa. Kura yako
ni zaidi ya mamilioni ya fedha. Kura yako isilinganishwe na pesa.
“Hawa wagombea (baadhi)
wanazo pesa ambazo ni za wizi. Wametuibia hapa. Wanayo mapesa mengi, kuleni
pesa zao, lakini kura yako ni zaidi ya thamani ya pesa hizo.
“Pili, fika kwenye
Mkutano Mkuu (CCM) halafu kituo cha kura baadaye mpigie mtu unayemuona ni mtu
safi. Na usafi huo unatokana na uwezo wa kukataa rushwa.
“Kwa upande wangu nasema
mimi sijajaza fomu. Lakini kama nisingekuwa mwadilifu, ningetaka kuwa na mapesa
mengi, ningekuwa na mapesa hayo, mengi kuliko wote hawa wanaotaka urais.
“Ningekuwa nachota kule
Usalama wa Taifa wakati niko mkubwa na kisha leo ningetoa rushwa. Lakini siwezi
kuchanganya pesa na uongozi wa nchi,” alisema Kitine katika mahojiano ambayo
yamechapwa ndani ya gazeti hili.
Katika mahojiano hayo
ambayo Kitine ameongea kwa kirefu kuhusu historia ya maisha yake ya utumishi,
alisema kama Watanzania watamuona anafaa kuwa Rais, yeye yuko tayari
kuwatumikia.
Alisema anajua ana
ufahamu mkubwa kuhusu Tanzania na watu wake pengine kuliko mwanasiasa yeyote
ambaye ametajwa kutaka kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
“Kama Watanzania wanaona
naweza sitaogopa. Lakini mimi sina pesa. Uongozi wa sasa ni pesa. Lakini naweza
kuwa rais bora zaidi. Nitakuwa rais bora zaidi kama nikipewa nafasi.
“Katika watu
waliojitokeza kutaka urais hakuna hata mmoja anayeifahamu hii nchi kuliko mimi.
Naijua nchi hii, pia ni msomi niliyebobea nina digrii nne.
“Mimi ni mchumi. Naujua
uchumi wa nchi. Najua usalama. Hakuna hata mmoja anayejua usalama kama mimi.
“Hakuna mtu anayejua matatizo ya ulinzi kama mimi. Hakuna mtu anayejua usalama
wa nchi kama mimi.
“Hatutaki mambo kama ya
Tanga (ugaidi) lazima kuwe na wa kukemea. Simtishi mtu, nazungumza habari ya
nchi. Sina cha kulipiza kisasi,” alisema.
Katika mahojiano hayo ya
kusisimua, Kitine alieleza namna uamuzi wake wa kuagiza gari kutoka nje ya nchi
ulivyomletea matatizo mbele ya Nyerere.
No comments :
Post a Comment