Kwarara Msikitini

airbnb

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Saturday, April 18, 2015

Chanzo cha kuyumba kwa Taifa letu

Image result for julius nyerere
KONGAMANO la Mwalimu Nyerere lililoitishwa na Taasisi ya Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam tarehe 30 Novemba hadi tarehe 2 Desemba, 2009 liliitishwa wakati huo kama sehemu ya maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 10 ya kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Kwenye kongamano hilo liliofanyika katika Ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam, pamoja na mambo mengine, kongamano lilijadili juu ya hali halisi ya taifa letu pamoja na chanzo cha CCM kupoteza dira na kuyumba kwa Taifa letu.
Kwa miaka mingi taifa letu limekuwa likiongozwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM). Matatizo yaliyokikumba chama hiki kwa kiasi kikubwa ndiyo chanzo cha kuyumba na kulifikisha taifa letu hapa lilipo.
Kupitia mjadala wa kongamano la Taasisi ya Mwalimu Nyerere (MNF) ilibainika kuwa kiini cha matatizo yanayoikumba CCM leo ni uasi wa wana-CCM wachache waliokuwa wameamua kutumia Umoja wa Vijana ya chama hicho (UV-CCM) kama chama ndani ya CCM kujitafutia umaarufu na nafasi za uongozi.

Hawa walikuwa na uchu wa madaraka na hawakukubaliana na itikadi ya chama chao ya kutotaka viongozi kujilimbikizia mali. Pia hawakuridhika na mfumo wa CCM wa kuchagua viongozi wake. Waliutaja mfumo huo kama “mizengwe”. Kwa hiyo, waliamua kuondokana na yote hayo.
Mtakumbuka mwaka 1995, wakati wa uchaguzi vijana wa CCM, walikuwa na ilani yao ya uchaguzi, sambamba na ile ya CCM. Ilani ya vijana ndiyo ilikuwa mwanzo wa nguvu na kauli za vijana wa CCM ya leo. UVCCM leo imekuwa kama chama. Wote tumeshuhudia kwa nyakati tofauti namna inavyokemea CCM na kutoa vitisho kwa uongozi wa chama wa ngazi zote.
UVCCM siyo jumuiya tena isipokuwa ni chama kilicho ndani ya chama. Kundi ndani ya CCM linaloshabikia rushwa na ufisadi limetokana na jumuiya hiyo baada ya wana-CCM wenye uchu wa madaraka kuwatumia.
Mtakumbuka pia kuwa mwaka 1995, kundi hili la vijana lilimtaka Edward Lowassa ateuliwe kugombea urais wa Tanzania. Hata hivyo, ilitolewa kauli kuwa Lowassa alikuwa na tuhuma za rushwa, kujilimbikizia mali na kupungukiwa na maadili, kinyume na Katiba ya CCM na kanuni za chama hicho.
Kamati Kuu ilipopeleka mapendekezo ya kutompendekeza kugombea urais. Lowassa alitetewa kwa makelele, kihuni, bila kufuata taratibu za kikao cha NEC Dodoma. Kundi moja lilikuwa limejiandaa kumpitisha kwa hoja ya nguvu na si kwa nguvu ya hoja.
Waliyatetea maelezo ya Kamati Kuu, lakini waliyakataa yale ya nyongeza aliyoyatoa Mwenyekiti Ali Hassan Mwinyi (Rais wa wakati huo) ambaye alielezea tuhuma hizo zilizokuwa zinamkabili Lowassa. Hivyo. Naomba kusisitiza kwamba Lowassa hakuwa chaguo la CCM katika uchaguzi wa mwaka 1995.
Katika kikao hicho cha Kamati Kuu, Mwalimu Nyerere aliamua kusaidia kikao kwa kutoa maelezo ya nyongeza. Aliwauliza wajumbe wa NEC maswali, kwamba wao ni wahuni au ni viongozi wa CCM? Ikiwa wao ni viongozi wa CCM, je, hivyo ndivyo wanavyopaswa kumtafuta mgombea wa urais, kwa makelele?
Kama Watanzania wangewaona walivyokuwa wanafanya katika kikao hicho, je, wangeamini kuwa wao ni viongozi kweli? (Wajumbe walibaki kimya). Kisha Mwalimu aliendelea kusisitiza maelezo aliyoyatoa Mwenyekiti Ali Hassan Mwinyi akisema:
“Mwinyi amemstahi sana Lowassa. Hakuwaambia wajumbe wa NEC baadhi ya tuhuma mbaya kabisa kuhusu Lowasa. Ikiwa NEC inachoombwa ni kuchagua kati ya wenye tuhuma za rushwa kuchaguliwa kwa nafasi ya urais, na wale wasioitaka, basi huu ni wakati muafaka kwao kuipeleka hoja hiyo mbele ya Watanzania waiamue kwa kuwa ndani ya NEC hakuna mwenye uwezo wa kumfukuza mwenzie, wote ni wajumbe sawa kwa mujibu wa Katiba ya CCM.”
Hatimaye kikao cha NEC kiliondoa jina la Lowassa, kikawateua Benjamin William Mkapa, Cleopa David Msuya na Jakaya Mrisho Kikwete kuwa wagombea. Majina yao yaliwasilishwa kwenye Mkutano Mkuu ambao ndio uliopaswa kumchagua miongoni mwa mgombea urais wa CCM.
Kwenye Mkutano Mkuu wa CCM, wagombea hao watatu walijinadi kwa wajumbe. Kikwete alipokuwa akijinadi aliwaeleza wajumbe kwamba endapo wangempitisha kugombea na akashinda, angemteua Lowassa kuwa Waziri Mkuu wake. Lakini hapa pia tujiulize, pamoja na maelezo ya Mwalimu Nyerere na Kamati Kuu kuondoa jina la Lowassa kwa nini bado Kikwete alidiriki kumtaka Lowassa awe Waziri wake Mkuu?
Hapa kwa akili za kawaida inaonekana dhahiri kuwa Kikwete alimhitaji Lowassa na si vinginevyo. Hata hivyo Kikwete hakuchaguliwa kuwa mgombea urais. Kama alivyokuja kusema mwenyewe, kura zake katika mkutano huo “hazikutosha”.
Kutokana na ushawishi wa Mwalimu Nyerere, Mkapa ndiye aliyeteuliwa kuwa mgombea urais wa CCM na mkutano ule. Historia hii inatoa mfano hai wa jinsi matatizo yanayolikumba taifa letu yalivyoanza. Ni dhahiri kabisa kuwa watu walewale, wakiongozwa na tamaa zilezile za kuwa matajiri na kutaka urais kwa gharama yoyote hata kuhonga au kutumia fedha, ndio wanaolisumbua Taifa letu mpaka sasa.
Hivyo, kasi ya kuanguka kisiasa kwa CCM ilianza katika uchaguzi wa 1995 wakati wa kutafuta mgombea urais wa awamu ya tatu ndani ya CCM. Makundi makubwa yaliyoibuka mwaka ule na kuzaliwa kwa kundi maarufu la “wanamtandao” kutoka ngazi za juu hadi ngazi za kata, ndiyo yaliyoanza kuudhoofisha umoja na mshikamano wa wana-CCM. Dhambi ya ubaguzi, udini, ukabila na ukanda ilianza kuitafuna CCM.
Sehemu ya barua aliyoandika Mkurugenzi wa MNF, Joseph Butiku, kwa Rais Mkapa mwezi Agosti mwaka 2005 ni sehemu ya ushahidi uliopo unaofafanua kwa kirefu na kwa uwazi chanzo cha CCM kupoteza dira.
Mzee Butiku ni mwanachama wa CCM mpaka sasa. Barua hii, mbali na CCM pia inaeleza chanzo cha matatizo yanayolikabili taifa letu. Barua yenyewe ni hii ifuatayo:
“Mheshimiwa Rais Benjamin William Mkapa,
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM),
S.L.P 9151,
DAR ES SALAAM.
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Kwa heshima na unyenyekevu mkubwa nakuomba uvumilie na uisome barua hii kuanzia mwanzo hadi mwisho. Ni barua yangu kwako kama Mwenyekiti wa chama chetu, nami naileta kwako nikiwa Mwana-CCM mwaminifu wa chama changu – CCM – na viongozi wake wote.
Lakini pia nimeandika barua hii kwa kuzingatia haja ya kukidhi ahadi moja ya CCM isemayo: “Nitasema kweli daima, fitina kwangu mwiko.”
Hii siyo barua ya tuhuma, wala dharau au kiburi. Nimeandika kwa imani kubwa niliyo nayo kwako na kwa chama chetu na misingi yake iliyotudumishia Amani na Umoja. Nimeandika kwa sababu zifuatazo:
CCM imeanza kushindwa kusema na kutetea Haki na Ukweli. Imeanza kuvumilia na kutetea ubaguzi: Imeanza kuwa CCM ya viongozi wafanyabiashara wanaoonyesha nia ya kutaka kubinafsisha CCM, na wasioonyesha nia thabiti ya kujali maadili ya chama chetu na ya Taifa letu; si viongozi wa wanyonge tena.
CCM inaanza kushindwa kutofautisha kati ya wema na uovu; kati ya mwenendo unaoweza kuvunja Utaifa wetu, na ule unaoweza kudumisha Amani na Umoja wa Taifa na raia zake na kati ya rafiki na adui.
Sasa CCM imeanza kuachana na siri kuu ya uhai wake – kuheshimu watu na kuwa na mazungumzo ya waziwazi ndani na nje ya vikao, juu ya jinsi ya kuendesha na kusimamia mambo ya Watanzania.
Badala ya uongozi wa CCM kuheshimu wanyonge na kutetea haki za wote, pamoja na wanyonge, chama kimeanza kujenga tabaka la viongozi wenye mali au wanaowekwa katika nafasi za uongozi na wenye mali au kwa kutumia mali zao wao wenyewe ili wapate nafasi za kufanya mambo yao.
Mali imeanza kuchukua nafasi ya uzalendo na kutumiwa na viongozi wengi wa CCM kama nyenzo ya uongozi bora wa kisasa. CCM imeanza hata kutoona haya, na viongozi wakuu, chini ya uongozi wako sasa wamenyamaza, wanaona haya kukemea uovu!
Katiba na kiapo cha Rais cha utii kwa katiba hiyo ndiyo mwiko mkuu wa msingi wa utendaji wa Mwenyekiti/Rais na viongozi wakuu wanaomsaidia. Hata wale wasiokula viapo wanalazimika kutambua kwamba mkubwa wao – Mwenyekiti na Rais wa Jamhuri – amekula kiapo cha utii, uaminifu, ujasiri, kutopendelea na kukataa woga.
Mwiko huu ukivunjwa, Taifa litakosa msingi imara wa kulisimamisha na kulihimili.Mwiko huu ukivunjwa unaondoa uhalali wa maamuzi. Vyombo vyote vinaweza kubabaika; visiweze kuelewa kama viapo vyao vina maana yoyote, na labda vikadhani kazi zake ni kutetea ubaya: maana vikifanya kazi nzuri, matokeo yake yakikataliwa au kupuuzwa vinaweza visielewe.
Maana ikiwa kweli kazi ya vyombo hivyo vya maadili inaweza ikaonekana haifai, haitoshelezi au haisaidii lolote, huku vyombo vyenyewe vinaamini vimefanya kazi nzuri, iliyostahili kuwasilishwa kwa kiongozi wao mkuu wa nchi, lipo tatizo la msingi sana hapa – nalo ni utovu wa imani.
Maadili ya Taifa yakianza kuvujwa, huku Taifa lina vyombo vya kumsaidia Mwenyekiti / Rais, na viongozi wenzake, kulinda maadili hayo yasivunjwe – rais anayo haki ya kuwa na wasiwasi na kutaka vyombo hivyo vijieleze na viwajibike kwa wananchi – maana vyombo hivyo ni vyao. Taifa zima linapiga kelele “Rushwa! Rushwa! Rushwa!” Labda si rushwa tu, ni kuuza nchi, kwani fedha zinaonekana ni nyingi sana lakini zisizojulikana zinatoka wapi!
Wanayo pia haki ya kutaka maelezo ya Mwenyekiti/Rais wao kuhusu vyanzo vya fedha hizi zinazotumiwa kuvuruga Chama na Taifa. CCM, itake isitake, inayo kasoro katika eneo hili. Na viongozi wa CCM hawana budi kukubali kuwajibika kwa wananchi kwa madhara yoyote yanayoweza kusababishwa na hali hii ya rushwa sugu. …Mwisho wa kunukuu.
Sehemu hiyo niliyoinukuu inadhihirisha jinsi CCM ilivyoanza kupoteza dira.
Kutokana na CCM kuanza kupoteza dira, Mwalimu Nyerere katika kitabu chake, Nyufa, cha mwaka 1995, alisema: “Sasa Tanzania inanuka rushwa… tunataka kiongozi anayejua hivyo, ambaye atasema rushwa kwangu mwiko, mwaminifu kabisa kabisa, hawezi kugusa rushwa na… watoa rushwa watamjua hivyo.
“Lakini hatutaki aishie hapo tu, maana haitoshi wewe mwenyewe uwe mwaminifu… Unaweza ukawa wewe mwaminifu kabisa kabisa, lakini una shinikizo la ndugu zako, jamaa zako na marafiki zako.
“Kwa hiyo sio inatosha wewe kuwa mwaminifu tu, lakini uwe na uwezo wa kuwaambia jamaa zako kwa kauli ambayo wataiheshimu na hawatarudia tena. Unawaambia jamaa na rafiki zako kwa dhati kabisa… Ikulu ni mahali patakatifu, mimi sikuchaguliwa na wananchi wa Tanzania kuja kupageuza pango la walanguzi na hakuna serikali yoyote duniani inayoongozwa bila miiko.”
Baada ya Kikwete kuapishwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 2005, alimteua Lowassa kuwa Waziri wake Mkuu. Ni dhahiri kwamba alitimiza dhamira yake ya mwaka 1995. Hata hivyo, baada ya muda mfupi uongozi wa Kikwete uliingia kwenye kashfa ya Richmond uliosababisha Lowassa kujiuzuru uwaziri mkuu.
Watanzania wengi mnakumbuka kashfa hii ilivyolitikisa Taifa letu. Baadae CCM ilitaka kumvua gamba Lowassa pamoja na makada wengine kwa tuhuma za ufisadi. Lowassa aligoma na kusema yeye anaonewa kwani yeye kama Waziri Mkuu alikuwa akitoa taarifa juu ya suala hilo kwa mamlaka iliyokuwa juu yake, Ikulu.
Lakini tatizo la utetezi wake huu ni kwa nini utetezi huu hakuutoa Bungeni? Hakuwa na uzalendo. Ni dhahiri alikuwa akimlinda Kikwete ambaye inasemekana ni rafiki yake kwani kwa nyakati tofauti Lowassa aliwahi kusema urafiki wake na Kikwete si wa kukutana barabarani.
Minyukano ya kuwania kuteuliwa kugombea nafasi ya urais ndani ya CCM na mbinu chafu zinazotumika leo kuelekea uchaguzi mkuu mwaka 2015 oktoba ambazo watanzania tunazishudia ni mbinu zile zile zilizotumika mwaka 1995 na 2005 na zinatumiwa na watu walewale na nichanzo cha CCM kuanguka na taifa letu kuyumba.
Na Lowassa ameonyesha nia ya kutaka kugombea urais kupitia CCM. Zipo dalili za wazi kwamba CCM isingependa kumpitisha Lowassa kutokana na tuhuma za mbinu chafu. Wapo wanaomtetea kwama hana tuhuma na wapo wanaoona kwamba tuhuma hizo ni za kweli. CCM imegawanyika.
Mgawanyiko huu umeingia hadi nyumba za ibada, vyuo vikuu, vyombo vya usalama na kadhalika. Jamii nzima imegawanyika. Taifa limegawanyika. Sababu za kugawanyika kwa Taifa zinatokana na mbinu chafu zinazotumika wala si kwamba jamii inamhitaji sana Lowassa. Inawezekana kabisa Lowassa hajui, lakini chanzo kikuu ni wapambe wake.
Ningependa tujiulize, Lowassa aliwania kugombea urais 1995 akaondolewa na CCM kwa tuhuma za kutumia mbinu chafu ikiwemo kujilimbikiza mali. Mwaka 2007 akajiuzulu Uwaziri Mkuu kwa tuhuma za ufisadi. Kwa sasa anataka kugombea tena urais na bado anatuhumiwa na chama chake kwa kutumia mbnu chafu.
Kwa nini mwenzetu huyu, Lowassa anataka sana kwenda Ikulu kwa gharama yoyote? Tunafahamu uongozi ni utumishi. Huwezi kung’ang’ania au kulazimisha kuongoza au kuitumikia jamii wakati huo huo jamii hiyo ina mashaka na uadilifu wako. Haiwezekani.
Ningependa kumshauri Edward Ngoyai Lowassa kwa dhati kabisa kutoka kwenye sakafu ya moyo wangu aache wazo la kugombea urais bali apumzike na siasa.
Akichukua uamuzi huo ataiponya nchi yetu na inawezekana akaheshimika na Watanzania watamkumbuka kichanya. Pia napenda kuwashauri wapambe wake Lowassa watumie busara zao kumshauri Lowassa afute wazo la kugombea urais ili nchi yetu itulie.
Aidha, Rais wetu ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM anayo nafasi kusaidia kutoa ufafanuzi na hatimaye kufikia maamuzi ya kuliponya taifa letu kama alivyofanya Mwalimu Nyerere. Nyerere alitanguliza utaifa kwanza, akasema ukweli na maamuzi sahihi yakafanyika.
A friend in power is a friend lost. Taifa letu kwanza urafiki baadae. Kikwete amshauri Lowassa aache kugombea urais kwa ajili ya kuliponya Taifa letu.
Ninapohitimisha makala hii napenda kusisitiza: Heri wenye njaa na kiu ya haki, maana hao watashibishwa. Mabadiliko yanawezekana,tukiamini. Pasipo imani,hakuna kinachowezekana.

http://www.raiamwema.co.tz/chanzo-cha-kuyumba-kwa-taifa-letu

No comments :

Post a Comment