Kwarara Msikitini

airbnb

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Sunday, March 1, 2015

POLEPOLE: Mambo 70 muhimu ya wananchi yaliyofutwa katika Katiba Inayopendekezwa-2

Image result for katiba

Wiki iliyopita tulianza kukuletea mambo 70 muhimu ya wananchi yaliyofutwa katika Katiba Inayopendekezwa. Mambo haya yalikuwa kwenye rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba ambayo Mwenyekiti wake alikuwa Jaji Joseph Warioba. Leo tunaendelea na maeneo mengine 20.
20. Misingi ya utendaji wa Jeshi la Polisi
Rasimu ya Warioba ilipendekeza kwamba katika utekelezaji wa majukumu yake, Jeshi la Polisi la Jamhuri ya Muungano litazingatia (a) Viwango vya juu vya kitaaluma na nidhamu miongoni mwa wafanyakazi wake; (b) Ulinzi na ukuzaji wa haki za binadamu; (c) Kanuni za uwazi na uwajibikaji; na (d) Kukuza uhusiano na jamii. Warioba akaendelea kusema, Jeshi la Polisi, katika kutekeleza majukumu yake, litashirikiana na vyombo vinavyohusika na kupambana na uhalifu vya nchi washirika katika kufanya uchunguzi na kushughulikia makosa ya rushwa na ufisadi.
Misingi hii yote imefutwa na Katiba Inayopendekezwa.
21. Kuhusu Wabunge wa Kuteuliwa
Wananchi walipendekeza Rais asiwe na mamlaka ya kuteuwa wabunge na baadhi ya sababu zao ni Kutekeleza kikamilifu dhana ya mgawanyo wa madaraka. Kuwa na wabunge wanaotokana moja kwa moja na ridhaa ya wananchi kupitia kura zao na kuwa na wabunge walio huru katika kutekeleza majukumu yao. Rasimu ya Warioba ilipendekeza katika Ibara ya 113(2)(b) kumpa Rais nafasi ya kuteua wabunge watano wanaowakilisha watu wenye ulemavu na ikumbukwe kwamba wabunge hawa watano wanachaguliwa na watu wenye ulemavu wenyewe na Rais anafanya kazi ya kuwateua, hii ni tofauti na Rais kuwateua yeye mwenyewe. Ukisoma kifungu cha 45(2) utaona utaratibu wa kisheria unawekwa kuhakikisha watu wenye ulemavu wanashiriki katika nafasi za uwakilishi.
Katiba Inayopendekezwa katika Ibara ya 129(2)(c) inampa Rais uhuru wa kuchagua wabunge wasiozidi kumi kutoka watu wenye sifa ya kuwa wabunge. Pendekezo hili ni kinyume na maoni ya watumishi wa Ofisi ya Rais Tume ya Utumishi wa Umma na kukiuka msingi wa wabunge kuwa wawakilishi wa wananchi moja kwa moja.
22. Kuhusu sifa ya kielimu kwa mbunge
Rasimu ya Warioba ilipendekeza sifa mojawapo ya kuwa mbunge ni kuwa na elimu isiyopungua kidato cha nne na ajue kusoma na kuandika lugha ya Kiswahili au Kiingereza. Baadhi ya sababu za kuunga mkono pendekezo hili ni pamoja na maendeleo ya sayansi na teknolojia pamoja na changamoto zilizoko katika sekta za uchumi, elimu na utandawazi ipo haja ya mbunge kuwa na elimu ya kutosha kuweza kukabiliana na changamoto zinazosababishwa na mabadiliko haya.
Katiba Inayopendekezwa inapendekeza sifa mojawapo ya kuwa mbunge ni kujua na kusoma lugha ya Kiswahili au Kiingereza. Pendekezo hili liko mbali kabisa na chini ya kiwango cha maoni ya watumishi wa Ofisi ya Rais Tume ya Utumishi wa Umma.
23.Nafasi za Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu Kikatiba
Rasimu ya Warioba ilipendekeza kuwako na nafasi kikatiba za Makatibu Wakuu watakaoteuliwa na Rais kutoka miongoni mwa watumishi waandamizi katika utumishi wa umma kama watakavyopendekezwa na Tume ya Utumishi wa Umma.  Kila Katibu Mkuu atakuwa kiongozi na Mtendaji Mkuu wa Wizara ya Serikali aliyopangiwa na Rais na atashika nafasi ya madaraka ya Katibu Mkuu na kutekeleza majukumu yake kama itakavyoainishwa katika sheria za nchi.
Rais anaweza, kwa mapendekezo ya Tume ya Utumishi wa Umma, kumteua mtumishi mwandamizi katika Utumishi wa Umma kuwa Naibu Katibu Mkuu.  Kila Katibu Mkuu atakuwa mshauri wa mwisho kwa Waziri kwa masuala yote ya utendaji na atatoa ushauri kwa Baraza la Mawaziri katika vikao na Kamati zitakazoitishwa na Katibu wa Baraza la Mawaziri. Katibu Mkuu au Naibu Katibu Mkuu hatashika madaraka yake hadi awe ameapa mbele ya Rais kiapo cha utii na uaminifu au kiapo kingine chochote kinachohusu utendaji wa kazi zake kitakachowekwa kwa mujibu wa sheria za nchi.
24. Kamati Maalumu ya Makatibu Wakuu
Rasimu ya Warioba ilipendekeza kuwapo kikatiba kwa Kamati Maalum ya Makatibu Wakuu itakayoongozwa na Katibu Mkuu Kiongozi ambayo itakuwa na majukumu ya kuchambua na kulishauri Baraza la Mawaziri juu ya masuala mbalimbali kabla ya kuwasilishwa na kufanyiwa uamuzi na Baraza hilo na itatekeleza majukumu mengine kama itakavyopangiwa na Baraza la Mawaziri.
Katiba Inayopendekezwa imefanikiwa kufuta msharti hayo yote mahususi licha ya kwamba huu ulikuwa wakati muafaka wa kuiimarisha sekta ya utumishi wa umma kikatiba ili iendelee kutuhudumia wananchi ikiwa na ari, kujiamini na kutenda kwa weledi pasina ya kuvurugwa na mara kadhaa na wanasiasa wabaya.
25. Malengo mahususi ya kiuchumi
Masharti yafuatayo katika malengo mahususi la kiuchumi yamefutwa na Katiba Inayopendekezwa;-kuwaletea wananchi maisha bora kwa kuondoa umaskini
kuweka mazingira bora kwa ajili ya kuanzisha na kuendeleza vyombo vya uwakilishi wa wakulima, wafugaji na wavuvi kuhakikisha kuwa kila mtu mwenye uwezo wa kufanya kazi anapata fursa ya kufanya kazi, kwa maana ya kufanya shughuli yoyote halaliinayompatia kipato kuweka utaratibu wa usimamizi wa kiuchumi nauandaaji wa mipango, kuwezesha malengo ya muda mfupi, muda wa kati na muda mrefu kutekelezwa.
26. Haki ya kutokuwa mtumwa
Katiba Inayopendekezwa imefuta masharti yaliyokuwa yanapiga marufuku mtu kulazimishwa kufanya kazi bila hiari yake, hii ni kinyume na sheria na mikataba ya kimataifa ambayo Tanzania imeiridhia.
27. Uhuru wa habari na vyombo vya habari
Katiba Inayopendekezwa imeweka masharti “pokonyezi” (claw-back clauses) kwenye ibara ya Uhuru wa Habari na Vyombo vya Habari. Rasimu ya Warioba inatoa wajibu kusambaza habari na taarifa kwa wananchi. Katiba Inayopendekezwa inatoa wajibu wa kusambaza habari na taarifa sahihi na za ukweli kwa wananchi.
Kuweka maneno taarifa sahihi na za ukweli ni kuminya haki hii, Katiba inapasa kuweka msingi na sheria ingetoa ufafanuzi. Kuweka hapa kutapelekea kutumika kifungu hiki ndivyo sivyo. kuzingatia miiko ya taaluma ya uandishi na utangazaji wa habari ni suala la sheria na kanuni, na ikumbukwe ulimwengu wa leo hautegemei pekee wanataaluma wa habari kutoa habari, kifungu hiki kitaminya haki hii. Kwa kuweka maneno haya katika masharti ya ibara hii, Uhuru wa Habari na Vyombo vya Habari uko mashakani kabisa.
28. Haki ya Elimu na Kujifunza
Wananchi walipendekeza kutolewa kwa elimu bora ya msingi bure na bila vikwazo ikiwemo kupata elimu bora inayotolewa nje ya utaratibu wa umma kwa gharama nafuu.
Masharti yafuatayo yamefutwa na Katiba Inayopendekezwa:-
Kila mtu ana haki ya: kupata fursa ya kupata elimu bora bila ya vikwazo;
kupata elimu bora ya msingi bila ya malipo na inayomtayarisha kikamilifu mwanafunzi ama kuendelea naelimu ya ngazi inayofuatia au kuweka msingi wa kuanzakujitegemea; kupata elimu bora inayotolewa nje ya utaratibu wa umma kwa gharama nafuu.
29. Haki ya Mtoto
Wananchi walipendekeza kutolewa ulinzi zaidi kwa haki za mtoto na Rasimu ya Katiba Mpya Toleo la Pili iliweka masharti yaliyoelekeza mamlaka ya nchi kuweka utaratibu wa Kisheria utakaowezesha utekelezaji na usimamizi wa haki za mtoto kwa kufuata msingi wa kutoakipaumbele kwa maslahi na manufaa ya mtoto. Masharti haya yamefutwa na Katiba Inayopendekezwa na kufanya haki zilizowekwa katika Ibara hii kuwa kiini macho.
30.Haki za watu wenye Ulemavu
Wananchi na hasa watu wenye ulemavu walipendekeza mamlaka ya nchi kuweka utaratibu wa sheria utakaowezesha watu wenye ulemavu kushiriki kwenye nafasi za uwakilishi.
Katiba inayopendekezwa imeondoa jukumu hili na tafsiri yake ni kwamba wawakilishi wa watu wenye ulemavu wataendelea kuteuliwa pasina ya kuwa na msingi wa kikatiba na kisheria kuhakikisha watu wenye ulemavu wanawachagua wawakilishi wao tofauti na sasa.
31. Haki za wanawake
Wananchi waliotoa maoni hasa wanawake na wanaume walipendekeza kwa sauti moja kuona haki za wanawake zinalindwa, zinahifadhiwa, zinatolewa na kutekelezwa kwa wakati na mamlaka za nchi. Wananchi walipendekeza kuona wanawake wanalindwa dhidi ya unyonyaji na ukatili. Katiba Inayopendekezwa siyo tu imefuta kifungu kinachomlinda mwanamke dhidi ya unyonyaji bali pia imefuta masharti elekezi yaliyokuwamo katika Rasimu ya Warioba ambayo yalikuwa yanazielekeza Mamlaka za nchi kuweka utaratibu wa kisheria utakaosimamia masuala yanayohusu utekelezaji wa masharti ya Ibara hii ikiwa ni pamoja na kukuza utu, heshima, usalama na fursa za wanawakewakiwemo wajane.
 32. Haki za wazee
Katiba Inayopendekezwa imefuta masharti yaliyokuwa yanaelekeza “kutambua utu wa wazee na kuheshimiwa kwao pasipo kudharauliwa”.
33. Wajibu wa Raia
Katiba Inayopendekezwa imefuta masharti yaliyokuwemo katika Rasimu ya Warioba juu ya mamlaka ya Bunge kutunga sheria kwa ajili ya kuwawezesha raia kutekeleza masharti ya ibara hii. Kufuta masharti hayo ni kuacha Katiba bila utaratibu mzuri wa kuhakikisha raia wanawajibika kwa taifa letu.
34. Hifadhi ya Haki za binadamu
Katiba Inayopendekezwa imefuta haki na uhuru ambao umeainishwa katika mikataba ya kikanda na ya kimataifa kuhusu haki za binadamu ambazo Jamhuri ya Muungano imeridhia. Huu ni mfano mbaya kabisa hasa kwa Taifa linaloheshimu haki za binadamu kama zilivyoainishwa katika mikataba ya kikanda na kimataifa ambayo Tanzania imeridhia.

No comments :

Post a Comment